Featured Post

RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG - (SEHEMU YA 8)



Nyuma ya makao makuu ya polisi kuna uwanja mkubwa uliozungukwa na ukuta wenye kimo cha futi nane. Hapa ndipo polisi wanapoegesha magari ya doria, magari ya dharura na magari ya kasi ambayo yanaweza kukimbia kwenye dharura yoyote.
Katika ukuta mmoja kuna bango kubwa jeupe linalosema katika herufi kubwa nyeusi kwamba eneo hili ni maegesho ya gari za polisi tu.

Niliingiza gari langu kwenye geti na kuegesha pembeni mwa gari la doria. Wakati nikizima injini, polisi akatokea kusikojulikana, uso wake mwekundu ukionyesha hasira na ghadhabu.
“Hey! Una matatizo gani? Huwezi kusoma?” alimaka kwa sauti ya juu ambayo ingeweza kusikika katika majengo mawili ya mbele.
“Sina tatizo kabisa,” nilisema huku nikiondoa ufunguo, “na ninaweza kusoma—hata maneno marefu.”
Nilidhani angeweza kuvimba na kupasuka. Kwa muda alifungua na kuufunga mdomo wake wakati akijaribu kupanga maneno makali zaidi kwa tukio hilo.
Kabla hajatamka lolote, nikasema, nikitabasamu kupitia kwenye dirisha la gari langu, “Luteni Retnick, shemeji yake Meya, ameniambia niegeshe hapa. Nenda kamwambie kama unaona limekukera, lakini usinilaumu kama utapigwa.”
Alionekana kana kwamba amemeza nyuki. Kwa sekunde mbili alinitazama, mdomo ukiwa wazi, halafu akaondoka.
Nilikaa nikiangalia juu kwa karibu dakika ishirini, baadaye gari likaingia mahali pa maegesho umbali wa futi kumi kutoka nilipokuwepo. Retnick aliteremka na kuelekea katika mlango katika jengo la mawe ambalo ndilo lilikuwa makao makuu ya polisi.
“Luteni. . .”
Nilisema kwa sauti ya chini lakini akanisikia. Akageuka kunitazama. Akaganda kama mtu aliyeunguzwa na chuma, halafu akaja haraka.
“Unadhani unafanya nini hapa?” akauliza.
“Nilikuwa nakusubiri,” nikamwambia.
Akatafakari hayo, akinitazama kwa makini.
“Sawa, niko hapa —unasemaje?”
Nikatoka nje ya gari.
“Umenipekua, Luteni, lakini umesahau kupekua gari langu.”
Akaendelea kuganda, akipumua kwa nguvu kupitia kwenye pua zake kubwa, macho yake makubwa yakiwa yamemtoka pima.
“Kwa nini nipekue gari lako, shamus?”
“Ulitaka kujua yule mwenye ngozi ya manjano, kama unavyomwita, alikuwa nacho kwenye mkoba wake ambacho kimenishawishi nimuue ofisini kwangu na kwa bastola yangu. Hukukiona ofisini kwangu wala kwenye mifuko yangu. Nilidhani polisi mdadisi angeweza kupekua gari langu kujiridhisha kwamba sijaficha chochote katika mauaji haya. Kwa hiyo nimeleta gari langu ikiwa una haja ya kuwa polisi mdadisi.”
Uso wake ukafura kwa hasira.
“Sikia, wewe mwanaharamu,” akatamka. “Sitaki kusikia maneno ya ujanja ujanja kwa mpuuzi kama wewe. Nitamwambia Pulski akushughulikie! Atakutoa pumzi! Una bahati ya kuendelea kuwa hivi!”
“Vyema uangalie kwenye gari kwanza kabla hujanikabidhi kwa huyo msagaji wa nyama, Luteni. Tazama kwenye saraka. Itaokoa muda.” Nikasogea pembeni ya gari, nikiuacha mlango wazi.
Macho yake yakiwa yanapepesa, Retnick akainama kwenye gari na kufungua saraka.
Nilikuwa namtazama mwitikio wake. Hasira zake zikatoweka. Hakuweza kugusa bastola wala mkoba. Aliangalia kwa muda, kisha akanigeukia.
“Hii ndiyo bunduki yako?”
“Ndiyo.”
“Mkoba wake?”
“Inaongeza, au siyo?”
Akanitazama, akiwa amechanganyikiwa.
“Ni nini kinachoendelea? Uko tayari kuandika maelezo kukiri kwamba umemuua?”
“Ninaziweka karata wazi kwa kadiri zinavyochezwa dhidi yangu,” nilimwambia. “Siwezi kufanya zaidi ya hivyo. Ni juu yako utakavyo amua mwenyewe.”
Akamuashiria polisi aliyekuwa akilinda geti. Polisi huyo alipokuja, Retnick alimwambia amwite Pulski haraka.
Wakati tukisubiri, Retnick kwa mara nyingine akaitazama bastola na mkoba bila kuugusa.
“Nisingeweza kuunganisha mambo mawili kwa nafasi yako ya kujinasua,” akasema. “Siyo mambo mawili.”
“Nisingeweza kuunganisha mambo mawili peke yangu kama nisingekuja hapa kukuonyesha kile nilichokiona,” nikamwambia, “lakini kwa vile nimekuja, nitacheza bahati nasibu ya mambo mawili, si zaidi.”
