Featured Post

WATUMISHI MKOANI SINGIDA WAAGIZWA KULIMA MAZAO YANAYOTUMIA MAJI KWA UFANISI



Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi akionyesha mbegu bora ya muhogo aina ya Momba inayozalishwa katika shamba la Mpambaa halmashauri ya Singida, katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo na anayefuata ni Afisa Kilimo halmashauri ya Singida  Abel Mungale.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi akiandaa mashimo ya kupanda mbegu bora ya mbaazi inayozalishwa katika shamba la Mpambaa halmashauri ya Singida.
 
 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi akipamba mbegu bora ya mbaazi inayozalishwa katika shamba la Mpambaa halmashauri ya Singida, anayefuata ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Singida Eliya Digha.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi akiwaonyesha watumishi wa  halmashauri namna ya kupanda mbegu bora ya mbaazi katika shamba la Mpambaa halmashauri ya Singida.
Watumishi wa halmashauri ya Singida wakizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi (hayupo pichani).
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi akipanda mti wa mwembe katika eneo la sekondari ya Ilongero Wilayani Iramba.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi akipanda viazi lishe na mihogo katika shamba la mkulima bora wa eneo la Old Kiomboi Wilayani Iramba.

Watumishi wa halmashauri zote saba za Mkoa wa Singida wameagizwa kulima nusu ekari ya mazao yanayotumia maji kwa ufanisi hasa zao la muhogo, viazi au mtama ili kuwa na uhakika wa chakula cha kutosha msimu ujao huku shule zote zikiagizwa kulima ekari moja ya mihogo au mtama ili wanafunzi wapate chakula shuleni.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimi ametoa agizo hilo alipotembelea na kuzindua shamba la mbegu bora ya mihogo la ekari kumi lililopo kijiji cha Mpambaa, Halmashauri ya Singida ambalo litazalisha mbegu kwa ajili ya wakulima wa Mkoa wa Singida.
Dokta Nchimbi ametumia kauli mbiu ya kuongoza ni kuonyesha njia kwa kulima mihogo shamba lake mwenyewe lenye ukubwa wa ekari tatuna hivyo kuwaagiza watumishi na viongozi wote kuonyesha mfano kwa kulima mazao hayo kwa msimu huu.
Pamoja na upandaji wa mbegu za Muhogo, Dokta Nchimbi pia amezindua shamba la mbegu bora za mbaazi kwa kupanda mbegu hizo pamoja na kupalilia shamba la mbegu bora za mtama ambapo aina 25 za mtama zinafanyiwa majaribio ili kupata mbegu itakayofaa kwa mkoa wa Singida.
Aidha ametembelea mashamba ya wakulima wa mtama wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi pamoja na kushiriki upandaji wa mtama wa shamba la shule ya Msingi Mampanta wilayani Iramba na kupanda viazi na mihogo katika shamba la Mkulima wa Old Kiomboi wilayani Iramba.
Amesema wakulima wakielimishwa juu ya mazao yanayotumia maji kwa ufanisi watapanda mazao hayo ambayo ni mtama, viazi, muhogo na mbaazi ambapo wakulima watakuwa na uhakika wa chakula pamoja na kujipatia fedha kwa kuuza mazao hayo.
Dokta Nchimbi ametoa hamasa kwa wakulima wote kulima mazao hayo yanayotumia maji kwa ufanisi na wajitume kwa bidii kuliko kulalamikia serikali bila kufanya kazi kwakuwa awamu ya sasa ya uongozi ni ya kuchapa kazi kwa bidii.
Wakati huo huo Dokta Nchimbi amefanya vikao na watumishi wa halmashauri za Singida, Ikungi na Iramba mara baada ya kutembelea mashamba ya wakulima na kushiriki nao katika kupanda mtama, kupalilia baadhi ya mashamba, kupandqa mihogo na viazi.
Dokta Nchimbi amewaasa watumishi wote Mkoani Singida kuwa waadilifu, wachape kazi na hasa kulima mazao yanayotumia maji kwa ufanisi pamoja na kufanya shughuli nyingine za kuwaingizia kipato kama vile kufuga kuku na kuwa na mizinga ya nyuki ili wawe na kipato kingine nje ya mshahara.
Amesema watumishi wengine hujiingiza kwenye wizi kutokana na tamaa tu ila endapo watakuwa na vyanzo vingine vya fedha nje ya mshahara itapunguza kutokuwa waaminifu pamoja na kutokulalamika mara kwa mara.
Baadhi ya watumishi waliohudhuria vikao hivyo wamempongeza Mkuu wa Mkoa Dokta Nchimbi kwa nasaha alizowapa huku wakiahidi kuchapa kazi kwa bidii na uadilifu pamoja wakijishughulisha na kilimo ili wawe na kipato cha ziada.


Comments