Featured Post

SERIKALI KUTUMIA MFUMO KUDHIBITI AJALI BARABARANI

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akizungumza na wataalam wa mfumo wa kieletroniki wa usalama barabarani katika kikao kazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Eng. Hamad Masauni.

Serikali imetoa mwezi mmoja kwa Mamlaka zinazohusika na masuala ya usalama barabarani kuhakikisha zinakamilisha uboreshaji wa mfumo wa kielektroniki wa uwekaji wa vifaa vya kufuatilia udhibiti mwendo barabarani ikiwa lengo ni kushughulikia matatizo ya kiusalama barabarani kupitia vyombo vya usafiri.

Akizungumza hayo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amesema kuwa mfumo huo uendane na utengenezaji wa mpango wa Taifa wa kufuatilia masuala ya kiusalama barabarani utakaohusisha wataalam kutoka Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) na Wataalam wa Idara ya Usalama na Mazingira (Sekta ya Ujenzi).
"Shirikianeni kutengeneza mfumo ambao utasaidia kutambua matatizo mbalimbali yanayoweza kujitokeza barabarani ili kubaini mwenendo wa mabasi na malori mwanzo hadi mwisho wa safari zake",  amesema Naibu Waziri Ngonyani.
Amesisitiza kuwa mfumo ambao utaandaliwa na wataalam hao unatakiwa kukidhi mahitaji ya kila mmoja ili kuleta matokeo chanya kwa manufaa ya nchi yatakayosaidia kupunguza ajali za barabarani zinazotokana na mwendo kasi, kupambana na uhalifu na kulinda usalama wa abiria.

Aidha, Eng. Ngonyani amefafanua kuwa katika juhudi za kuhakikisha serikali inapunguza ajali za barabarani wizara yake kupitia Idara ya Usalama na Mazingira tayari imesaini mkataba wa kufunga kamera za udhibiti mwendo kasi katika barabara kuu ya TANZAM (Dar es Salaam - Tunduma), ambapo sehemu ya majaribio ya mradi huo imefanyika katika maeneo ya
Dar es Salaam - Chalinze - Morogoro.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Eng. Hamad Masauni, amesema kuwa taratibu za kutengeneza mfumo huo zinatakiwa kukamilika haraka ili kusaidia Jeshi la Polisi kutumia mfumo huo kuweza kupambana na uhalifu katika maeneo mbalimbali ya nchi. 

Ametanabaisha kuwa Serikali itamchukulia hatua kali za kisheria mtu yeyote atakaejaribu kuhujumu mfumo huo kwani serikali itatumia fedha nyingi kuutekeleza kwa lengo la kuhakikisha usalama wa raia unalindwa ipasavyo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, Gilliard Ngewe, ameeleza manufaa ya mfumo huo kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri wa magari ya abiria na mizigo kuwa ni itasaidia kupunguza matumizi ya mafuta, uharibifu wa matairi ya magari mara kwa mara na kupunguza gharama za matengenezo ya magari.

Mfumo huo wa kieletroniki wa usalama barabarani ni moja ya mbinu zinazotumiwa na Serikali katika kuhakikisha matumizi ya usalama barabarani yanazingatiwa kwa mujibu wa Sheria, Taratibu na Kanuni.

Comments