- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Unknown
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Jumia Travel Tanzania
Miongoni mwa tasnia zinazokua kwa kasi sasa hivi nchini Tanzania ni uandishi wa mtandaoni au blogu. Kuenea na ukuaji wa matumizi ya mtandao wa intaneti kumepelekea watu waliokuwa wanatamani kuingia kwenye tasnia ya uandishi kufungua blogu zao mitandaoni.
Blogu zinatoa fursa kubwa kwa watu mbalimbali wanaopenda uandishi kuandika masuala mbalimbali juu ya mada tofauti na kuwashirikisha wasomaji wao kwa njia ya mtandao. Jumia Travel ingependa kukufungua macho kwamba miongoni mwa masuala ambayo mpaka sasa hayajaangaziwa kwa kiasi kikubwa ni pamoja na vivutio vilivyopo sehemu tofauti za nchi ya Tanzania. Zifuatazo ni baadhi tu ya faida chache za kuanza kuandika na kuwashirikisha wasomaji wako juu ya maeneo tofauti unayoyatembelea.
Ni fursa ya kuwashirikisha wasomaji wako sehemu tofauti ulizotembelea. Sio watu wote wamebahatika kusafiri na kujionea maeneo tofauti mbali na pale wanapoishi. Zipo sababu nyingi zikiwemo shughuli zao kutowaruhusu, kutokuwa na kipato kinachokidhi au kuwa na majukumu mengine. Hivyo basi kama umepata fursa ya kusafiri sehemu mbalimbali kuna haja ya kuwasimulia wale ambao hawajawahi kufika. Kwa kufanya hivyo utajikuta bila ya kujijua unatoa elimu, kutoa mwamko na hamasa ya watu juu ya sehemu hiyo na hata kutembelea siku za usoni.
Kunaweza kuwa chanzo cha kukuingizia kipato. Unaweza ukaanza kama masihara kuwa unaandika juu ya sehemu unazotembelea kwa kuwa unapenda lakini huweza kujua kwamba inawezekana kuna watu wanafuatilia kazi zako na kuzipenda. Matokeo ya kuwa mwandishi mzuri wa makala za kuvutia na wasomaji wako wakazipenda kunaweza kukufungulia milango ya biashara. Kampuni au mashirika mbalimbali yanaweza kupendezewa na kazi zako na kutaka kuzitumia au wakakulipa ili uandike kwa ajili yako.
Kwa nchi ambazo zimeendelea hususani za Ulaya, Marekani na Asia wapo waandishi wengi wa namna hii wanasafiri na kuandika vile wanavyoviona na kujiingizia kipato cha kutosha na kuendesha maisha yao. Mbali na njia hiyo yapo pia makampuni, mashirika au wafanyabiashara watakaokutafuta kutaka kutangaza kupitia blogu yako. Kenya wenzetu wamekwishaanza na wanafanyaa vizuri hivyo ni wakati sasa kwa watanzania nao kuchangamkia fursa hii.
Blogu yako inaweza kutumika kama sehemu ya kutoa elimu. Ukiwa ni mwandishi mzuri na uliyobobea kwenye sekta unayoiandikia kuna fursa kubwa ya kujijengea uaminifu na mamlaka kwa wasomaji wako. Ukishajijengea uaminifu miongoni mwa wasomaji wengi basi unakuwa na mamlaka juu ya kile unachokiandikia na hivyo blogu yako ikatumika kama kielelezo muhimu. Kwa hiyo ili kufanikiwa katika hili hakikisha kwamba unaijua vema sekta uliyopo ili kutoa taarifa ambazo watu wataziamini na kuzitumia.
Uandishi wa kwenye blogu ni miongoni mwa taaluma yenye soko kubwa kwa sasa. Katika ulimwengu huu wa kidigitali hakuna taasisi, shirika, kampuni au mfanyabiashara ambaye hayupo mtandaoni. Na hii ni kutokana na uwezo wa njia hiyo kuwafikia watu wengi na tofauti kwa haraka ndani ya muda ukizingatia hakuna gharama kubwa zinazotumika. Hivyo basi kwa kuonyesha uwezo wako wa kuandika unaweza kupata fursa ya kutafutwa na makampuni yenye uhitaji na watu wenye sifa kama zako. Hivyo basi ni vema kuonyesha bidii na ueledi mkubwa kwenye kile unachokiandika ili kuwavutia watu makini.
Ni fursa ya kuitangaza nchi yako. Bila ya kujijua kwamba kupitia maandiko juu ya sehemu mbalimbali unayoyachapisha kwa wasomaji wako yanaweza kuwa na mchango mkubwa kwenye kuvitangaza vivutio vya nchi yako. Mwisho wa siku simulizi za maeneo unayokwenda huwavutia watu wa ndani na nje ya nchi na kutamani kwenda kujionea wenyewe kwa macho yao. Lakini isingekuwa hivyo bila ya nguvu ya ushawishi wa makala zako. Hivyo ni vema kuandika kwa ustadi mkubwa ambao utamfanya mtu akisoma ajikute naye ni sehemu ya safari uliyoipitia.
Kuna matukio mengi sana ya kuvutia na kusisimua ambayo tunajionea sehemu mbalimbali tunazozitembelea ambayo kwa hakika kuwasimulia marafiki pekee haistoshi. Jumia Travel inaamini kwamba kuanzisha blogu yako unaweza kuushirikisha ulimwengu na kusafiri nawe sehemu mbalimbali za Tanzania. Ni rahisi, haichukui muda na hakuna malipo ili kufungua blogu, tembelea tovuti kama vile Blogger au Wordpress ambayo inaweza kukuwezesha kufungua blogu yako bure kabisa.
Comments
Post a Comment