- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
MAELEZO YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB) AKIWASILISHA MAPENDEKEZO YA SERIKALI YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA YA KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18
MACHI
2017
DODOMA
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, awali ya yote napenda
kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha Wabunge wote
kukutana hapa Dodoma kuanza kazi ya kuchambua mapendekezo ya Mpango na Bajeti
ya Serikali kwa mwaka wa fedha unaofuata, ikiwa ni mara ya kwanza tangu
kukamilika kwa awamu ya kwanza ya utekelezaji wa uamuzi wa Serikali kuhamia
rasmi Makao Makuu Dodoma.
Aidha, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijalia
nchi yetu umoja, mshikamano na amani. Vile vile, napenda kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kuwaponya Wabunge wenzetu ambao walinusurika katika ajali za
barabarani na majini. Nichukue fursa hii
kuwapa pole sana Wabunge husika na pia wale wote waliofiwa na Ndugu na jamaa
zao.
2.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kutumia nafasi hii kuwapongeza wenzetu
walioteuliwa na Mheshimiwa Rais hivi karibuni nikianza na Mheshimiwa Dkt.
Harrison Mwakyembe, Mbunge wa Kyela ambaye sasa amepewa dhamana ya kuongoza
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mheshimiwa Prof. Palamagamba
A. Kabudi (Mb), Waziri wa Katiba na Sheria.
Aidha, natoa pongezi za dhati kwa Mama yetu Mheshimiwa Salma Kikwete kwa
kuteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile, ninawapongeza Waheshimiwa Wabunge
wote waliofunga ndoa baada ya Mkutano wa Sita wa Bunge la 11.
3.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, taarifa hii inawasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango
wa Maendeleo wa Taifa na ya kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao
wa fedha 2017/18. Mapendekezo haya yanawasilishwa kwa Wabunge kwa mujibu wa
Kanuni ya 97 fasili ya (1) na (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la
Januari 2016 ili hatimaye Mheshimiwa Spika naye awasilishe Mapendekezo haya
kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti ili yafanyiwe uchambuzi na Kamati hiyo na
kuzishauri kamati za kisekta pamoja na Serikali kuhusu mapendekezo haya kama
inavyoelekezwa na Kanuni ya 97 fasili ya (4) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
4.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, taarifa hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu. Sehemu
ya kwanza ni tathmini ya mwenendo wa uchumi na ustawi wa Jamii. Sehemu ya pili
ni Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2016/17 na Mapendekezo
ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2017/18. Sehemu
ya tatu ni tathmini ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2016/17 na
mapendekezo ya kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha
2017/18.
SEHEMU YA KWANZA
TATHMINI YA MWENENDO WA UCHUMI NA USTAWI WA JAMII
5. Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa za awali zinaonesha kuwa, Pato la Taifa kwa
mwaka 2016 lilikua kwa wastani wa asilimia 7.0, sawa na ilivyokuwa mwaka 2015.
Hali hii imechangiwa na kasi kubwa ya ukuaji katika shughuli za: Uchimbaji
Madini na Mawe (asilimia 16.5); Usafirishaji na Hifadhi ya Mizigo (asilimia
15.6); Habari na Mawasiliano (asilimia 13.5); na Huduma za Kifedha (asilimia
11.3). Aidha, kwa upande wa utekelezaji wa azma ya Taifa ya kujenga uchumi wa
viwanda, shughuli za uzalishaji viwandani zilizidi kuimarika, zikiongezeka kwa
asilimia 7.8, ikilinganishwa na asilimia 6.5 mwaka 2015.
6. Mheshimiwa Mwenyekiti, wastani wa mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 5.2
mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 5.6 mwaka 2015, ukipungua kutoka asilimia
6.5 Januari 2016 hadi asilimia 5.0 Desemba 2016. Kwa mwezi Februari 2017, mfumuko wa bei
ulifikia asilimia 5.5. Wastani wa riba
za mikopo ya mwaka mmoja ambayo hutolewa na mabenki ya biashara ulipungua
kutoka asilimia 14.22 Desemba 2015 hadi asilimia 12.87 Desemba 2016, wakati
riba za amana za mwaka mmoja zilipungua kutoka asilimia 11.16 hadi asilimia
11.03 katika kipindi hicho. Hivyo, tofauti kati ya riba za mikopo na amana za
mwaka mmoja imeendelea kupungua, kutoka wastani wa pointi 3.06 za asilimia
(percentage points) mwezi Desemba 2015 hadi pointi 1.83 za asilimia mwezi Juni
2016. Katika kipindi kinachoishia Desemba 2016, mauzo ya bidhaa na huduma nje ilikuwa dola za Kimarekani milioni
9,381.6 ikilinganishwa na dola za Kimarekani milioni 8,921.9 katika kipindi
kama hicho mwaka 2015, sawa na ongezeko la asilimia 5.2. Ongezeko hili
lilitokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa asilia, dhahabu, bidhaa za
viwadani na mapato ya sekta za huduma, hususan utalii.
7. Mheshimiwa Mwenyekiti, Akiba ya fedha za kigeni
ilifikia dola za Kimarekani milioni 4,325.6 Desemba 2016, kiasi ambacho
kinatosheleza gharama ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 4.2.
Katika kipindi hicho, thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi
ya dola ya Kimarekani ilibaki kuwa imara kufuatia usimamizi madhubuti wa sera
za fedha na bajeti, ikishuka kwa wastani wa asilimia 1.2 kutoka shilingi 2,144.27
mwezi Desemba 2015 hadi shilingi 2,170.44 Desemba, 2016. Kwa upande wa Deni la Taifa, likijumuisha deni la
ndani na nje, liliongezeka kufikia dola za Kimarekani milioni 19,021.9 Desemba
2016 ikilinganishwa na dola za Kimarekani milioni 18,459.3 Juni 2016, sawa na
ongezeko la asilimia 3.05, lakini likibaki ndani ya vigezo vyote vya uhimilivu.
Napenda kusisitiza kuwa, nchi kuwa na deni sio dhambi! Jambo muhimu ni
kuhakikisha kuwa fedha tulizokopa zinatumika kujenga rasilimali (capital
assets) ambazo ni msingi wa kuongeza uwezo wetu wa kuzalisha mali na kuendeleza
Taifa lakini pia uwezo wa kulipa mikopo hiyo.
8.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa ustawi wa jamii, idadi ya watu wanaoishi chini ya
mstari wa umaskini imeendelea kupungua kufuatia utekelezaji wa mikakati na sera
za Serikali zinazolenga kuboresha maisha ya watu. Katika kufikia azma hiyo
Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya elimu, afya, upatikanaji wa maji
safi na salama, umeme, barabara vijijini, nyumba na makazi bora. Kwa mujibu wa
Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania 2015/16,
vifo vya watoto wachanga chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka 51 kwa vizazi
hai 1,000 mwaka 2010 hadi 43 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2015/16. Vile vile,
vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 81 kwa vizazi hai 1,000
mwaka 2010 hadi 67 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2015/16. Pamoja na kupunguza
umasikini wa mahitaji ya msingi, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kuwa idadi
ya Watanzania wanaokosa mlo kwa siku au kuishi kwa mlo mmoja inapungua kutoka
kiwango cha sasa cha asilimia 9.7 na kufikia asilimia 5.7 na 4.4 mwaka 2020 na
2025 kwa mtiririko huo. Hatua zinazochukuliwa ni kufikia lengo hilo ni pamoja
na kuimarisha uzalishaji wa chakula na tija katika kaya, kuongeza fursa za
ajira mijini na vijijini, na mpango wa kusaidia kaya masikini, kutoa mikopo
nafuu kwa wajasiriamali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Mfuko wa
Wanawake.
