- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Nilijiuliza nani ambaye atakuwa amemwambia hayo, lakini nikakausha
na kuuweka uso wangu katika taswira nzuri bila kusema neno.
“Nimekuita hapa,” Jefferson akaendelea, “kwa sababu ningependa
kusikia kutoka kwako moja kwa moja kuhusu huyu mtu aliyekupigia simu na namna,
baadaye, ulivyomkuta mwanamke wa Kichina akiwa amekufa ofisini kwako.”
Nikabaini kwamba hakuwa anamwita mkamwana wake. Nikagundua pia
kwamba wakati aliposema ‘mwanamke huyu wa Kichina’, mdomo wake uliyoa beuo na
sauti yake ilikuwa ya dharau. Nahisi kwa mtu mzee na tajiri na maarufu kama
yeye, taarifa kwamba mwanao pekee ameoa mwanamke wa Kichina zingekuja kama mshtuko.
Nikamweleza hadithi nzima, nikikumbuka kupaza sauti yangu.
Baada ya kumaliza, akasema, “Asante sana, Bwana Ryan. Unaweza
kujua kwa nini alikuwa anataka kukuona?”
“Siwezi hata kubashiri.”
“Wala hujui nani aliyemuua?”
“Hapana.” Nikatulia kabla ya kuongeza, “Kuna uwezekano kwamba mtu
huyu anayejiita John Hardwick anaweza kuwa ndiye aliyemuua ama ameshirikishwa.”
“Sna imani na Retnick,” Jefferson akasema. “Ni mjinga asiye na
akili na hana hadhi ya kuwa katika nafasi aliyonayo. Ninataka mtu aliyemuua mke
wa mwanangu akamatwe.” Akaangalia kwenye mikono yake iliyosheheni misuli,
akafura kwa hasira. “Bahati mbaya, mwanangu na mimi hatukuwa tunaelewana. Kulikuwa
na makosa ya kila upande kama yalivyo daima, lakini baada ya kufa ndiyo
ninatambua kwamba ningeweza kumvumilia. Naamini ukosefu wangu wa stahamili na
kukataa kwangu tabia yake ndiko kulikomfanya aharibike zaidi kuliko ambavyo
alipaswa awe kama angekuwa ameeleweka. Mwanamke aliyemuoa ameuawa. Mwanangu
asingeweza kutulia mpaka ampate muuaji. Naijua tabia yake ndiyo maana nina
uhakika na hili. Mwanangu amekufa. Nahisi kitu pekee ambacho ninaweza kumfanyia
sasa ni kumtafuta mtu aliyemuua mkewe. Kama nitafanikiwa, nitakuwa nimemtendea
hisani kubwa ambayo ingeweza kuturejesha pamoja japo kwa uchache,” Alitulia na
kutazama bustanini, uso wake wa kizee ukiwa mgumu na wenye huzuni. Upepo
mwanana ulizitimu nywele zake nyeupe. Alionekana mzee sana lakini mwenye
dhamira kubwa. Akageuka kunitazama. “Kama unavyoona, Bwana Ryan, mimi ni mzee. Siku
zangu zimekwisha. Ninachoka haraka. Siko katika hali ya kuweza kumwinda muuaji
na hiyo ndiyo sababu nimekuita wewe. Wewe ni mtu muhimu sana. Mwanamke huyu
alikutwa ofisini kwako. Kwa sababu zozote muuaji alitaka kukutwisha mzigo.
Ninakusudia kukulipa vizuri. Unaweza kumtafuta mtu huyu?”
Ingekuwa rahisi kusema ndiyo, nichukue fedha zake halafu nisubiri
kama Retnick ataweza kumpata muuaji, lakini sikuwa nafanya kazi kwa staili
hiyo. Nilikuwa na uhakika nisingeweza kumpata muuaji mimi mwenyewe.
“Upelelezi uko mikononi mwa polisi,” nikasema. “Ndio watu pekee
watakaoweza kumpata mtu huyu—mimi siwezi. Kesi ya mauji iko nje ya kazi za
mpelelezi wa kujitegemea. Retnick haruhusu watu wa nje wamtimulie vumbi. Mimi
siwezi kuwahoji mashahidi wake. Atapata taarifa na nitajikuta matatani. Ningependa
sana kupata fedha zako, Bwana Jefferson, lakini haitawezekana.”
Hakuonekana kushangazwa, lakini akaonekana kuwa mwenye dhamira
kama awali.
“Ninalitambua hilo,” akasema. “Retnick ni mjinga. Anaonekana hana
wazo lolote la namna ya kushughulikia kesi hii. Nilimshauri awasiliane na
mamlaka za Uingereza huko Hong Kong kuona kama tunaweza kugundua chochote
kuhusu mwanamke huyu. Hatujui chochote kumhusu yeye isipokuwa aliolewa na
mwanangu na alikuwa mkimbizi kutoka Bara China. Ninajua hayo kwa sababu
mwanangu aliniandikia barua mwaka jana akiniambia alikuwa anaoa mkimbizi wa
Kichina.” Kwa mara nyingine akatazama bustanini
wakati akisema, “Kwa ujinga wangu niliikataa ndoa hiyo. Sikusikia
chochote tena kutoka kwake.”
