Featured Post

RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG (17)




Kama nilivyotarajia, uchunguzi ulifanyika bila mvuto wala vurugu zozote. Mtu mmoja mnene mwenye macho makubwa aliyejitambulisha kwa Afande Retnick kwamba ni mwanasheria wa Jefferson aliketi nyuma, lakini hakuchangia chochote katika maelezo wakati wa uchunguzi.
Janet West, akionekana mrembo na maridadi katika nguo nyeusi, alimweleza mchunguzi mambo mengi au machache ya aliyoniambia mimi. Retnick alitoa maelezo yake na mimi nikajieleza. Uchunguzi huo uliahirishwa ili kuwapa nafasi polisi waendelee kufanya upelelezi na mahojiano. Nilihisi kwamba hakuna aliyekuwa akijali kwamba mkimbizi wa Kichina alikuwa ameuawa.
Wakati mchunguzi alipoondoka mahakamani, nikamwendea Retnick ambaye alikuwa akichokonoa meno yake kwa njiti ya kiberiti.
“Ninaruhusiwa kuondoka sasa?” Nikamuuliza.
“Oh, kweli, ruksa,” alisema akiwa na mawazo mengi. “Hakuna kinachokuzuia.” Alimtazama kwa chati Janet West, ambaye alikuwa akizungumza na mwanasheria wa Jefferson. “Umegundua chochote kama alikuwa amelala wakati mwanamke wa manjano alipouawa?”
“Ninakuachia wewe ufanyie kazi.” Nikamweleza. “Ni wakati huu akiwa na mwanasheria. Nenda moja kwa moja ukamuulize.”
Akatabasamu, akitingisha kichwa.
“Mimi siyo mwendawazimu,” akasema. “Kuwa na wakati mzuri. Jihadhari na mabinti wa Kichina. Kwa nilivyosikia siyo tu wako tayari bali wanatafuta kwa nguvu.”
Akaondoka, akiwapa Janet West na mwanasheria nafasi kubwa. Nilizurura kidogo pale mpaka mwanasheria alipoondoka, na wakati Janet West alipokuwa akielekea mlangoni kutaka kuondoa, nikaungana naye.
“Ninaweza kuondoka kesho,” nilimwambia wakati aliposimama kunitazama kwa jicho la udadisi. “Kuna uwezekano wa kupata ndege?”
“Ndiyo, Bwana Ryan. Nitapata tiketi yako jioni ya leo. Kuna chochote cha ziada unachotaka?”
“Ninahitaji picha ya Herman Jefferson. Unaweza kunipatia?”
“Picha?” Akauliza kwa mshtuko.
“Inaweza kusaidia. Nitapata picha ya mkewe hata hapo mochwari. Picha mara nyingi husaidia unapokuwa katika kazi kama hizi.”
“Ndiyo: nitakupatia mojawapo.”
“Unaonaje kama tutakutana mimi na wewe mjini baadaye jioni? Itanipunguzia safari ya kuendesha hadi nyumbani kwako. Kuna mambo mengi ninapaswa kufanya kabla ya kuondoka. Unaonaje kama tukikutana Astor Baa majira ya saa mbili usiku?”
Alisita kidogo, halafu akakubali, “Sawa: basi saa mbili.”
“Asante sana: itanisaidia kwa kiasi kikubwa.”
Akaitikia tena kwa kutikisa kichwa, akatabasamu kidogo na kuondoka. Nilimtazama wakati akiingia kwenye gari la milango miwili aina ya Jaguar na kuondoka kwa kasi.
Usithubutu kumkaribia, tafadhali, nikajiambia mwenyewe. Kama anastahili kupata mamilioni ya Jefferson, atampata mtu mwingine anayevutia zaidi yako: na hiyo haitakuwa vigumu hata kidogo.
