Featured Post

SERIKALI YAKUSANYA SHILINGI BILIONI 32.5. KATIKA KODI YA MAJENGO

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akiwaomba wananchi kulipa kodi ya Majengo mapema kwa mwaka wa Fedha 2017/18 ili kuepuka usumbufu wa msongamano, alipofanya Mkutano na Waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akivipongeza Vituo vya Mafuta vya Puma na Total kwa kuonesha mfano wa kufunga mashine za EFDs katika Pampu zote za mafuta kwenye vituo vyao, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
(Picha: Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)

Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh bilioni 32.5 ya  kodi ya majengo, kwa mwaka wa fedha 2016/17 kutoka katika Majiji, Miji na Manispaa 30 nchini.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb) amewaambia waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kwamba makusanyo hayo ni sawa na asilimia 56 ya lengo lililowekwa Mwaka wa Fedha uliopita la kukusanya shilingi bilioni 58.

Alisema kuwa hatua niyo ni mafanikio makubwa tangu TRA ipewe jukumu la kukusanya kodi hiyo ambapo mwaka wa fedha 2015/2016 katika maeneo hayo, Halmashauri zilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 28.3 wakati TRA imekusanya kiasi hicho cha shilingi bilioni 32.5 tangu ianze kukusanya kodi hiyo mwezi Oktoba mwaka wa fedha 2016/2017.

“Mpaka kufikia tarehe 15 Julai mwaka huu TRA imekusanya sh. bil 32.5 kipindi ambacho ni kifupi, na kwamba mapato hayo yanatarajiwa kuongezeka kutokana na mwitio mkubwa wa wananchi kulipa kodi ya majengo”Alisema Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango aliwapongeza wananchi kwa mwitio wao mkubwa wa kulipa kodi ya majengo na kwamba wameonesha uzalendo wa kweli na ndio maana Serikali imeamua kuongeza muda wa kulipa kodi hiyo bila adhabu hadi Julai 30 mwaka huu, hali anayoamini itapandisha zaidi mapato hayo.

Katika hatua nyingine Dkt, Philip Mpango aliwapongeza  wamiliki wa vituo vya mafuta waliotii  maagizo ya Serikali, kwa kufunga mashine stahiki za EFDs, akitolea mfano vituo vya PUMA na TOTAL ambavyo vimefunga  mashine hizo kwenye pampu zao zote.

Aliwaonya wamiliki wote wa vituo vya mafuta ambao hawatafunga mashine hizo za EFDs ndani ya siku 14 kama agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli linavyoelekeza na kwamba yeye kama Waziri mwenye dhamana atahakikisha analisimamia kikamilifu na kwamba baada ya muda huo mtu asijekuilaumu Serikali baada ya kuanza kuchukua hatua kali za kisheria.

Aliwataka wamiliki wa vituo hivyo kupitia chama chao cha wamiliki wa vituo vya mafuta TAPSOA kuheshimu maelekezo ya Serikali na kuacha majibizano yasiyo na tija kuhusu amri hiyo ya Rais kwenye vyombo vya habari kwa kuwa huo ni utovu wa nidhamu.

Aliwageukia wenye maduka ya vifaa vya ujenzi, vileo na maduka makubwa ‘supermarket’ nao watumie mashine hizo za kukusanyia mapato ya Serikali (EFDs) kikamilifu na kutoa risiti kwa wateja wao huku akiwaasa wateja nao kudai risiti wanapofanya manunuzi kulingana na kiwango halisi cha bidhaa wanazonunua.

Alipiga marufuku wafanyabiashara wanaosingizia mashine za EFDs kuwa mbovu na kuwaonesha wateja wao makaratasi waliyotoa taarifa TRA kwamba mashine zao zilikuwa mbovu kwa kipindi kifrefu na kuaigiza Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kusimamia jambo hilo ili kuhakikisha kuwa linakoma kabisa.

“TRA mtimize majukumu yenu mliyodhaminiwa na Serikali na kuhakikisha kuwa wafanyabiashara ambao mashine zitakuwa hazitumiki ndani ya saa 48 kwa kisingizio cha kuharibika zifungiwe na wamiliki watozwe faini na kulipa kodi ya Serikali ipasavyo” aliagiza Dkt. Mpango.

“Serikali ya Awamu ya Tano haijaribiwi, tumeazimia tutafanya kazi kwa niaba ya wanyonge ili nchi yetu iende mbele na kwa hili watusamehe.” Alisisitiza Dkt. Mpango

Dkt Mpango alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kujitoa kwake kuwatumikia wananchi na kuongoza mapambano ya uchumi yatakayo ifikisha nchi kwenye uchumi wa kati ambao hata watu wa kawaida watajisikia kuwa unakua kwa kutatua changamoto zao za maisha.

Alisitiza watanzania wafanye kazi kwa bidii kujenge nchi ili kila Mtanzania apate huduma bora, barabara bora, tiba nzuri, maji, yote haya hayawezi kufanyika bila mapato yakutosha na kwamba Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe. 

Comments