Featured Post

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUANDIKA HABARI ZA MAENDELEO


Na Immaculate Makilika- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaasa waandishi wa habari nchini kuandika habari zinazohamasisha maendeleo ya nchi badala ya kuandika habari ambazo hazina manufaa kwa taifa.

Akizungumza wakati ya hafla ya kuwaapisha mawaziri, mabalozi pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu jijini Dar es Salaam leo, Rais Magufuli alisema kuwa waandishi wa habari wanatakiwa kuwa wazalendo kwa kuandika habari za kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo pamoja na kuunga mkono jitihada mbalimbali za Serikali.
“Nchi yetu ina sifa nzuri nje, Rais wa Benki ya Dunia alipotembelea katika nchi yetu hivi karibuni alitupatia  jumla ya shilingi trilioni 1.74 na benki hiyo ipo mbioni  kutupatia fedha nyingine shilingi trilioni 2.8, lakini vyombo vyetu vya habari haviandiki kwa mapani juu ya taarifa ” alisema Rais Magufuli.
Alibainisha kuwa fedha hizo zitatumika katika miradi ya Ujenzi wa barabara za juu eneo la Ubungo, maboresho ya miji, pamoja na Vyuo Vikuu vya  Sokoine na Mandela  na kuleta maendeleo ya nchi yetu lakini taarifa zake hazikupewa uzito unaostahiki katika vyombo vya habari.
Rais Magufuli aliwataka wamiliki wa vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari kufuata uweledi wa taaluma ya habari pamoja na kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi ya mtu mmoja mmoja.
Aidha, Rais Magufuli amewapongeza viongozi aliowaapisha  na kuwataka kufanyakazi kwa bidii na juhudi ili kutimiza azma ya serikali ya kuwa nchi ya uchumi wa kati kwa kutekeleza agenda ya viwanda.
Viongozi walioapishwa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Katiba na Sheria Prof.  Palamagamba Kabudi na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Alfayo Kidata.
Wengine ni Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dkt. Abdallah Possi, Balozi wa Tanzania nchini Israel, Job Masima, Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Sylvester Mabumba, pamoja na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Stellah Mugasha.

Comments