Featured Post

MGEJA: BULEMBO WATAJE WALIOKUPA MILIONI 180 ZA KAMPENI JUMUIYA YA WAZAZI


Na Hastin Liumba, Tabora
KAULI ya mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi(CCM), Mjumbe wa Kamati Kuu na Mbunge wa Kuteuliwa, Abdallah Majura Bulembo, kuwa alipewa Shs. 40 milioni kutoka kwa Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa ili imsaidie kumpatia ushindi wa jumuiya hiyo mwaka 2014 ina utata mkubwa, imefahamika.


Mwenyekiti  wa taasisi ya inayoshughulikia utawala bora ya Tanzania, Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja, alisema hayo wakati akiongea na wandishi wa habari mkoani hapa akiwa njiani kuelekea mkoani Kigoma, ambapo alimtaka pia Bulembo ataje alikozitoa Shs. 180 milioni nyingine.
Mgeja alisema kuwa kauli ya Bulembo ni ya kumdhihirishia mwenyekiti wake wa CCM, Rais Dk. John Pombe Magufuli, kuwa rushwa ndani ya CCM imetamalaki na haiepukiki katika uchaguzi wa wazazi uliopo ngazi ya chama.
Alisema kauli ya Bulembo ni ya kukiri wazi mbele ya chama chake na umma kuwa katika kutafuta nafasi ya uenyekiti wazazi taifa alitumia mamilioni ya fedha kutokana na michango ya watu mbalimbali iliyopelekea yeye kushinda.
Alisema hata hivyo hatuamini Lowassa alimpa fedha ili zimsaidie kwenye kampeni bali Bulembo anachofanya sasa ni propaganda ya muendelezo wake wa kila siku wa kumdhalilisha, kumdhihaki, kumtukana na kumkejeli waziri mkuu huyo mstaafu na kutaka kujipatiwa umaarufu wa kisiasa.
Aidha, alisema kama Bulembo amekiri pasipo shaka na kushurutishwa na mtu yoyote basi ataje majina mengine ya waliompa msaada wa mamilioni ya fedha Shs. 80 milioni pamoja na nyingine Shs. 100 milioni, kwani haitoshi tu kumtaja Lowassa peke yake aliyempa Shs. 40 milioni na kuwaficha wengine.
“Tatizo la rushwa ndani ya CCM siku zote limekuwa donda ndugu na kupelekea CCM kupoteza haiba yake ya asili, shabaha, malengo na madhumuni yake ya chama kiasi cha kupelekea Watanzania wengi kuendelea kila siku kupoteza imani na CCM,” alisema.
 Aidha Mgeja aliongeza kuwa hivi sasa ile falsafa yake kuwa CCM ni chama cha wakulima na wafanyakazi haipo na ilishatoweka siku nyingi kwa sasa kinachoangaliwa na CCM hivi sasa ni fedha na wenye fedha.
 Hata hivyo, Mgeja amempongeza Bulembo kuwa mkweli na muwazi yeye amekuwa kinara wa kutafuta michango ya mamilioni ili kutoa rushwa ndani ya CCM wakati wa uchaguzi.
 Mgeja aliongeza imekuwa tabia ndani ya CCM siku zote kila anayetafuta cheo ni lazima amtusi Lowassa.
 “Tunajua kwa muda mrefu ana hamu na kutamani sana nafasi ya katibu mkuu wa CCM taifa na atambue Bulembo na wenzake dhambi hii ya kukosa fadhila, uzushi na uongo iko siku lazima itamtafuna yeye na wenzake wenye tabia zinazofanana na yeye,” alisema.

Comments