Featured Post

RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG - (SEHEMU YA 9)


Kulikuwa na ukimya, mara mlango ukafunguliwa na kijana mmoja ambaye alivalia nguo za kiraia akaingia. Alikuwa mtu wa aina ya wale wenye uchu wa kazi. Nilimuona kwamba kazi ya polisi haikuwa imemchosha. Alimtazama Retnick kama mbwa anavyomtazama bosi wake amrushie mfupa.
Akiwa anaonekana kutokuwa na hamu yoyote, kana kwamba anamtambulisha mtu asiye na uhusiano naye, Retnick akamuashiria kwangu.

“Huyu ni Nelson Ryan: mpelelezi wa kujitegemea. Mchukue na umchangamshe mpaka nitakapomhitaji.” Akanitazama. “Huyu ni Patter – ndiyo kwanza ameijiunga na jjeshi: usimhonge haraka kuliko inavyotakiwa.”
Nikaongozana na Patterson kwenye korido na kwenye chumba kingine kidogo ambacho kinuka uvundo wa jasho, hofu na dawa za kuulia wadudu. Niliketi karibu na dirisha wakati Patterson, akionekana kushangaa, akichuchumaa kwenye kona ya meza.
“Tulia,” nikamwambia. “Tutakuwa hapa kwa saa kadhaa. Bosi wako anataka kujirisha kama kweli nimemuua mwanamke wa Kichina na hana nafasi ya kuthibitisha hilo.”
Aliyakodoa macho yake wakati akinitazama.
Nikijaribu kumweka sawa, nikampatia sigara kubwa niliyovuta nusu ambayo Retnick alinipatia. “Hii inafaa kukaa makumbusho. Unaweza kuchukua ili uiweke kwenye orodha yako ya vitu vya makumbusho? Ni cigar kutoka kwa Retnick. Mna makumbusho hapa?”
Uso wake wa ujana ukabadilika kama jiwe. Akaonekana kama polisi halisi.
“Sikia wewe mwehu, ngoja nikueleze kitu. Hatutaki…”
“Ndiyo, ndiyo, ndiyo,” nikasema nikipunga mono kumkatisha. 
“Nimekwishasikia hilo kabla. Retnick analielezea vizuri. Mimi huwa nawatimulia vumbi. Ninaingia kwenye anga zenu. Ninawasumbua ninyi vijana. Sawa, kwahiyo nini? Ninatafuta mkate wangu kama ninyi. Siwezi kukutania kidogo au unataka uwe makini tu?”
Nikatabasamu, na baada ya kusita kidogo, naye akatabasamu. Tangu wakati huo tukaanza kuelewana.
Wakati wa mchana polisi mmoja akatuletea vipande vya nyama na maharage ambavyo tulivishambulia. Patterson alionekana akiamini kwamba chakula hicho kilikuwa kitamu, lakini ni kwa vile alikuwa bado kijana na alikuwa na njaa. Nilijilazimisha kula cha kwangu lakini nikakirudisha chote. Baada ya hicho kilichoitwa chakula cha mchana, akachukua kadi na tukaanza kucheza. Baada ya kumlamba kadi zote nikamuonyesha namna nilivyokuwa nikimwibia. Hiyo ikaonekana kumshtua hadi nikaamua kumfundisha namna nilivyokuwa nikifanya. Alikuwa mwanafunzi mzuri kwa sababu alielewa haraka.
Majira ya saa mbili usiku polisi yule yule akatuletea nyama nyingine na maharage. Tulikula kwa sababu kwa wakati huu tungekula chochote ambacho kingeletwa. Tukaendelea kucheza kadi ambapo naye akaniibia boksi zima. Wakati wa usiku mnene, simu ikaita. Akanyanyua mkonga, akasikiliza, halafu akasema, “Sawa, afande,” na kukata. “Luteni Retnick anakuhitaji sasa,” akasema akiinuka.
Sote tulijisikia kama vile watu wanavyojisikia wakati treni linapowasili stesheni na wanaweza kuacha kuongea kama watu wanavyoongea wakati wanapowasindikiza jamaa zao stesheni.
