Featured Post

RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG (27)




Baadaye, nikachoka kulala kitandani na kuamua kwenda mahali kupata chakula. Mara nilipofungua mlango, nikamuona Leila, akiwa ameuegemeza mwili wake kwenye kizingiti cha mlango. Alikuwa amebadili nguo na kuvaa Cheongsam ya rangi ya dhahabu. Alikuwa amefunga kiremba kwenye nywele zake.
“Hakukaa sana,” akauliza. “Kwanini umemleta hapa wakati mimi niko hapa?”
“Yalikuwa ni masuala ya biashara tu,” nikamwambia, nikifunga mlango kwa ufunguo. “Nilitaka kuzungumza naye.”

“Kuhusu nini?” akauliza kwa udadisi.
“Hili na lile.” Nikamtazama. Alikuwa anavutia sana. “Ungependa tukapate chakula cha jioni pamoja?”
Uso wake ukachanua kwa furaha.
“Hilo ni wazo zuri sana,” akasema. Akaingia kwenye chumba chake kidogo, akakwapua mkoba na kunifuata kwenye korido. “Nitakupeleka kwenye mgahawa mzuri sana. Nina njaa mno. Tutakula chakula kizuri sana, lakini hakina gharama kubwa.” Akatangulia kwenye korido na kkuziendea ngazi. Nikamfuata. Tukampita mhudumu wa mapokezi ambaye alikuwa anafanya mahesabu yaliyomchanganya akisaidiwa na kikokotozi. Vidole vyake vikongwe vilikuwa vinahangaika kubonyeza kwa kasi ya ajabu. Hakujisumbua kuinua uso kututazama wakati tunaondoka.
Nikamfuata Leila wakati tukikatisha barabara hadi mahali zilipoegeshwa teksi.
“Tutalazimika kuchukua teksi hadi Star Ferry,” akasema. “Mgahawa mzuri ambao tutakwenda kula uko ng’ambo.”
Tulichukua teksi na kuelekea Star Ferry, tukaingia kwenye boti. Wakati safari ikiendelea, aliniambia kuhusu filamu aliyoitazama mchana wa siku hiyo. Alisema huwa anakwenda kutazama sinema kila siku mchana. Wachina, alisema, walikuwa wanapenda sana sinema na kila wakati huenda kutazama. Kutokana na msururu niliouona nje ya majumba ya sinema niliamini kauli yake. Leila alisema huanza kupanga msururu kuanzia saa tano asubuhi ili wapate viti vya mbele.
Tulipofika ng’ambo, Leila akashauri tutembee hadi Nathan Road. Alisema zoezi la kutembea litaongeza hamu ya kula.
Haikuwa rahisi kutembea karibu karibu huku nikiongea naye. Wakati huo mitaa ilikuwa imejaa watu. Kutembea kwenye mitaa ya Kowloon kulikuwa ni uzoefu mwingine. Kila mahali kulikuwa na mabango yaliyong’ara kwa rangi mbalimbali. Herufi za Kichina, niliwaza, zilileta taswira nzuri kwenye mabango hayo. Yaliondoa uwezekano wa bango unaloweza kulisoma na kugeuka kuwa kama sanaa nzuri ya kuchora. Magari, mikokoteni na baiskeli zilikuwa zimejaa mitaani zikipishana. Eneo la pembeni la barabara lilikuwa limejaa watu wakipishana: kama siafu.
Hatimaye tukafika kwenye mgahawa wa mtaa wa pembeni ambao ulikuwa umejaa watoto wakicheza kwenye viambaza, wauzaji wa mboga mboga wakiwa wameweka makapu yao kutafuta wateja wa usiku, magari yaliyoegeshwa na mabango yaliyong’ara.
“Hapa ndipo tutapata mlo wetu,” Leila alisema, akasukuma mlango na kuingia ndani ya mgahawa ambao ulijaa kelele kiasi cha kushindwa kusikilizana.
Hatukuweza kuwaona hata watu waliokuwa wakipata chakula. Kila meza ilionekana kufichwa kwenye mapazia maalum. Sauti za terazo za Mah Jong, sauti za juu wa Kichina na kelele za vyombo zilikuwa zimepamba mgahawa huu.
Mmiliki wa mgahawa akafunua mapazia mawili, akainama na kutabasamu kwa Leila, na ghafla tukaondoka kwenye kelele na kuingia kwenye faragha.
Leila akaweka mkoba wake mezani, akaweka vizuri sidiria yake, akaweka makalio yake madogo vizuri kwenye kiti na kunionyesha meno yake mazuri meupe kwa tabasamu pana.
“Nitaagiza,” akasema. “Kwanza, tutakula vyakula vya kukaanga, halafu supu ya pezi la papa, kisha tutapata kuku — ndicho chakula maalum hapa. Halafu tutaangalia nini kkingine cha kula.”
Akazungumza haraka kwa Kicantonese kwa mhudumu na baada ya mhudumu kuondoka, akasogea na kuinama kwenye meza akiupapasa mkono wangu.
“Napenda wanaume wa Kimarekani.” akaniambia. “Wana umuhimu wa kipekee. Ni wazuri kitandani na wana fedha.”
“Usiamini katika yote unayoyasema,” nikamwambia. “Unaweza kushangaa. Umekuwepo muda gani hapa Hong Kong?”
“Nimekuja Canton miaka mitatu iliyopita. Mimi ni mkimbizi. Nilifanikiwa kutoroka kwa sababu binamu yangu anamiliki boti. Alinipeleka Macau na sasa niko hapa.”
Mhudumu akatuletea wine ya Kichina. Akamimina kwenye vikombe viwili. Ilikuwa kali na yenye nguvu. Alipoondoka, nikasema. “Pengine unamfahamu Jo-An Wing Cheung ambaye pia ni mkimbizi.”
Akaonyesha mshangao.
“Ndiyo. Ninamfahamu vizuri sana. Unamfahamu vipi wewe?”
“Simfahamu,” nikamwambia.
Kulikuwa na ukimya wa muda wakati mhudumu akiweka bakuli la chakula.
“Lakini unalijua jjina lake. Umejuaje jina lake lakini?” Leila akauliza, akichukua shrimp kwa vijiti na kuichovya kwenye mchuzi wa Soya.
“Alikuwa ameolewa kwa rafiki yangu mmoja ambaye alikuwa kiishi hapa mjini,” nikamwambia, nikidondosha shrimp mezani. Nikaiokota tena kwa vijiti na kwa uangalifu nikaiweka mdomoni. Ilionekana na ladha nzuri. “Uliwahi kukutana naye huyo mumewe? Jina lake ni Herman Jefferson.”
“Oh, ndiyo.” Leila alikuwa anakula kwa kasi ya ajabu. Robo tatu ya chakula hicho ilikuwa imepotea kabla mimi sijachukua ya tatu. “Jo-An na mimi tuliotoroka na kuja hapa Canton pamoja. Alibahatika kupata mume Mmarekani ingawa hivi sasa amekufa.”
Itaendelea kesho…

Comments