- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na
Eleuteri Mangi, MAELEZO
Miongoni mwa vitu vinavyomhangaisha
mwanadamu ni dhoruba za kimaisha, ameumbwa akiwa amekamilika kwa afya ya mwili,
inapotokea afya yake haipo sawasawa, hali hiyo hujulikana kama anaumwa au
mgonjwa.
Ugonjwa humfanya mtu ashindwe kutimiza
majukumu yake ya kila siku kiufasaha katika jamii na taifa bila kujali umri,
jinsia, kabila au rangi, awe mtoto, kijana, mtu mzima au mzee.
Mfumo wa maisha ya watu umekuwa chanzo
cha magojwa yanayomsumbua mwanadamu, sonona imekuwa tishio kwa maisha na humpata
mtu kutokana na maisha yasio na mpangilio yakiambatana na kujihisi huzuni.
Hali hii inaweza kuchukuwa wiki mbili au
zaidi kama haitadhibitiwa na kupelekea mtu kutotamani kuendelea kuishi, upweke,
kukosa tumaini na kuathiri utendaji wake wa kazi wa kila siku.
Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo Tanzania
ni mwanachama, limetenga Siku ya Afya Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka
Aprili 7, mwaka huu siku hii imetengwa kwa ajili ya kuwapa watu uelewa na
kutambua juu ya hali ya sonona ili jamii zote duniani wahamasike na kujikinga na
hali hiyo waweze kuokoa maisha ya watu wengi zaidi.
Ni dhahiri Sonona siyo udhaifu wa kitabia,
na wala haina maana kuwa mtu mwenye hali hiyo hana uwezo wa kufanya kitu chochote,
bali ni hali ya kimedikali kama yalivyo magonjwa ya kisukari au vidonda vya
tumbo, hivyo ni muhimu kwa mtu mwenye sonona kupata matibabu sahihi na stahili
kwa wakati.
Katika kuadhimisha siku hii, WHO hutoa kaulimbiu
inayobeba ujumbe maalum ambao
unalenga kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya suala mojawapo
muhimu na lenye manufaa kiafya kwa nchi zote wanachama.
Ndiyo maana Tanzania imeungana na WHO kusimamia
afya za wananchi kupitia Wizara yenye dhamana kwa kuunganisha nguvu pamoja
katika maadhimisho ya mwaka huu kuelimisha jamii kujua na kumtambua hali ya sonona
ili kuokoa maisha ya watu.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu
“Sonona, Tuzungumze”, hii ni dira na
mwongozo wa kuhamasisha wadau wote
na jamii kwa ujumla kutambua ukubwa wa tatizo hilo kwa kila taifa na kimataifa.
Hatua hii itasaidia jamii kujua visababishi
vyake, umuhimu wa kubadili tabia na mienendo hatarishi ili kudhibiti na
kujikinga na namna ya kupata huduma ya matibabu ya sonona mara baada ya
kugundulika ana hali hiyo.
Watafiti wameonesha kuwa sonona huathiri watu
wa rika zote na jinsia zote hasa vijana, wanandoa na kubainisha kuwa watu wenye
umri mkubwa wako kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa huo.
Hali hiyo inatokana na unyanyasaji wa
kijinsia na kimwili unaosababishwa na mambo mbalimbali yaliyotokea mwanzoni
wakati wa utoto ama karibuni, huzuni baada ya kufiwa na rafiki au mpenzi ama
ndugu, kuvunjika kwa mahusiano kama uchumba au kuachwa (TALAKA), hatua hiyo hupelekea
mtu kuwa na msongo wa mawazo.
Hali chanya katika maisha kama kuoa,
kupata kazi mpya, navyo vinaweza kusababisha mtu kupata ugonjwa wa sonona baada
ya kuwa na furaha isiyo na kifani.
Katika Ulimwengu wa leo, pombe na
matumizi ya madawa ya kulevya ni hatari zaidi kwa mtu mwenye sonona, akitumia
vilevi hivyo vinaweza kuchagia hali yake kuwa mbaya zaidi.
Kwa mujibu wa tamko la Waziri wa Afya,
Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alilolitoa hivi
karibuni amesema kuwa wizara yake inaendelea kushirikiana na wadau katika kutoa
elimu kuhusu namna ya kukabiliana na hali ya sonona kwa Watanzania.
Ni dhahiri jamii yenye afya bora inauwezo
wa kuchangia kujenga taifa na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati
ifikapo 2025 kulingana na Dira ya Maendeleo ya Taifa.
