Featured Post

MFUMO WA STAKABADHI GHALANI MKOMBOZI KWA WAKULIMA

Na Jovina  Bujulu- MAELEZO
Kuwepo na mfumo wa stakabadhi ghalani kumekuwa ni mkombozi pekee kwa  wakulima wadogo na wa kati  kwa kuwawezesha kupata bei nzuri ya mazao yao, ukilinganisha na bei zilizokuwa zinatolewa na wafanyabiashara wanaponunua mazao yakiwa shambani kwa kutumia vipimo ambavyo sio sahihi.

Taarifa iliyotolewa na bodi ya usimamizi wa Stakabadhi za Ghala  imesema kuwa kabla ya mfumo huo kuanza wakulima walikuwa wakipunjwa bei ya mazao  na wafanyabiashara na kutolea mfano zao la korosho ambapo katika msimu wa 2015/2016, kilo moja ya korosho ilinunuliwa kwa shilingi 2900 na msimu wa 2016/2017 bei ilipanda na kufikia shilingi 4,000 kwa kilo ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 15.9
Mfumo huo umewanufaisha wakulima kwa kutumia ghala ambazo ziliachwa kwa muda mrefu bila matumizi ambazo zimekuwa na tija kwa wakulima.
Kupitia ghala hizo zenye ujazo wa kuanzia tani 200 hadi 5000 na kuendelea wameweza kuhifadhi mazao yao vizuri  na kwa ubora unaotakiwa kwa matumizi ya sasa nay a baadaye.
Aidha, mfumo huo umeongeza ajira kwa wakina mama na vijana hasa katika maeneo ya kuchambua, kupokea na kupanga mazao ghalani. Vijana wengi wameajiriwa kwa kazi ya kushusha, kupanga na kupakia mazao na wameweza kujiajiri katika kilimo baada ya kuona mfumo huo unavyofanya kazi vizuri  na kuwa na uhakika wa soko la mazao yao.
Wakulima pia wamepata  mafanikio  kwa kuwa na uhakika wa vipimo vya mazao yao yanayohifadhiwa ghalani  kupimwa kwa kilogramu  na si vinginevyo ambapo kabla ya mfumo huo wakulima walikuwa wakiibiwa mazao yao kutokana na  matumizi ya vipimo ambavyo si sahihi.
Kwa kuhifadhi mazao yao katika ghala zenye leseni, wakulima wamekuwa wanatumia mazao hayo kama dhamana ya kupata mikopo kutoka katika taasisi mbalimbali za fedha. Hii imewezekana kutokana na wakulima hao kujiunga katika umoja kupitia vikundi au vyama vya ushirika .
Wafanyabiashara pia wameneemeka na mfumo huu, ambapo kwa sasa wameweza kupunguza gharama za kufuata mazao maeneo mbalimbali mazao yanapatikana kwa wingi badala yake mazao hayo wanayapata katika eneo moja kkwenye ghala zilizosajiliwa na hivyo kuondoa hatari ya kuibiwa pesa zao na madalali wasio waaminifu.
Mfumo huo pia umekuwa  na faida kwa bodi za mazao katika kuandaa bajeti za mahitaji ya pembejeo  na kuongeza ili kuboresha na kuongeza uzalishaji.
Aidha, mfumo huo umechochea na kuharakisha uanzishwaji wa soko la bidhaa nchini, kutokana na kuwepo kwa bidhaa zenye ubora na zinazopatikana kwa wakati. Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi  za Ghala, inatoa wito kwa wakulima  kuunga mkono uhamasishaji wa matumizi ya soko hilo ili kuongeza tija na kasi ya  kukuza biashara ya mazao ya kilimo hapa nchini.
Mfuko wa Stakabadhi Ghalani ulianza mwaka 2000 ukifadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Bidhaa. Lengo la mfuko huo ni kuwezesha wakulima kufaidika na ongezeko la bei katika msimu wa mazao, kuongeza mapato ya wakulima na kuboresha kipato chao ikiwa ni pamoja na kuwapa wakulima nguvu ya soko kwa kuhamasisha  utumiaji  wa vikundi vya wakulima na ushirika.


Comments