Featured Post

DKT. PHILIP MPANGO ABAINI BAADHI YA WAFANYABIASHARA DODOMA HAWATUMII IPASAVYO EFDs

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) akikagua mashine ya EFD na risiti ya kieletroniki aliyopewa baada ya kununua bidhaa kwenye moja ya maduka mjini Dodoma, alipofanya ziara ya kushitukiza kukagua kama wafanyabiashara wa mji huo wanatumia ipasavyo mashine hizo.

BENNY MWAIPAJA, DODOMA

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dokta Philip Mpango, amefanya ziara ya kushitukiza katika mitaa ya mji wa Dodoma na kubaini baadhi ya wafanyabiashara hawatumii ipasavyo mashine za kieletroniki za kukusanyia kodi ya Serikali-EFDs na kuwaonya wafanyabiashara kote nchini kuacha mchezo huo.

Dkt. Mpango aliyeambatana na baadhi ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato hapa nchini-TRA mkoa wa Dodoma amebaini baadhi ya wafanyabiashara hao wasio waaminifu hawatoi risiti huku wengine wakiandika kiwango kidogo cha fedha kwenye risiti hizo.

Mmoja wa wafanyabiashara aliyekumbana na mkono wa Waziri Dokta Mpango, ni Bwana ISDORI SHIRIMA ambaye amekiri kufanya makosa ya kutotumia mashine hizi ipasavyo

“naomba unisamehe Mheshimiwa, sitarudia tena unajua sisi vijana tunabangaiza, lakini nimebaini nimefanya makosa” aliomba msamaha Bw. Shirima

Hata hivyo Dkt. Mpango ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA mkoa wa Dodoma, kufanya ukaguzi wa kina wa mahesabu ya mfanyabiashara huyo ili kubaini kiwango cha kodi alichokwepa na kumchukulia hatua stahiki.

Aidha, Dokta Mpango ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA mkoa wa Dodoma kuwapeleka ofisini kwake mawakala wote mkoani humo wanaosambaza mashine za kieletroniki za kukusanyia mapato EFDs baada ya kubaini kuwa zaidi ya mashine 100 zimeharibika na hazitumiki tangu jana.

“Kuna kitu sikielewi na hakiingii akilini, inakuwaje mashine ziharibike kwa kiwango hicho, mashine 100 kuharibika kwa siku mbili ni nyingi na ina maana nimekosa mapato mengi” alielezea kwa masikitiko Dkt. Mpango.

Aliagiza mawakala wote wanaosambaza ama kuuza mashine hizo wakutane naye ofisini kwake mjini humo ili kubaini tatizo na kuongeza kuwa haiwezekani wafanyabishara walipie mashine hizo zaidi ya mwezi uliopita lakini hawapelekewi hali inayozidi kuikosesha Serikali mapato yake.

Baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wamepongeza uamuzi wa Serikali wa kulivalia njuga suala la kodi na kwamba wako tayari kuiunga mkono Serikali kwa kutoa risiti wanapouza bidhaa na kudai risiti zenye viwango sahihi vya manunuzi waliyoyafanya ili kuijengea Serikali uwezo wa kuihudumia jamii.

Dokta Mpango ametembelea pia baadhi ya vituo vya mafuta mjini humo na kuwakumbusha wamiliki wote wa vituo vya mafuta kuzingatia agizo la Serikali linalowataka wafunge mashine maalumu za kielektroniki zinazofungwa kwenye pampu za mafuta ndani ya siku 14 ambazo ziko ukingoni.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (katikati) akiwa na katika mitaa ya mji wa Dodoma alipofanya ziara ya kushitukiza, kukagua matumizi ya mashine za kutolea risiti kwa njia ya kielektroniki (EFDs) kwa wafanyabiashara wa maduka mjii humo.
Kiongozi wa Timu Maalumu ya Ukaguzi wa Mashine za EFD’s kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Dodoma, Bw. Godfrey Patrick (wa pili kushoto) akifafanua jambo wakati wa ziara ya kushitukiza iliyofanywa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb), kwenye maduka mjini Dodoma.
(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)

Comments