Featured Post

JENEZA KUTOKA HONG KONG - (SEHEMU YA 14)



“Kiasi hicho kisingeweza kumtosha kwa mwaka mzima. Pengine allikuwa na kipato kingine zaidi ya hapo.”
“Ninadhani.”
Nililikuna taya langu wakati nikitazama nje ya dirisha, kichwa kikiwa kkimechanganyikiwa.

“Nadhani hakuna kitu kingine cha ziada?” hatimaye nikasema. Kisha nikauliza swali ambalo nilitamani kuliuliza tangu nilipobaini kwamba alikuwa akificha jambo. “Ulikuwa unamfahamu Herman Jefferson?”
Hilo likapata mshtuko. Nilimuona akiganda taratibu na ile hali ya kuwa mbali ikaondoka machoni kwake kwa muda, lakini ikarejea.
“Kwanini, ndiyo, hakika. Nimekuwa mfanyakazi wa Bwana Jefferson kwa miaka nane. Herman aliishi hapa kabla hajaenda Mashariki ya Mbali, Ndiyo: Nilimfahamu.”
“Alikuwa ni mtu wa namna gani? Baba yake anasema alikuwa mkorofi lakini hivi sasa anasema kama angeweza kumwelewa mwanaye wala asingekuwa mkorofi. Unakubaliana na hilo?”
Macho yake yakapoteza umakini aliokuwa ameuonyesha lakini nikashangaa kuona jinsi alivyoonekana na roho ngumu wakati ile sura ya kuigiza ilipoondoka.
“Bwana Jefferson alipatwa na mshtuko kusikia mwanaye amekufa,” alisema, sauti yake ikiwa kali. “Kwa sasa anahisi huzuni kubwa. Herman alikuwa katili, mbabe na asiye na huruma. Alikuwa mwizi. Aliiba fedha kutoka kwa baba yake: aliwahi kuiba hata fedha zangu. Ni vigumu kuamini alikuwa mtoto wa Bwana Jefferson. Bwana Jefferson ni mtu mwema: hajawahi kufanya jambo la kipumbavu maishani mwake!”
Niliona maelezo yake yananichanganya.
“Haya, asante,” nilisema na kuinuka. “Nitafanya kadiri niwezavyo kwa ajili ya Bwana Jefferson, lakini nitahitaji kuwa na bahati.”
Akapekua lundo la hundi zilizosainiwa, akaiona moja na kuisukuma kwenye dawati upande wangu.
“Bwana Jefferson ameona akupe malipo ya awali, kishika uchumba. Nitakuandalia tiketi yako ya ndege mara utakaponiambia uko tayari kwa safari. Kama utahitaji fedha zaidi, tafadhali nijulishe.”
Niliitazama hundi. Ilikuwa imesainiwa kwa mkono wake na ilikuwa ya dola elfu moja.
“Mimi sina gharama kubwa kiasi hiki,” nikamwambia. “Doma mia tatu zingetosha.”
“Bwana Jefferson ameniambia kwamba anataka uchukue,” alisema kana kwamba amenipatia dola tano tu.
“Sawa, sijawahi kukataa fedha.” Nikamtazama. “Unayasimamia mamsuala yote ya Bwana  Jefferson?”
“Mimi ni katibu wake,” alisema, kwa sauti ya mkato.
“Sawa. . .” Hapakuwa na jambo lolote la kusema, hivyo badala yake, nikasema, “Nitakuarifu mara nitakapojua lini ninaondoka.”
Wakati nikielekea mlangoni, akauliza, “Alikuwa (mwanamke wa Kichina) mzuri sana?”
Kwa sekunde sikuweza kuelewa, halafu nikageuka kumtazama. Alitulia tu, na kulikuwa na mtazamo wa udadisi machoni kwake ambao sikuweza kuuelewa.
“Mke wake? Ninadhani ndiyo. Baadhi ya wanawake wa Kichina ni wazuri sana. Ndivyo alivyokuwa — hata alipokuwa amekufa.”
“I see.”
Alichukua peni yake na kuvuta kitabu cha hundi. Ilikuwa ni namna ya kunifukuza.
Nilimkuta korokoroni akinisubiri ukumbini. Alinifungulia huku akiinama kidogo. Hakuna ambaye angeweza kumlaumu kwa kuwa mzungumzaji.
Nikatembea taratibu kuliendea gari langu. Mazungumzo ya mwisho yalikuwa yamenipatia mwanga. Nilikuwa na uhakika kwamba wakati fulani Janet West na Herman Jefferson walikuwa wapenzi. Taarifa za ndoa yake na kifo chake zinaweza kuwa za mshtuko mkubwa kwake kama ilivyokuwa kwa Mzee Jefferson. Haya yalikuwa maendeleo ambayo sikuyatarajia na yalisisimua. Nikaamini kwamba itakuwa vyema kama nitafahamu mengi zaidi kumhusu Janet West.
Niliingia kwenye gari yangu na kuendesha hadi makao makuu ya polisi. Nililazimika kusubiri kwa nusu saa kabla ya kuonana na Retnick. Nilimkuta ameketi kwenye dawati lake, akitafuna mtemba ambao umezima na katika hali ya kuchanganyikiwa.
“Sidhani kama ninahitaji kupoteza muda na wewe, mpekenyuzi,” alisema wakati nikifunga mlango na kwenda kuketi kwenye dawati lake. “Unataka nini?”
“Hivi sasa nimeajiriwa na J. Wilbur Jefferson,” nikasema. “Nilidhani unahitaji kufahamu.”
Uso wake ulibadilika.
“Kama utaharibu upelelezi wangu, Ryan,” akasema, “Nitahakikisha unapoteza leseni yako. Ninakuonya.” Alitulia, kisha akaendelea, “Anakulipa nini?”
Nikaketi kwenye kiti.
“Kiasi cha kutosha. Sitakuwa na nafasi ya kuingilia chochote. Ninakwenda Hong Kong.”
“Nani ambaye asingependa kuwa mpekenyuzi,” akasema. “Hong Kong, eh? Nisingesita kwenda huko binafsi. Unadhani utafanya nini utakapokuwa huko?”
“Yule kizee anataka kujua mwanamke yule ni nani. Anadhani hatutafika popote mpaka nichimbe kujua habari zake za nyuma na kuzichunguza. Anaweza kuwa sahihi.”
Retnick aliishikilia peni yake kwa muda, halafu akasema, “Itakuwa upotevu wa fedha na muda, lakini sidhani kama hilo litakusumbu hususan kama unalipwa.”
“Haliwezi kunisumbua,” nilimweleza kwa furaha. “Anaweza kugharamia na ninaweza kuutumia muda. Ninaweza pia kupata bahati.”
“Ninajua mengi kuhusu yeye kuliko unayoweza kuyapata huko. Sikuhitaji kwenda Hong Kong kutafuta habari zake. Nilichokifanya tu ni kutuma ujumbe wa haraka.”
“Na nini ulichokigundua?”

Itaendelea kesho...

Comments