Featured Post

ESRF: SEKTA YA USINDIKAJI, CHACHU YA MAENDELEO YA VIWANDA

Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) kwa kushirikiana na CUTS International Geneva kupitia ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo Sweden (SIDA), wamezindua Ripoti ambayo inaelezea namna bora ya kuboresha viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya viwanda kama jinsi ulivyo Mpango wa Serikali kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17-2020/21.
Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dkt. Tausi Mbaga Kida alisema, ripoti hiyo imeonyesha kuwa, kama viwanda vya ndani vitaboreshwa vitawezesha kuwa na uwezo wa kuchakata mazao mengi ya kilimo yanayozalishwa na wakulima zaidi ya asilimia 75 ya watanzania.
Pia itasaidia kuongeza ajira, kuwahakikishia wakulima soko la uhakika wa mazao yao, na serikali kujiongezea vyanzo vipya vya mapato kutokana na bidhaa zitakazouzwa baada ya usindikaji na kwa kufanya hivyo, uchumi wa wakulima, wasindikaji, wafanyabiashara na wa Taifa kwa ujumla utaongezeka.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kijamii na Uchumi (ESRF), Dk. Tausi Kida akitoa neno la ufunguzi katika uzinduzi wa ripoti ambayo inaelezea namna bora ya kuboresha viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo. 
“Utafiti umeonyesha ili uweze kunufaika na kilimo lazima tuweze kuongeza thamani katika mazao yetu na hilo tutaweza kulipata pale ambapo tutakuwa na viwanda vyetu ambavyo vitaweza kuchakata mazao yetu katika ubora na kuweza kuwafikia walaji sehemu mbalimbali. Kikubwa katika hilo ni jinsi gani viwanda vya usindikaji, vikubwa na vidogo, vitaweza kuwa karibu na wakulima,” alisema Dk. Kida.
Akisoma hotuba ya uzinduzi wa Ripoti hicho kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji (Viwanda na Biashara), Dr. Adelhem Meru, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Masoko na Utafiti wa wizara hio, Bwana Leo Lyayuka, alisema Serikali inafahamu kuwa katika safari ya kuelekea katika nchi ya viwanda ni muhimu viwanda vyetu viwe na uwezo wa  kuchakata mazao ya kilimo ili kuyaongezea thamani.
Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Masoko na Utafiti wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Leo Lyayuka akizungumza kuhusu changamoto zilizopo na jinsi serikali ilivyojipanga kuzimaliza.
Aidha alitoa rai kwa Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa sekta ya usindikaji mazao ya kilimo katika kubuni mashine zenye uwezo wa kuchakata mazao mbalimbali na kuyauza ndani na nje ya nchi katika thamani kubwa zaidi.
Ndugu Lyayuka alisema pia msingi mzima katika utafiti uliopo kwenye Ripoti hio ni kuoanisha changamoto ambazo zipo katika mabadiliko ya tabia nchi na jinsi gani zinaweza zikaathiri uzalishaji na usalama wa chakula, biashara, na jitihada za kuendeleza viwanda vya usindikaji.
“Ni muhimu sana kwa sera zetu za viwanda na kilimo kuoana ili kuchagiza maendeleo haya ya sekta ya usindikaji, huku maswala mazima ya mabadiliko ya tabia nchi yakitiliwa mkazo kuepukana na athari zinazoweza kuletwa nazo.”
Mmoja wa watafiti walioandaa ripoti ambayo inaelezea namna bora ya kuboresha viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, Solomon Baregu akitoa maelezo kwa ufupi kuhusu ripoti hiyo.
Kwa upande wa mmoja wa watafiti, Ndugu Solomon Baregu alisema utafiti huo ni muhimu kwa Tanzania na kama ukifanyiwa kazi kikamilifu unaweza kuisaidia nchi kuingia katika uchumi wa viwanda.
 “Utafiti huu ni muhimu na umekuja wakati muafaka ambapo Serikali inatilia mkazo sana suala la kujenga Tanzania ya viwanda. Sekta ya kilimo ni sekta mama ambayo kwa kiasi kikubwa inaweza kuchochea ukuaji wa viwanda,” alisema Bwana Baregu.
Bwana Baregu aliongeza kuwa “Ni muhimu sana Serikali kufikiria sasa kuja na sera mahususi itayoweza kutambua ukuzaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo (Agro-Industrial Development Policy) huku ikitilia maanani mabadiliko ya tabia ya nchi na athari zake katika biashara, usalama wa chakula na uchakataji mazao ya kilimo.”
Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Masoko na Utafiti wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Leo Lyayuka akikata utepe kuashiria uzinduzi wa ripoti ambayo inaelezea namna bora ya kuboresha viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kijamii na Uchumi (ESRF), Dk. Tausi Kida na kulia ni Makmu Mwenyekiti Mstaafu wa Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa TCCIA, Peter Lanya.
Wa kwanza kulia ni mmoja wa watafiti walioandaa ripoti ambayo inaelezea namna bora ya kuboresha viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, Solomon Baregu, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kijamii na Uchumi (ESRF), Dk. Tausi Kida, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Masoko na Utafiti wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Leo Lyayuka na Makmu Mwenyekiti Mstaafu wa Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa TCCIA, Peter Lanya wakionyesha vitabu vya ripoti hiyo.
Picha juu na chini ni baadhi ya watoa mada wakitoa maelezo kuhusu mada zilizokuwa zikijadiliwa baada ya ufunguzi wa ripoti ambayo inaelezea namna bora ya kuboresha viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo.
Picha juu na chini ni baadhi ya watu ambao wamehudhuria ufunguzi katika uzinduzi wa ripoti ambayo inaelezea namna bora ya kuboresha viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo.
Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja.

Comments