- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
BARUA YA WAZI TOKA KWA MAHABUSU WA UTUHUMIWA WA
UGAIDI GEREZA LA SEGEREA
Kumb:DA.13/PI:29,2014/2016
Mahabusu PI/29/2014
Gereza la Mahabusu
Segerea, Dar es Salaam
28/12/2016
Dar es Salaam
MH. JAJI MKUU
MAHAKAMA KUU YA TANZANIA
DAR ES SALAAM-TANZANIA.
YAH: UVUNJWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA
BORA
Tafadhali
husika na mada iliyotajwa hapo juu.
Mheshimiwa
Jaji Mkuu, tunaelezea uvunjwaji wa haki za Binadamu katika maeneo mawili
makubwa, kwa upande wa Mahakama na pili ni kwa upande wa Jeshi la Magereza,
hasa kwa Gereza la Mahabusu Segerea Dar es Salaam.
Tukianza
kwa upande wa Mahakama kwa kupitia Mahakama ya rufaa (TCA), kwa muda wa miaka
mitatu sasa kuanzia tarehe 24/12/2014 mpaka leo hii tarehe 28/12/2016,
imeshindwa kupanga tarehe ya kusikiliza rufani ya upande ya mashitaka
inayopinga maamuzi ya mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam yaliyotolewa na Mhe.
Jaji Dr Fauzi Twaibu ya kuiambia Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu inao uwezo wa
kutoa maamuzi kwenye hatua za mchakato wa ufunguaji wa shauri.
Sambamba
na hilo Mahakama ya Kisutu pamoja na kuelezwa na Mhe. Jaji Dr. Fauzi kuwa inao
uwezo wa kutoa maamuzi imeshindwa kutoa maamuzi kwa madai kuwa upande wa
mashtaka umekata rufaa.
Vile vile
upande wa mashitaka umekuwa ukitumia mgongo wa kutokamilika kwa upelelezi ili
wazidi kutuweka jela kwa lengo la kutukomoa na huku wakiidanganya mahakama kuwa
upelelezi utakamilika ''Very soon'' na huku ikichukua zaidi ya miezi tisa.
Pia Hakimu
kuegemea upande mmoja wa wanaoshtakia (Upande wa DPP), mfano Mhe. Hakimu
Mwijage akiwa katika kiti cha uhakimu alitoa maelezo kuwa ''Anaongea kama afisa
wa Magereza'' wakati magereza ndio wanaolalamikiwa na yeye akajisahau kuwa ni
Hakimu hapaswi kuegemea upande wowote. Hata hivyo tulimuandikia hakimu mfawidhi
wa mahakama ya Kisutu kuhusu jambo hili yenye Kumbukumbu namba DA.10/PI.29.2014/2016.
Vile vile
mnamo tarehe 15/12/2016, Mheshimiwa Hakimu Wilbrod Mashauri, tulipo mlalamikia
juu ya vitendo vibaya tunavyofanyiwa na jeshi la magereza hapa Segerea kwa
kupigwa mshtakiwa namba sita (6) Mohammed Ishaq Yusuph, PI:29/2014 na kupelekwa
chumba cha adhabu kijulikanacho kwa ufupi PC kwa muda miezi mitatu (Siku tisini
bila ya mapumziko) huku akikoseshwa matibabu baada ya kujeruhiwa vibaya kwa
kipigo na waliompiga ni maaskari aitwaye 2upaki na Bahati.
Kufungiwa
kwenye chumba cha adhabu ambacho ni choo kwa muda wa siku tisini bila ya
mapumziko ambayo ni kinyume na wanavyo adhibiwa wengine (Kila wiki wanatolewa
siku moja kama ni mapumziko na vile vile kuyasaidia macho kuona vitu vya mbali
kutoka kutizama karibu).
Amezuiliwa
kufanya ibada kutokana na kuwekwa ndani ya choo, alichukua mswala ili atandike
kwa ajili ya kufanya ibada nao amenyang'anywa na afisa usalama anayeitwa
Rashid, pia wamemnyang'anya vitabu alikuwa akivisoma.
Mhe, Jaji
Mkuu wamezuia wanafamilia yake kumtembelea na kumletea huduma yeyote kwa muda
wa miezi mitatu akiwa ndani ya adhabu.
Hasa
ukizingatia ni mgonjwa mwenye matatizo ya kuanguka na kuzimia ambayo ni matokeo
ya mateso na vipigo akiwa mikononi mwa Polisi, aliandikiwa akafanyiwe kipimo
cha CT-Scan katika Muhimbili Hosptali tokea 2015 mpaka sasa hajapelekwa
Hospitali na tarehe 25/12/2016 ameanguka na kuzimia akiwa ndani ya chumba cha
adhabu (pc) na hata alipopata fahamu alilejeshwa tena chumba cha adhabu (PC).
