Featured Post

'JAMII IKIUNGE MKONO KITUO CHA YATIMA CHA MALAIKA'

 Meneja Uhusiano wa Umma wa Jumia Travel nchini Tanzania, Geofrey Kijanga, akizungumza na waandishi wa habari  Dar es Salaam leo wakati wafanyakazi wa kampuni hiyo walipokitembelea Kituo cha kulelea watoto wanaoshi katika mazingira magumu cha Malaika Kids Tanzania  na kutoa msaada wa vyakula na vitu mbalimbali kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka. Kituo hicho kipo Kinondoni jijini Dar es Salaam.

 Mwanzilishi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kituo cha Malaika Kids Reception, Najma Manji akizungumza na wanahabari kuhusu kituo hicho.
 Meneja Uhusiano wa Umma wa Jumia Travel nchini Tanzania, Geofrey Kijanga (kulia), akimkabidhi Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kituo hicho msaada huo.
 Meneja Uhusiano wa Umma wa Jumia Travel nchini Tanzania, Geofrey Kijanga (kulia) akimkabidhi katoni ya sabuni Leila Mustafa anayelelewa katika kituo hicho
 Ofisa kutoka Jumia Travel, Patricia Muthama, akimkabidhi msaada huo, Amina Rodvick anayelelewa kwenye kituo hicho.
Ofisa wa Jumia Travel,  Mustafa Ali (kulia), akimkabidhi 
msaada huo mtoto, Najma Mohamed
 Muonekano wa vitanda vinavyotumiwa na watoto wa kituo hicho.
Kituo hicho kinavyoonekana kwa nje.

Na Dotto Mwaibale

JAMII imetakiwa kuunga mkono jitihada za kituo cha kulelea watoto wanaoshi katika mazingira magumu cha Malaika Kids Tanzania kinachopokea watoto, kuwalea, kuwasomesha na kuwatafutia kazi ili kuweza kujitegemea.

Hayo yamesemwa na Meneja Uhusiano wa Umma wa Jumia Travel nchini Tanzania, Geofrey Kijanga Dar es Salaam leo wakati wafanyakazi wa kampuni hiyo walipokitembelea na kutoa msaada wa vyakula na vitu mbalimbali kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka.

“Kwanza kabisa ningependa kuchukua fursa hii kuupongeza uongozi wa kituo cha Malaika Kids Reception kwa jitihada wanazozifanya. Kuanzisha kituo cha kuwapa hifadhi watoto ambao wanakosa malezi aidha kutokuwa na wazazi, ndugu au kutelekezwa mitaani kuna changamoto nyingi. Lakini changamoto hizo zinawezekana endapo tu jamii itaungana kwa pamoja kwa kutoa msaada wa hali na mali, uwe mdogo au mkubwa ili kuvipa uwezo vituo hivi,” alisema Kijanga.

“Kuna usemi unaosema mcheza kwao hutunzwa, nasi kama Jumia Travel Tanzania tukiwa tunafanyia shughuli zetu eneo hili tumeonelea ni vema kwa kuanza kusaidia jamii inayotuzunguka kabla ya kwenda mbali zaidi. Tunaunga mkono juhudi zinazofanywa na kituo hiki kwani hawa watoto wanaolelewa hapa nao wanatamani wangekuwa wanaishi na familia zao. Kwa kufanya hivi tunaamini kuwa tutakuwa tunaikumbusha jamii ya watanzania kuwa tatizo la watoto yatima au wa mitaani lipo na linahitaji nguvu za ziada katika kupamba nalo,” aliongezea Meneja huyo wa Uhusiano wa Umma kampuni inayojihusisha na huduma za hoteli kwa njia ya mtandao.

“Ningependa kutoa wito kwa kampuni nyingine, serikali, watu binafsi na jamii kwa ujumla kukitupia macho kituo hiki na kuunga mkono jitihada wanazozifanya. Nilifanya mazungumzo na Mkuu wa kituo hiki na amenieleza kuwa mbali na kuwalea watoto lakini pia wanawasomesha pamoja na kuwatafutia ajira ili waweze kuanza maisha yao ya kujitegemea. Hivyo ili kukipunguzia mzigo kituo hiki, jamii inaweza kusaidia kusomesha baadhi ya watoto au kuwatafutia kazi wale wanaomaliza masomo yao,” alisema Kijanga.

Mwanzilishi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kituo cha Malaika Kids Reception, Najma Manji amesema kuwa inatia moyo kuona jamii inayozunguka inatambua uwepo wao na kujitokeza kuwasaidia.

“Kwanza kabisa ni jambo la kumshukuru Mungu kuona kwamba jamii inayotuzunguka inatambua jitihada tunazozifanya katika kuwalea watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Hatua ya kuanzisha kituo hiki sikuifanya kana kwamba ninao uwezo mkubwa, la hasha, bali ni kwa kuguswa tu na magumu wanayoyapitia watoto hawa wanaokosa msaada. Na huwa najaribu kuvuta picha kama endapo wangekuwa ni watoto wangu,” alisema Manji.

Akielezea kwa ufupi shughuli wanazozifanya kituoni hapo pamoja na changamoto wanazokumbana nazo mwanzilishi wa kituo hiko alisema kuwa, “Mpaka hivi sasa tunao watoto takribani 80, sina idadi kamili ya wanawake ni wangapi na wanaume ni wangapi lakini wanaume ni wengi kidogo kuliko wanawake. Tunawapokea watoto kuanzia miako 0 mpaka 7 kutoka ustawi wa jamii, hatupendelei watoto wanaozidi umri huo kwani inakuwa ni vigumu kuwabadili tabia zao.”

“Mbali na malezi lakini pia tunawasomesha pamoja na kuwatafutia kazi ili waweze kujitegemea. Kwa mfano, hivi sasa tunao wawili ambao wamekwisha maliza masomo yao katika masuala ya hoteli lakini bado hawajapata kazi. Na tayari kuna wengine ambao walishalelewa hapa na kusomeshwa wapo makazini wakijetegemea na maisha yao. Ningependa kutoa wito kwa watanzania wenzangu kuja kutusaidia kwa chochote walichonacho iwe ni vyakula, nguo, vifaa vya shule, kusaidia kulipa ada na hata kuwatafutia au kuwapa kazi wale wanaohitimu masomo yao ili nao waweze kujitegemea na kuendelea na maisha yao,” alisema Manji.

Msaada wa vyakula uliotolewa na wafanyakazi wa kampuni hiyo walipotembelea kwenye kituo hiko ni pamoja na unga, mchele, maharage, mafuta ya kupikia, sukari, chumvi, sabuni na mengineyo. Dhumuni kubwa la kufanya hivyo ni kuwafanya watoto hao nao kufurahia sikukuu ya Pasaka itakayosherehekewa siku ya Jumapili na Jumatatu duniani kote.

Comments