SEHEMU YA PILI
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA
MPANGO WA MWAKA 2016/17 NA MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA MWAKA 2017/18
A: TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA
2016/17
9.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwa mwaka 2016/17 Serikali
ilitenga shilingi bilioni 11,820.503 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. Kati ya
fedha hizo, shilingi bilioni 8,702.697 zilikuwa za ndani na bilioni 3,117.805 fedha
za nje. Hadi Februari 2017, fedha zilizokuwa zimetolewa ni shilingi bilioni
3,975.4, ikijumuisha fedha zilizotolewa kwa Halmashauri, sawa na asilimia 34 ya
bajeti ya maendeleo. Kati ya kiasi hicho, fedha za ndani zilikuwa shilingi
bilioni 3,103.6 na fedha za nje shilingi bilioni 871.8. Kiwango kidogo cha
fedha ya maendeleo iliyotolewa kilisababishwa na sababu mbalimbali, ikiwa ni
pamoja na kuelekeza sehemu ya fedha za maendeleo kwenda kulipia madeni ya
miradi ya maendeleo, lakini kiuandishi wa taarifa za kibajeti zinahesabiwa
upande wa matumizi ya kawaida; Kuchelewa kupatikana kwa misaada na mikopo
kutokana na majadiliano na Washirika wa Maendeleo kuchukua muda mrefu; na pia kupanda
kwa riba ya mikopo ya kibiashara katika soko la fedha kimataifa. Hata hivyo, ni
vema kutambua kuwa, mwenendo huu wa kupungua kwa misaada na mikopo haikuwa kwa
Tanzania pekee. Nchi nyingine za Afrika zimekumbwa na hali hii. Mathalan,
misaada ya maendeleo kwa kipindi cha 2009 hadi 2014 kwa nchi kama Zambia
imepungua kutoka dola za Kimarekani milioni 1,267 hadi milioni 995; Cote
d’Ivoire kutoka dola milioni 2,402 hadi milioni 922; Botswana kutoka dola
milioni 209 hadi dola milioni 100; na Algeria kutoka dola milioni 318 mwaka
2009 hadi dola milioni 158. Kupungua kwa misaada kunafuatia kudorora kwa uchumi
kwa baadhi ya nchi zinazotoa misaada, na kuchoka kuendelea kutoa misaada (aid
fatigue) na mtazamo mpya kuhusu mfumo wa ushirikiano baina ya mataifa hayo na
Afrika.
10.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, vile vile, shilingi bilioni 161.639 za matumizi ya
kawaida zimetumika katika mafungu mbalimbali kwa shughuli zenye asili ya
maendeleo; na shilingi bilioni 192.609 zilipelekwa moja kwa moja na Washirika
wa Maendeleo kwenye miradi ya maendeleo (D-funds) na hivyo kufanya fedha
iliyotumika kwa shughuli za maendeleo kufikia shilingi bilioni 4,168.009 sawa na asilimia 35.26 ya bajeti ya maendeleo
hadi Februari 2017. Aidha, kiasi cha shilingi bilioni 59.896 zilichangiwa na
mashirika ya umma na binafsi katika kutekeleza shughuli za maendeleo ya kijamii
(corporate social responsibility).
11.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Baadhi ya hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi
ya maendeleo ni pamoja na zifuatazo:
(i)
Makaa ya Mawe Mchuchuma na Chuma Liganga – Njombe: maandalizi yote
ya ujenzi wa miradi hii yamekamilika, ikiwa ni pamoja na kutenga fedha kwa
ajili ya malipo ya fidia kwa wananchi watakaopisha mradi. Vile vile, kampuni ya
Sichuan Hongda (Group) Corporation Ltd, ambayo
ndio mbia katika miradi hii, wametenga jumla ya dola za Kimarekani milioni 300
kwa ajili ya kulipia sehemu ya mtaji (equity)
wao katika miradi. Hatua iliyobaki ni kukamilisha mazungumzo kuhusu vivutio vya
kodi vilivyoombwa na wawekezaji na bei ya mauziano ya umeme na TANESCO.
(ii) Ujenzi wa Reli ya Kati: Mkandarasi
kampuni ya YAPI MERKEZI ya Uturuki kwa kushirikiana na MOTA-ENGIL AFRIKA ya
Ureno wamesaini mkataba wa kusanifu na kujenga awamu ya kwanza ya mradi kutoka
Dar – Morogoro (Km 205) na ujenzi unatarajiwa kuanza katika mwaka huu wa fedha.
Kwa sehemu za reli hiyo kati ya Morogoro
na Makutupora (Km 336), Makutupora hadi Tabora (Km 294), Tabora hadi Isaka (Km
133) na Isaka hadi Mwanza (Km 249) taratibu zinaendelea za kupata fedha na
Wakandarasi.
(iii) Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania: Kazi
zilizofanyika ni pamoja na kununua ndege mbili (2) zenye uwezo wa kubeba abiria
76 kila moja. Ndege hizo zilianza kutoa huduma tangu Oktoba 2016. Maandalizi ya
kununua ndege nyingine 4 yamekamilika na mikataba kusainiwa. Utekelezaji wa
mkataba huu utagharimu dola za Marekani milioni 231.3, ambapo malipo ya awali
ya kiasi cha dola za Marekani milioni 56.89 tayari yamefanyika. Kati ya ndege
hizo, moja inategemewa kuwasili Julai 2017; mbili zinategemewa kuwasili Juni
2018, na ya mwisho, ambayo itakuwa ya masafa marefu inategemewa kuwasili Julai
2018.
(iv)
Ujenzi wa Mitambo ya Kusindika
Gesi Kimiminika, Lindi: Hatua iliyofikiwa ni pamoja na: kupatikana kwa eneo la
mradi, kule Likong’o mkoani Lindi; kuundwa kwa timu ya majadiliano na
imefanikisha kuandaliwa kwa hadidu za rejea, kupitia nyaraka muhimu zinazohusu
mradi (sera, sheria, mikataba, kanuni na mikakati ya Serikali); na kuanza kwa
majadiliano na kampuni zinazoshiriki katika mradi juu ya masuala
yatakayozingatiwa katika kuandaa mkataba kati ya makampuni husika na Serikali
(Host Government Agreement – HGA).
