Featured Post

JAPAN YAISAIDIA TANZANIA SHILINGI TRILIONI 74 KUTEKELEZA MIRADI KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MITANO

Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan-JICA, Bw. Shinichi Kitaoka (katikati) akizungumza kuhusu ushirikiano imara kati ya Tanzania na nchi yake, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), Jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Balozi wa Japan hapa nchini Bw. Masaharu Yoshida na kushoto kwake ni Mwakilishi Mkazi wa JICA hapa nchini Bw. Toshio Nagase.
Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan-JICA, Bw. Shinichi Kitaoka (Kulia) akimweleza jambo Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), walipokutana na kufanya mazungumzo Jijini Dar es Salaam
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)


Benny Mwaipaja, WFM-Dar es Salaam

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amelishukuru Shirika la Maendeleo la Japan-JICA, kwa uwekezaji mkubwa uliofikia kiasi cha Shilingi trilioni 74.93 katika miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Dkt. Mpango ametoa shukrani hizo Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirika hilo, aliyepo katika ziara ya kikazi hapa nchini, Bw. Shinichi.

Kiasi hicho cha fedha kinahusisha ruzuku asilimia 76.0, mikopo yenye masharti nafuu asilimia 3.8 na usaidizi wa kiufundi asilimia 20.1.

Amemwomba Rais huyo wa JICA, kuongeza ufadhili kwenye miradi ya nishati ya umeme, miundombinu, afya, kilimo na uvuvi kusaidia kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kukuza uchumi wa viwanda.


“Sekta ya viwanda haiwezi kuendelea kama hakutakuwa na uwekezaji mkubwa kwa upande wa nishati ya umeme pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara” alisisitiza Dkt. Mpango.

Amesisitiza pia umuhimu wa Shirika hilo kuisaidia Tanzania kuboresha sekta ya afya kwa kujenga Hospitali zitakazo hudumia magonjwa makubwa kama ya moyo na mengine mengi pamoja na kuweka vifaa vya kisasa kwa kuwa Japan inafanya vizuri katika masuala hayo.

“Eneo lingine tunaloona ni muhimu ni kusaidia kutoa ufadhili wa masomo ya ujuzi wa aina mbalimbali kwa vijana wetu ili waweze kusaidia nchi katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya kiuchumi” aliongeza Dkt. Mpango.

Kwa upande wake, Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan-JICA, Bw. Shinichi Kitaoka, ameahidi kuwa shirika lake litaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutatua changamoto zinazokwaza maendeleo yake.

Amesema kuwa pamoja na kuendelea kusaidia ujenzi wa miundombinu, Shirika lake litaangalia namna ya kusaidia Sekta ya afya kwa kuboresha lishe kwa watoto ili kujenga kizazi imara na chenye nguvu.

Bw. Shinichi Kitaoka ameahidi kwenda kuwahamasisha wawekezaji mbalimbali kutoka nchini mwake kuja kuwekeza Tanzania kwa kuwa kuna fursa nyingi za kiuchumi.

Japan, kupitia Shirika lake la Maendeleo-JICA, inatarajia kutekeleza miradi mipya maendeleo hapa nchini ukiwemo awamu ya pili ya ujenzi wa barabara kutoka Moroco hadi Mwenge Jijini Dar es Salaam, utakayogharimu shilingi bilioni 1.38, ambao mkataba wake utasainiwa majuma mawili yajayo.

Mradi mwingine ni upanuzi na uboreshaji wa barabara ya kuanzia makutano ya eneo la Kamata na barabara ya Kilwa, unaotarajiwa kuanza wakati wowote baada ya masuala ya changamoto za kiufundi kukamilika, utakao gharimu shilingi bilioni 24.2.

Aidha, Japan, imefadhili mradi wa ujenzi wa Barabara ya Arusha hadi Holili utakaogharimu Dola milioni 269.8 utakapo kamilika huku mradi mwingine unaoendelea ni ule wa ujenzi wa barabara za juu katika eneo la TAZARA, Jijini Dar es Salaam.

Kuhusu biashara kati ya Tanzania na Japani, imeendelea kuimarika ambapo kati ya mwaka 2015/2016 nchi hiyo imeingiza bidhaa nchini zenye thamani ya Dola milioni 363.0 hadi kufikia Dola milioni 371, sawa na ongezeko la asilimia 2.2

Katika kipindi hicho Tanzania haikufanya vizuri ambapo kiwango cha mauzo ya bidhaa nje ya nchi kilishuka kutoka Dola za Marekani milioni 229.7 hadi Dola milioni 138.5 sawa na asilimia 39.7 hali iliyosababishwa na ushindani mdogo wa wazalishaji wa Tanzania ikilinganishwa na wenzao wa Japani.

Comments