Featured Post

LOWASSA ALIPOGOMA KUJIVUA GAMBA, AKAKWEPA KUZUNGUMZIA. SOMA HOTUBA YAKE KWA WANAHABARI ALIYOITOA MONDULI, OKTOBA 19, 2011



Edward Ngoyayi Lowassa akiwa na Sophia Simba

JUMATANO Oktoba 19, 2011 aliyekuwa Mbunge wa Monduli na kada maarufu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Edward Ngoyayi Lowassa, alizungumza na waandishi wa habari mjini Monduli.
Katika mkutano huo ambao ulifanyika huku mambo yakiwa hayaendi sawa kwake na makada wenzake ndani ya Chama, Lowassa aligoma kabisa kuzungumzia suala la 'kujivua gamba', uamuzi ambao ulikuwa umeanzishwa na Mwenyekiti wa CCM wa wakati huo, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, katika harakati za kukinusuru chama kutokana na kashfa mbalimbali zikiwemo za ufisadi.

Lowassa pia aligoma kabisa kuzungumzia kashfa za Richmond/Dowans/Simbion kwa maelezo kwamba angezungumzia wakati mwingine.
Hatua ya CCM kuwawajibisha viongozi na makada wa chama hicho ikiwemo kuwaonya, kuwavua madaraka na wengine kuwafukuza uanachama kwa kiasi kikubwa imechangiwa na msimamo wa wanachama hao kuwa na 'mahaba' na kambi ya Lowassa, hasa baada ya waziri mkuu huyo wa zamani kuenguliwa katika kinyang'anyiro cha kugombea urais mwaka 2015.
Wengi walitegemea kwamba mkutano huo wa Monduli ungekuwa wa kulipua bomu ikiwemo pengine kutangaza kujivua gamba, lakini haikutokea hivyo.
Maswali yote ya kichokonozi ya waandishi yaligonga mwamba, na akaahidi kwamba angeyazungumzia lakini kwa siku hiyo haukuwa wakati wake, hali iliyowafanya waandishi hao wamuulize kama alikuwa 'ametishwa' ndiyo maana hakutaka kuyazungumzia, lakini akayajibu baadhi yake ambayo yalikuwa nje ya hotuba yake rasmi.

Akazungumzia kuhusu ajira na kusema: "Si kama napuuza jitihada za serikali juu ya suala la ajira kwa vijana, lakini hali ni mbaya sana. Nashauri tuvunje kanuni, serikali ikope fedha na ijenge viwanda tuweze kuwaajiri Watanzania wengi. Fedha zipo!"


Kuhusu suala la urais wa 2015, akasema; "Hata mimi nashangaa, miaka bado sana, kwanini tuanze kuongelea urais wa 2015? Waandishi acheni propaganda, msipoandika chokochoko hizi hakuna atakayehangaika nazo. Mitikisiko ndani ya CCM ni ya muda tu, tutapita katika hali hii."

Akaonya kuhusu vyombo vya habari vilivyokuwa vikimchafua: "Naomba vyombo vya habari tusaidie nchi yetu. Tunapoandika propaganda za chuki kwa nia ya 'kulipuana' tujue tunalipeleka taifa kubaya. Sasa niseme rasmi, IMETOSHA. Sitaendelea kuvumilia kuchafuliwa na vyombo vya habari. Nitachukua hatua kali dhidi ya magazeti yatakayonichafua na vyombo vya habari vyote vinavyonichafua. Ukinichafua nitakupeleka kwenye vyombo husika na niseme uhuru usio na nidhamu ni fujo. Uhuru wa vyombo vya habari umekuwa 'abused' sana.
"Gazeti fulani linaloniandama lilishafikia hatua ya kusema ndo nahusika na maasi ya vijana wa UVCCM, ni uwongo na wala sihusiki kwa namna yoyote na vijana wa Arusha. Nilikuwa nje kwa matibabu, ningejuaje nini wanapanga vijana?
"Sijakutana na rais Kikwete barabarani, waache kunichonganisha naye na waache kunichafua mbele za watanzania. Walishasema eti nagombea urais mwaka 2010. Naamini hata Rais Kikwete anajua kuwa huu ni uzushi tu.
"Masuala ya Chama huwa yanaishia kwenye vikao, hii ya kubomoana nje ya vikao hayana maana. Siwezi kukihujumu chama changu mwenyewe. Kuna waliofikia kudai eti namhujumu Mhe. Rais. Wengine eti nina mpango wa kumpindua kwenye Halmashauri Kuu ijayo. Sina mpango wa hujuma na hata mabaya ya Rais Kikwete siyafahamu. Toka nilipojiuzulu uwaziri mkuu nilikaa kimya, kimya ni hekima toka kwa Mwenyezi Mungu."
MaendeleoVijijini inakuletea hotuba kamili ya Lowassa aliyoitoa wakati huo mjini Monduli:

NDUGU wana habari nimewaita katika mkutano huu leo kwa sababu moja kubwa, kutoa ufafanuzi kuhusu matukio ambayo yamekuwa yakitokea huku yakinihusisha mimi binafsi kwa namna ambayo sasa yanatishia ustawi na mshikamano wa kimaadili, kihistoria na kikazi miongoni mwa viongozi na baina ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).