(v)
Uendelezaji wa Maeneo Maaalum ya
Kiuchumi
a. Kituo cha Biashara cha Kurasini: kiasi
cha fidia kilicholipwa kwa ajili ya kupata eneo la mradi ni Shilingi bilioni
101.04 na wananchi 1,019 tayari wamelipwa fidia na eneo hilo limetangazwa kwa
wawekezaji tangu Desemba, 2016.
b. Eneo Maalum la Uwekezaji la Bagamoyo: Hatua iliyofikiwa ni kulipwa fidia, ambapo
shilingi bilioni 26.6 zimetumika kulipa
fidia kwa wananchi 1,155 kati ya 2,273 wanaopaswa kupisha mradi kwenye
eneo la hekta 2,339.6. Kiasi cha Shillingi 51.3 bilioni kimebainishwa kuwa
kinahitajika kukamilisha malipo katika eneo lililothaminishwa. Aidha, kiasi cha
Shillingi billioni 81.45 kinakadiriwa kuhitajika kulipa fidia ili kupata eneo
la hekta 3,257 ambalo bado halijafanyiwa uthamini.
c. Eneo Maalum la Uwekezaji la Mtwara: Tayari
eneo la hekta 110 kati ya hekta 2600 za eneo lililotengwa kwa ajili ya Mtwara
SEZ limetangazwa kwa ajili ya matumizi ya bandari huru (Freeport Zone) na
tayari maandalizi ya kuweka miundombinu, hususan barabara, kwa eneo hilo
yanaendelea.
(vi)
Uanzishwaji wa Shamba la Miwa na
Kiwanda cha Sukari Mkulazi: Shilingi
Billioni 2 ziliwekezwa katika mradi huu. Hatua iliyofikiwa pamoja ni: kupima
ubora wa udongo; vitalu vya mbegu za miwa vimeandaliwa; na taratibu za kupata
huduma ya wataalam wa kufanya upembuzi yakinifu, uchunguzi wa mbegu za miwa,
upembuzi wa mazingira na utengenezaji wa barabara za kuingia katika eneo la mradi
zinaendelea.
(vii) Ununuzi na Ukarabati wa Meli Kwenye Maziwa Makuu: Hatua iliyofikiwa ni kuendelea na taratibu za ununuzi
wa ujenzi wa meli mpya kwa ajili ya usafirishaji wa abiria na mizigo katika
ziwa Victoria na ukarabati mkubwa wa Mv. Viktoria na Mv. Butiama. Kwa upande wa
Mv. Liemba katika ziwa Tanganyika, mjenzi amepatikana ambaye ni M/S LEDA
SHIPYARD. Kwa upande wa Ziwa Nyasa tayari meli mpya mbili za mizigo
zimetengenezwa na zimeshafanyiwa majaribio. Fedha zimetengwa katika bajeti ya
2016/17 kwa shughuli zote hizi.
12.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika
kutekeleza azma ya kujenga uchumi wa viwanda, mwelekeo umeanza kujipambanua
vizuri. Miradi ya viwanda mbalimbali imeanzishwa
kutokana na mchango wa sekta binafsi katika mikoa mbalimbali nchini, ambapo
mkoa wa Pwani unaongoza, ukiwa na jumla ya miradi mipya ya viwanda 82. Baadhi
ya miradi mikubwa iliyozinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi kwa mkoa wa Pwani ni
pamoja na:- viwanda viwili vya kutengeneza marumaru (tiles), ambavyo vitakuwa
vikubwa katika Afrika Mashariki na Kati vya Tywford Tiles (Chalinze) na
Goodwill Ceramic (Mkuranga), ambapo uzalishaji unategemea kuanza mwezi Aprili,
2017; kiwanda cha nondo cha Kiluwa Steel Industries Ltd (Mlandizi Pwani)
ambacho kimeanza uzalishaji; kiwanda cha Global
Packaging (Mailimoja Pwani) kimefunguliwa na kinafanya kazi; kiwanda cha Bahkresa
Food Product Ltd (Mkuranga) cha kutengeneza juisi ya matunda kimezinduliwa na
kinafanya kazi; kiwanda cha Elyven Agric Co. Ltd (Bagamoyo); kiwanda cha Juisi
cha Sayona Fruits Ltd (Mboga Pwani); kiwanda cha KEDS Tanzania Co. Ltd (Kibaha
Pwani). Serikali imekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia ujenzi wa viwanda
hivi, ikiwa ni pamoja na kusaidia upatikanaji wa ardhi, kuweka miundombinu
inayohitajika, na kutoa vibali vya ujenzi na pia vivutio. Aidha, Halmashauri na
Serikali za Mitaa katika maeneo haya zimekuwa na msaada na ushirikiano mkubwa
kwa wawekezaji ikiwemo kutoa maeneo ya viwanda ili kuhamasisha uwekezaji. Mathalan,
Maswa wameanzisha kiwanda cha kuzalisha Chaki cha Maswa Youth Enterprises Ltd
kwa utaratibu huo. Nitumie fursa
hii kuwapongeza kwa dhati viongozi wa mikoa, wilaya, halmashauri na Serikali za
Mitaa walioitikia kwa dhati wito wa Serikali kujielekeza katika kuvutia na
kuwezesha uwekezaji. Niwatake pia viongozi wote nchini kuiga mfano wa wenzao wa
mkoa wa Pwani.
13.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali pia kupitia mashirika yake mbalimbali imeanza
kuwekeza katika ujenzi wa viwanda, Mwitiko wa pekee na wa kupongezwa ni wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ambapo PPF na
NSSF wanashirikiana kuwekeza katika kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari
katika eneo la Mkulazi na Mbigiri (Morogoro); LAPF wanajenga machinjio ya
kisasa ya nyama (kwa Makunganya – Morogoro) na mifuko mingine inashiriki katika
miradi mabalimbali. Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) linashirikiana na sekta
binafsi kwa ajili ya uwekezaji katika eneo la viwanda la TAMCO – Kibaha kwa
uendelezaji wa viwanda vya nguo na uunganishaji wa magari na matrekta, ambapo
kiwanda cha kuunganisha matrekta kimefikia hatua ya kuanza majaribio. Aidha,
ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza mifuko/vifungashio umeanza. Hatua nyingine
zinazoendelea chini ya mashirika ya umma ni pamoja na jitihada za kufufua
Kiwanda cha General Tyre (Arusha); hatua za awali za uwekezaji katika mradi wa
uchenjuaji wa Magadi Soda (Bonde la Engaruka); na matayarisho ya kuanza kwa
ujenzi wa kituo cha Biashara na Huduma Kurasini (Dar es Salaam), ambapo tayari
makampuni mawili kutoka China yameonesha nia ya kujenga miundombinu ya majengo
ya viwanda (industrial sheds).
14.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, ujenzi wa uchumi wa viwanda unahitaji miundombinu ya
kuaminika. Kwa ajili hii Serikali imeendelea na utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya kuimarisha na kuboresha miundombinu na huduma za uchumi wa
viwanda. Miongoni mwa miradi hii ni: ujenzi wa msingi kwa ajili ya mtambo wa
kufua umeme wa Kinyerezi II (MW 240); ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kV
400 Iringa – Singida - Shinyanga (km
670); kV 220 Makambako – Songea (km
250); North West Grid kV 400 (Mbeya – Sumbawanga – Mpanda - Kigoma – Nyakanazi
km 1,148); usambazaji umeme Vijijini
na Makao Mkuu ya Wilaya (REA Turnkey Phase III), ambapo wateja 146,831 sawa na
asilimia 58.7 ya lengo wameunganishwa; ukarabati wa njia ya reli ya kati na
kuanza kwa taratibu za ujenzi wa reli ya kati kwa Standard Gauge na mkandarasi kwa ajili ya kusanifu na kujenga awamu
ya kwanza amepatikana; ununuzi wa ndege mbili (2) za Serikali na nyingine
kulipiwa malipo ya awali; kwa upande wa barabara mafanikio ni mazuri, ambapo
barabara ya Masasi – Songea – Mbambabay, sehemu ya Namtumbo – Tunduru (km 193),
na Tunduru – Mangaka – Mtambaswala (km 202.5) zimekamilika; kwa barabara ya
Ifakara – Mahenge Daraja la Kilombero limekamilika; ujenzi wa barabara ya
Dodoma – Babati (km 261) umefikia asilimia 86.4; kwa barabara ya Bagamoyo –
Msata na daraja la Ruvu chini imekamilika; barabara ya Kidahwe – Kasulu –
Kibondo – Nyakanazi ujenzi unaendelea na umefikia asilimia 16.4; na ujenzi wa
barabara za juu za TAZARA na Interchange
ya Ubungo umeanza.
