Featured Post

VITA YA MADAWA YA KULEVYA NI YA MANUFAA KWA UMMA




Na Immaculate Makilika - MAELEZO
Mtandao wa Merriam Webster (2016) umeelezea manufaa ya umma  kama jambo ama kitu chenye manufaa kwa kila mwanajumuiya ama jamii. Wakati nayo kamusi ya Encyclopedia Brtitannica  (2016) ikisema kuwa hili ni jambo lenye faida kwa jamii.

Nashawishika kusema kuwa vita hii ya madawa ya kulevya ni ya kwa manufaa kwa umma, na hivyo hatuna budi kuiunga mkono kwa akili na nguvu zetu zote.

Lakini pia kama ilivyo ada maendeleo ya kitu chochote yanahitaji utashi wa kisiasa, uamuzi pamoja na  dhana ya uendelevu wa jambo, kwa mantiki hiyo vita ya madawa ya kulevya ni lazima iwe na maendeleo kwa faida ya vizazi vya sasa na hata vijavyo, hii si vita ya Rais Magufuli ,Makonda, wala Kamishna Sianga ni ya watanzania wote.

Ni takribani siku kadhaa tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda  aanzishe vuguvugu la kutaja majina ya watu 65  wenye tuhuma mbalimbali kuhusu utumiaji, uuzaji na usambazaji wa madawa ya kulevya na baadae Mheshimiwa Rais akasisitiza mapambano dhidi ya madawa ya kulevya kwa kumteua Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia  na Kupambana na Madawa ya Kulevya Bw. Rogers Sianga.

Kamishna Sianga, hivi karibuni akihojiwa na kituo cha televisheni cha Azam, anasema kuwa aina zote za madawa ya kulevya zina madhara makubwa na Serikali haitasita kuendelea kupiga marufuku ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na biashara hiyo haramu nchini, japokuwa baadhi ya nchi zinaruhusu matumizi ya dawa hizo.

“ Hatuwezi kuiga nchi jirani kwa kuwa kuna madhara makubwa, mfano wagonjwa wengi wa akili katika hospitali zetu wanatokana na matumizi ya madawa ya kulevya aina ya bangi”, anasema Kamishna Sianga.

Ni dhahiri kuwa tunawaona ndugu zetu, rafiki zetu na wasanii mbalimbali ambao wamekuwa waraibu wa madawa ya kulevya, wakifikwa na maswaibu mbalimbali ambayo yaliyasabisha kupoteza mwelekeo wa maisha yao na kusababisha vifo.

Athari hizi pia,  zinaikumba Serikali na Taifa kwa ujumla kwa  kutumia fedha nyingi  kwa ajili ya kununua madawa aina ya methadone, pamoja na kuendesha proramu maalumu kwa vijana kuhusu madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya.

Ikumbukwe kwamba, Sheria mpya ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya ya mwaka 2015, inaruhusu kuwakamata waraibuni kuzungumza nao na kisha kuwapatia matibabu.

Lakini pia hatua hiyo inasaidia Mamlaka zinazohusika kupata taarifa muhimu za waauzaji na wasambazaji wa dawa hizo mitaani. Nadhani kitu pekee tunachotakiwa kufanya katika  kuunga mkono jitihada hizi ni  kuwaripoti na kuwapeleka waraibu wa dawa hizi hatari katika sehemu husika kwa lengo la kuwasaidia watu hao.

Aidha, Serikali imejitoa kuwasaidia waraibu hawa kwa kuwatibu magonjwa mbalimbali ambayo mhusika atakutwa nayo, yakiwemo magonjwa ya TB na Virusi vya Ukimwi. Hii ni dhahiri kuwa serikali ina nia njema.

Mkazi wa Dar es Salaam, Antony Shedrack ,mwenye umri wa miaka 23 anasema ametumia madawa kwa muda wa miaka 6, na madhara aliyoyapata ni makubwa kwa vile hakuweza kumaliza shule, hana kazi anayofanya na hivyo amekua tegemezi kwa ndugu na marafiki.

Hali  hii si ngeni kwa vijana wengi wa kitanzania, kwa vile utumiaji wa madawa ya kulevya umekuwa sehemu ya maisha yao kiasi ambacho wamepoteza mwelekeo na dira ya maisha. Ili kulinda utu, heshima na kwa faida ya vizazi vijavyo na ustawi wa taifa hili, ni lazima tuunge mkono vita  dhidi ya madawa kwa vile hii ni vita yetu sote na ni vita ya manufaa  kwa umma.

Comments