Featured Post

MAKONDA NG’ATUKA HARAKA KABLA YA KUNG’OLEWA, RIPOTI YA KAMATI YA NAPE ITAKUUMBUA!



Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
Wakati kamati ya watu watano iliyoundwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake leo hii kuhusu uchunguzi wa tukio la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwa madai ya kuvamia kituo cha matangazo cha Clouds Media Ijumaa usiku Machi 17, 2017.

Ukweli wa ripoti hiyo unaweza kuleta taswira nyingine nchini hasa kutokana na ukweli kwamba, ni mara ya kwanza kwa kiongozi mkubwa wa serikali hapa nchini kutumia silaha kuvamia chombo cha habari kama jambazi.
Hata hivyo, pamoja na ukweli wa ripoti ya kamati hiyo, kuna kila dalili kwamba kiongozi huyo hawezi kuwajibishwa.
Hali hiyo imewafanya wachunguzi wa masuala ya siasa kumshauri Makonda kung’atuka mwenyewe hata kama kuna watu wanaomkingia kifua ili kulinda hadhi yake pamoja na majaliwa yake ya baadaye.
“Makonda bado kijana mdogo hata miaka 30 hajafikisha, ajitafakari sana katika hili kwa sababu leo anaweza kuwa salama kwa sababu ya kulindwa, kesho wanaomlinda hawatakuwa madarakani, na haya yatakuja kumhukumu.
“Kama atajiuzulu na kuomba radhi pia kwa kitendo hicho kisicho cha kiungwana, anaweza kuwapa watu imani,” wamesema wananchi mbalimbali waliohojiwa na MaendeleoVijijini.
Makonda alidaiwa kuvamia kituo hicho akiwa na askari polisi nane wenye bunduki na kuingia moja kwa moja hadi chumba cha kurushia matangazo wakati kipindi kinaendelea na kuwashambulia watangazaji wawili wa kipindi cha Da’Weekend Show (Shilawadu) kinachorushwa kila siku ya Ijumaa.
Habari za awali zinasema, Makonda alikuwa amechukiwa na kipindi hicho kutorusha video ya mwanamke anayedai kuzaa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, katika kile kinachoonekana ‘vita baina yao’.
Waziri Nape aliiteua kamati hiyo jana, Jumatatu asubuhi, Machi 20, 2017, na kuipa saa 24 ifanye uchunguzi ili kubaini ukweli wa kilichotokea huku akilaani tukio hilo kwamba ni kunajisi uhuru wa habari.

Kamati hiyo ya Nape inaongozwa na Dkt. Hassan Abbas, Mkurugenzi wa Idara ya Habari - MAELEZO, Deodatus Balile ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Jesse Kwayu, Mhariri MTendaji wa gazeti la Nipashe, Nengida Johannes Lailumbe kutoka Upendo Radio, na Mabel Masasi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
"Tumezoea kuona matukio haya yanatokea kwenye nchi ambazo zimepinduliwa kwenda kwenye vyombo vya habari na mabunduki si sawa, kwa jambo hili tunataka kutenda haki tumsikilize Mkuu wa Mkoa ili tujue kwanini amefanya jambo hili.
"Matukio kama haya hutokea wakati nchi inapotaka kupinduliwa, lakini kama Rais yupo na nchi haijapinduliwa, basi kuingia ndani ya chombo cha habari na silaha, huku ni kunajisi uhuru wa habari," alisema Nape.
Pamoja na hayo Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Dkt. Reginald Mengi amesema hawezi kutoa lawama kwa mtu yoyote mpaka pale ukweli utakapofahamika japokuwa ameonekana kukerekwa.
"Kwetu sisi hili ni jambo ni la hatari sana, linatuogopesha na linatishia maisha ya waandishi wa habari," alisema Dkt. Mengi.
 Siku Makonda alipomshambulia Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba mwaka 2014.

