Featured Post

TGNP YAWANOA MADIWANI DAR KUHUSU UONGOZI WA KIJINSIA


Grace Kisetu, Mkuu wa Idara ya Ijenzi wa Nguvu Pamoja wa TGNP Mtandao, akizungumza na washiriki katika warsha ya Uongozi wa Kijinsia kwa Madiwani wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Husna Masoud, Diwani wa Viti Maalum, Kata ya Buguruni.

Diwani wa Viti Maalum Kata ya Mtoni wilayani Temeke, Kubra Abdallah.

Baadhi ya Madiwani wanaoshiriki warsha hiyo ya siku tatu.

Na Daniel Mbega
MADIWANI wanawake wa vyama mbalimbali vya siasa katika Mkoa wa Dar es Salaam wamesema suala la kubadili mtazamo katika ushirikishwaji wa wanawake kwenye maendeleo ni la msingi na linapaswa kutekelezwa kuanzia ngazi za chini.
Wakizungumza katika warsha ya siku tatu ya Uongozi wa Kijinsia iliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP Mtandao), madiwani hao wamesema haki za wanawake bado zinakandamizwa katika jamii huku vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vikishika kasi.
Husna Masoud, Diwani wa Viti Maalum, Kata ya Buguruni (Chadema), amesema katika kata yake hakuna usawa hata wa uongozi na kwamba bado vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vinaendelea.
 “Suala la unyanyasaji wa kijinsia bado limetamalaki katika jamii na lazima tulizungumzie kwa mapana ili kukomesha vitendo hivyo,” alisema Husna.
Kwa upande wake, Honorata Mashoto Mrisho, Diwani wa Viti Maalum Kata ya Ubungo (Chadema), amesema maamuzi mengi kuanzia ngazi ya kijiji hadi kata yamekuwa yakiwaacha nyuma wanawake, jambo ambalo linawanyima fursa za maendeleo.
Amesema kama wawakilishi wa jamii kwenye vikao mbalimbali vya Kata, watajitahidi kupigia kelele masuala yote ya jinsia ili kuweka usawa pamoja na kuchochea maendeleo.
Salma Said El Maamry, Diwani wa Viti Maalum, Kata ya Mburahati, Ubungo, amesema haki za mtoto wa kike bado zinakandamizwa na jamii, hivyo ni lazima kupambana kuhakikisha wanapata mahitaji yao yanayostahili.
Amesema watoto wengi wa kike wanalazimishwa kuolewa kabla ya umri na jamii inafumbia macho, jambo ambalo linawanyika haki ya kutimiza ndoto zao katika maisha, hasa suala la elimu.
Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum Kata ya Mtoni wilayani Temeke, Kubra Abdallah, amesema watoto wa kike wanakosa vipindi vya masomo kutokana na ukosefu wa elimu ya kujihifadhi hasa wanapokuwa katika hedhi.
“Elimu ya hedhi bado duni sana, hasa vijijini, kwa sababu watoto wengi wa kike wanapokuwa katika hedhi huhisi kwamba ni wagonjwa, hivyo hushindwa kuhudhuria vipindi ipasavyo… lazima elimu hii itolewe kwa jamii ili kuwawezesha watoto hawa wapate elimu kama ilivyo kwa wale wa kiume,” alisema Kubra.
Awali, mmoja wa wawezeshaji kutoka TGNP Mtandao, Anna Kikwa, amesema warsha hiyo imelenga masuala mbalimbali kwa madiwani hao ikiwa ni pamoja na kubadilisha mawazo na uzoefu wa namna ya kufuatilia bajeti zinazohusu jinsia.
“Malengo ya warsha hii ni kuongeza uelewa katika masuala ya uongozi na jinsia pamoja na bajeti kwa mlengo wa kijinsia,” alisema Anna Kikwa.
Aidha, alisema malengo mengine ni kushirikishana uzoefu, changamoto, mbinu na mikakati ya uongozi kwa wanawake ili kukuza uwezo wao kama viongozi bora na kuboresha utendaji wao.
Aliongeza pia kwamba, warsha hiyo imelenga kushirikishana masuala yaliyoibuka kwenye uraghibishi na tafiti mbalimbali zilizofanywa na TGNP Mtandao pamoja na taasisi nyingine.
“Pia tunatakiwa kuweka mikakati ya pamoja ya kuongeza nafasi ya mwanamke katika kuchangia, kushawishi na kufanya maamuzi katika ngazi mbalimbali ikiwemo kuanzisha umoja wa madiwani wanawake nchini.
Naye Grace Kisetu, Mkuu wa Idara ya Ijenzi wa Nguvu Pamoja wa TGNP Mtandao, amesema suala la haki ya mwanamke katika uongozi ndilo la msingi na kwamba taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele kulitetea.
“TGNP imekuwa ikijihusisha katika utetezi wa haki za jamii kuanzia wanawake, watu wenye ulemavu, wanaume walio katika umaskini na kadhalika, lakini pia tunatetea makundi mbalimbali ya wanawake katika uzalishaji mali ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo katika shughuli mbalimbali ikiwemo kwenye uchimbaji wa madini,” alisema.


Comments