15.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Kwa upande wa kufungamanisha
ukuaji wa viwanda na maendeleo ya watu Serikali inaendelea kutekeleza sera ya
elimumsingi bila malipo, uboreshaji wa miundombinu na huduma za ufundishaji na
kufundishia, ujenzi wa mabweni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
kutoa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo
Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Kampasi ya Mloganzila; na kukamilika kwa ukarabati wa vyuo vya ualimu
kumi. Aidha, katika kuimarisha ujuzi na stadi za kazi matayarisho ya Sera ya
Taifa ya Ajira ya mwaka 2017, Miongozo ya Mafunzo Kazini kwa vitendo kwa
wanafunzi (Apprenticeship Framework) na mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu
(Internship Framework) yamekamilika na kuingiwa kwa mikataba na viwanda vya
TOOKU Garment na Mazava Fabrics kwa ajili ya kutoa mafunzo ya stadi za ubunifu
na ushonaji wa nguo. Maeneo
mengine yaliyozingatiwa ni pamoja na kupanua upatikanaji wa maji mijini na
vijijini; huduma za afya na upimaji wa maeneo ya makazi.
16.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, maeneo mengine yaliyoendelea kutekelezwa ni yale
yaliyotoa fursa za ajira na ushiriki wa wananchi wengi katika shughuli za
uchumi wa viwanda, ikiwa ni pamoja na: kuandaliwa kwa program ya muda mrefu na
mfupi ya upimaji na umilikishaji wa ardhi hususan kwa matumizi ya kilimo;
kukamilika kwa ukarabati wa maghala 106 katika Halmashauri za Wilaya za Iringa,
Mufindi, Mbeya, Songea, Kalambo, Mbozi, Momba na Njombe; kuingizwa nchini kwa
tani 231,140 za mbolea; na tani 23,330 za mbegu bora zipo madukani kwa ajili ya
matumizi katika msimu huu wa kilimo.
17.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika Kuhamishia Shughuli za Serikali Kuu Dodoma: awamu ya kwanza imekamilika ambapo majengo ya ofisi za
wizara katika kipindi cha mpito na nyumba za makazi kwa baadhi ya viongozi
zimepatikana. TBA na CDA wanaendelea na kukamilisha kukarabati nyumba za makazi
na ofisi. Shirika la Nyumba la Taifa linajenga nyumba mpya 300 za makazi na
zinazotarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2017. Aidha, Serikali inaendelea na
mazungumzo na makampuni binafsi kutoka Switzerland, China na Zimbabwe na pia ya
ndani ambayo yameonesha nia ya kushiriki
katika ujenzi wa miundombinu ya maji kwa mji mpya wa Dodoma. Taasisi za
Serikali kama vile TBA, CDA, TANESCO, SUMATRA, TEMESA, TANROADS, TTCL na
Manispaa ya Dodoma zimekamilisha maandalizi ya awali ya kuboresha miundombinu
muhimu inayohitajika kuwezesha uendeshaji wa
Serikali bila vikwazo katika kipindi hiki.
Changamoto za Utekelezaji wa Mpango wa Mwaka 2016/17 hadi
Februari 2017
18.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, changamoto za
utekelezaji wa Mpango wa mwaka 2016/17 ni pamoja na ufinyu wa rasilimali fedha na matayarisho hafifu ya miradi. Aidha,
Serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hizo ikiwa ni
pamoja na kuziba mianya ya uvujaji wa mapato na kuhakikisha fedha zinazopatikana zinaelekezwa kwenye
miradi yenye tija; Vile vile, hatua za makusudi zimechukuliwa kuboresha
mazingira ya uwekezaji na uendeshaji biashara kwa wawekezaji ikiwa ni pamoja na
kuimarisha upatikanaji wa mikopo nafuu, kuhuisha Sheria, Kanuni, Taratibu
na kupunguza ada, kodi na tozo za uwekezaji na uendeshaji biashara.
B: MPANGO WA MAENDELEO WA MWAKA 2017/18
19.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2017/18 ni wa pili
katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 –
2020/21) na dhana yake kuu ni “Kujenga
Uchumi wa Viwanda ili Kuchochea Mageuzi ya Kiuchumi na Maendeleo ya Watu”.
Maandalizi ya Mpango huu yameshirikisha wadau mbalimbali ikijumuisha
Waheshimiwa Wabunge kupitia Mkutano wa Tano wa Bunge la 11 walipojadili
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18, Wizara, Idara, Taasisi za
Serikali, Taasisi za Utafiti na Elimu ya Juu, Sekta Binafsi na Washirika wa
Maendeleo.
20.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika mkutano tajwa, waheshimiwa wabunge walitoa maoni
na mchango mkubwa uliotuwezesha kuandaa Mpango huu. Miongoni mwa maoni mahsusi
ya Waheshimiwa Wabunge ni kuwa: Serikali ipunguze kukopa kutoka vyanzo vya
ndani; Kukamilisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa njia za
kielektroniki; Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge upewe kipaumbele; TRA iandae mapema awamu ya pili ya
ukusanyaji wa kodi ya majengo katika halmashuri na miji midogo iliyosalia;
kutenga fedha za kutosha kugharamia utekelezaji wa uamuzi wa Serikali kuhamia Makao
Makuu – Dodoma; kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato, hususan, bandari bubu na
biashara za magendo na kubuni vyanzo vipya vya mapato; kuboresha mazingira ya
uwekezaji na kufanya biashara; utekelezaji wa mkakati wa kujenga zahanati
katika kila kijiji na vituo vya afya kila kata; kuimarisha upatikanaji wa
madawa na vifaa tiba; kuongeza wigo wa fedha za mfuko wa maji; kuendeleza
maeneo ya viwanda vidogo, na maeneo mahsusi ya EPZ/SEZ; kutoa kipaumbele kwa
utekelezaji wa miradi ya makaa ya mawe - Mchuchuma na chuma - Liganga;
kuboresha elimu ya juu na kuongeza wigo wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi;
kuboresha miundombinu ya barabara; na kugharamia programu za kukabiliana na
athari za mabadiliko ya tabianchi.
