Featured Post

MAKAMU WA RAIS MHE. SAMIA ATOA TUZO ZA RAIS KWA WAZALISHAJI BORA WA VIWANDA 2016

  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa hafla ya utoaji waTuzo za Rais za Mzalishaji Bora wa Viwanda kwa mwaka 2016 zilizofanyika kwenye Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi mshindi wa jumla Tuzo za Rais za Mzalishaji Bora wa Viwanda kwa mwaka 2016 Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TBL, Bw. Devis Deogratius (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja  na washindi wa  Tuzo za Rais za Wazalishaji Bora wa Viwanda kwa mwaka 2016.
                                 ............................................................................... 
 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  amelitaka Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) kuongeza kasi katika uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa zenye ubora nchini ili tufike tunakotaka yaani uchumi wa viwanda ifikapo 2025.
 
Akizungumza katika hafla ya Tuzo ya Rais ya Mzalishaji bora kwa mwaka 2016, Makamu wa Rais alisema kwamba Serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta binafsi katika kukuza uchumi na kwamba mambo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa mengi yanatafutiwa ufumbuzi.
Alisema mwaka wa kwanza wa Serikali ulikuwa ni wa kazi nyingi na hivyo serikali ilikuwa ikitafuta fedha na kwamba sasa wametulia na wataleta nafuu kwa mujibu wa sheria na matakwa ya sasa ya kukuza uchumi.
 
Alisema Serikali ipo tayari kufanyakazi na wenye viwanda kwa sababu inaamini mchango mkubwa wa sekta binafsi katika kuondoa umaskini, kukuza ajira na kuimarisha mwelekeo kwenda katika uchumi wa kati.
Makamu wa Rais ambaye  hotuba yake ilizungumzia mafanikio na changamoto zinazokumba sekta binafsi katika kutekeleza wajibu wake, amesema kwamba serikali ya awamu ya tano inatambua changamoto hizo na imechukua hatua kadhaa kuhakikisha kwamba zinamalizwa.
Hatua hizo ni pamoja na  ujenzi wa miundombinu kama bandari na reli na pia kuwapo kwa kamati inayoangalia kero zinazosumbua sekta ili serikali ifanye maamuzi.
 
Kwa sasa kuna Kamati inayoangalia namna bora ya kuboresha mazingira ya biashara inayofanyakazi  chini ya Wizara ya Viwanda , Bisahara na uwekezaji na inakaribia kumaliza kazi yake na kuikabidhi Serikalini.

Comments