Featured Post

MKUTANO NA WANAHABARI KUHUSU SHINDANO LA HOJA JUU YA SIFA ZA RAIS BORA WA NCHI KAMA TANZANIA

TAREHE 1 APRILI, 2017 WASHINGTON
Ndugu Wanahabari na Watanzania wenzangu;
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii. Pia niwashukuru ninyi nyote mlioweza kufika hapa. Vilevile nawashukuru wote walioanza kuunga mkono harakati hizi na hatimae tumeweza kufikia hatua hii ya kuwepo kwa mkutano huu muhimu sana katika mstakabali wa taifa letu.
Ndugu Wanahabari na Watanzania wenzangu;
Tumekutana hapa kwa nia ya kukumbushana sisi kwa sisi, wapi hapajakaa sawa na ni vipi tutaweza kurekebisha kwa haraka, ili taifa letu liwe katika hali ya kuridhisha na kuheshimika.
Katika kutimiza nia hii ya kukumbushana, imeonekana ni muhimu tutumie njia ya kuweka Shindano la Hoja juu ya “jambo mtambuka” ambalo likisimamiwa na kuenziwa inavyostahili, tutaweza kuondokana na hali ya sintofahamu inayolikumba taifa letu sasa. Shindano hili litajenga hoja juu ya Sifa za Rais Bora wa Nchi kama Tanzania.
Shindano hili ni mwendelezo wa Kampeni ya Kuinua Maadili Kitaifa ambayo ilizinduliwa tarehe 14 Januari 2017 na kilele chake ni tarehe 10 Disemba, 2017. Taarifa zaidi ya Kampeni hii inapatikana: www.maadilkitaifa.blogspot.com
Lengo Kuu la Shindano hili la Hoja:
Ndugu Wanahabari na Watanzania Wenzangu;
Lengo kuu la shindano hili la hoja ni kulinda na kudumisha uhuru na umoja wa Taifa, ambavyo ndio ngao yetu.
Katika kutimiza lengo kuu hilo shindano hili litasaidia mambo yafuatayo:
i) litadhibiti kauli zenye kushusha hadhi ya kiti cha Urais
ii) litasaidia vyama vyetu vya siasa kupata muongozo wa sifa za wagombea Urais zenye kulenga maslahi ya taifa na sio ya chama
iii) litaiongezea nguvu katiba yetu katika suala la sifa za mgombea Urais
iv) litawasaidia wale wote wenye ndoto za kuwania nafasi ya kiti cha Urais siku za mbeleni, waweze kujipima kabla hawajatangaza nia zao na kabla hawajaingia kwenye mchakato wa kupimwa na vyama vyao, ili taifa liwe na chaguzi zenye wagombea wenye hadhi ya uongozi unaoenzi ngao ya taifa
v) litajenga umoja wa kitaifa katika masuala yote ya kuliimarisha na kuliendeleza taifa letu
Washindanaji: Wasimamizi/Viongozi wa Vyombo vya Habari vyote Tanzania
Muda wa Shindano: 3 Aprili - 3 Mei, 2017 (Siku ya Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani)
Maelezo ya Msingi juu ya Shindano hili:
Ndugu Wanahabari na Watanzania wenzangu;
Katika mstakabali wa Taifa lolote duniani, suala la wadhifa wa Urais wa nchi ni muhimu sana kuliangalia kwa jicho la tatu kwani Rais wa nchi ni taswira ya taifa analoliongoza. Maana yake, hadhi ya Rais wa nchi, inawakilisha hadhi ya watu wake. Inapotokea mtu yeyote wa ndani au nje ya nchi kumdhalilisha au kumbeza Rais wa nchi kwa namna yeyote ile, mtu huyo anakuwa amedhalilisha na kubeza taifa zima.
Katika nyakati hizi, tumekuwa tukisikia kauli zenye utata zinazoligawa, kulidhalilisha na kulidhoofisha taifa letu.
Kwa mfano utasikia; Rais aliyepo madarakani ni wa kundi fulani (wa chama fulani; au Rais wa wanyonge; masikini; au wa dini fulani). Kauli kama hizi kwa hakika zinashusha hadhi na pia zinadharilisha, kubeza na kudhoofisha nafasi ya kiti cha urais.
Vile vile utasikia watu wanatumia lugha zisizo na staha kudhalilisha, kubeza na kudhoofisha nafasi ya kiti cha Urais. Hii yote imetokana na kutokuwa na muongozo wa kitaifa katika kubainisha wadhifa wa kiti cha urais wa nchi.