Gwajima vs Makonda:
Vita baina ya Gwajima na Makonda imeendelea kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, ambapo inatokana na hatua ya mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam kuanzisha operesheni ya kupambana na dawa za kulevya, ambapo Gwajima ni miongoni mwa watuhumiwa walioitwa na kuwekwa mahabusu kwa madai ya kujihusisha na biashara hiyo haramu.
Kutokana na kitendo hicho, Gwajima, akidaiwa kushirikiana na mwanadada Mtanzania aishiye Marekani, Mange Kimambi, walifichua kwamba Makonda siyo jina lake bali jina lake halisi ni Daudi Albert Bushite, na kwamba hata vyeti vyake ni vya kufoji.
Jumatatu asubuhi wakati wa kipindi cha Power Breakfast, Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media, Ruge Mutahaba alieleza kusikitishwa na matumizi mabaya ya madaraka yaliyooneshwa na Mkuu huyo wa Mkoa.

Rais amkingia kifua:
Lakini wakati wananchi wengi wakishinikiza kupitia mitandao ya kijamii kwamba makonda afukuzwe kazi, Rais Dkt. John Magufuli, jana Jumatatu aliwaacha wengi midomo wazi baada ya kusema kwamba yeye hapangiwi nini cha kufanya.
Akizungumza wakati wa sherehe za kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara za juu (flyovers) pale Ubungo Mataa jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema hawezi kufanya uamuzi kwa shinikizo la mitandao na akaonya kwamba, wale waliodhani kuandika hivyo ndiko kungemfanya aamue cha kufanya wamekosea.
"Mimi ni Rais ninaejielewa. Ninajiamini. Mimi ndiye niliyemteua, msinipangie cha kufanya. Mimi sionyeshwagi njia ya kupita. Sipangiwi na mtu nani wa kumchagua na kumuweka wapi. Watu wafanye kazi, waache majungu. Makonda endelea kuchapa kazi," alisema.

Tunachokifahamu sisi:
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Makonda kuvamia chombo cha habari, kwani taarifa tulizonazo zinaeleza pia kwamba, siku chache kabla hajapandishwa kuwa Mkuu wa Mkoa, wakati huo akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, aliwahi kuvamia ofisi za Global Publishers wanaochapisha magazeti ya Uwazi, Ijumaa, Risasi, Amani, Championi na Ijumaa Wikienda akimsaka mwandishi mmoja aliyeripoti kuhusu uhusiano wake wa kimapenzi na msanii mmoja wa runinga.
Taarifa zinasema, ingawa mwandishi huyo alikuwa amempigia simu kupata upande wa pili, lakini hakuwa ametoa ushirikiano, hivyo akairipoti habari hiyo kwa kadiri ilivyokuwa, jambo ambalo lilionekana kumkera na kuamua kuchukua polisi kuvamia hapo huku akilazimisha aingie ndani ili kumkamata.
MaendeleoVijijini inazo kumbukumbu za kuvamiwa kwa vyombo vya habari na wenye mamlaka ambapo Mei Mosi, 2005, Lucy Muthoni Kibaki (R.I.P.) aliyekuwa mke wa Rais Emilio Mwai Kibaki wa Kenya, alivamia chumba cha habari cha Nation Media Group baada ya gazeti la Daily Nation kuripoti kitendo chake kisicho cha kiungwana cha kuvamia sherehe ya jirani yake, Makhtar Diop, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia aliyekuwa akiagwa, na kuagiza muziki uzimwe kwa sababu unampigia kelele.
 Lucy Muthoni Kibaki (R.I.P.) siku alipovamia ofisi za Nation Media Group jijini Nairobi, Mei Mosi, 2005. 

Katika tukio hilo, alimzaba kibao Clifford Derrick, cameraman wa KTN, ambaye alikuwa akichukua matukio yake, na akawanyang’anya waandishi notebook na vinasa sauti (tape recorders).

