Featured Post

DKT. NCHIMBI AMUUNGA MKONO RAISI KWA KUPIGA MARUFUKU MCHANGA WA DHAHABU YA SINGIDA KUSAFIRISHWA NJE YA NCHI

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza katika baraza la biashara la mkoa kwenye ukumbi wa ofisi yake. Wa kwanza kulia ni mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Singida Kitila Mkumbo na kushoto ni katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Anjelina Lutambi.

Baadhi ya wajumbe wa kikao cha baraza la biashara la mkoa wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa kwenye kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ofisi ya mkuu wa mkoa.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu akisisitiza jambo wakati akichangia mada kwenye kikao cha baraza la biashara la Mkoa wa Singida.
Mfanyabiashara Mkoani Singida Mzee Aklan akichangia mada kwenye kikao cha baraza la biashara la Mkoa wa Singida. 

Mkuu wa Mkoa wa Singida amefuata nyayo za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe John Pombe Magufuli kwa kuzuia mchanga wa dhahabu unaopatikana mkoani hapa kutosafirishwa nje ya nchi kwa kitendo chake cha kuzuia mchanga wa dhahabu kutoka nje ya mkoa.

Akizungumza katika kikao cha baraza la biashara la Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amesema wadau kutoka sekta binafsi na  ya umma waliohudhuria kikao hicho wamekubaliana kwa kauli moja kupiga marufuku mchanga wenye dhahabu kusafirishwa nje ya mkoa kwa ajili ya uchenjuaji.

Dkt. Nchimbi amesema ili kuendana na kasi ya Mhe rais ya kuwaletea maendeleo watanzania wanyonge, mchanga huo wa dhahabu uchenjuliwe hapa hapa mkoani Singida ili malipo ya mrabaha yaongezeke na kukuza pato na uchumi wa mkoa.

Mmoja wa wadau wa sekta binafsi Angasen Nkya amesema kuwa kwa muda mrefu baadhi ya wachimbaji madini wamekuwa wakisafirisha mchanga wenye madini nje ya mkoa, badala ya kuuchenjua hapa mkoani.

“Mchanga wenye madini kutoka machimbo mbalimbali mkoani hapa yakiwemo ya kijiji cha Mahintiri wilaya ya Ikungi umekuwa ukisafirishwa kupelekwa mikoa mingine ukiwemo mkoa wa Mwanza. Kitendo hichi kinapunguza kwa kiasi kikubwa mapato ya halmashauri na serikali ya mkoa, yatokanayo na tozo la mrabaha”,amefafanua Nkya.

Aidha Dkt. Rehema Nchimbi amewaagiza wakuu wa wilaya na wakuu wa vituo vya polisi vya wilaya zote mkoani hapa kuhakikisha mchanga wenye madini hautoki nje ya mkoa na mchimbaji atakayekiuka agizo hilo achukuliwe hatua stahiki.

Naye Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu amesema utaratibu uliopo wa leseni za uchimbaji madini kutolewa na wizara bila kushirikisha mamlaka za wilaya unawanyima uhuru wa kusimamia shughuli za uchimbaji madini katika maeneo yao kwa ufanisi.

“Wizara ya nishati na madini inachofanya ni kuipa ofisi ya mkuu wa wilaya nakala ya barua ikielekeza kampuni fulani imepewa leseni ya kuchimba madini kwenye eneo la wilaya yake. Migogoro ikizuka ndipo mkuu wa wilaya anapoonekana ana umuhimu katika shughuli za uchimbaji madini", amesema Mtaturu.

Ameongeza kuwa ni jambo njema endapo wizara ya nishati na madini ikashirikisha uongozi wa wilaya kuanzia shughuli za utafiti  na uchimbaji madini mapema kabisa ili kurahisisha ufuatiliaji na kuzuia uwezekano wa ktuokea migogoro au uvamizi wa maeneo ya shughuli za madini.

Awali Dkt. Nchimbi amesema baraza la biashara la mkoa sio sehemu ya kupeleka malalamiko na kuikosoa serikli tu bila ya kuwa na mbinu mbadala za kushauri na kutoa maoendekezo yenye lengo la kukuza sekta ya bishara kwa mkoa wa Singida.

Ameongeza kuwa baraza hilo liimarishwe zaidi ili liweze kutengeza umoja kati ya sekta ya umma na binafsi huku kamati mbalimbali zikipendekezwa kuundwa ili zitatue kero na kubuni mbinu za kuboresha biashara Mkoani Singida.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amewataarifu wafanyabiashara na wananchi wote wa Mkoa wa Singida kuwa bomba kubwa la mafuta kutoka Nchini Uganda hadi bandari ya Tanga litapitia katika baadhi ya vijiji vya wilaya ya Iramba, Singida na Ikungi.

Dkt. Nchimbi amesema kila mahali bomba hilo litakapopita viongozi na wananchi kwa ujumla watoe ushirikiano wa karibu ili kufanikisha ujenzi huo na pia kuzitumia fursa zilizopo kwa uaminifu, uadilifu na ubunifu mkubwa.

Comments