21.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, maoni na ushauri wa wadau wengine ambao umezingatiwa
katika maandalizi ya Mpango huu ni pamoja na: Kuimarisha ufuatiliaji na
tathmini ya utekelezaji wa Mpango; kuendelea kuboresha mazingira wezeshi ya
kufanyia biashara, hususan, upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu na nafuu na miundombinu
msingi ya barabara, reli, bandari na nishati ya umeme; na kuboresha utoaji wa
huduma msingi za ustawi wa jamii zikijumuisha elimu, afya, maji, nyumba na
makazi bora, umeme vijijini na utunzaji wa mazingira.
22.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, kitabu cha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2017/18,
kimegawanyika katika sura kuu saba: Sura ya kwanza ni Utangulizi; Sura ya pili
ni mapitio ya Hali ya Uchumi Duniani, Kikanda na Kitaifa; Sura ya tatu ni
Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2016/17; Sura ya nne ni
Maeneo ya Vipaumbele katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18; Sura ya tano
ni Ugharamiaji wa Mpango; Sura ya sita ni usimamizi wa utekelezaji ikiainisha
Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji Taarifa; na Sura ya saba ni Vihatarishi vya
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo na Kinga.
Maeneo ya Kipaumbele 2017/18
23.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, ipo miradi iliyobainishwa kuwa ya kielelezo. Miradi hii
ni mahsusi kwa kuwa inatarajiwa kutoa matokeo makubwa kuendana na malengo ya
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wenyewe. Miradi hiyo ni:-
(i)
Ujenzi wa Reli ya Kati: ujenzi wa reli hususan sehemu
ya Dar es Salaam hadi Morogoro (km 205); kumpata mkandarasi wa kusanifu ujenzi
kwa maeneo ya Morogoro hadi Makutupora (Km 336), Makutupora hadi Tabora (Km
294), Tabora hadi Isaka (Km 133) na Isaka hadi Mwanza (Km 249); kupata maeneo
ya ardhi ya kuunganishia na kuanzishia treni ndefu kati ya Mpiji na Soga
(Pwani), Buhongwa (Mwanza), na Ihumwa (Dodoma) kwa ajili ya kituo kikubwa cha
treni za mizigo na makasha;
(ii)
Kuhuisha Shirika la Ndege Tanzania: kukamilisha malipo ya
ununuzi wa ndege 3;
(iii)
Chuma Liganga – Njombe: kuimarisha ufuatiliaji na
uratibu wa utekelezaji wa mradi ikiwa ni pamoja na kuratibu ulipaji wa fidia
kwa wananchi watakaopisha mradi; kupokea na kusafirisha mitambo, mashine na
vifaa vya mradi hadi eneo la mradi; uwezeshaji wa ujenzi wa njia ya umeme ya
Mchuchuma-Liganga, usimamizi wa ujenzi wa mgodi wa chuma na kiwanda cha chuma;
(iv)
Makaa ya Mawe Mchuchuma – Njombe: kusimamia ulipaji wa fidia
kwa wananchi watakaopisha mradi; kuratibu ununuzi, mapokezi na usafirishaji wa
mitambo, mashine, na vifaa kutoka bandarini hadi eneo la mradi; na kusimamia
ujenzi wa mgodi wa makaa ya mawe na kituo cha kufua umeme;
(v)
Uanzishwaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi: kuwezesha uanzishwaji wa
kanda maalum za kiuchumi za Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Ruvuma na Mtwara, ikiwa ni
pamoja na kusimamia ulipaji fidia; kufanya upembuzi yakinifu na kuandaa Mipango
Kabambe kwa uendelezaji wa miradi; kupima na kugawa viwanja kwa wawekezaji;
kuandaa nyaraka za kisheria na kupata hati miliki za maeneo ya mradi;
(vi)
Mradi wa Liquified Natural
Gas (LNG): kusimamia uhakiki wa thamani za mali za wananchi
watakaolipwa fidia ili kupisha mradi; kuandaa michoro ya maeneo na mpango kazi
wa kuwahamishia waathiriwa wa mradi; kuendesha majadiliano ya makubaliano baina
ya makampuni na Serikali (Host Government Agreement); na kuandaa wataalam
wazawa kwa ajili ya kuajiriwa na kuendesha shughuli za mradi; na
(vii)
Shamba la Kilimo na Uzalishaji Sukari Mkulazi: Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF
itaendelea na hatua za kuwekeza kwa ajili ya kilimo cha miwa kwa mashamba ya
Mkulazi na Mbigiri na ujenzi wa kiwanda cha sukari.
24.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutekeleza miradi mingine ya
kipaumbele, hususan, katika maeneo yafuatayo:
(a)
Ujenzi
wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda: eneo hili litahusisha miradi ya:-
Uendelezaji wa Eneo la Viwanda TAMCO - Kibaha; Kiwanda cha General Tyre –
Arusha; Mradi wa Magadi Soda – Bonde la Engaruka, Arusha; kuimarisha Mfuko wa
Taifa wa Maendeleo ya Wajasiriamali (NEDF); uendelezaji wa maeneo ya viwanda
vidogo katika mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Kigoma na Mtwara;
ujenzi wa ofisi za SIDO katika mikoa mipya; kuendeleza viwanda vya ngozi, pamba
hadi nguo na madawa na vifaa tiba nchini. Aidha, hatua za kuhamashisha uwekezaji
wa viwanda vinavyotumia malighafi inayopatikana kwa wingi nchini ikiwa ni
pamoja na nyama, maziwa, maji, misitu, chokaa, mawe urembo, gypsum na mazao ya vyakula na matunda.
(b)
Kufungamanisha
Uchumi na Maendeleo ya Watu: Miradi katika eneo hili ni ile inayolenga kuimarisha: Elimu na Mafunzo ya Ufundi hususan: ugharamiaji wa
Elimumsingi bila malipo; kutoa ruzuku na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu;
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi na Sekondari; ununuzi wa
vifaa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum; ukarabati na upanuzi wa
Maktaba ya Mkoa – Dodoma; na ujenzi wa Vyuo vitano vya VETA katika Mikoa ya
Geita, Simiyu, Njombe, Rukwa na Kagera. Afya na Maendeleo ya Jamii: hatua
zitaendelezwa za kuboresha Hospitali za Rufaa na mikoa; kuhakikisha upatikanaji
wa vifaa vya kisasa; kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na
vitendanishi katika hospitali, vituo vya afya na zahanati; kuongeza udhibiti wa
magonjwa ya kuambikiza; na kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI,
hususan kwa vijana. Hatua zingine ni pamoja na kupanua
upatikanaji wa Maji Safi, Usafi
wa Mazingira, na Kinga dhidi ya Mabadiliko ya Tabia nchi. Miradi ya
ujenzi, ukarabati na upanuzi wa huduma za maji Vijijini; kuboresha Huduma za
Maji katika Jiji la Dar es Salaam; mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda
Kahama, Nzega, Igunga, Tabora hadi Sikonge; ujenzi, ukarabati na upanuzi wa
huduma za maji mijini na vijijini; na kutoa maji mto Ruvuma kwenda Manispaa ya
Mtwara-Mikindani; kujenga na kuimarisha hifadhi ya vyanzo vya maji na misitu,
upandaji miti, uvunaji wa maji, kuhimiza matumizi ya teknologia jadidifu na
hifadhi ya mazingira.
