Featured Post

SERENGETI BOYS KUPAA KESHO MCHANA

Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kama Serengeti Boys, inatarajiwa kusafiri kesho saa 10.45 jioni kwa Ndege ya Shirika la Ndege la Emirates kwenda Morocco kupitia Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).


Timu hiyo yenye wachezaji 23 na viongozi wanane watakuwa Uwanja Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J.K. Nyerere kuanzia saa 7.00 mchana kwani wanatakiwa kuanza kuingia uwanjani saa 7.45 kwani saa tatu baadaye ndipo ndege itakapopaa.
Wanahabari wanaweza kupata mahojiano ya mwisho kadhalika kupata picha za habari wakati huo wa mchana kabla hawajaingia ndani kwenye ukaguzi wa taratibu za (check in logistics).
Kabla ya kusafiri, timu hiyo ilikuwa kambini hapa nyumbani tangu Januari 29, mwaka huu na baada ya kambi ya mwezi mmoja na nusu, ilicheza mechi tatu za kirafiki za kimataifa.
Machi 30, 2017 ilicheza Burundi ‘Intamba Murugamba’ na kushinda mabao 3-0 kabla ya kurudiana tena Aprili 1, mwaka huu na kushinda mabao 2-0. Mechi zote mbili zilifanyika Uwanja wa Kaitaba, ulioko Bukoba mkoani Kagera.
Mechi ya mwisho hapa nyumbani ilifanyika Aprili 3, mwaka huu dhidi Ghana ‘Black Starlets’ na kutoka sare ya 2-2 katika mchezo ulifanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Serengeti Boys ilitumia mchezo kama ishara ya kuwaaga mamilioni ya Watanzania kabla ya kusafiri kwenda kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana zitakazofanyika Gabon kuanzia Mei 14, mwaka huu.
Serengeti Boys itakuwa Rabat, Morocco kufanya kambi ya takribani mwezi mmoja kuanzia Aprili 5, mwaka huu. Ikiwa huko angalau itacheza mechi za kirafiki zisizopungua mbili dhidi ya wenyeji morocco na timu nyingine ya jirani ama Tunisia au Misri.
Kambi hiyo ya Morocco itamalizika Mei mosi, mwaka hu ambako timu itasafiri hadi Cameroon. Ikiwa Cameroon, timu itacheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa dhidi ya wenyeji yaani Mei 3 na 6, mwaka huu kabla ya kusafiri Mei 7, mwaka huu kwenda Gabon ambako Serengeti Boys imepangwa kundi B pamoja na timu za Mali, Niger na Angola.
Vipimo vya mechi dhidi ya Ghana kadhalika hapo baadaye Cameroon, vitakuwa mwafaka kwenye kufanya tathmini ya uwezo wa Serengeti Boys kwani wapinzani hao wamekuwa na rekodi nzuri kwenye soka la vijana na kwa kipindi hiki zimepangwa kundi A pamoja na wenyeweji Gabon na Guinea.
Kila la kheri Serengeti Boys katika mapambano ya kuwania ubingwa wa Afrika kadhalika kucheza fainali za Kombe la Dunia hapo Novemba, mwaka huu zitakazofanyika India. Serengeti Boys inaweza na Mtanzania tunakuomba kuichangia timu hii kwa namna ya 223344 kupitia mitandao yote ya simu.

Comments