Featured Post

NJIA NYINGI ZA UMEME KUJENGWA ILI NCHI ZIUZIANE

NA VERONICA MHETA, ARUSHA
TANZANIA imeanza kujenga miundombinu ya kusafirisha umeme mwingi, ili nchi nyingine zinunue na kuuza kwenye maeneo mbalimbali Afrika, kwa lengo la kuondokana na umeme wa mafuta wa bei ya juu, unaonunuliwa kutoka kwenye nchi unakozalishwa barani humo.

Akizungumza baada ya kufunga mkutano wa wanachama wa ushirikiano wa mambo ya umeme, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo mwishoni mwa wiki alisema kuwa wakati umefika kwa nchi za Afrika kujenga njia za umeme ili kuuziana nishati hiyo kwa wingi, uhakika na kwa bei nafuu.
Alisema nchi nyingine duniani kama Marekani hununua umeme Canada.
Alisema ili biashara ya kuuziana umeme ifanikiwe, lazima kuwe na njia za kuusafirisha.
Alisema Tanzania imeanza kwa kujenga njia kutoka Singida hadi Kenya na Kenya wanajenga hadi Ethiopia, hivyo zitakapokamilika na kupitisha maamuzi katika kikao cha Uganda kitakachofanyika Aprili mwaka huu, wataanza utekelezaji.
Pia, alisema njia nyingine zinajengwa Mbeya hadi Zambia na wanaendelea kujenga pale watakapoona kuna uhitaji wa kufanya hivyo ili Tanzania inunue na kuuza umeme.
Alisema wanaamini pia watakapokamilisha hatua hizo, nchi itapata wawekezaji wengi, kwa sababu hivi sasa uwekezaji wa nishati upo juu na wawekezaji wengi wanataka kuja nchini.
Alisisitiza kuwa serikali ipo makini kwani umeme unaozalishwa katika Mradi wa Backbone kutoka Iringa hadi Shinyanga umeongezeka mara mbili uzalishaji wake na kunufaisha wananchi wa mikoa inayopata huduma hiyo.
CHANZO: HABARILEO

Comments