(c)
Mazingira
Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara: kazi zitakazotekelezwa ni pamoja
na kuendelea na utekelezaji wa miradi inayoendelea katika eneo hili; ukarabati
wa miundombinu ya reli; miradi ya barabara na madaraja ikijumuisha barabara ya
Kidahwe – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi, Manyoni – Tabora – Uvinza, Tabora –
Koga – Mpanda, barabara za juu za TAZARA na
Ubungo Interchange. Daraja la
Selander na miundombinu ya mabasi
yaendayo haraka (awamu ya II, III na IV) jijini Dar es Salaam. Aidha, miradi ya
bandari ikijumuisha bandari za Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Bagamoyo, na
bandari kavu ya Ruvu na bandari za Maziwa Makuu (Victoria, Tanganyika na
Nyasa). Kwa usafiri wa anga ni kuendelea na ujenzi wa jengo la
abiria (terminal III) katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere;
upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma, Tabora, Mwanza; ujenzi na ukarabati wa
viwanja vya ndege vya Geita; Sumbawanga, Shinyanga, Mtwara, Musoma, Iringa na
Songea; na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa Kilimanjaro.
(d)
Maeneo
Mengine Muhimu: hatua za
kuimarisha mitaji na kutumia benki za ndani za maendeleo (TIB na TADB) kama vyombo
vya kupanua upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu na nafuu kwa wawekezaji; eneo
hili linajumuisha miradi ya kuendeleza na kusimamia matumizi ya ardhi, maendeleo ya nyumba na makazi; ushirikiano wa kikanda na kimataifa; utawala bora na kuimarisha
utawala wa sheria.
(e)
Kuhamishia
Shughuli za Serikali Kuu Makao Makuu Dodoma: katika mwaka 2017/18 Serikali itaendelea na utekelezaji wa
azma ya kuhamishia shughuli za Serikali makao makuu Dodoma. Katika utekelezaji
wa azma hii, Wizara zimeelekezwa kutenga fedha za kugharamia stahiki za
watumishi kwa kutumia ukomo wa bajeti uliotengwa kwenye mafungu yao. Ofisi ya
Waziri Mkuu inaendelea kuratibu upatikanaji wa maeneo ya kujenga ofisi na
nyumba za viongozi wa Serikali kwa kuzingatia mahitaji na maboresho ya mpango wa
ardhi katika mji wa Dodoma.
25.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali imeweka bayana imani yake katika mchango wa
sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. Lakini pia kuwa ushirikiano
wake utakuwa kwa sekta binafsi ya kweli na yenye kufuata sheria na taratibu za
nchi. Katika mwaka 2017/18, Serikali
itaendelea kujenga mazingira wezeshi ili kuchochea ushiriki na maendeleo ya
sekta binafsi, hususan, sekta binafsi ya ndani, katika utekelezaji wa Mpango na
ujenzi wa viwanda. Kwa ajili hii, Serikali itaendelea kuboresha kanuni,
taratibu na mifumo taasisi ya usimamizi wa biashara na uwekezaji nchini. Kwa
kuzingatia hili, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja
na:
(i)
Kuweka sera, sheria na
taratibu zinazochochea ushiriki wa sekta binafsi, ama kuwekeza moja kwa moja au
kwa ubia na sekta ya umma;
(ii)
Kutenga maeneo ya
uwekezaji ili kupunguzia sekta binafsi usumbufu hususan upatikanaji wa ardhi
ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo mahsusi ya uwekezaji (EPZ, SEZ na kuanzisha land bank chini ya TIC), na kuyawekea maeneo
hayo miundombinu msingi, na kuikodisha kwa wawekezaji kwa gharama nafuu;
(iii) Kujenga miundombinu wezeshi (barabara, umeme, maji na
reli) na kuifikisha katika maeneo ya shughuli za wawekezaji;
(iv)
Kusimamia utekelezaji wa
sheria na taratibu na kuhakikisha kuwepo kwa amani na usalama;
(v)
Kuanzisha mifuko maalum
ya kuchochea ushiriki wa sekta binafsi, kwa mfano SAGCOT Catalytic Fund na PPP Facilitation Fund;
(vi)
Kuboresha huduma kwa
wawekezaji, ikiwa ni pamoja na kuanzisha “one stop centre” chini ya TIC,
bandari ya Dar es Salaam na vituo vya utoaji huduma ya pamoja mipakani (one
stop border post); na
(vii) Kuweka utaratibu utakaoboresha upatikanaji wa mikopo ya
muda mrefu kwa gharama nafuu ikiwa ni pamoja na kuimarisha mitaji ya benki
maalum za maendeleo (TADB) na (TIB).
Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji wa Taarifa
27.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vihatarishi mbalimbali ambavyo vinaweza kuathiri
utekelezaji wa miradi ya maendeleo, vya ndani na nje. Baadhi ya vihatarishi vya
nje ni pamoja na: mitikisiko ya kiuchumi, kikanda na kimataifa; majanga asilia
na athari za mabadiliko ya tabianchi; na mabadiliko ya kiteknolojia. Kihatarishi
kikuu cha ndani ni ufinyu wa rasilimali fedha na watu.
28.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau itakabiliana na
vihatarishi kwa kuchukua hatua zifuatazo:- kupunguza utegemezi kwa kuwianisha
mapato na matumizi, kuongeza mapato ya ndani; kuboresha mazingira ya biashara;
na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Mpango na namna bora ya utekelezaji
ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi.
SEHEMU YA TATU
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2016/17 NA
MAPENDEKEZO YA KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2017/18
A: TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA
BAJETI YA MWAKA 2016/17
Mwenendo
wa Mapato na Matumizi ya Serikali Hadi Februari 2017
29.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Februari 2017,
mapato kutoka vyanzo vyote yalifikia sh. bilioni 15,372.4 sawa na asilimia 79
ya lengo la kipindi hicho. Kati ya hizo:
(i)
Mapato ya kodi yalifikia
shilingi bilioni 9,306.0 sawa na asilimia 95 ya lengo la kukusanya shilingi
bilioni 9,764.2;
(ii)
Mapato yasiyo ya kodi
yalifikia shilingi bilioni 1,305.7 sawa na asilimia 72.5 ya lengo la kukusanya
shilingi bilioni 1,806.2;
(iii)
Mapato ya Mamlaka za Serikali
za Mitaa yalikuwa shilingi bilioni 310.6 sawa na asilimia 70 ya lengo la
kukusanya shilingi bilioni 443.6;
(iv)
Mikopo ya ndani ilifikia shilingi
bilioni 3,506.7 sawa na asilimia 78 ya makadirio ya shilingi bilioni 4,479.6
katika kipindi hicho; na
(v)
Misaada na mikopo nafuu kutoka
kwa Washirika wa Maendeleo ilikuwa
shilingi bilioni 1,253.6, sawa na asilimia 40 ya lengo la kipindi hicho la
shilingi bilioni 3,117.2.
