- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
MAUAJI YA ALBINO - 1: NILIPAMBANA, NIKASIKIA PA! KICHWANI, NILIPOZINDUKA KIGANJA CHA BARAKA KILIKUWA KIMEKATWA
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mtoto
Baraka (6) akilia kwa maumivu makali wakati akiuguza mkono wake katika
Hospitali ya Rufaa Mbeya baada ya kukatwa kitanga.
Bi. Prisca Mpesya akiwa na jeraha kichwani na mimba ikimuelemea huku mgongoni amembeba mwanawe Lucia (3) wakati akimuuguza mwanaye Baraka ambaye alikatwa kitanga cha mkono kwa kuwa tu ni albino. (PICHA NA DANIEL MBEGA/MAENDELEOVIJIJINI BLOG)
Na Daniel Mbega, Sumbawanga
PRISCA Shaaban Mpesya (29), mkazi wa
Kitongoji cha Kikonde, Kijiji cha Kaoze katika Kata na Tarafa ya Kipeta wilayani
Sumbawanga mkoani Rukwa, alikuwa analia kimya kimya.
Alimtazama mwanaye Baraka (6) aliyening’iniza
mkono wa kulia huku akilia kwa maumivu baada ya kukatwa kitanga cha mkono na ‘watu
wasiojulikana’ wanaosaka utajiri, kwa sababu yeye ni albino na wanadai viungo
vyake ni ‘dili’.
Kwa Prisca, kuzaa watoto wenye albinism
inaonekana ni majanga kwake na kizazi chake, hasa katika kipindi ambacho
matukio ya mauaji, kutekwa nyara na kukatwa viungo vya albino yameshamiri
Tanzania na Afrika Mashariki na Kati.
Anajaribu kukumbuka tukio hilo la usiku wa
Jumamosi, Machi 7, 2015 alivyonusurika kufa yeye na mwanaye Baraka.
“Nilikuwa natoka nje kwenda kujisaidia,
sijui ilikuwa saa ngapi kwa sababu sikuwa na saa, nje juu ya mlango tuliweka
taa ya Mchina ya solar ambayo ilikuwa inaangaza, hivyo sikuwa na hofu,” ndivyo
anavyoanza kumsimulia mwandishi wa MaendeleoVijijini wakati alipokuwa amelazwa kwenye
Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Anasema ghafla tu alipofika mlangoni
akashtuka kuona mtu akija mbio, akaipiga taa na kuivunja, kukawa giza.
“Nikajua huyu hakuwa mwema, hivyo
nikajiandaa kupambana naye, alikuwa mwanamume mwenye nguvu kunishinda, lakini
nilimdhibiti kwa sababu alitaka kuingia ndani kwa nguvu nami sikutaka kwa
sababu wanangu walikuwa wamelala chini angeweza kuwaumiza.
“Mara nikasikia kitu kikinipiga kichwani
pa! Nikaanguka na kupoteza fahamu. Nilipozinduka nikamwona mwanangu Baraka
analia, kitanga cha mkono kimekatwa.” Akaongeza: “Natamani watu wanaofanya
mambo haya wauawe hadharani.”
Michirizi ya damu na alama za panga mahali ambapo Baraka alikatwa kiganja wakati akiwa amelala na ndugu zake.
Mwandishi wa makala haya (mwenye jezi nyekundu na kofia la sweta) akiwa katika eneo la tukio pamoja na wanausalama.
Nyumba ya Cosmas Songoloka, baba wa Baraka, mahali tukio lilipofanyika.
Anasema, mumewe Cosmas Yoramu Songoloka hakuwepo
kwani alikuwa ameaga tangu mchana kwamba anakwenda kilabuni kunywa pombe, na
mpaka majira hayo hakujua kama alikuwa kilabuni ama alikwenda kwa mke mdogo
ingawa haikuwa zamu yake.
Baraka Cosmas Yoramu alikatwa kitanga cha
mkono wa kulia na watu ‘wasiojulikana’ Machi 7, 2015 majira ya saa 2 usiku kwa
imani za kujipatia utajiri wa kishirikina.
Jitihada za kupata tiba katika kituo cha
afya Kamsamba wilayani Sumbawanga zilishindikana, hivyo kukimbizwa katika
Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Prisca anasema, pamoja na ujauzito aliokuwa
nao wakati huo, lakini hakuhisi chochote zaidi ya kuwalinda wanawe, zawadi
pekee aliyopewa na Mwenyezi Mungu.