Tukafuata korido kuiendea ofisi ya Retnick. Retnick alikuwa ameketi mezani kwake. Alionekana amechoka na mwenye hofu. Aliniashiria niketi na kumwashiria Patterson aondoke. Wakati Patterson alipondoka, nikaketi.
Kulikuwa na ukimya mrefu wakati tukiwa tunatazamana. “Wewe ni mtu mwenye bahati, Ryan,” hatimaye akasema. “Sawa, sikudhani kwamba umemuua, lakini nilikuwa na uhakika kwamba Mwanasheria angeweza kuamini umemuua kama nikekukabidhi wewe wake. Sasa ninaweza kumshawishi kwamba hukumuua. Chukulia kwamba una bahati ya mtende mwanaharamu.”
Nimekuwepo kwenye jengo hili kwa saa 15. Kuna nyakati ambazo nilikuwa nafikiria kama nimeweza kuzichanga vyema karata zangu. Nilikuwa na nyakazi ambazo nilikuwa na mashaka, lakini sasa baada ya kusikia alichoniambia, nikatulia, nikivuta pumzi ndefu.
“Kwa hiyo nina bahati,” nikasema.
“Yeah.” Akatoka kwenye kiti chake ni kuiendea sigara yake kubwa. Lakini baada ya kugundua kwamba alikuwa na kipisi mdomoni mwake, akakitoa, akakitazama na kukitumbukiza kwenye ndoo ya takataka. “Niliamuru karibu jeshi lote la polisi kuifanyia kazi kadhia hii kwa saa 14 zilizopita. Tumemuona shahidi ambaye alikuona ukiwa kwenye gari yako saa nane na nusu leo asubuhi kwenye mtaa wa Connaught Boulevard. Shahidi anaonekana kwamba ni mwanasheria ambaye anamchukia Mwanasheria wa Wilaya na alikuwa na mkewe. Ushahidi wake ungeweza kuacha shimo kubwa katika mashtaka yoyote ambayo Mwanasheria wa Wilaya angeweza kukushtaki nato. Kwahiyo, sawa, hukumuua.”
“Itakuwa vibaya ikiwa nitauliza kama mna taarifa zozote ni nani aliyemuua?”
Akanipatia boksi lake la cigar: safari hii niliweza kumkatalia. Wakati akiliweka boksi hilo mfukoni mwake, akasema, “Ni mapema mno. Yeyote aliyefanya hivyo, amehakikisha anafanya kwa usahihi. Hakuna dalili: hakuna chochote mpaka sasa.”
“Hamkuweza kupata chhochote kuhusiana na mwanamke wa Kichina?”
“Oh, kweli, hilo halikuwa gumu. Hakukuwa na kitu chochote  bali ni vitu vya kawaida ambavyo wanawake hubeba kwenye mikoba yao, lakini alionekana uwanja wa ndege. Ametokea Hong Kong. Jina lake ni Jo-An Jefferson. Amini usiamini, ni mkamwana wa J. Wilbur Jefferson, milioni wa mafuta. Aliolewa na mwanawe, Herman Jefferson, huko Hong Kong takriba mwaka mmoja uliopita. Alikufa kwenye ajali ya gari na huyu mwanamke akaurejesha mwili wa mumewe kwa mazishi.”
“Kwanini?” nikauliza, nikimtazama.
“Mzee Jefferson alitaka mwanawe azikwe kwenye makaburi ya familia. Alimlipa mwanamke huyu aje na maiti.”
“Nini kilichotokea kuhusu maiti?”
“Ulichukuliwa uwanja wa ndege na kampuni maalum inayojihusisha na mazishi majira ya saa moja asubuhi, kwa maelekezo maalum. Maiti iko nyumbani kwake ikisubiri kuzikwa.”
“Umechunguza kuhusu hilo?”
Akapiga miayo, akinionyesha nusu ya meno yake ya bandia.
“Sikia, bwana mdogo, hutakiwi kuniambia majukumu yangu. Nimeliona jeneza na kukagua karatasi zote: kila kitu kiko sawa. Aliwasili kutoka Hong Kong, majira ya saa saba na nusu. Akachukua teksi kutoka uwanja wa ndege hadi ofisini kwako. Kinachonishangaza ni kwa nini alikuja kukuona wewe haraka baada ya kuwasili na muuaji wake alijuaje kwamba atakuja kukuona.  Nini ambacho alikuwa anakitaka kutoka kwako?”