30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo kingine ambacho kilitarajiwa kuipatia Serikali fedha za
utekelezaji wa bajeti ni mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara. Katika
mwaka 2016/17, Serikali ilipanga kukopa fedha kutoka kwenye vyanzo vya kibiashara
kiasi cha shilingi bilioni 2,100.9 ili kugharamia miradi mbalimbali ya
maendeleo. Hata hivyo, hadi kufikia Februari, 2017 Serikali haikuweza kukopa
kutoka katika chanzo hiki kutokana na hali ya soko la fedha la kimataifa
kutokuwa nzuri hasa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2016/17. Katika
kipindi hicho, riba ilipanda kutoka wastani wa asilimia 6 hadi wastani wa
asilimia 9. Kutokana na sababu hiyo, Serikali iliahirisha mchakato wa kukopa
kutoka kwenye masoko hayo. Hata hivyo, gharama za ukopaji katika masoko ya
Ulaya imeanza kuimarika, ambapo hadi sasa Serikali imesaini mkataba na Kuwait Fund wa dola za Marekani milioni 51 kwa
ajili ya ujenzi wa barabara ya Chaya – Nyahua. Vile vile, Serikali itasaini hivi
karibuni mkataba na OPEC Fund wa dola za Marekani milioni 18 na Abudhabi Fund
for Development (ADFD) wa dola za Marekani milioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Uvinza – Ilunde
– Malagarasi. Aidha, Serikali ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na
taasisi mbalimbali za kifedha ili kupata fedha za kugharamia miradi ya
maendeleo. Baadhi ya taasisi hizo ni Credit Suisse ya Uingereza (dola za
Marekani milioni 300) na majadiliano yanaendelea na benki ya Barclays, HSBC na
Citi Bank kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria katika Uwanja wa Ndege
wa Julius Nyerere ambao unatarajia kugharimu Euro milioni 121.
31.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai, 2016 – Februari, 2017 jumla ya shilingi
bilioni 16,152.5 zilitolewa kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za
Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni
12,177.1 zilizotolewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikijumuisha makusanyo ya
Halmashauri shilingi bilioni 126.3. Aidha, shilingi bilioni 3,975.4 zilitolewa kwa
ajili ya matumizi ya maendeleo ikijumuisha makusanyo ya Halmashauri shilingi
bilioni 177.6.
32.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za matumizi ya kawaida zilizotolewa zinajumuisha shilingi bilioni
4,266.9 kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi wa Serikali, shilingi bilioni
6,135.0 kwa ajili ya mahitaji ya Mfuko Mkuu wa Serikali na shilingi bilioni
1,775.1 za Matumizi Mengineyo. Fedha za maendeleo zilizotolewa zinajumuisha shilingi
bilioni 3,103.6 kama fedha za ndani na shilingi bilioni 871.8 fedha za nje sawa
na asilimia 34 ya bajeti yote ya maendeleo.
Changamoto za Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2016/17 hadi
Februari 2017
33.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, changamoto za
utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka 2016/17 ni pamoja na:
(i)
Mwamko mdogo wa kulipa
kodi na hususan kuzingatia matumizi ya mashine za kielektroniki;
(ii)
Kuchelewa kupatikana kwa
mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka nje; na
(iii)
Majadiliano ya muda mrefu
yaliyopelekea kuchelewa kupatikana kwa fedha za Washirika wa Maendeleo.
34.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto hizo ni
pamoja na:
(i)
Kusimamia dhana ya kulipa kodi kwa hiari kupitia udhibiti
wa matumizi ya mfumo wa EFDs;
(ii)
Kuendelea na majadiliano
baina ya Serikali na Washirika wa Maendeleo ili kuhakikisha fedha za misaada na
mikopo nafuu zinapatikana kama zilivyoahidiwa. Ili kupata suluhu ya kudumu,
Serikali kwa sasa inafanya tathmini ya ushirikiano na Washirika wa Maendeleo
kazi ambayo inayoongozwa na aliyekuwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Hatua hii inatarajia kuimarisha ushirikiano na kuwezesha upatikanaji wa fedha
za uhakika katika bajeti ya Serikali;
(iii)
Kuendelea kutoa elimu juu ya umuhimu na faida za kulipa
kodi kwa kutumia mitandao ya kielektroniki. Aidha, Wizara, Idara
zinazojitegemea na Wakala za Serikali
zinahimizwa kutumia mabenki katika kukusanya maduhuli.
(iv)
Kuendelea kusisitiza nidhamu katika utekelezaji wa bajeti
kama ilivyoidhinishwa kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015;
(v)
Kuendelea kuwianisha mapato na matumizi kwa kuhakikisha
kuwa mgawo wa fedha utaendana na upatikanaji wa mapato; na kuendelea kuchukua hatua za kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
B: SERA
ZA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2017/18
35.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika mwaka 2017/18, mapato ya ndani ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kupunguza
nakisi ya bajeti. Malengo ya mwaka 2017/18 ni: kuongeza mapato
ya ndani hadi kufikia asilimia 15.9 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18; Kuongeza
mapato ya kodi kufikia asilimia 14.1 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18; na
kupunguza nakisi ya bajeti kutoka asilimia 4.5 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17
hadi asilimia 3.8 mwaka 2017/18. Katika kutekeleza hili,
Serikali imedhamiria kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa
kuchukua hatua zifuatazo:
(i)
Kuendelea kusimamia kikamilifu
matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ili
kuongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato;
(ii)
Kuendelea kupanua wigo wa
walipa kodi;
(iv)
Kupanua wigo wa kukusanya mapato yatokanayo na kodi ya majengo; na
(v)
Kuendelea kuchukua hatua za
kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija.
36.
Mheshimiwa mwenyekiti, katika mwaka 2017/18, Serikali itaendelea kupanua soko la fedha la
ndani (domestic financial markets) ili kuwa na washiriki wengi kutoka ndani na
nje ya nchi kwenye soko watakaowezesha Serikali kupata fedha za kuziba nakisi
kwenye bajeti bila kulipa riba kubwa. Kuhusu fedha za nje, serikali
itahakikisha kuwa mchakato wa upatikanaji wa fedha za mikopo yenye masharti ya
kibiashara unaharakishwa kwa kuzingatia maslahi ya Taifa na kuhakikisha fedha
zitakazopatikana zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo. Aidha, serikali
itaboresha utaratibu wa mashauriano na majadiliano na Washirika wa Maendeleo
ili kuhakikisha kuwa fedha zinapatikana kama zilivyoahidiwa na kwa wakati. Kwa
sasa Serikali inafanyia kazi mapendekezo yaliyomo katika taarifa ya washauri elekezi
walioongozwa na Bwana Donald Kaberuka
aliyekuwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kuhusu namna bora zaidi ya
kushirikiana na Washirika wa Maendeleo.
37.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matumizi, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya
fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015. Lengo kuu
ni kupunguza matumizi yasiyo na tija, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma
na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi ya maendeleo.
C: MAPENDEKEZO YA KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI
YA SERIKALI KWA MWAKA 2017/18
Mapato
38.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura ya Bajeti ya mwaka 2017/18 inaonesha kuwa jumla ya shilingi bilioni
31,699.7 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho. Jumla ya
mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri yanatarajiwa kuwa shilingi
bilioni 19,977.0 sawa na asilimia 63.0 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo,
mapato ya kodi ni shilingi bilioni 17,106.3 sawa na asilimia 85.6 ya mapato ya
ndani. Aidha, mapato yasiyo ya kodi na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri ni shilingi
bilioni 2,183.4 na shilingi bilioni 687.3 kwa mtiririko huo. Ili kuhakikisha
upatikanaji wa mapato hayo, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa mapato
na kuziba mianya ya uvujaji wa mapato.