Ingawa Derrick alishtaki kwa kushambuliwa, lakini Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo, Amos Wako, aliifuta kesi hiyo mara mbili kwa kutumia sheria ya nolle prosequi.
Aidha, MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, Jumatatu, Desemba 29, 2014, Polisi nchini Bosnia kutoka kikundi cha Serb Rupublika Srpska wakisaidiwa na polisi wa Sarajevo walivamia chumba cha habari cha mtandao maarufu wa Klix baada ya kuchapisha video iliyodaiwa kumtuhumu Waziri Mkuu wa Serbia kwamba alinukuliwa akisema ‘angenunua’ kura za uchaguzi.
Ilielezwa kwamba, maofisa hao walipoingia wakaanza kunyonya taarifa zote kutoka kwenye kompyuta.
Machi 26, 2016, maofisa wanaodaiwa kutoka Idara ya Usalama ya Zimbabwe (Central Intelligence Organization-CIO) walivamia ofisi za taasisi ya habari ya The Source na kuondoka na kompyuta na vifaa vingine.
Jumanne, Julai 12, 2016 maofisa wa Polisi na Jeshi la nchini Thailand walivamia chumba cha habari cha gazeti tando la Prachatai lenye mrengo wa kushoto wakiwa wanapekua kutafuta ushahidi unaohusiana na mwandishi wao, Taweesak Kerdpoka, aliyekamatwa Julai 10, 2016 pamoja na wanaharakati wa kundi la New Democracy Movement (NDM), Pakorn Areekul, Anucha Rungmorakot na Anan Loked.
 Maofisa wa polisi wakipekua nyaraka mbalimbali.
Kumbukumbu za MaendeleoVijijini zinaonyesha kwamba, Jumatano Septemba 7, 2016, Polisi wa Visiwa vya Maldives walivamia ofisi za gazeti tando maarufu visiwani humo la Maldives Independent mara tu baada ya kutangaza kupitia runinga yao waraka mmoja uliomtuhumuwa Rais Abdulla Yameen kwa rushwa, utakatishaji fesha na uongozi mbaya.
Zaheena Rasheed, mhariri wa gazeti hilo, alisema kwamba polisi hao waliingia na hati ya mahakama ikiwatuhumu kwa "njama za kuipindua serikali."
Polisi waliondoka na mikanda yote ya kamera za usalama pamoja na kompyuta.
Mnamo Novemba 12, 2016, majira ya saa 3:33 (kwa saa za Washington), kikosi cha maofisa wa Mambo ya Ndani kutoka Idara ya Uhamiaji na Forodha (Immigration and Customs Enforcement-I.C.E.) walivamia ofisi za gazeti kongwe la Washington Post wakiwa na hati zilizotolewa na kikosi maalum cha sheria cha Donald Trump.
Hati hizo ambazo zilionyesha kughushiwa zilieleza kwamba walikuwa wanatafuta vielelezo kwamba gazeti hilo lilikuwa linawahifadhi wahamiaji haramu, wakiwemo wafanyakazi.
Kompyuta, simu na taarifa binafsi za wafanyakazi vilichukuliwa katika uvamizi huo ambao maofisa hao walitumia gesi ya CN (phenacyl chloride) ambayo wakati mwingine hujulikana kama “kesi ya matapishi’, ambayo ilisababisha wafanyakazi wengi kukimbizwa hospitali baada ya kuzidiwa.

Kile kilichotokea pale Clouds Media kinasimuliwa hivi:
 
Jengo la Clouds Media Group lililopo Mikocheni B jana lilishuhudia sekeseke la aina yake baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuvamia akiwa na Walinzi wenye Bunduki.

Tukio hilo tukoea majira ya Usiku wakati kipindi SHILAWADU kikiwa hewani ambapo Makonda alivamia kwa lengo la kushinikiza Shilawadu waonyeshe mahojiano yenye lengo la kumchafua Askofu Gwajima.

Vyanzo vya uhakika vinaeleza kwamba, mwanzoni wiki 2 zilizopita, SHILAWADU walipigiwa simu na watu wasiojulikana wakieleza kwamba wana 'ubuyu' mzito wa kuhusu Askofu Gwajima na mwanamke anayedaiwa kuzaa nae. Mwanzo Shilawadu walikataa habari hiyo, lakini siku moja walikutana na Makonda akawashawishi SHILAWADU wafuatilie stori hiyo. Kama kawaida yao kupenda umbea, SHILAWADU wakiongozwa na Soudy Brown walimtafuta mwanamke anayedaiwa kuzaa na Gwajima kisha wakamhoji.