Siku
tisini za adhabu alizopewa mahabusu Mohammed Ishaq Yussuf amaeanza kuitumikia
kuanzia tarehe 05/12/2016 mpaka tarehe 06/03/2017 ambacho atakuwa akipewa robo
ya resheni ya chakula cha mchana na maji ya chumvi lita nne (4lita) kwa siku.
Maji hayo
atakunywa, atatumia kwa choo (kwenda haja) atakogea, lita nne hizi itakuwa ndio
kipimo cha matumizi ya maji kwa muda wote wa adhabu wa siku tisini (90) Miezi
mitatu.
Mheshimiwa
Jaji Mkuu, Malalamiko haya kuhusu mshtakiwa namba sita (Mohammed Ishaq
Yusssuf,) tulipomueleza Mheshimiwa hakimu Wilbrod Mashauri ametutaka malalamiko
yetu tuyalete mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam, lililotushangaza
hakuwauliza magereza chochote kuhusu tulichokilalamikia, isipokuwa alisema
mahakama yake imefungwa mdomo na mikono.
Mheshimiwa
Jaji Mkuu kwa upande wa magereza kumekuwa na udhalilishaji uliopindukia mipaka,
utu wa mtu umekuwa haujaliwi kwani mahabusu wote wanaonekana kuwa ni wahalifu
wakati sheria iko wazi ambayo inaelekeza kuwa mahabusu hatakuwa ni mhalifu hadi
pale mahakama itakapo mtia hatiani.
Mhe. Jaji
Mkuu wakati tukiingia gerezani tarehe 17/07/2014 tulimuomba mkuu wa gereza
Segerea muongozo wa gereza na kurudia kukumbushia kwa mkuu wa gereza mpya,
lakusikitisha mpaka tunaandika maandiko haya hatujapatiwa bila ya sababu za
msingi isipokuwa tunaambiwa tutii bila shuruti.
Mahabusu
kupigwa na kutukanwa matusi ya nguoni haya ni mambo ya kawaida hapa gerezani,
huku wenyewe magereza wakiwa wanajisifu kwa kusema hizi rungu walizo nazo
ZIMEPITISHWA NA BUNGE KWA AJILI YA KUWAPIGA MAHABUSU. Mfano Mhabusu Hassan
Khamis namba PI:41/2014, siku ya tarehe 21/12/2016 wa mahakama ya Kisutu
amepigwa marungu kadhaa kwa kukutwa na mchuzi. Askari aliyempiga anaitwa 2paki
huku akijisifu kupandishwa vyeo kwa kufanya kazi nzuri.
Mahabusu
Kassim Mkadam Khamis alipigwa kwa kukutwa na peni ya high lighter, pia mahabusu
Rajabu ambaye ni mgonjwa wa ngiri ambae anakaa cell namba tatu (3) ambayo ni
sehemu yanayokaa wagonjwa kesi namba PI:14/2015 tarehe 24/12/2016 pamoja na
mahabusu wengine wakati wa zoezi lao magereza la kusachi mahabusu wote alipigwa
sana na kila alipojaribu kusema mimi naumwa alijibiwa hivi ''Wagonjwa wako
Muhimbili''.
Mahabusu
Salim Ali Salim namba PI:41/2014 ambaye amelazwa katika Hospitali ya gereza
ijulikanayo Cell namba samba (7) alilazimishwa kutoka ndani huku wakijua hawezi
hata pale afisa wa zamu aliposema muacheni amri hiyo haikuheshimiwa
inavyostahiki. Je Mhe. Jaji Mkuu, hivi ndivyo sheria inavyosema pamoja na haki
za Kibinadamu, mahabusu na wafungwa wa kisiasa?
Mhe. Jaji
Mkuu, adhabu zinazotolewa hapa gerezani nyingi haziendani na kosa husika na
hazitolewi kwa mujibu wa sheria bali ni kwa utashi tu wa watu.
Mhe. Jaji
Mkuu, Mshtakiwa namba sita Mohammed Is'haq Yussuf wa PI:29/2014 adhabu hii
aliyopewa kuishi ndani ya chumba cha adhabu kwa muda wa miezi mitatu, siku
tisini (90) bila kutolewa na kupewa mlo mdogo usiozidi gramu 80 (80grams) na
huku mahabusu huyu akiwa amesharipoti juu ya suala la afya yake na huku
magereza wakiwa na taarifa zake kamili, hapa ni wazi jeshi la magereza
linaendeleza maelekezo walioyaanza Jeshi la polisi kuhakikisha japo mtu mmoja
lazima afariki dunia ndani ya mikono yao.
Kwani
adhabu hii hailingani na kosa analodaiwa kulitenda bali inaonekana wazi kuwa ni
chuki ndizo zinashawishi utoaji wa adhabu hiyo ambayo tokea tumefika hapa
gerezani Segerea tarehe 17/07/2014 haijawahi kutolewa kwa mahabusu yeyote yule
wala mfungwa.