39.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh. bilioni 3,971.1 ambayo
ni asilimia 12.6 ya bajeti yote. Misaada na mikopo hii inajumuisha fedha kwa ajili
ya miradi ya maendeleo; mifuko ya pamoja ya kisekta; na ya kibajeti (GBS).
Aidha, Serikali inatarajia kukopa Sh. bilioni 6,156.7 kutoka soko la ndani.
Kati ya kiasi hicho sh. bilioni 4,948.2 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na
dhamana za Serikali zinazoiva (rollover) na kiasi cha Sh. bilioni 1,208.4 sawa
na asilimia moja ya Pato la Taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia
miradi ya maendeleo. Ili kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu, Serikali
inatarajia kukopa sh. bilioni 1,595.0 kutoka soko la nje kwa masharti ya
kibiashara.
Matumizi
40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa upande wa matumizi, katika mwaka 2017/18, Serikali inapanga kutumia shilingi
bilioni 31,699.7 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi
bilioni 19,700.2 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha shilingi
bilioni 7,205.8 za mishahara ya watumishi wa Serikali na taasisi na shilingi
bilioni 9,461.4 kwa ajili ya kulipia deni la Taifa. Bajeti ya kulipia deni la
Taifa imeongezeka kwa asilimia 18.3 kutoka shilingi bilioni 8,000 mwaka 2016/17
kutokana na kuiva kwa mikopo ya miaka ya nyuma iliyogharamia miradi ya
maendeleo ambayo fedha za kulipia mtaji
na riba zimetengwa kwenye bajeti ya matumizi ya kawaida. Matumizi mengineyo
(OC) yametengewa jumla ya shilingi bilioni 3,033 ambapo kiasi cha shilingi
bilioni 2,085.2 ni matumizi yaliyolindwa na shilingi bilioni 274.9 ni matumizi
yanayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri. Aidha, matumizi ya maendeleo
yatakuwa shilingi bilioni 11,999.6 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 8,969.8 ni
fedha za ndani na shilingi bilioni 3,029.8 ni fedha za nje.
41.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2017/18, Serikali imeendelea kutenga fedha nyingi kwenye miradi
ya maendeleo kama ilivyoanishwa katika
Awamu ya Pili ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo 2016/17 – 2020/21. Katika
sura ya tano ya Mpango huo ambao ulipitishwa na Bunge, bajeti ya maendeleo
inatakiwa kuwa kati ya asilimia 30 hadi asilimia 40 ya bajeti yote. Hivyo,
fedha zilizotengwa katika bajeti ya maendeleo zimeongezeka kutoka shilingi
bilioni 11,820.5 mwaka 2016/17 hadi shilingi bilioni 11,999.6 kwa mwaka 2017/18,
sawa na asilimia 38 ya bajeti yote. Ongezeko hili limezingatia misingi ya
kibajeti pamoja na masuala mbalimbali kama ifuatavyo:
(i)
Kukamilika kwa baadhi ya
miradi ya maendeleo kama vile Chuo Kikuu
cha Afya Muhimbili – Kampasi ya Mloganzila ambayo inahitaji kutengewa fedha za
uendeshaji badala ya fedha za maendeleo;
(ii)
Kuendelea kutenga fedha katika
miradi inayoendelea kama vile ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge ambao katika mwaka
2016/17 ulitengewa shilingi trilioni moja na kwa mwaka 2017/18 umetengewa
shilingi bilioni 800 kulingana na mahitaji ya hatua ya ujenzi itakayoweza
kutekelezwa katika kipindi hicho (absorptive capacity);
(iii)
Kuzingatia viwango vya
mikataba katika miradi mbalimbali kama vile ununuzi wa ndege ambapo Serikali ilitenga
kiasi kikubwa cha fedha katika bajeti ya mwaka 2016/17 kugharamia ununuzi wa
ndege mbili za Serikali na kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa ndege 4. Kiasi
kilichobaki kitalipwa kwa awamu katika bajeti ya mwaka 2017/18 na 2018/19
kulingana na viwango vya mikataba; na
(iv)
Kuendelea kupunguza mikopo ya
masharti ya kibiashara ili kutekeleza azma ya Serikali ya kuongeza mapato ya
ndani na kupunguza nakisi ya bajeti ambayo kwa mwaka 2017/18 inakadiriwa
kufikia asilimia 3.8 kutoka asilimia 4.5 mwaka 2016/17 na hivyo kuendelea
kuimarisha uhimilivu wa deni la Taifa.
42.
Mheshimiwa Mwenyekiti,. kwa kuzingatia maelezo hayo, kiwango na ukomo wa bajeti kwa mwaka
2017/18 ni kama inavyooneshwa katika Jedwali
Na. 1.
Jedwali Na. 1: Mfumo wa Bajeti ya
Mwaka 2017/18
HITIMISHO
43.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya kiwango na ukomo wa Bajeti ya mwaka
2017/18 yanalenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kuondoa vikwazo
vya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya viwanda. Aidha, Serikali itaendelea kujizatiti
katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuendelea kudhibiti mianya ya ukwepaji
wa kodi. Vile vile, Serikali itaendelea
kuweka mkazo katika usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma ili
zitumike katika uwekezaji wa miundombinu ya umma na uboreshaji wa huduma
za kijamii kwa lengo la kuleta maendeleo ya haraka. Suala hili linahitaji
ushirikiano wa karibu wa wadau wote kwa kulipa kodi na kuwafichua wakwepa kodi.
44.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zinazopendekezwa katika
Mpango huu zinalenga katika kujenga msingi madhubuti wa uchumi wa viwanda na
kupanua fursa za ajira na biashara. Dhamira yetu sote ni kufikia kiwango cha
uchumi wa kipato cha kati ifikapo 2025. Ili kushiriki katika mafanikio tarajiwa,
kila mmoja wetu sharti ashiriki katika shughuli yoyote ya uzalishaji na afanye
hivyo kwa juhudi na ufanisi ili kuleta tija. Kwa kila tunachokizalisha katika
shughuli msingi (primary production) za kilimo, mifugo, uvuvi, madini na misitu
hakina budi kuongezewa thamani. Kwa kufanya hivi tutakuwa tumewajumuisha
wananchi wengi katika mkondo wa uchumi wa kimataifa na mnyororo wa thamani kuwawezesha
kuboresha maisha yao kwa kasi zaidi. Watanzania tukiwa na nia na kufanya
jitihada, jambo lolote linawezekana na kila kitu kiko ndani ya uwezo wetu.
45.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwashukuru wananchi, mashirika ya umma na sekta
binafsi kwa mwitikio wao walioonesha kwa kutekeleza kwa dhati azma ya Serikali
ya kujenga uchumi wa viwanda. Mwitikio huu unatuhakikishia kuwa tutaweza.
Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi hizi kwa kufanya kila linalowezekana
kuboresha mazingira ya uwekezaji na uendeshaji biashara. Aidha, Serikali itaendelea kudumisha majadiliano na
ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi kuhusu mwenendo wa uchumi,
utungaji sera na wajibu wa kila upande katika utekelezaji wa mpango na bajeti
ya Serikali.
46.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha
Comments
Post a Comment