Featured Post

SERIKALI YASAINI MKATABA WA KUBORESHA HUDUMA ZA MAWASILIANO VIJIJINI NA MIPAKANI

Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano , Profesa Makame Mbarawa akizungumza na watendaji wa Mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF) pamoja na Wadau wa kampuni za simu zilizokubali kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya  mawasiliano vijijini hapa nchini( hawapo pichani), Jijini Dar es Salaam.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Eng. Peter Ulanga akitoa maelezo kuhusu huduma za mawasilino nchini kwa Waziri Wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano , Profesa Makame Mbarawa (Hayupo pichani), Jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Eng. Peter Ulanga (Kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya simu Vodacom Bw. Ian Ferrao(Kushoto), wakisaini mkataba wa ujenzi wa miradi ya mawasiliano ya simu katika Sehemu za mipakani na maeneo maalumu.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Eng. Peter Ulanga (Kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya simu Halotel Bw. Le Van Dai (Kushoto), wakisaini mkataba wa ujenzi wa miradi ya mawasiliano ya simu katika Sehemu za mipakani na maeneo maalumu.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Eng. Peter Ulanga (Kulia) na Eng. Cecil Nkomola  kutoka  kampuni ya simu Tanzania (TTCL) Kulia, wakisaini mkataba wa ujenzi wa miradi ya mawasiliano ya simu katika Sehemu za mipakani na maeneo maalumu.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Eng. Peter Ulanga (Kulia) na Mkurugenzi wa Mawasilino wa kampuni ya simu Airtel Bi. Beatrice Singano (Kushoto), wakisaini mkataba wa ujenzi wa miradi ya mawasiliano ya simu katika Sehemu za mipakani na maeneo maalumu.
Waziri Wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (Katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote pamoja na Watendaji wa kampuni zinazotoa huduma za simu nchini, Jijini Dar es Salaam.
Waziri Wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na Watendaji wa Mfuko wa Mawasiliano kabla ya kusaini mkataba wa ujenzi wa miradi ya mawasiliano ya simu katika Sehemu za mipakani na maeneo maalumu.

Picha na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (WUUM)

Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano  kwa wote (UCSAF) imesaini mkataba wa ujenzi wa mradi wa miundombinu ya mawasiliano ya simu katika Sehemu za mipakani na maeneo maalumu ili kuweza kufikisha huduma bora za Mawasiliano.
Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema kupitia utiaji saini  wa kampuni tano za mawasiliano ya simu  nchini kutawezesha kata 75 za vijijini kufikiwa na huduma za mawasilino ya simu.
“Lengo ni kuendelea kutoa huduma bora za mawasiliano kwa wananchi, leo tumesaini mkataba huu utakaogharimu kiasi cha pesa sh. Bilioni 10.4 ili kujenga miundombinu bora na kukamilika kwake kutawanufaisha takribani wananchi Milioni 3.4,” amesema Profesa Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa amezipongeza kampuni tano za mawasiliano ya simu  zilizokubali kushirikiana na Serikali katika kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo ambayo yanaonekana hayana mvuto wa kibiashara hapa nchini.
“Nazipongeza kampuni za Simu kwa kuwa na muitikio wa kuungana nasi katika kuboresha huduma hizi, mmeonyesha moyo wa upendo kwa watanzania wenzetu ambao na wao wanahitaji huduma za uhakika za mawasiliano,” amesisitiza Waziri Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa pia ameahidi kutoa ushirikiano kwa kampuni hizo endapo zitakutana na changamoto wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo ili ikamilike kulingana na makubaliano ya mkataba.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Eng. Peter Ulanga amezihimiza kampuni za simu nchini kujenga miundombinu ya utoaji wa huduma za data kwa 3G na 4G katika sehemu za vijijini ili kuwezesha wakazi wa maeneo hayo kuendana na sayansi na teknolojia.
“Wakati wa utekelezaji wa mkataba huu tuhakikishe kuwa utoaji wa huduma kwa njia ya data unaimairishwa katika sehemu hizo ili kuwezesha watanzania wote wanapata huduma sawa na wakazi wa mijini,” amesema Eng. Ulanga.

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (Mfuko) ulianzishwa na Serikali kwa sheria namba 11 ya mwaka 2006 ambayo ilipewa jukumu kuu la kupeleka mawasiliano vijijini. 

Comments