Featured Post

UNAIKUMBUKA HII? MISUKULE YAMUUMBUA GWAJIMA!



‘MISUKULE’ ama kuwarudisha kwa ‘kuwafufua’ watu waliokufa ndicho kitu kilichomjengea umaarufu mkubwa Mchungaji, Askofu Josephat Gwajima, wa Kanisa la Ufufuo na Uzima.
Tangu alipoanzisha kanisa hilo ambalo awali lilikuwa Ubungo kabla ya kuhamishiwa Kawe jijini Dar es Salaam, watu wengi walifurika kwa sababu ya ‘miujiza’ au ‘mauzauza’ ya kushuhidia ‘wafu wakifufuliwa’.

Kutokana na kukusanya waumini wengi kiasi cha kuhatarisha usalama wao kwa vile kanisa liko barabarani ndiyo maana aliamriwa alihamishe Ubungo na kulipeleka Kawe liliko sasa.
 Askofu Josephat Gwajima
Katika zama ambazo ‘kizazi cha nyoka’ kinaishi kwa kutegemea miujiza zaidi kuliko uhalisia na kutegemea ‘mana iendelee kudondoka kutoka mbinguni’, ni rahisi kwa Mchungaji Gwajima kuendelea kuwakuanya waumini kila siku.
Haishangazi kuona kwamba pamoja na kusoma Biblia na kukariri maneno kwamba “Kizazi cha nyoka kinachotafuta ishara hakitaipata isipokuwa ishara ya Yona” bado hawaelewi na kila uchao wanahaha kutafuta ishara na miujiza.
Imani za kidunia, hasa za kishirikina zilizotawala katika jamii, ndizo zinazowasukuma wanadamu wa kizazi cha sasa kutafuta ‘makanisa yanayotoa miujiza’ na haishangazi hivi sasa kuona makanisa ya ‘majina ya watu’.
Lakini Aprili 14, 2010 iliandikwa habari hii na gazeti moja, ambayo inawezekana hukuiona wakati huo ama umeisahahu, ndiyo maana MaendeleoVijijini inakukumbusha:
MISUKULE inayodaiwa kutolewa na Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima imemuumbua baada ya kuandikiwa barua na taasisi moja inayotetea watu hasa wanyonge ya Liberty International Foundation (LIF) inayoongozwa na Mchungaji Christopher Mtikila ikimtaka kiongozi huyo wa kiroho kuomba radhi kwa Bw. Faustin George Kahabi kwa madai ya kumdhalilisha mtoto wake, Happiness Kahabi ambaye anadaiwa kutangazwa kuwa ni mmoja wa misukule waliookolewa katika kanisa hilo.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa barua hiyo inayojulikana kisheria kama Demand note ya Aprili 7, mwaka huu, iliyoandikwa na taasisi hiyo inasema, Bw. Kahabi anadai kuwa Mchungaji Gwajima aliutangazia umma kuwa mtoto wake Happiness ambaye ni mke wa Isaya Ndambo alichukuliwa Msukule na yeye (baba) na kupelekwa chini ya Ziwa Victoria baada ya kufariki dunia mwaka 2008 katika Hospitali ya Bugando na kwamba kutokana na maombi yake (Gwajima) alifanikiwa kumtoa kuzimu katika kundi la Misukule.

Waraka huo (nakala tunayo) unazidi kueleza kuwa tukio hilo la kutolewa kama Msukule Happiness, lilirekodiwa na kuwekwa katika kanda (DVD) na kusambazwa sehemu mbalimbali za dunia hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa Bw. Kahabi.

“Umesababisha Bw. Kahabi agombane na mkewe Edda Faustine Kahabi na ndugu na kumsababishia hatari katika jamii na pia kupandikiza unyanyapaa,” imesema sehemu ya waraka huo.

Aidha, barua hiyo imesema upo ushahidi kutoka kwa jamaa wa Bw. Kahabi, marafiki na majirani kuwa katika familia hiyo (ya Kahabi) hapajawahi kutokea msiba wa Happiness na wala hawajawahi kuwa na Msukule na kwamba aliyetajwa kuwa Msukule hajawahi kutoweka nyumbani hata kwa wiki moja.



Mchungaji Mtikila

Barua hiyo imemtahadharisha Mchungaji Gwajima kuwa kuzusha habari za Msukule ni kosa la jinai kama litafikishwa katika vyombo vya sheria, hivyo taasisi ya LIF imemtaka amuombe radhi Bw. Kahabi ndani ya siku saba kuanzia siku iliyoandikwa barua hiyo Aprili 7, mwaka huu.

Aidha, pamoja na radhi hiyo, Mchungaji Gwajima ametakiwa kuambatanisha shilingi bilioni moja kama fidia ya kuikashifu familia hiyo na pia kuhakikisha mke wa Bw. Kahabi anarudi kwa mumewe akiwa na watoto wao George pamoja na Amos.

Taasisi hiyo imemuonya Mchungaji Gwajima kuwa bila kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria bila kupewa taarifa ya ziada.

Uchunguzi wetu umegundua kuwa aliyepewa kusimamia shauri hilo ni Mchungaji Christopher Mtikila ambaye anaaminika kwa kufuatilia kesi mahakamani. Chanzo chetu cha habari kilisema kigezo kilichotumika kumchagua ni kutokana na uhodari wake wa kushughulikia kesi ngumu, wakatoa mfano wa kesi ya mgombea binafsi ambayo imelazimu Mahakama ya Rufaa nchini kuisikiliza ikiwa na majaji saba.


Demand Note aliyopelekewa Mchungaji Gwajima

Aidha, Mtikila anatajwa kuwa amekuwa na historia nzuri ya kushinda kesi na wakatolea mfano wa kesi ya vyama vya siasa kuomba kibali cha kufanya mikutano ya hadhara ambapo kiongozi huyo wa Chama cha Democratic Party aliishitaki serikali na kuishinda.

Gazeti hili liliwasiliana na Mchungaji Mtikila na kumuuliza kama kweli amepewa jukumu la kuisimamia kesi ya Bw. Kahabi akasema kwa sasa hawezi kusema chochote kwa kuwa Mchungaji Gwajima kapewa masharti ya kutimiza na atakuwa tayari kusema iwapo aliyoandikiwa katika barua atashindwa kutekeleza.

“Mimi kwa sasa siwezi kunena chochote kwa sababu kuna barua kapelekewa, sasa kama atashindwa kutekeleza alichoambiwa na siku saba alizopewa zikaisha, nitazungumza,” alisema Mtikila. Siku saba hizo zinaisha leo (Aprili 14, 2010).

Mchungaji Gwajima hakuweza kupatikana licha ya waandishi wetu kufika katika kanisa lake Ubungo.

Hivi karibuni Mchungaji Gwajima amejizolea umaarufu kwa madai ya kutoa Misukule. Hata hivyo, watu wana hamu kubwa kuona kama atafanikiwa kumrejesha aliyekuwa Mbunge wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amina Chifupa ambaye aliwahi kudai kuwa ni msukule na wiki iliyopita gazeti hili lilibeba habari inayodai kuwa aliwahi kutoa misukule 70.


Comments