“Daima unafunga mlango wa gari lako?” akauliza, akinitazama huku ubongo wake ukitafakari.
“Ndiyo, lakini nina ufunguo wa ziada kwenye saraka mahali ninapoweka bastola yangu. Sikuangalia lakini ninadhani haupo kwa sasa.”
Retnick akajikuna shavuni kwa nguvu.
“Hiyo ni kweli. Nilipokuwa natafuta bastola, sikuuona ufunguo.”
Pulski akaja kwa kasi kwenye maegesho.
“Chunguza gari hili,” Retnick akamwamuru. “Chunguza kila itu. Kuwa makini unaposhughulikia bastola na mkoba. Endelea.”
Akaniashiria na tukaondoka pale, tukapandisha ngazi, hadi mlangoni na kwenye korido ambayo ilinukia harufu ile ile inayopatikana katika majumba yote ya polisi.
Tulipita kwenye korido, tukapandisha ngazi, tukafuanga korido nyingine na kuingia kwenye chumba kimoja kidogo kama kibanda cha kuku. Kulikuwa wa meza, viti viwili, kabati na dirisha. Kilikuwa chumba kisicholeta matumaini kama chumba cha yatima.
Retnick akaniashiria niketi kwenye kkiti cha wageni wakati mwenyewe akizunguka meza na kuketi kwenye kiti kilichokuwa nyuma ya meza hiyo.
“Hii ndiyo ofisi yako?” Nikamuuliza kwa shauku. “Nilitegemea kwa kuwa wewe ni shemeji yake Meya, wangekupatia sehemu nzuri zaidi.”
“Usijali namna ninavyoishi: fikiria kwenye mkasa ulio mbele yako,” alisema Retnick. “Kama ile ndiyo bastola iliyomuua yule msichana na kama ule ndio mkoba wake, wewe jihesabu kama maiti tayari.”
“ndivyo unanvyodhani?” Nikamwambia, nikijaribu kuketi vyema kwenye kiti. “Unajua kwa dakika kumi, pengine zaidi, nilikuwa nikipambana na dhamira yangu kwamba nikaitumbikize bastola na mkoba baharini na kama ningefanya hivyo, Luteni, si wewe wala vijana wako wapelelezi wanaosimamia sheria kwenye mji huu ambao wangeweza kuwa na busara za kujua, lakini nikaona bora nikupunguzie kazi.”
“Unamaanisha nini unaposema hivyo?”
“Sikuvitumbukiza baharini vitu hivi kwa sababu vimepandikizwa makusudi ndani ya gari langu. Yote hii inaongeza mashaka na ukweli kwamba huu ni mtego – tukio lote hili ni mtego. Kama ningevitumbukiza, usingekuwa na uwezo wa kuitatua kesi hii.”
Akainamisha kichwa chake upande: alikuwa amezowea kufanya hivyo.
“Kwa hiyo nina bastola na mkoba: nini kinachokufanya udhani kwamba nitaitatua kesi hii?”
“Kwa sababu hutaweza tena kunikazania mimi, utakwenda kujikita katika kumsaka muuaji na hicho ndicho kitu ambacho hataki wewe ukifanye.”
Alitafakari kwa muda mrefu, halafu akachukua kasha la sigara zake kubwa na kunipatia. Hili lilikuwa ni jambo la kwanza la kirafiki kulifanya kwangu katika kipindi cha miaka mitano tuliyofahamiana. Nilichukua hiyo cigar kumuonyesha kushukuru japokuwa mimi si mvutaji wa cigar.
Tuliwasha na kuanza kupuliziana moshi.
“Sawa, Ryan,” alisema. “Ninakuamini. Ningependa kufikiria kwamba ulimuua, lakini mambo yote naona kama yanarudi nyuma. Nitakuwa ninajipunguzia matatizo mengi na muda kama nitaamini, lakini siwezi. Wewe ni mpelelezi mjanja mjanja tu, lakini siyo mjinga. Sawa, kwa hiyo nimekubaliana na wewe. Umewekewa mtego.”
Nikapumua.
“Lakini usinitegemee sana,” akaendelea. “Tatizo litakuwa kumshawishi Mwanasheria wa Wilaya (D.A). Yule ni mwanaharamu ambaye hawezi kusikiliza kitu. Mara atakajua nini nilichokipata kwako, atakuja mbio kama faru. Kwanini ajjisumbue wakati tayari amepata kesi ya kusimamia?”
Hakukuwa na jambo lolote la kusema kuhusu hilo hivyo nikabaki kimya.
Akatazama nje ya dirisha ambako kulionekana taswira ya jumba ambako kulianikwa nguo zilizofuliwa bila kutakata na mbeleko za watoto zikiwa zimeanikwa kwenye ngazi.
“Ninapaswa kuchunguza kwanza kabla sijaamua kuhusu wewe,” hatimaye akasema. “Nitakufanya kama shahidi muhimu au nitakutaka uwepo hapa. Unasemaje kuhusu hayo?”
“Nitabaki hapa,” nikasema.
Akanyanyua mkonga wa simu yake.
“Ninakuhitaji,” alisema mara baada ya sauti ya upande wa pili kupokea simu hiyo.
Itaendelea kesho...

Comments