Featured Post

DOKTA PHILIP MPANGO ATEMBELEA KIWANDA CHA KUUNGANISHA MATREKTA YA URSUS-KIBAHA

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akiwasha moja ya matrekta yaliyounganishwa katika Mradi wa Kuunganisa Matrekta ya URSUS-TAMCO, uliopo katika eneo la Kibaha mkoani Pwani, alipotembelea mradi huo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati) akiwasili katika kiwanda cha kuunganisha Matrekta ya URSUS-TAMCO, kilichoko Kibaha mkoani Pwani kuangalia kazi ya uunganishaji matrekta zaidi ya 200 pamoja na kusikiliza changamoto zinazoukabili mradi huo.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)

Na Benny Mwaipaja-Kibaha
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ametembelea mradi wa kuunganisha matrekta ya Ursus, uliopo Kibaha mkoani Pwani na kusisitiza kuwa Serikali imedhamiria kuendeleza kilimo nchini ili kukuza sekta ya viwanda.
Tayari Matrekta 204 yenye uwezo wa HorsePower 50 yamekwisha unganishwa yakisubiri kuuzwa kwa watumiaji hatua ambayo Dkt. Mpango amesema itaongeza tija katika kilimo na kukuza ajira hususan kwa kundi kubwa la vijana.
Ameahidi pia kuwa Serikali itayafanyiakazi haraka maombi ya Shirika la Maendeleo la Taifa NDC la kutaka kupata kibali cha kuajiri zaidi ya wafanyakazi 90 watakaohusika na mradi huo pamoja na kutoa shehena ya Matrekta 267 yaliyokwama katika Bandari ya Dar es Salaam ili yaweze kuuzwa kwa wananchi kuendeleza kilimo.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi huo kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa-NDC, Mhandisi Adam Mbura, amesema mradi huo utahusisha pia uanzishwaji wa vituo vinane katika kanda mbalimbali kwa ajili kuuza matrekta, zana na vifaa vingine pamoja na  kutoa huduma kwa wateja.
Amesema kuwa kukwamuliwa kwa makontena 64 yaliyokwama bandarini yakiwa na matrekta hayo 267 pamoja na vipuri vya kuunganisha Matrekta hayo pamoja na baadhi yaliyopo katika eneo la Mradi la TAMCO, Kibaha mkoani Pwani, kutawezesha kukamilisha haraka kwa kazi hiyo.
Baadhi ya vijana wanaofanyakazi katika mradi huo wamesema kuwa wamenufaika na ujuzi wanaoupata kutoka kwa wataalamu wa ufundi kutoka nchini Poland na kuahidi kuuendeleza ujuzi huo kwa vijana wenzao ili mradi huo uweze kuwa na manfaa kwa kutatua changamoto mbalimbali za kiufunsi zitakazokuwa zikiwakabili wakulima.
Mradi wa kuunganisha Matrekta ya URSUS-TAMCO, Kibaha Mkoani Pwani unafadhiliwa na Serikali ya Poland ambapo kiwanda kikubwa cha kuunganisha matrekta kinatarajiwa kujengwa katika eneo hilo na yatauzwa kwa gharama nafuu, kati ya shilingi milioni 38 hadi milioni 42 kulingana na ukubwa na uwezo wa trekta.

Comments