Featured Post

JENEZA KUTOKA HONG KONG - (SEHEMU YA 11)


“Mimi ni katibu muhtasi wa Bwana J. Wilbur Jefferson,” sauti ya kike ikasikika kutoka upande wa pili ambayo ilikuwa rahisi kuisikiliza. “Nazungumza na Bwana Ryan?”
Nikamwambia mimi ndiye.
“Bwana Jefferson angependa kukuona. Unaweza kuja alasiri hii baada ya saa tisa?”

Nikapatwa na mshtuko wakati nikifungua shajara yangu na kupekua kurasa zilizo wazi. Sikuwa na miadi yoyote kwa saa tisa alasiri ya leo: na zaidi, sikuwa na miadi yoyote kwa wiki nzima.
“Nitakuja,” nikamwambia.
“Ni nyumba ya mwisho, itazama bahari kwenye Barabara ya Ufukweni,” akanieleza. “Mtaa wa Beach View.”
“Nitakuja.”
“Asante sana.”
Akakata simu.
Nikashikilia mkonga wa simu sikioni mwangu kwa muda kidogo nikijaribu kuikumbuka sauti yake. Nilifikiria kama sauti yake ilikuwa tamu yeye alikuwaje. Sauti yake ilionekana bado mbichi kabisa, lakini sauti daima hudanganya. Nikaurudisha mkonga chini.
Asubuhi ya siku hiyo ilipita bila tukio lolote. Nilimuonea wivu Jay Wayde ambaye simu yake ilikuwa ikilia kila mara. Pia niliendelea kusikia sauti mfululizo za clack-clack za mashine ya chapa. Daima alikuwa na kazi nyingi kuliko mimi, lakini bado nilikuwa na dola mia tatu na mtu wa ajabu Bwana Hardwick ambazo zingenitosha kupambana na njaa kwa japo wiki mbili.
Hakuna aliyekuja karibu yangu, na majira ya saa saba nikashuka kwenda Quick Snack Bar ili kupata sandwich yangu ya siku zote. Sparrow alikuwa na kazi nyingi kuwahudumia wateja hivyo hakujishughulisha kuniuliza maswali, japokuwa nilimuona akiwa na nia ya kutaka kujua kuhusu suala la mauaji. Niliondoka punde tu nikijua kwamba alikuwa akitaka nimweleze chochote.
Baadaye, nikaendesha gari kupitia Barabara ya Ufukweni, eneo la matajiri wa Pasadena City. Hapa, matajiri na wastaafu wanaishi wakiwa na fukwe zao wenyewe, mbali na umati wa watu wanaovamia jiji nyakati za kiangazi.
Nililifikia geti la Beach View dakika chache kabla ya kugonga saa tisa. Geti lilifunguliwa kana kwamba lilikuwa linanisubiri mimi na nikaendesha kwa umbali wa yadi arobaini, njia ambayo kila upande imepambwa kwa maua.
Jumba lilikuwa kubwa sana na lilikuwa na mazingira ya hali ya hewa ya kizamani. Ngazi sita kubwa zilielekeza kwenye mlango wa mbele wa kuingilia. Kulikuwa na kengele ya kuning’inia na mlango wa mbele ulikuwa wa mwaloni.
Nilivuta kamba ya kengele na baada ya kama dakika hivi, mlango ukafunguliwa. Bawabu alikuwa mzee mwenye umbile kubwa na mrefu ambaye alinitazama kwa makini; akiniangalia kwa jicho kali lililohoji.
“Nelson Ryan,” nikasema. “Ninasubiriwa.”
Akasimama pembeni na kuniashiria niingie kwenye sebule pana yenye samani aghali nyeusi ambapo mwanga wake ulikuwa hafifu. Nikamfuata kwenye korido hadi kwenye chumba kidogo kilichokuwa na viti vichache vigumu na meza moja ambayo juu yake kulikuwa na majarida mbalimbali: chumba ambacho kilifanana na chumba cha mapokezi cha daktari wa meno. Akaniashiria niketi kwenye mojawapo ya viti hivyo halafu akaondoka.
Nilisimama pale kwa karibu dakika kumi, nikitazama kupitia dirishani mandhari ya bahari, halafu mlango ukafunguliwa na msichana akaingia.
Alikuwa na umri kama miaka ishirini na nane au thelathini hivi, mrefu kuliko wastani, msomi na mwenye mawazo. Alivaa gauni la bluu nzito ambalo lilisawiri umbile lake maridhawa.
“Samahani kwa kukufanya usubiri sana, Bwana Ryan,” alisema. Tabasamu lake lilikuwa dogo na la kuigiza. “Bwana Jefferson yuko tayari kukuona sasa.”
“Wewe ni katibu muhtasi wake?” nikamuuliza, nikiikumbuka sauti yake tulivu.
“Ndiyo. Ninaitwa Janet West. Twende nikupeleke.”
Nikamfuata kupitia kwenye korido hadi kwenye mlango mkubwa na kuingia kwenye ukumbi wa kizamani uliopambwa na vitabu na dirisha pana likiwa limefunguliwa kuelekea kwenye bustani iliyojaa maua ya waridi yaliyokuwa yananukia vizuri.
J. Wilbur Jefferson alikuwa amejilaza kwenye kitanda cha kubembea, kilicho na magurudumu. Alijilaza kwenye kivuli nyuma ya dirisha: alikuwa mzee, mrefu, mwembamba na mwenye pua ndefu, ngozi ya manjano kama pembe ya ndovu kuu kuu, nywele nyeupe akiwa amevaa miwani na mikono myembamba ambayo mishipa ilitokeza. Alivaa suuti nyeupe ya kitambaa cha linen na viatu vya ngozi vyeupe. Aligeuza kichwa chake kunitazama wakati nikimfuta Janet West kwenye bustani.
“Bwana Ryan,” Janet West akasema kama kunitambulisha, akisimama kando na kuniashiria nisonge mbele, yeye akaondoka.
“Tumia kiti kile,” Jefferson akasema, akiniashiria niketi kwenye kiti kilichosukwa kama kikapu ambacho kilikuwa jirani naye. “Uwezo wangu wa kusikia siyo mzuri kama zamani kwa hiyo nitaomba uongeze sauti. Kama unataka kuvuta sigara. . . vuta. Ndio utumwa ambao nimelazimishwa kuachana nao kwa zaidi ya miaka sita.”
Nikaketi, lakini sikuwasha sigara. Nilitambua kwamba hakuwa anapenda sigara. Wakati alipokuwa anavuta, lazima alikuwa anavuta mitemba.
“Nimeulizia sana habari zako, Bwana Ryan,” aliendelea baada ya kutulia kwa muda mrefu wakati macho yake yakinikagua kwa makini, na kunipa taswira kwamba alikuwa akitazama mifuko yangu, akitazama alama yangu ya kuzaliwa nayo kwenye bega langu la kulia na kuhesabu fedha zangu kwenye pochi. “Nimeambiwa wewe ni mkweli, unaaminika na una akili.” 

Itaendelea kesho...
 

Comments