Featured Post

WACHINA WASHEHEREKEA MWAKA MPYA WAO KATIKA VIWANJA VYA MNAZI MMOJA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia  wakati wa maadhimisho ya sherehe za mwaka mpya wa Jamhuri ya Watu wa China zilizofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja  jijini Dar es Salaam.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea hundi ya shilingi milioni 70 kutoka kwa  Balozi wa China nchini Mhe. Dk. Lu Youqing iliyotolewa na Taasisi pamoja na Jumuiya ya Wachina wanaoishi Tanzania kuchangia shule ya msingi ya Chato iliyopo mkoani Geita wakati wa maadhimisho ya sherehe za mwaka mpya wa kichina zilizofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja  jijini Dar es Salaam.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na wageni wengine waalikwa pamoja na wasanii waliotumbuiza wakati wa maadhimisho ya sherehe za mwaka mpya wa kichina zilizofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja  jijini Dar es Salaam.
 Sehemuya watu waliohudhuria sherehe za mwaka mpya wa Kichina zilizofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa China nchini Mhe. Dk. Lu Youqing wakati wa maadhimisho ya sherehe za mwaka mpya wa Kichina zilizofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja  jijini Dar es Salaam
                                  ......................................................................................... 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Tanzania itaendelea kudumisha,kuimarisha na  kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na China kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa pande hizo MBILI.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam katika sherehe ya maadhimisho ya mwaka mpya wa Kichina hapa nchini sherehe ambazo zimehudhuriwa na mamia ya raia wa China na Tanzania.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa China imekuwa mshirika na mdau mkubwa wa maendeleo hapa nchini na hali hiyo inatokana na mahusiano mema na mazuri yaliyopo kati ya nchi hizi Mbili.


Makamu wa Rais amemhakikishia Balozi wa China hapa nchini Dkt Lu Youqing kuwa serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli itakuwa bega kwa bega na serikali ya China hasa katika uimarishaji wa sekta za biashara, utamaduni, elimu, afya  na masuala ya kijeshi kwa ajili ya maslahi na ustawi wa wananchi wa Tanzania na China.

Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kujifunza mambo mengi kutoka China ili kuharakisha shughuli za maendeleo za wananchi kutokana na Taifa la China kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo.


Amehimiza ubadilishanaji wa wataalamu kati ya Tanzania na China katika sekta mbalimbali kama hatua ya kuongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi nchini.

Kwa Upande wake, Balozi wa China hapa nchini Dkt Lu Youqing amepongeza hatua zinachukuliwa na serikali ya Tanzania katika kupambana na rushwa na ufisadi.

Dkt  Lu Youqing amesema serikali ya China na raia wake wanafurahishwa na hatua hizo kwa sababu zinalenga kuondoa na kukomesha rushwa na ufisadi kwani tabia hizo zikiachwa ziendelee zinachangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha utoaji wa huduma bora na za msingi kwa wananchi.


Akizungumzia mwaka mpya wa Kichina hapa nchini Balozi huyo amesema maadhimisho hayo ni muhimu kwa sababu raia Wachina na Tanzania wanajumuika pamoja katika kubadilisha mawazo na kutakiana heri na mafanikio kwa mwaka 2017.

Balozi huyo wa Tanzania hapa nchini Dkt  Lu Youqing pia amewashukuru wananchi wa Tanzania kwa kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Mnazi Moja katika kusheherekea sikukuu ya Mwaka mpya wa Kichina sherehe ambazo inapambwa na michezo mbalimbali ikiwemo sarakasi na vikundi vya ngoma asili kutoka China na maonyesho.
Katika Maadhimisho hayo, Balozi wa China nchini Tanzania Dkt  Lu Youqing amemkabidhi Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan mfano wa hundi ya shilingi milioni 70 fedha ambazo zitatumika katika ujenzi kwenye shule ya msingi Chato iliyopo mkoani Geita.

Comments