“Tunapozungumzia afya, tunamaanisha hali
ya ustawi wa mwanadamu kimwili, kiakili na kijamii. Mtu mwenye afya njema ya
akili anaaminika kutengemaa katika namna anavyofikiri, anavyohisi, na
anavyotambua mambo, ambayo kwa pamoja hujionyesha katika matendo yake ya kila
siku ikiwa ni pamoja na jinsi anavyohusiana na kushirikiana na wenzake katika
familia na jamii kwa ujumla” amesisistiza Waziri Ummy.
Kulingana na takwimu za hivi karibuni za
Shirika la Afya Duniani, zaidi ya watu milioni 300 wanaishi na hali ya kuwa na sonona
ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 18 kati ya mwaka 2005 hadi 2015.
Aidha, takwimu za WHO zinaonesha kuwa
kati ya watu 5, mmoja kati yao ana matatizo au alishapata matatizo ya Sonona
kutokana na ukweli kwamba watu wanaopata matatizo ya Sonona ni wachache tu
wanaweza kufikia na kupata huduma ya afya, hata hao wanaohudhuria katika vituo
vya Afya, wapo waliogundilika kuwa na tatizo la Sonona.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Afya ya
magonjwa ya Akili ya mwaka 2015/2016 inaonesha Tanzania kuna takribani Wagonjwa
41,789 waliogundulika kuwa na tatizo la Sonona. Idadi hiyo ni ndogo
ikilinganishwa na ukubwa wa tatizo linavyokisiwa kutokana na wagonjwa wachache kuudhuria
vituo vya kutolea huduma kwa matatizo mbalimbali ya afya ya akili na matatizo
ya kisaikolojia hapa nchini.
Naye Naibu Waziri Wizara hiyo Dkt. Hamis
Kigwangalla amesema kuwa dalili za mtu mwenye Sonona ni pamoja na kuwa na msongo
mkubwa wa mawazo, kukosa raha, usingizi na hamu ya kula, kujitenga na watu au
jamii inayomzunguka na mara nyingine kutaka kujiua au kuwaua watu wengine.
Kinga ni bora kuliko tiba, iwapo mtu ameonesha
kuwa na dalili zilizotajwa, familia na jamii wanashauriwa kuzungumza naye au
mtu wake wa karibu anayemwamini kuhusu matatizo yake yanayokukabili ili upate
ushauri na faraja itakayompunguzia msongo wa mawazo na kuondokana na tatizo
hilo.
Dkt. Kigwangala amesisitiza kuwa mtu anapoona
kuna dalili hizo ni vema apate muda wa kutosha, ale chakula, apumzika au kulala
na aendelee kufanya shughuli alizokuwa anafanya kabla ya kupata Sonona na
kuongeza iwapo dalili zinaendelea, mgonjwa apate ushauri wa kitaalam kutoka kwa
mtoa huduma za afya katika kituo cha afya kilicho karibu nae.
Katika kukabiliana na Sonona, Waziri Ummy
amesema ipo haja huduma za afya ya akili na saikolojia kutolewa katika maeneo
ya kutolea huduma za afya kwa jamii, kuwa na kitengo maalumu kinachotoa huduma
hizo katika hospitali zote nchini na kuboresha upatikanaji wa dawa.
Waziri Ummy ameongeza kuwa Serikali itapeleka
wataalamu wa afya ya akili wakiwemo Madaktari Bingwa ili kutoa huduma kwa wagonjwa
wa nje na wale waliolazwa pamoja na kuwajengea uwezo watoa huduma za afya ili
waweze kutambua na kubaini mapema dalili za ugonjwa huu na kutoa matibabu stahiki
au rufaa kwa wakati.
Ni vema Watanzania kutambua kuwa Sonona inazuilika
kwa kujenga familia zenye mahusiano mazuri, kupendana, kupeana faraja na
kusaidiana miongoni mwao.
Mwandishi wa makala haya anaunga mkono
msisitizo wa Waziri mwenye dhamana kuwa upo muhimu watu wakachagua marafiki
ambao wanaweza kuzungumza nao pindi wanapohitaji ushauri na faraja juu ya
matatizo yanayowakabili, ni vizuri kuwasaidia watu wenye Sonona wapate ushauri
wa kitaalam toka kwa watoa huduma za afya katika vituo vya huduma za Afya kwa
wakati.
Comments
Post a Comment