Mh. (jaji
Mkuu), mshtakiwa kwa kuliona hilo ameamua kugoma kutokula hicho chakula kidogo
na leo hii tarehe 28/12/2016 ni siku ya nne.
Mh. Jaji
Mkuu, hata unapodai kumuona mkuu wa greza sisi tunaoitwa ''wapemba'' PI.29/2014
nayo ni shida kumuona kwa ajili ya kutoa malalamiko.
Mhe. Jaji
Mkuu, kumekuwa na kauli mbali mbali za chuki na za ubaguzi dhidi yetu sisi
tunaoitwa ''Wapemba''. Kwa mfano siku ya tarehe 05/12/2016 askari anaehusika na
kitengo cha upekuzi alimueleza mahabusu Mohammed Is'haq Yussuf wa PI.29/2014
ambaye ni mshitakiwa namba sita kuwa sasa ataruka na wapemba na hata pale
Mohammed alipomueleza kuwa atawaambia wenyewe alijibu ninakutuma ukawaambie
''wapemba wenzio''.
Siku ya
tarehe 15/12/2016 sehemu hiyo hiyo ya upekuzi wakati tukirudi mahakamani
alimuambia mahabusu Hussen Mohamme Ali kuwa ni mchawi na tarehe 21/12/2016
alimwita Hassan Khamis wa PI.41/2014 kuwa ni Mshenzi. Kauli kama hizi
tuliziripoti kwa mkuu wa gereza aliepita ACP Abdallah Kiangi na zilikoma kwa
muda na sasa baada ya utawata huu mpya zimerudi tena kwa kasi kubwa.
Mhe. Jaji
mkuu hapa tunajiridhisha kuwa yale maneno tuliyoambiwa na ''Task force'' ya
kuwa tumeletwa Tanzania bara kuja kukomolewa ni ya kweli na huenda hizi chuki
na ubaguzi ni sehemu ya maagizo waliopewa jeshi la magereza watufanyie.
Mhe.Jaji
mkuu, ubaguzi tunayofanyiwa na askari magereza hapa gerezani Segerea haiendani
na sera ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli
aliyoitangaza siku ya uhuru wa Tanganyika tarehe 09/12/2016 ya kuwa Tanzania ni
moja.
Mhe. Jaji
mkuu, udhalilishaji huu unaofanywa na jeshi la magereza kupitia gereza la
mahabusu segerea ni kinyume cha katiba ya nchi, kinyume cha mikataba ya
kimataifa ya haki za binadamu, mahabusu na wafungwa wa kisiasa na ni kinyume
cha utawala bora wa sheria.
Mhe. Jaji
mkuu, tunakuomba kwa vile wewe ni ndiyo mkuu wa watoa haki katika Jamhuri ya
muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na vyombo vingine husika kwa mujibu wa
sheria za nchi hapa Tanzania muunde ''TUME HURU'' ili ichunguze usahihi wa
tunayoyaeleza ili zichukuliwe taratibu za kisheria kwa kasoro hizi zilizojitokeza
ili zisiendelee kuvunjwa haki za binadamu, mahabusu na wafungwa wa kisiasa.
Mhe. Jaji
Mkuu kwa sasa tunaishi katika hofu kubwa na hali ya wasiwasi na kuona kuwa
usalama wetu uko hatarini kwa namna tunavyotendewa hapa gerezani Segerea.
Uongozi wa
magereza unapaswa kuwajibishwa kwa madhara yoyote yanayoweza kutupata mbeleni.
Magereza kushindwa kutoa muongozo wa maisha ya gerezani ni kubariki kutokujua
haki zetu za gerezani na hivyo kila tunachofanyiwa tuone ni sheria kwetu.
Baada ya
miaka mitatu kupita wamejaribu kuweka karatasi mbili zinazoonyesha sehemu ya
makosa pasi na kuonesha ni nani anapaswa kusimamia mchakato mzima wa kesi kuwa
ni magereza au Hakimu, karatasi hizo mbili hazionyeshi haki wala wajibu wa
mahabusu akiwa gerezani.
Tunakutakia
kila la kheri na utendaji mwema katika kutekeleza majukumu yako kwa uadilifu.
Kwa niaba
ya Washtakiwa wote PI:29/2014 Mahakama ya Kisutu.
Mahabusu
Farid Hadi Ahmed
Gereza la
mahabusu Segerea Dar es Salaam.
NAKALA
1. Makamu wa Rais Jamhuri ya muungano Tanzania.
2. Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Tanzania.
3. Waziri wa Katiba na sheria Tanzania.
4. Mufti wa Tanzania (BAKWATA).
5. Kamishna Generali wa Magereza Tanzania.
6. Tanganyika law society(TLS) Tanzania.
7. Zanzibar law society (ZLS) Zanzibar.
Comments
Post a Comment