Featured Post

MAKONDA AWAJIBISHWE, RIPOTI YATUA KWA WAZIRI NAPE!

WAZIRI wa Habari, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye, leo hii amepokea ripoti ya Kamati aliyoiunda juzi kuchunguza uvamizi unaodaiwa kufanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, katika kituo cha runinga cha Clouds Media Ijumaa usiku Machi 17, 2017.
Dkt. Hassan Abbas, Mkurugenzi wa Idara ya Habari – Maelezo ndiye alimkabidhi ripoti hiyo akiwa mwenyekiti wa kamati ya watu watano walioteuliwa na kupewa muda wa saa 24.
Kamati hiyo ya Nape iliongozwa na Dkt. Hassan Abbas, Deodatus Balile ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Jesse Kwayu, Mhariri MTendaji wa gazeti la Nipashe, Nengida Johannes Lailumbe kutoka Upendo Radio, na Mabel Masasi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Akisoma ripoti hiyo, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deodatus Balile, alisema kamati yao imejiridhisha kwamba Makonda alikiunga kwa makusudu mamlaka yake pamoja na kuvunja sheria za nchi, ikiwemo Sheria Namba 3 ya Utangazaji, kwa kuingia ndani ya chumba cha matangazo bila idhini huku akiwa na askari wenye silaha.
Wamependekeza kwamba, Makonda ni vyema aombe radhi kwa Clouds Media na tasnia yote ya habari, lakini wakaiomba pia mamlaka ya uteuzi kumwajibisha kwa mujibu wa taratibu za uongozi.
“Ni kweli Makonda alivamia Clouds Media, alivamia akiwa na askari na kuwatisha wafanyakazi wa Clouds ambapo alikaa kwa saa moja, na akawatisha kwamba kilichotokea hapo kisitokee nje, kwani angewashughulikia kwa kuwaingiza kwenye orodha ya watuhumiwa wa dawa za kulevya.
“Kamati imeona kuwa hakuna mfanyakazi aliyepigwa lakini wafanyakazi walilia kwa kitendo kile,” alisema Balile.
Waziri Nape alisema kwamba ataipitia ripoti hiyo na kuiwasilisha kwa mamlaka zinazohusika kwa utekelezaji.
Rais amkingia kifua:
Hata hivyo, kuna uwezekano mdogo wa Makonda kuwajibishwa kwani mamlaka yake ya uteuzi, ambayo ni Rais, amekwishamtetea na kumwambia kwamba aendelee kuchapa kazi na aachane na maneno maneno ya mitandao.
Akizungumza wakati wa sherehe za kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara za juu (flyovers) pale Ubungo Mataa jijini Dar es Salaam Machi 20, 2017, Rais Dkt. John Magufuli alisema hawezi kufanya uamuzi kwa shinikizo la mitandao na akaonya kwamba, wale waliodhani kuandika hivyo ndiko kungemfanya aamue cha kufanya wamekosea.
"Mimi ni Rais ninayejielewa. Mimi ndiye niliyemteua, msinipangie cha kufanya. Mimi sionyeshwagi njia ya kupita. Sipangiwi na mtu nani wa kumchagua na kumuweka wapi. Watu wafanye kazi, waache majungu. Makonda endelea kuchapa kazi," alisema.
Ilivyokuwa
Makonda alidaiwa kuvamia kituo hicho akiwa na askari polisi nane wenye bunduki na kuingia moja kwa moja hadi chumba cha kurushia matangazo wakati kipindi kinaendelea na kuwashambulia watangazaji wawili wa kipindi cha Da’Weekend Show (Shilawadu) kinachorushwa kila siku ya Ijumaa.
Habari za awali zinasema, Makonda alikuwa amechukiwa na kipindi hicho kutorusha video ya mwanamke anayedai kuzaa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, katika kile kinachoonekana ‘vita baina yao’.
Waziri Nape aliiteua kamati hiyo jana, Jumatatu asubuhi, Machi 20, 2017, na kuipa saa 24 ifanye uchunguzi ili kubaini ukweli wa kilichotokea huku akilaani tukio hilo kwamba ni kunajisi uhuru wa habari.
"Tumezoea kuona matukio haya yanatokea kwenye nchi ambazo zimepinduliwa kwenda kwenye vyombo vya habari na mabunduki si sawa, kwa jambo hili tunataka kutenda haki tumsikilize Mkuu wa Mkoa ili tujue kwanini amefanya jambo hili.
"Matukio kama haya hutokea wakati nchi inapotaka kupinduliwa, lakini kama Rais yupo na nchi haijapinduliwa, basi kuingia ndani ya chombo cha habari na silaha, huku ni kunajisi uhuru wa habari," alisema Nape.
Pamoja na hayo Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Dkt. Reginald Mengi amesema hawezi kutoa lawama kwa mtu yoyote mpaka pale ukweli utakapofahamika japokuwa ameonekana kukerekwa.
"Kwetu sisi hili ni jambo ni la hatari sana, linatuogopesha na linatishia maisha ya waandishi wa habari," alisema Dkt. Mengi.
 Siku Makonda alipomshambulia Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba mwaka 2014.

Gwajima vs Makonda:
Vita baina ya Gwajima na Makonda imeendelea kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, ambapo inatokana na hatua ya mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam kuanzisha operesheni ya kupambana na dawa za kulevya, ambapo Gwajima ni miongoni mwa watuhumiwa walioitwa na kuwekwa mahabusu kwa madai ya kujihusisha na biashara hiyo haramu.
Kutokana na kitendo hicho, Gwajima, akidaiwa kushirikiana na mwanadada Mtanzania aishiye Marekani, Mange Kimambi, walifichua kwamba Makonda siyo jina lake bali jina lake halisi ni Daudi Albert Bushite, na kwamba hata vyeti vyake ni vya kufoji.
Jumatatu asubuhi wakati wa kipindi cha Power Breakfast, Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media, Ruge Mutahaba alieleza kusikitishwa na matumizi mabaya ya madaraka yaliyooneshwa na Mkuu huyo wa Mkoa.


Comments