Ndugu wana habari, naamini mmekuwa mkifuatilia kwa karibu habari zinazoripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari zinazolihusisha jina langu na harakati kadha wa kadha chafu ambazo hata mimi mwenyewe ninayehusishwa nazo huwa nazisikia na kuzijua baada ya kuwa zimesharipotiwa katika vyombo hivyo vya habari.



Uamuzi wangu wa kukutana nanyi leo hauna makusudi ya kuzozana na vyombo vya habari wala kwenda kinyume na utamaduni wa kimaadili wa ndani ya chama changu unaotutaka viongozi kujadili masuala yanayokihusu chama chetu ndani ya vikao vyetu rasmi vya kimaamuzi bali kutoa ufafanuzi na angalizo kwa pande zote hizo mbili ambazo zinaguswa na matukio yanayoendelea kutokea leo hii.



Moja ya mambo ambayo yameligusa jina langu kwa namna hiyo ni lile linalonihusisha eti na kundi moja la wanasiasa ambao wamekuwa na mikakati ya kumhujumu mwenyekiti wetu wa chama, Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete. Hakuna shaka ni madai ya kipuuzi, kizushi na yenye malengo machafu.



Hawakuishia hapo sasa wamefikia hatua ya kuvitumia vyombo hivyo hivyo vya habari na kufikia hatua ya kudai kwamba nimeanza kuandaa orodha ya kile wanachokiita madhambi ya Rais Kikwete ambayo wanadai nimepanga kuyasoma wakati wa kikao kijacho cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (CCM).



Ninaamini kwa dhati kabisa kwamba, waandishi wa habari wanaofuatilia kwa karibu na kwa umakini mwenendo wa masuala ya kisiasa nchini wanatambua kwamba, watu wanaopenyeza taarifa hizi katika vyombo vya habari wanafanya hivyo kwa malengo ya kufikirika ya kujisafishia njia kisiasa.



Ni jambo lisiloingia akilini kunihusisha na kile kinachoitwa mikakati ya kumhujumu rais au chama ambacho mimi ni kada wake wa muda mrefu, mbunge anayetokana na chama hicho hicho na mtu ninayeiongoza Kamati nyeti ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na zaidi ya yote kiongozi wa ngazi mbalimbali za kisiasa na kiserikali nilizowahi kushikilia.



Kuhusu hili napenda kusema kwa uwazi kwamba, mbali ya ukweli kuwa sijapata kufikiria hata mara moja kuhusu hicho wanachokiiita mabaya au madhambi ya rais, sina na wala siijui hiyo wanayoitaja kuwa ni orodha ya mabaya ya namna yoyote dhidi ya Rais Kikwete.



Mbali ya ukweli kwamba huo ni uongo wa wazi, silika yangu kama mwanasiasa na mtu mwenye dhamana kubwa kwa watu wa Monduli na kwa taifa langu haiwezi kamwe kunituma nianze kupanga mikakati ya kumhujumu kiongozi wetu mkuu au chama ambacho kimenilea na mimi mwenyewe nikakitumikia kwa uadilifu na kwa juhudi kubwa pengine kuliko ilivyo kwa hao wazushi.



Ndugu wana habari, nitakuwa ni mtu wa mwisho kufikiria au kupanga kumhujumu mwenyekiti wetu wa chama na rais ambaye nimemuunga mkono kwa dhati kwa muda mrefu na kushirikiana naye katika harakati nyingi za kifikra na za kiuongozi katika ngazi mbalimbali na kwa miaka mingi. Nilipata kulisema hili na leo nalirudia tena. Mimi na na Rais Kikwete hatukukutana barabarani.



Tangu serikali ya Awamu ya Nne iingie madarakani kuna kundi la watu limekuwa likifanya juhudi kubwa kunigombanisha na Rais wakitumia kila aina ya hoja za kupikwa.



Kundi hilo ambalo sasa limekuja na uzushi mpya, ndilo ambalo mwaka juzi lilipenyeza ndani ya chama chetu na katika jamii hoja kwamba nilikuwa nimejipanga kugombea urais kwa tiketi ya chama chetu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, likidai kwamba nilikuwa na malengo ya kumpinga Rais Kikwete ambaye wakati huo alikuwa ndiyo kwanza anaelekea kukamilisha ngwe yake ya kwanza madarakani.



