Featured Post

MASHIRIKA YA UMMA JIANDAENI KUCHANGIA BAJETI YA SERIKALI

 Mkurugenzi Miliki na Miradi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) Victoria Kamagenge akiwa anawaonyesha wajumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PAC) moja ya mradi unaojegwa na kituo hicho jijini Arusha ambao umegharimu Shs. 2.8  bilioni.


 baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Umma (PAC) wakiwa wanateta jambo

 wakiendelea kukagua
 mbunge wa jimbo la  Bunda mjini   Ester Bulaya akiwa anakula na wakandarasi wa jengo jipya la maonyesho linalojengwa na kituo cha mikutano cha AICC wakati walipofanya ziara na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Umma (PAC

Kamati ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Umma (PAC) wakiwa katika picha ya pamoja
Na Woinde Shizza, Arusha

Kamati ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Umma (PAC) imeyataka mashirika ya umma 265 yaliyopo nchini, kuanza kujiandaa kuchangia Bajeti ya  Serikali kuanzia mwaka ujao wa fedha.

Aidha, wakurugenzi na wenyeviti wa bodi wa mashirika hayo kuanzia mwakani  watatakiwa  kuwasilisha bajeti zao bungeni ili kuweza kupitishwa na Bunge na hakuna shirika lolote la serikali litakaloweza kupitishwa  bajeti bila kuidhinishwa  na Bunge.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti  wa Kamati hiyo, Albert Obama Mtabaliba ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Buhigwe, mkoani Kigoma, wakati kamati hiyo ilipotembelea miradi ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) na kujionea miradi mbalimbali inayoendeshwa na kituo hicho ikiwemo ujenzi wa nyumba za kupangisha, hospitali pamoja na jengo la maonyesho na mikutano linaloendelea kujengwa na kituo hicho.

Alisema kuwa  licha ya mashirika hayo kuwa na thamani kubwa ya Shs. 26 trilioni lakini yamekuwa hayachangii ipasavyo bajeti ya serikali, hivyo yanatakiwa yabadilike na kuanza kulipa kodi ipasavyo pamoja na kutoa gawio serikalini.

‘’Mashirika yote ya umma yaliyopo hapa nchini yana thamani ya Shs. 26 trilioni na kwa mwaka yamekuwa yakitoa faida ya Shs. 450 bilioni pekee ambayo ni sawa na asilimia 1.08% kitu ambacho hakiwezekani ukilinganisha na mtaji uliopo, hivyo wakurugenzi na wenyeviti wa bodi wametakiwa wahakikishe mapato yao kwa serikali yanapanda na angalau waweze kuchangia trilioni mbili kwa mwaka," alisema Mtabaliba.

Akizunguzia kituo hicho cha AICC, alipongeza miradi inayoendeshwa na kituo hicho na kushauri waanze kuchukua hatua ya kukabiliana na soko na pia wajitahidi kuwekeza zaidi katika ujenzi wa vituo vya mikutano vya kisasa, na kuwataka kuelekeza nguvu zaidi ya kujenga kituo kikubwa cha mikutano Dodoma ambao ni Mji Mkuu wa Tanzania.

Hata hivyo, mmoja wa wajumbe wa  kamati hiyo, Ester Bulaya, alikosoa  gharama za ukarabati zilizotumika kukarabati ukumbi wa Simba Hall uliopo katika kituo hicho ambapo kiasi cha Shs. 3.5 bilioni zilitumika jambo ambalo hawakuafiki na kushauri kwamba fedha hizo ni nyingi sana na zingeweza kutumika kwenye uwekezaji mwingine.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa AICC, Elishilia Kaaya, alisema kuwa amefurahishwa na ujio wa Kamati hiyo kuwatembelea  na pia wamekutana nao na wamepewa elimu nzuri ya uwekezaji na wametaja baadhi ya  mambo ambayo hayajaenda sawa wamewarekebisha na kwamba mtazamo utabadilika kulingana na hali ilivyo.

Hata hivyo, alisema kwa sasa wameanzisha mradi wa ujenzi wa kumbi za mikutano, hoteli na maonyesho unaogharimu kiasi cha Shs. 2.8 bilioni.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika Mei 4, 2017 ambapo wanategemea utasaidia kuongeza mapato ya kituo hicho pamoja na ajira kwa Watanzania.

Comments