“Yeah. Kama ametokea Hong Kong, amenifahamuje mimi?” nikasema.
“Maelezo yako kwamba alipiga simu kuweka miadi na wewe majira ya saa moja baada yaw ewe kuondoka ofisini hayana maana. Wakati huo alikuwa bado angani. Kama angekuwa ameandika, lazima ungekuwa umejua.”
Nikatafakari kwa muda.
“Chukulia kama Hardwick alikutana naye uwanja wa ndege? Alinipigia kutoka uwanja wa ndege saa kumi na mbili. Pengine alimsubiri awasili na kumweleza kwamba alikuwa pamoja nami. Pengine alimfuata wakati akiwa anaendelea kushughulikia kupitisha jeneza na kufunga kitasa kwa nje. Kitasa siyo kigumu kukifungua na baadaye akamsubiri.
Retnick hakuonekana kuyapenda mawazo haya: hata mimi sikuyapenda.
“Lakini nini ambacho alikuwa anakihitaji kwa mwanamke huyu?” akauliza.
“Kama tungejua hayo tusingekuwa tunaulizana maswali. Vipi kuhusu mizigo yake? Umeweza kuipata?”
“Ndiyo. Aliihifadhi kwenye ofisi mojawapo pale kabla ya kuondoa uwanja wa ndege: mkoba mmoja mdogo; hakuna kitu cha mamana isipokuwa nguo za kubadili, kinyago kidogo cha Buddha na vijiti vya kulia chakula. Alisafiri kirahisi sana.”
“Umezungumza na Mzee Jefferson?”
Akatafakari.
“Ndiyo, nimezungumza naye. Alionekana kana kwamba alikuwa akichukia uwepo wangu. Nadhani ananichukia. Hilo ndilo tatizo la kuolewa katika familia tajiri. Shemeji yangu na Jefferson wanaelewana sana kama ambavyo mimi ninavyoelewa na majipu shingoni mwangu.”
“Bado kuna fadhila zake,” nikamwambia.
Kaipapasa tepe yake.
“Wakati mwingine. Huwezi amini, kizee yule hakutaka nywele zake  zidondoke. Alisema ananitaka nimkamate mara moja mtu aliyemuua mkamwana wake, vinginevyo kutakuwa na matatizo.” Akapangusa pua yake ndefu. “Anafanya mambo makubwa kwenye mji huu. Anaweza kunisababishia matatizo.”
“hakuweza kukusaidia?”
“hakuweza kabisa, hakuwa na msaada wowote.”
“Vipi kuhusu mesenja wa kampuni ya Express aliyeniletea dola mia tatu? Pengine anaweza kuwa amemuona muuaji.”
“Tazama, bwanamdogo, wewe haufikii hata nusu ya mpira wa moto kama unavyodhani. Nimechunguza: hakuna. Lakini kuna hili linalovutia: bahasha iliyokuwa na fedha ilikabidhiwa majira ya saa kumi kwenye makao makuu ya kampuni ya Express ambayo kama unavyojua iko jirani na kwako. Hakuna karani yoyote anayekumbuka nani aliyepeleka bahasha hiyo, lakini maelekezo yalikuwa kwamba lazima wawasilishe kwako saa kumi na mbili na robo.”
“Umechunguza kampuni ya Herron Corporation kujiridhisha kama  Hardwick anafanya kazi pale?”
“Ndiyo. Nimechunguza kila kitu. Hafanyi kazi pale.” Alipiga mwayo, akajinyoosha, halafu akasimama. “Ninakwenda kulala. Pengine kesho ninaweza kupata chochote. Kwa sasa inatosha.”
Nami nikasimama pia.
“Ni bastola yangu ndiyo iliyomuua?”
“Ndiyo. Hakuna  alama: hakuna hata kwenye gari. Muuaji ni mtaalamu, lakini atafanya kosa mahali tu . . . daima huwa wanafanya makosa.”
“Baadhi yao.”
Alinitazama kwa jicho la usingizi.
“Nimekusaidia, Ryan, jaribu kunisaidia pia. Mawazo yoyote utakayoyapata, hakikisha unanishirikisha. Kwa sasa ninahitaji mawazo.”
Nilimwambia katu sitamsahau. Nilishuka chini hadi nilipoliacha gari langu na kuendesha haraka mpaka nyumbani na kitandani.

Itaendelea kesho...

Comments