- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
James Hadley
Chase
Kionjo
KIFO CHA BINTI . . .
ZILIKUWA ni dola mia tatu rahisi zaidi ambazo Nelson Ryan ameweza kuzipata,
lakini ghafla akagundua kwamba alikuwa amejiingiza mtegoni. Mwito wa simu,
ukionekana hauna kasoro yoyote, ulimwongoza kwenye mauaji ya binti wa Kichina
aliyepiga simu huku akiongea sana. Simu hiyo pia ikamwongoza moja kwa moja
kwenye maisha ya kihalifu ya Hong Kong. Tangu sasa na kuendelea, Ryan hakuweza
kufanya chochote mpaka atakapompata muuaji ambaye amemwingiza kwenye majanga.
Sauti ya mtu asiyefahamika kutoka kwenye simu; msichana mrembo wa
Kichina ameuawa; mzee tajiri ambaye anaonekana kuchanganyikiwa; mpelelezi wa
kujitegemea anayehusishwa na mauaji; kahaba wa Kichina aliyezungumza maneno
mengi; na jeneza. Kuna vionjo vingine vya kuvutia vya riwaya hii ya kusisimua
ya James Hadley Chase. Ni kitabu ambacho kitapeperusha usingizi wako na
kukufanya uendelee kukisoma hawa wenzako wanapokuwa wanakoroma usiku.
Sura
ya Kwanza
Nilikuwa
najiandaa kufunga mlango wa ofisi jioni hii wakati kengele ya simu ilipolia. Ilikuwa
yapata saa kumi na mbili na dakika kumi. Ilikuwa siku mbovu, ndefu na isiyo na
tija: hakuna mgeni aliyekuja, barua niliyoitumbukiza kwenye kasha la takataka
bila hata kuifungua, na sasa hii simu ya kwanza.
Nilinyanyua mkonga wa simu na kusema, “Nelson Ryan.” Sauti yangu
ikionyesha mshtuko na tashwishi kwa kadiri nilivyoweza.
Kulikuwa na utulivu. Kwenye laini iliyokuwa wazi niliweza kusikia
sauti ya injini ya ndege ikianza kuunguruma. Muungurumo ukasikika kwa muda,
kisha ukapotelea kwenye kelele za upande wa pili kana kwamba mpigaji wa simu
hiyo alikuwa ameufunga mlango wa kibanda cha simu.
“Bwana Ryan?”
Sauti ya mwanamume: nzito na yenye msisitizo.
“Ndiye mimi.”
“Wewe ni mpelelezi wa kujitegemea?”
“Ni sahihi pia.”
Kulikuwa na ukimya wa muda. Nilisikiliza jinsi alivyokuwa akipumua
taratibu na kwa nguvu: ni wazi alikuwa akisikiliza nilivyokuwa napumua. Kisha
akasema: “Nina dakika chache tu. Niko uwanja wa ndege. Nataka nikukodi.”
Nikachukua kidaftari kidogo.
“Unaitwa nani na uko wapi?” Nikamuuliza.
“John Hardwick, 33 Connaught Boulevard.”
Wakati nikiandika anuani hiyo kwenye karatasi, nikamuuliza, “Nini
unachotaka nikifanye, Bwana Hardwick?”
“Nataka umchunguze mke wangu.” Kulikuwa na ukimya mwingine wakati
ndege nyingine ikiruka. Alisema kitu fulani ambacho hakikusikika vizuri
kutokana na miungurumo wa injini za ndege.
“Sijasikia vizuri, Bwana Hardwick.”
Alisubiri mpaka ndege ilipokuwa imeruka, halafu akizungumza kwa
haraka, akasema, “Biashara zangu mara nyingi zinanifanya niende New York mara
mbili kwa mwezi. Ninahisi kwamba ninapokuwa safarini, mke wangu anakuwa na
mwenendo usiofaa. Nataka umfuatilie. Nitarejea keshokutwa - Ijumaa. Nataka
kujua nini anachokifanya ninapokuwa safarini. Itagharimu kiasi gani?”
Hii haikuwa aina ya kazi nilizokuwa nazipokea, lakini walau
ilikuwa nzuri kuliko kutokuwa na kazi. “Kazi yako hasa ni nini, Bwana Hardwick?”
Alizungumza kwa namna ya ghadhabu kidogo. “Nikon a Herron, watu
wanaotengeneza maplastiki.”
Herron Corporation ilikuwa moja ya kampuni kubwa kwenye ukanda huu
wa Pwani ya Pacific. Robo ya ustawi wa Jiji la Pasadena ulitokana na kampuni
hii.
“Dola hamsini kwa simu na gharama nyinginezo,” nilisema,
nikizidisha kuliko gharama zangu za kawaida kwa ziada ya dola kumi.
“Hakuna shida. Nitakutumia dola mia tatu sasa hivi kama malipo ya
utangulizi. Nataka umfuatilie mke wangu popote anakokwenda. Kama haondoki
nyumbani, nataka kujua nani anayemtembelea.
Unaweza kufanya hivyo?”
Kwa dola mia tatu ningeweza kufanya mambo magumu zaidi.
Nikamwambia, “Nitafanya, lakini huwezi kuja hapa unione, Bwana Hardwick? Ninapenda
kukutana na wateja wangu.”
“Ninatambua hilo lakini nimeamua tu kuchukua hatua. Niko njiani
kuelekea New York, lakini nitakuona Ijumaa. Nataka tu kuhakikisha kama unaweza
kumchunguza ninapokuwa safarini.”
“Usiwe na shaka kabisa,” nilimwambia, halafu nikatulia kupisha
muungurumo wa ndege nyingine iliyokuwa ikitua. “Nitapenda kupata maelezo ya
jinsi alivyo mkeo, Bwana Hardwick.”
“Thelathini na tatu Connaught Boulevard,” alisema. “Wananiita. Lazima
niondoke. Tutaonana Ijumaa,” na simu ikakatwa.
Nilirejesha mkonga wa simu na kuchukua sigara kutoka kwenye boksi
lililokuwa juu ya dawati. Nikawasha sigara kwa kiwashio cha kwenye dawati na
kupuliza moshi kuelekea kwenye ukuta niliokuwa natazamana nao.
Nimekuwa nikifanya kazi hii ya upelelezi kwa miaka mitano
iliyopita, na katika kipindi hicho, nimekumbana na utapeli mwingi. Huyu John
Hardwick anaweza kuwa mmoja wao, lakini kwa namna fulani nilifikiri kwamba
hawezi kuwa hivyo. Alionekana kama mtu aliyekuwa katika shinikizo. Pengine
alikuwa ana hofu kwa miezi kadhaa kuhusu mwenendo wa mkewe. Pengine kwa muda
mrefu amekuwa akimhisi akimfanyia hiana wakati yeye akiwa safarini na ghafla,
wakati akiwa anaondoka kwa safari nyingine ya kikazi, hatimaye akawa ameamua
kumchunguza. Ilikuwa ni jambo la kawaida kwa mtu mwenye hofu, asiye na furaha
kulifanya baada ya wazo kumjia bila kusubiri. Yote kwa yote, sikuipenda sana.
Siwapendi wateja wasiofahamika. Sipendi kusikia sauti za ajabu kwenye simu.
Napenda kujua ninafanya kazi na nani. Mpango huu ulionekana wa ghafla na wenye
utata.
Wakati nikitafakari taarifa nilizozipata kwa mtu huyo, nilisikia
vishindo vikija ofisini kwangu. Mlango uligongwa, kisha ukafunguka.
Itaendelea
kesho…
Comments
Post a Comment