Katika kuthibitisha kwamba watu hao walikuwa na hila, nilipohojiwa na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam miezi kadhaa kabla ya Uchaguzi Mkuu nilijibu kwa kifupi nikisema, hatutukutana na Rais Kikwete barabarani.



Nayasema haya na kurejea baadhi ya mambo huku nikiwa na imani ya dhati kabisa kwamba, viongozi wenzangu ndani ya CCM na wale walio na nia njema na chama chetu na taifa hili, akiwapo Mwenyekiti wetu wa Taifa, Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete hawawezi kamwe kuamini au kushawishiwa na propaganda chafu zinazoendeshwa na kikundi kidogo cha wanasiasa hao kwa zaidi ya miaka mitatu sasa ambao malengo yao ya kisiasa yako wazi na yanayojulikana.



Kama hiyo haitoshi, wanasiasa hao hao baada ya kulitumia jina langu kama ajenda yao ya uzushi wa kila namna, sasa wameanza kunihusisha hata na matukio ya kisiasa kama yale yaliyotokea majuzi tu hapa Arusha.



Ndugu wana habari baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu sasa, nimeamua kuanza kuchukua hatua mbalimbali za kisiasa na kisheria ambazo naamini zitatoa majibu sahihi dhidi ya wale wote walio nyuma ya ajenda hizi chafu kwa lengo la kuweka kumbukumbu sawia ndani ya chama changu na kwa jamii nzima ya Watanzania ambao kwa muda mrefu wamelishwa mambo mengi ya kizushi na wakati mwingine ya hatari dhidi yangu.



Tayari nimepanga kuanza kuwasiliana na kuwasilisha malalamiko yangu kwa mamlaka husika zinazosimamia mienendo ya kimaadili na weledi wa kitaaluma wa vyombo vya habari kama vile Msajili wa Magazeti na Baraza la Habari Tanzania.



Kama hiyo haitoshi, baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu nimeshaanza kufikiria na kujipanga kuanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandishi wa habari na wahariri ambao kwa makusudi wameamua kutumia vibaya uhuru wa habari ambao serikali imeutoa. Naamini sote tunakubaliana kuwa; ‘UHURU USIO NA NIDHAMU NI FUJO.'



Ndugu zangu wana habari napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa viongozi wa chama na wale wa serikali kumsaidia rais na chama chetu kwa kutimiza ipasavyo wajibu wao badala ya baadhi yao tena wakiwamo wale wenye dhamana nyeti kuwa vinara wa kutunga mambo ya kufikirika kama haya wanayofanya leo.



Viongozi wenye mawazo ya namna hiyo wanapaswa kutambua kwamba, muda adhimu wanaoutumia kubuni na kuzusha uongo kila kukicha mbali ya kuwavunjia heshima wao wenyewe unavidhalilisha vyombo vya dola ambavyo vinafanya kazi kubwa kuhakikisha hujuma za namna yoyote dhidi ya viongozi na taifa zinadhibitiwa.



Nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ya Bunge na mtu aliyepata kuwa Waziri Mkuu ninatambua na kuiheshimu kwa dhati kazi hiyo kubwa inayofanywa kwa weledi mkubwa na taasisi mbalimbali za dola zenye wajibu wa kuhakikisha ulinzi na usalama wa viongozi wetu na taifa kwa ujumla.



Ndugu wanahabari nazungumza nanyi baada ya kurejea nikitokea katika nchi za Nigeria, Malaysia, Singapore, India, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ambako nilipata fursa ya kujifunza mambo mengi lakini moja muhimu likiwa ni namna vyombo vya habari (kwa maana ya waandishi wa habari) na wanasiasa wanavyotumia muda wao mwingi kujadili masuala yanayogusa maisha na maendeleo ya watu wao.



Tofauti na kile wanachofanya wenzetu hapa nyumbani, ninyi wanahabari na sisi wanasiasa tumekuwa tukitumia muda wetu mwingi kujadili watu na propaganda za kisiasa zisizo na tija wakati tukitambua kwamba, taifa linakabiliwa na changamoto nyingi kama zile za kuhamasisha uwekezaji wa ndani na nje ya nchi, kuimarisha mifumo ya utawala bora, kuporomoka kwa thamani ya shilingi kila kukicha, mdororo wa uchumi, tatizo kubwa la ajira kwa vijana, kushuka kwa kiwango cha elimu na ugumu wa maisha kwa ujumla. TUNAPASWA KUJISAHIHISHA.



AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA


Comments