Ndugu Wanahabari na Watanzania wenzangu;
Taifa linaundwa na watu wa aina zote (Wanyonge, wenye nguvu za kifedha, kifikra, kitaaluma, masikini, matajiri, wabaya, wazuri, wenye Imani tofauti na watanzania wa aina zote).
Jukumu la msingi katika nafasi ya Urais wa nchi yoyote ile ni kuinua na kuboresha ubora wa taifa, na sio kuibua na kuthibitisha ubaya wake. Mfano; Rais anapoona baadhi ya watu wake hawako vizuri, hapaswi kuwathibitishia mabaya yao, bali anatakiwa atumie mkakati wa kiuongozi kuhakikisha watu wake wanakuwa sawa; na hivyo kutunza hadhi na heshima ya taifa zima. Ule msemo wa “Samaki mmoja akioza ni wote” hujidhihirisha sana katika hadhi na heshima ya taifa.
Daima tuwe makini sana katika kauli zinazodhalilisha, kubeza na kudhoofisha hadhi ya kiti cha urais kwani tusipokuwa makini tutaondoa heshima ya taifa letu ambayo ni heshima yetu wenyewe. Daima tukumbuke maana ya taifa ni watu. Na watu wenyewe ndio mimi, wewe na watanzania wote. Tuwe makini, tusikubali kujidhalilisha, kujitukana wala kujidhoofisha kwa namna yoyote ile kupitia kwa kiti cha urais.
Tumesikitika sana, tumesononeka sana, na tumeumiza sana mioyo yetu, hatuwezi kuendelea kuvumilia, lazima tuchukue hatua madhubuti za kudhibiti hali hii ili tustiri utu wetu na hatimae kwa furaha tulionee fahari taifa letu Tanzania.
Wapi Hapajakaa Sawa?
Ndugu Wanahabari na Watanzania wenzangu,
Uchunguzi nilioufanya kupitia tasnia ya Maendeleo ya Watu unaonyesha kuwa, kauli za kushusha hadhi ya kiti cha Urais zimetokana na vigezo vinavyotumika kupata wagombea wa nafasi ya urais hapa nchini Tanzania. Imeonekana kwamba vyama vya siasa vinatumia vigezo vya kichama kutafuta mgombea urais , vigezo ambavyo havikidhi maslahi ya taifa. Kwa kuwa hali ya kudhihakiwa na kufedheheshwa kwa taifa inashusha kasi ya maendeleo nchini, ni jambo la busara taifa likachukua hatua za haraka kuondokana na hali hii ili tuweze kuwa na kasi katika kutafuta maendeleo.
Kwa kuwa tupo katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia, ulimwengu wa digitali, ni lazima mfumo wetu wa maendeleo ufuate kasi ya sasa. Kwa minajili hiyo imetulazimu tutafute mbinu yenye nguvu ya haraka ya kuondoa kabisa hali hii, ambayo siyo mbinu nyingine bali ni: Shindano la Hoja juu ya Sifa za Rais Bora wa Nchi.
Ni vipi tutaweza kuparekebisha kwa haraka?
Ndugu Wanahabari na Watanzania wenzangu,
Katika kufikia malengo ya kuendesha shindano hili ilibidi tubuni njia ya uhakika na itakayokuwa na ufanisi mkubwa. Ndio maana tukaamua kuchagua viongozi/wasimamizi wa vyombo vya habari wawe washindanaji katika shindano hili la kihistoria. Nia ya kuwashindanisha hawa ni kwa sababu:
i) Wanauwezo wa kusambaza ujumbe kwa haraka nchi nzima
ii) Wanarasirimali watu yenye uwezo mkubwa wa kuchambua na kupanga hoja vizuri
iii) Wana mbinu za kukusanya hoja kwa namna nyingi kuliko viongozi/wasimamizi wa tasnia zingine
iv) Tutakapo hitimisha shindano hili na kupata vigezo vya sifa za mtu anayefaa kuwa rais bora, washindanaji hawa wanauwezo wa kufikisha taarifa kwa jamii nzima na hasa wanasiasa wanaotuletea wagombea urais na wale wote wenye ndoto za kuwainia nafasi ya kiti cha urais siku za usoni.
v) Wanauwezo mkubwa wa kuitengeneza jamii kimtazamo na hivyo watasaidia sana kufanya chaguzi za nafasi ya kiti cha Urais kuwa za ushabiki wa kitaifa Zaidi na sio wa kichama.