“Unadhani polisi wa Kiingereza watakuwa na taarifa za mwanamke
huyu?” nikamuuliza.
Akatingisha kichwa chake.
“Inawezekana, lakini siyo sana. Kila mwaka zaidi ya mamia kwa
maelfu ya wakimbizi wanaingia Hong Kong. Hawajulikani wanatoka nchi gani kwa
sababu hawana nyaraka zozote. Nina watu kadhaa huko Hong Kong na ninajaribu
kuwasiliana nao mara kwa mara kuhusu suala hili. Kwa kadiri ninavyojua, ni
kwamba: wakimbizi wanaokimbia kutoka Bara China wanavushwa na kundi la watu na
kuingia Macau ambako, kama unavyojua, ni himaya ya Wareno. Macau haiwezi
kukabiliana na uvamizi huo na wala haipendi. Baadaye wakimbizi hawa
wanasafirishwa na kundi jingine na kupelekwa Hong Kong. Polisi wa Uingereza wanafanya
doria kuangalia uingiaji huo Hong Kong, lakini Wachina ni watulivu na wajanja
wanapotafuta njia zao wenyewe. Kama meli itaonekana ikiwa na wakimbizi, boti za
polisi zinaifuatilia, lakini baharini kuna mashua nyingi za uvuvi ambazo
zinakwenda kisiwani humo. Kwa kawaida mashua zenye wakimbizi zinafanikiwa kwa
kuchanganyika na zile za wavuvi ambazo zinazizingira kwa hifadhi na kwa kuwa
mashua zote zinafanana, inakuwa vigumu kwa boti za polisi kuziona. Natambua
kwmaba polisi wa Kiingereza wana huruma sana kuhusu wakimbizi: hata hivyo,
walikuwa katika nyakati ngumu na wanakimbia kutoka kwa adui yule yule ambaye
Waingereza wanapigana naye. Upekuzi wao hukoma mara baada ya mashua kuingia
katika eneo la bahari la Hong Kong. Polisi wanaona kwamba kwa kuwa watu hao
maskini wamefika mbali, haitakuwa jambo la kibinadamu kuwarudisha walikotoka.
Lakini watu wote hawa hawafahamiki. Hawana nyaraka. Polisi wa Kiingereza
wanawapatia nyaraka mpya, lakini hakuna namna yoyote ya kuchunguza hata majina
yao. Mara tu wanapoingia Hong Kong, wanaanza maisha mapya wakiwa na majina
mapya: wanakuwa wamezaliwa upya. Mke wa mwanangu alikuwa mmoja wao. Mpaka tujua
alikuwa nani hasa na maisha yake ya nyuma yalikuwaje, vinginevyo sidhani kama
tutaweza kujua ni kwa nini aliuawa na nani alimuua. Kwahiyo ninataka wewe uende
Hong Kong na kuona kama unaweza kupata jambo lolote kuhusu yeye. Haitakuwa
rahisi, lakini ni jambo ambalo Retnick hawezi kufanya na polisi wa Kiingereza
hawawezi kulifanya pia. Nadhani unaweza kulifanya na nitagharamia kila kitu.
Unasemaje kuhusu hilo?”
Nilikuwa nimevutiwa na wazo lake, lakini siyo furaha ya kufanya
nisahau kwamba kunaweza kusiwe na mafanikio.
“Nitakwenda,” nikamwambia, “lakini itakuwa ni kupoteza muda. Siwezi
kusema ninaweza kufanikiwa au la mpaka nifike kule, lakini kwa sasa, sidhani
kama kuna uwezekano mkubwa.”
“Nenda azungumze na sekretari wangu. Atakuonyesha baadhi ya barua
kutoka kwa mwanangu ambazo zinaweza kukusaidia. Jitahidi kwakadiri ya uwezo
wako, Bwana Ryan.” Akaniashiria niondoke. “Utamkuta Bi. West katika chumba cha
tatu kwenye korido upande wa kulia.”
“Unajua siwezi kwenda haraka hivyo?” nikamwambia, nikisimama. “Ninapaswa
kudhuria uchunguzi wa daktari na ninatakiwa kupata ruhusa kutoka kwa Retnick
kabla ya kuondoka.”
Akaitikia kwa kichwa. Alionekana amechoka sana.
“Nitahakikisha Retnick hawi kizuizi kwako. Nenda haraka unavyoweza.”
Nikaondoka, nikimwacha akitazama mbele yake: mpweke na mawazo
machungu ya kumbukumbu za nyuma zilizokuwa zikimtafuna.
Itaendelea kesho...
Comments
Post a Comment