Featured Post

MAWAKALA MPAKA WA TUNDUMA/NAKONDE WAONYWA KUKWAMISHA BIASHARA



Na Benny Mwaipaja, WFM, Songwe 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda, amewaonya mawakala wa forodha katika mpaka wa Tanzania na Zambia wa Tunduma/Nakonde kuacha Mara moja tabia ya kuwachelewesha madereva wa malori yaendayo masafa marefu kwa makusudi ili wapewe rushwa.


Prof. Mkenda ametoa onyo hilo katika mpaka huo wa Tunduma na Nakonde, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya madereva wa malori waliodai wamekuwa wakicheleweshwa kuvuka mpaka huo kwa zaidi ya siku tatu hadi tano.

Wadereva hao wameeleza kuwa mawakala wa forodha wamekuwa wakiwaambia kuwa nyaraka zao zinazohusika na mizigo wanayosafirisha zimekuwa zilicheleshwa na kituo cha Forodha upande wa Zambia.

Hata hivyo Meneja wa Mamlaka ya Mapato Zambia (ZRA), Kituo cha Nakonde, Bw. Nase Lungu, amekana kuhusika na ucheleweshaji huo na baada ya ukaguzi wa moja ya nyaraka hizo ilibainika kuwa upande wa Zambia unatoa nyaraka hizo kwa wakati lakini zimekuwa zikifichwa na Mawakala wa Forodha upande wa Tanzania.

Wakitoa ufafanuzi wa tuhuma hizo, madereva hao wamesema kuwa mawakala wa forodha kwa muda mrefu wamekuwa wakiwaeleza kuwa mtandao wa intaneti wa Upande wa Zambia unaotumika kuchakata nyaraka zao uko chini, hivyo walitakiwa kutoa shilingi 10,000 kwa kila nyaraka ili "kurahisisha" kazi hiyo kwa kuwapa kitu kidogo maafisa wa forodha wa Zambia.

"Mawakala wengine wa forodha wana nyumba zao za kulala wageni hapa Tunduma kumbe wanatulazimisha kukaa hapa ili tulale kwenye nyumba hizo hali inayotutia hasara na wanatumia kutokujua kwetu kutudanganya kwamba mtandao uko chini wakijua hatuna uwezo wa kufuatilia huko Zambia" alieleza kwa masikitiko dereva mmoja 

Baada ya kubaini uwepo wa vitendo hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda, ameagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA upande wa Tunduma kuandika kibao chenye namba za simu za Mkuu wa TRA mpakani hapo zitakazotumiwa na madereva wanaocheleweshwa kwa makusudi kutoa malalamiko yao.

"Tunataka madereva mtumie siku moja tu kukamilisha nyaraka zenu ili muendelee na safari yenu vinginevyo tutadumaza biashara kati ya Zambia na Tanzania na pia tutaifanya Bandari yetu ya Dar es salaam kushindwa kuleta tija" aliongeza Prof. Mkenda 

Alisema kuwa wakala wa forodha atakayebainika kufanya mchezo huo mchafu wa kuwarubuni madereva na kuwachelewesha kupeleka mizigo nchini Zambia, watanyang'anywa leseni zao za biashara.

Meneja Msaidizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, mikoa ya Songwe na Mbeya, Bw. Jomimassa Nsindo, amesema kuwa ofisi yake itashirikiana na madereva kukomesha vitendo hivyo ambavyo amesema vinaharibu uchumi na biashara mpakani hapo.

Naye Mkuu wa wilaya ya Momba, mkoani Songwe, Bw. Juma Irando, alisema kuwa ataitisha kikao cha Madereva, Mawakala wa Forodha na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA katika Mpaka huo wa Tunduma/Nakonde mapema, ili kuweka msimamo wa serikali na kuwaeleza wahusika wanaokiuka taratibu hatua watakazochukuliwa.

Prof. Mkenda na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, walikwenda katika mpaka huo wa Tunduma na Nakonde, kuangalia maandalizi ya uanzishwaji wa Kituo cha Pamoja cha Mpakani kati ya Tanzania na Zambia, unaotarajiwa kuanza Februari mosi, 2017, baada ya kusainiwa kwa mikataba kati ya nchi hizo mbili, juzi.

Comments