Featured Post

RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG (29)




Nilitumia dakika kumi na tano bila mafanikio nikitembea kumtafuta Leila hapo Star Ferry bila kumuona, halafu kwa hisia za uchovu na mchanganyiko wa mawazo nikachukua teksi na kurudi hotelini kwangu.
Mhudumu mzee alikuwa amelala nyuma ya meza.
“Leila amerudi?” nikamuuliza.
Alifunua jicho koja, akanitazaa na kusema, “Sizungumzi Kiingereza.” Na jicho likafumba.

Nikaelekea chumbani kwangu. Mlango wa Leila ulikuwa umefungwa. Nilishika kitasa na kushangaa mlango ukifunguka na kuingia kizani. Nikapapasa na kubonyesha swichi na baada ya taa kuwaka nikaangalia chumba hicho kisafi kidogo: Leila hakuwemo.
Baada ya kukiacha chumba hicho huku taa ikiwaka, nikaingia chumbani kwangu, pia nikiwa nimeacha mlango wazi. Nikaketi kitandani, nikawasha sigara na kusubiri.
Nilisubiri kwa karibu saa moja. Na kwa sababu kulikuwa na nafasi kubwa, nikajilaza kitandani. Baada ya nusu saa, kutokana na joto, nikalala usingizi.
Niliinuka usingizi, nikihisi joto kali, uchovu na kukosa  utulivu. Jua la asubuhi liliangaza kupitia kwenye vioo vya dirisha. Niliinua kichwa changu na kutazama saa yangu ya mkononi. Ilikuwa saa mbili kasoro dakika ishirini asubuhi. Niliinuka na kuketi nikitazama kwenye ukumbi katika chumba tupu cha Leila. Hisia za hofu zikagonga kwenye uti wa mgongo. Nikapata hisia mbaya kwamba jambo baya litakuwa limempata. Hakunikimbia. Nilikuwa na uhakika na hilo. Alinyakuliwa ghafla tu na ninaweza kuhisi ni kwa nini. Inaonekana kuna mtu aliamua kufanya hivyo kwa sababu siyo tu alijua mengi lakini pia alikuwa akizungumza mno.
Nikaamua jambo la kufanya. Niliinuka kitandani, nikaufunga mlango wangu, nikanyoa ndevu na kuoga kwa kadiri nilivyoweza kulitumia beseni. Nikavaa shati safi, halafu nikijiona katika hali nzuri kuliko mfu, nikatoka ukumbini, nikafunga mlango na kwenda nje kushuka ngazi.
Kijana wa Kichina aliketi mapokezi: huenda ni mjukuu wa yule karani.
“Leila hakurudi chumbani kwake,” nikamwambia.
Aliitikia kwa fadhaa na kuinama kuonyesha heshima. Nina uhakika hakuelewa hata neno moja nililosema.
Nikashuka kwenye ngazi, nikampungia kijana wa mkokoteni asinifuate na badala yake nikaita teksi. Nikamwambia dereva anipeleke makao makuu ya polisi.
Nilikuwa na bahati. Inspekta Mkuu MacCarthy alikuwa anatoka nje kwenye gari lake wakati ninawasili. Akanipeleka kwenye mgahawa wa polisi ambako tulihudumiwa chai nzito kwenye vikombe vizito vyeupe.
Nikamweleza habari kamili.
Niliona hashtuki kabisa. Hii ilikuwa ndiyo mara yangu ya kwanza kufanya kazi na polisi wa Kiingereza. Hali yake ya kutulia na kutoonyesha mshtuko ilifanya mapigo yangu ya moyo yaongezeke.
“Lakini inawezekana kuna kitu kimemtokea,” nikamwambia, nikijitahidi nisiseme kwa nguvu. “Nina uhakika! Mara moja alikuwa name – muda mfupi baadaye anatoweka na hajarejea hotelini.”
Akachukua mtemba wake wa Dunhill na kuanza kuujaza tumbaku.
“Rafiki yangu kachero,” akasema, “huna haja ya kujishughulisha na hilo, nina uzoefu wa miaka kumi na tano kuwashughulikia hao wasichana. Leo wako hapa – kesho wameondoka. Pengine alimuona mtu mwingine mwenye fedha nyingi kuliko wewe. Ni mchezo unaofahamika wa hawa wasichana. Wanapata chochote wanachoweza kukipata kwako – halafu wanatoweka.”
Nilikunywa chai na kupambana na dhamira yangu ya kuyasaga meno.
“Hii ni tofauti. Tulikuwa tunarejea hotelini—oh, haijalishi! Pengine kuna mtu alihisi kwamba anazungumza sana. Ametekwa tu huyu.”
“Alikuwa anazungumza nini?”
“Ninajaribu kupambanua kesi ya mauaji,” nikamweleza. “Alikuwa ananipatia taarifa.”
MacCarthy alipuliza moshi aghali upande wangu. Alitabasamu kwa namna mtu anavyotabasamu wakati mwanaye wa kwanza anapokuwa amezungumza jambo jema. Nilihisi alinichukulia kama Mmarekani yeyote mkenyuzi.
“Taarifa gani ambazo anaweza kukupatia zikasaidia kesi ya mauaji yaliyotokea Amerika?” akauliza.
“Aliniambia kuhusu Herman Jefferson kukodi hekalu la kifahari huko Repulse Bay. Aliniambia alikuwa ameanza kutengeneza fedha nyingi miezi mitatu baada ya ndoa yake na kwa sababu alikuwa anatengeneza fedha nyingi akaamua kumtelekeza mkewe.”
Akatoa tabasamu angavu la Kiingereza ambalo limewahi kuwapumbaza hata Warusi.
“Rafiki yangu kachero, usisadiki chochote ambacho kahaba wa Kichina atakueleza – hupaswi kabisa kusadiki.”
“Yeah. Pengine niko rahisi. Unadhani alikuwa ananidanganya na amelala nje ya chumba chake kunifanya niwe na wakati mgumu usiku kucha?”
Akapuliza tena moshi upande wangu.
“Ni sehemu ya kazi ya kahaba kulala nje.”
“Unafahamu Wamarekani wowote wanaoishi huko Repulse Bay?”
“Ninaamini wako wachache.”
“Ulikuwa unafahamu kwamba Jefferson alikuwa na makazi huko?”
“Kama alikuwa nayo, ningejua tu, lakini hakuwa na makazi kule.”
“Kwahiyo alikuwa ananidanganya?”
Akatoa tabasamu la kidiplomasia.
“Kwa uhakika hayo ndiyo maelezo yake.”
Nikasimama. Nilijua napoteza muda wangu tu.
“Asante kwa chai. Tutaonana tena.”
“Daima ninafurahi kusaidia.”
Nikachukua teksi na kurejea hotelini. Mhudumu mzee alikuwa amechukua nafasi yake nyuma ya meza ya mapokezi. Aliinama kidogo aliponiona. Nilitamani kumuuliza maswali, lakini tatizo la lugha likawa kikwazo. Kama nilitaka kufika mahali, lazima nitafute mkalimani. Ni wakati huo nikamkumbuka mwongoza watalii anayezungumza Kiingereza, Wong Hop Ho, ambaye alikuwa amenipatia kadi yake uwanja wa ndege. Angeweza kunisaidia.
Itaendelea kesho…

Comments