Hata hivyo, kwa kuhofia nguvu ya Gwajima katika kupambana na shutuma dhidi yake, na kwa kuzingatia maadili ya kazi, SHILAWADU waligoma kurusha habari hiyo hewani mpaka wapate kauli za upande wa pili ( upande wa Gwajima ). Baada ya kuhangaika huku na kule , SHILAWADU walishindwa kupata upande wa pili wa habari ( walishindwa kubalance story ).

Kutokana na hilo, na kujua kwamba Gwajima asingewaacha salama kwa kutoa story ya uongo dhidi yake, #SHILAWADU na wasimamizi wa vipindi wa Clouds Tv waliamua kuachana kabisa na story hiyo.

MAKONDA ANAINGIAJE? : Imefahamika kwamba watu ambao walipiga simu kwa Shilawadu kuhusu uwepo wa Mwanamke huyo ni watu wa Makonda. Makonda alitaka story hiyo itolewe kupitia #SHILAWADU ambao wana kawaida ya kuripoti matukio ya Watoto/wanawake waliokataliwa. Kwa kuwa Makonda ana marafiki wengi pale Clouds, aliamini kwamba story hiyo lazima ingetolewa na hivyo kumchafua adui yake GWAJIMA (kuzima sakata la vyeti ).

Akiwa nyumbani kwake Masaki, Makonda alikaa kwenye Tv yake Ijumaa kusubiri SHILAWADU wamvue nguo Gwajima. Cha kumsikitisha, Makonda alipata habari kwamba SHILAWADU wamegoma kupeleka habari hiyo. Hata viongozi akiwemo swahiba wake Ruge walikaataa kabisa kupeleka habari ambayo haiko 'balanced' na mbaya zaidi inawaingiza kwenye vita na mtu wa aina ya Gwajima.

Kama kawaida yake, Makonda aliamua kutumia ubabe. Kwa kuwa amezoea kuingia Clouds, Makonda alifahamu kuwa muda huo viongozi hawapo na watu waliopo anawamudu. Hivyo aliamua kwenda Clouds kuhakikisha Shilawadu wanaonyesha habari hiyo ya kumchafua Gwajima. Hivyo alibeba wanaume zaidi ya 8 wakiwa wamebeba silaha za moto.

Alipofika Clouds, walinzi wa Getini walimruhusu kupita yeye na gari iliyokuwa nyumba yake akisema ni rafiki zake wamekuja mara mara moja kwenye SOSOO FRESH kwani Adamu Mchomvu amewaalika. Lakini alipofika Reception, Mlinzi wa zamu alisitia baada ya kuona Makonda amekuja na watu wengi. NA HAPO NDIPO KASHESHE ILIANZA.

Walinzi wa Makonda walitoa Bunduki, walimtishia Mlinzi wakampiga sana na wakatumia nguvu kubwa hadi walifanikiwa kuingia ndani. Walipofika na Bunduki zao, Makonda aliamuru kila mtu kukaa alipo huku akilazimisha habari ya Gwajima iende. Kwisa kama kiongozi wa kipindi ndiye ambaye alipingwa mitama na ngumi za kutosha.

Kwa walioangalia kipindi wanajua kwamba kipindi hakikuisha, hiyo ni kutokana na kwamba Makonda na waligawa kipigo cha maana kwa Shilawadu kisha wakawabeba kwenda nao nje akisema wanaenda Cental.

Pia alitumia Bunduki kuwalazimisha Shilawadu wampe Video ya Mama anayedaiwa kuzaaa na Gwajima (alipewa). Makonda aliwaambia wapambe wake kama Shilawadu wamekataa kuonyesha habari hiyo baasi yeye atahakikisha inasambaa kupitia mitandao ya kijamii.

Hivi sasa Shilawadu hawako sawa kisaikolojia huku Suod Brown akiwa hana amani kwani alipigwa picha na Makonda alimuambia kama anaogopa kumdhalilisha Gwajima baasi yeye atadhalilishwa kwani Sura yake itawekwa hadharani kila mtu afahamu.

Baadae Makonda aliondoka baada ya kupigiwa simu ambayo haijulikani nani alipiga lakini Makonda alipoondoka Ruge alingia Clouds akiwa na watu huku na yeye amebeba bastola. Inaaminika ile simu ilipigwa kumuambia aondoke maana Ruge anakuja.





Comments