Niliendesha hadi ofisini kwangu na kutumia muda huo wa asubuhi kusafisha na kupanga baadhi ya mambo ambayo nilistahili kuyafanyia kazi. Kwa bahati nzuri, sikuwa na kazi yoyote niliyotakiwa kuifanyia upelelezi: haikuwepo ambayo isingeweza kusubiri japo kwa wiki kadhaa, lakini nikategemea kwamba sitakuwa safarini kwa muda mrefu.
Nilikuwa ninafikiria kushuka chini nikachukue walau sandwich wakati mlango ulipogongwa na Jay Wayde akaingia.
“Siwezi kukuchelewesha,” akasema. “Nilitaka kujua muda wa maziko ya Herman. Unafahamu? Ninadhani ninastahili kushudhuria.”
“Ni kesho,” nikamwambia, “lakini sijui ni muda gani.”
“Oh.” Akaonekana kufadhaika. “Sawa, pengine nitamuuliza Bi. West. Sidhani kama hawatapenda mimi nihudhurie?”
“Nitaonana na Bi. West leo jioni. Nitamuuliza kama unapenda.”
“Nadhani itakuwa vyema.” Akasema kwa furaha. “Ni jambo la kuchanganya kidogo kwangu mimi kuuliza. Nina maana sijamuona muda mrefu. Ilinitokea tu. . .” Akaiacha sentensi hiyo ielee.
“Hakika,” nikamwambia.
“Uchunguzi umekwendaje?”
“Kama nilivyotegemea: umeahirishwa.” Nikatulia kuwasha sigara. “Ninakwenda Hong Kong kesho.”
“Unakwenda?” Akaonyesha mshangao mkubwa. “Hiyo ni safari ndefu. Ni kuhusu suala hili hili?”
“Ndiyo. Mzee Jefferson ameniajiri nikachunguze rekodi za huyu mwanamke. Anagharamia: kwahiyo nakwenda.”
“Hivi ni kweli? Unajua huko ni miongoni mwa sehemu ninazopenda kutembelea. Ninakuonea wivu.”
“Najionea wivu mwenyewe.”
“Sawa, nitafurahi kusikia mambo utakayoyapata.” Akabadilisha mguu aliousimamia na kuukunja. “Unadhani utagundua chochote?”
“Sijui chochote. Ninaweza kujaribu.”
“Kwahiyo ulikutana na Mzee Jefferson. Umemuonaje?”
“Havutii sana. Haonyeshi kama ana muda mwingi wa kuishi.”
“Ninasikitika kusikia hivyo. Ni mzee sana.” Akatikisa kichwa chake. “Itakuwa alipata pigo wakati Herman alipoondoka.” Akaanza kuelekea mlangoni. “Sawa, nimekuja tu mara moja. Kuna mtu atakuja kuonana name. nakutakia safari njema. Kuna loote ninaloweza kufanya wakati ukiwa safarini?”
“Hakuna lolote, asante. Nitafunga tu na hiyo inatosha.”
“Sawa, basi tutaonana. Tutapata kinywaji pamoja utakaporejea. Nitapenda kujua umeishije na unaionaje hong Kong. Usisahau kuhusu maziko? Unaweza kuuliza kama mtu yeyote anaweza akaleta maua.”
“Nitakujulisha kesho.”
Baadaye mchana, nikaelekea makao makuu ya polisi na kuchukua picha ya Jo-An Jefferson ambayo Retnick aliniahidi. Ilikuwa picha nzuri. Kwa kuucha mwanga upige kwenye macho yake yaliyokufa, mpigapicha alikuwa amemfanya awe na mtazamo wa mtu aliye hai lakini amelala. Niliketi kwenye gari langu kwa dakika kadhaa, nikiichunguza picha. Alikuwa mrembo hasa. Nilimuuliza mhudumu wa mochwari namna mazishi yalivyokuwa yamepangwa. Akaniambia kwamba mwanamke huyo angezikwa kwa gharama za Jefferson kwenye makaburi ya Woodside keshokutwa. Hiyo ilimaanisha kwamba alikuwa anatengwa na makaburi ya familia. Makaburi ya Woodside hayakuwa kwa ajili ya watu matajiri, bali maskini wa Jiji la Pasadena.
Itaendelea kesho…

Comments