Vigezo vya kupata washindi:
Kwa kuwa suala la sifa za Rais bora ni kwa ajili ya kulinda na kutunza hadhi ya Taifa letu tunasisitiza washindanaji wote watumie mbinu mbalimbali kuwashirikisha watanzania wote katika kuchangia hoja za sifa za rais bora.
Katika mchujo wa kutafuta mshindi wa kwanza hadi wa kumi (1-10) vigezo vifuatavyo vitazingatiwa:
1. Hoja zenye mantiki zinazoelezea vigezo/sifa za rais bora
2. Mbinu zilizotumika kuwashirikisha wadau wengine katika kukusanya hoja
3. Idadi ya watanzania walioshiriki kuchangia hoja kwenye chombo cha habari husika (takwimu zitahitajika ziainishwe) – tunahitaji Watanzania wa fani zote washiriki katika utoaji wa sifa za rais wanaemtaka.
Zawadi:
Zawadi za washindi zitakuwa kama zifuatazo:
A: Washindanaji wote watapata Cheti cha Ushiriki wa Shindano. Kwa washiriki wote wa shindano waliotoa hoja zao kwa kupitia vyombo vya habari wa washindanaji wanaowaunga mkono watapata:
Nakala za kitabu cha Kampeni ya Kuinua Maadili Kitaifa 2017 (Kinaitwa: Chombo Mhuhimu kwa Maendeleo Yako) zitakabidhiwa kwa washindanaji (Tunaomba wadau Zaidi wajitokeze kufadhili uchapishwaji wa nakala zaidi) kupitia email yetu: maadilikitaifa2017@gmail.com.
B: Mshindi wa kwanza hadi wa kumi (1- 10) waliokidhi vigezo vya shindano hili watapata zawadi zilizotajwa kwenye A pamoja na pesa kwa viwango vifuatavyo:
1. 10m
2. 9m
3. 8m
4. 7m
5. 6m
6. 5m
7. 4m
8. 3m
9. 2m
10. 1m
(Pesa hizi tayari zimepatikana).
Zawadi zote zitatolewa siku ya kilele cha Kampeni ya Kuinua Maadili Kitaifa tarehe 10 Disemba, 2017 ambapo washiriki wote waliochangia hoja kwa kupitia ofisi za vyombo vya habari watapewa nakala ya kitabu cha kampeni ya kuinua maadili kitaifa.
Kwa heshima na taadhima Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) Dr. Reginald Mengi amependekezwa kuwa mgeni rasmi siku ya utoaji zawadi hizo. Hivyo nachukua fursa hii kumtaarifu rasmi Dr. Reginald Mengi ili aweke siku hiyo katika ratiba yake. Na tunamuomba atutumie email ya kukubali pendekezo letu hili kupitia: maadilikitaifa2017@gmail.com
Maelezo juu ya Kampeni ya Kuinua Maadili Kitaifa pamoja na maelezo kuhusu kitabu yanapatikana: www.maadilikitaifa.blogspot.com
Wito kwa Watanzania:
Ndugu Wanahabari na watanzania wenzangu;
Shindano hili ni la kihistoria na linamhusu kila mtanzania.
Nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza watanzania walio hapa Marekani kwa kukubali kuunga mkono shindano hili. Wamefanya jambo muhimu sana katika kutunza heshima na hadhi ya taifa letu zuri la Tanzania.
Kwa ajili ya mstakabali wa taifa letu tunaomba sana vyombo vyote vya habari vishiriki kwa dhati shindano hili ili tuwafikie makundi yote ya watanzania nchi nzima.
Pia nichukue fursa hii kuwaomba watu mbalimbali wajitokeze kuwezesha (kifedha au kihuduma) shindano hili ili tufanikiwe. Katika kufanikisha Shindano hili tunahitaji kukamilisha mambo yafuatayo:
1. Fedha taslimu TSh. 55 milioni pamoja na vyeti kwa ajili ya washindanaji – tayari wadau wamejitokeza kukamilisha
2. Watoa hoja nchi nzima – Tunategemea washindanaji walisimamie
3. Uchambuzi na uchujaji wa hoja – Tunategemea washindanaji walishughulikie na kututumia hoja za msingi
4. Nakala za kitabu kinachoambatana na shindano (zinahitajika nakala za kusambaza kwa wapiga kura nchi nzima ili tuwajenge kifikra kama msingi wa umadhubuti wa taifa letu) – Tunaomba wadau waliohamasika na shindano hili wasaidie gharama za uchapishaji pia wanaweza kulipia moja kwa moja kwa mchapishaji. Tunaomba tuwasiliane nasi kupitia email: maadilikitaifa2017@gmail.com

Comments