“Nimehangaika na mimba zao kwa nyakati
tofauti, sikuwa tayari kuona wanapata madhara, ndiyo maana niliisahau hata hali
yangu nikaamua kupambana,” anasema.
Maumivu ya jeraha lake la kichwani
alilopata kwa kupigwa na ‘kitu kizito’ yalionekana siyo kitu kwa wakati huo,
kwa sababu binti yake Lucia (3) ambaye ana albinism pia alikuwa anamsumbua
hospitalini, na kwa umri wake, alikuwa hajui kinachoendelea.
Lakini kubwa zaidi ni kwamba, mwanaye
mchanga wa kiume aliye albino, ambaye ndiyo kwanza alikuwa ametoka kujifungua,
naye alikuwa analia akitaka kunyonya.
Sasa anao watoto watatu wenye albinism kati
ya wanne, akiwemo huyo mdogo ambaye kwa sasa ametimiza mwaka mmoja na nusu tangu
alipozaliwa Aprili 2015 kwenye Hospitali ya Rufaa Mbeya wakati akiuguza jeraha
lake kichwani pamoja na kumuuguza mwanaye Baraka jeraha la mkono.
Bi. Prisca alifikishwa
hospitalini hapo Machi 8, 2015 huku akiwa amembeba mwanaye Lucia na mimba ya
miezi karibu nane ikiwa imemuelemea.
“Nisingeweza kumwacha Lucia kule porini kwa
sababu watu wabaya wangeweza kumjia,” alisema.
Mtoto wake mkubwa, Shukuru (8), alimwacha
kijijini wakati mumewe Cosmas akiwa mahabusu kuhusiana na tukio hilo.
Mwandishi wa MaendeleoVijijini, ambaye amefanya
utafiti wa mauaji ya albino kwa miezi nane mfululizo, alibahatika kuongozana na
polisi katika msako wa ‘watu hao wasiojulikana’ kwenye matukio yaliyotokea
mwaka 2015 likiwemo la kukatwa kiganja mtoto Baraka, ambapo alipiga kambi mjini
Sumbawanga kwa takriban miezi miwili na kushuhudia maofisa wa polisi
walivyowakamata wahusika wa tukio hilo, akiwemo Sajenti Kalinga Malonji, ‘tajiri’
ambaye ndiye aliyepelekewa kiganja hicho na kuahidi kuwapatia wenzake mamilioni
ya fedha.
Uchunguzi wa MaendeleoVijijini unaonyesha kwamba, haikuwa kazi rahisi kuwapata watuhumiwa, na
hasa ‘tajiri’ mwenyewe, Sajenti, mkazi wa Kijiji cha Hanseketwa wilayani Mbozi
mkoani Songwe, kwani mwanahabari huyu, akiongozana pia na maofisa hao wa
polisi, walikesha kwa siku tatu mfululizo wakimsaka mtuhumiwa jijini Dar es
Salaam na hatimaye saa 8:30 usiku wa kuamkia Aprili 25, 2015 akatiwa mbaroni na
kurudishwa kijijini kwake kuonyesha kilipo kitanga hicho cha mkono.
Kitanga cha mkono wa Baraka kikiwa kimeoza na kutoa funza baada ya kupatikana.
Mtuhumiwa Sajenti Kalinga Malonji akiwa na pingu mkononi baada ya kukishusha kitanga cha mkono wa Baraka ambacho alikuwa amekificha juu ya mti nyumbani kwake katika Kijiji cha Hanseketwa wilayani Mbozi mkoani Mbeya. Hii ni baada ya kukamatwa na wanausalama jijini Dar es Salaam na kwenda kukionyesha kiganja hicho.
Alikuwa amekificha juu ya mti, nje ya
nyumba yake, na Aprili 26, 2015 majira ya saa 4:00 asubuhi, mbele ya viongozi
wa kijiji na wananchi mbalimbali, akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi wenye
silaha, alipanda mwenyewe juu ya mti na kukiteremsha chini. Tayari
kilikwishaoza na kutoa funza.
Sajenti Kalinga, ambaye alitajwa na
watuhumiwa wenzake waliokuwa mahabusu, akaunganishwa kwenye kesi hiyo pamoja na
baba wa mtoto, Cosmas, Andius George Songoloka (mdogo wa Cosmas), Unela Jiloya
Shinji Kuwilu Seme (anayedaiwa kukiri polisi kwamba ndiye aliyekata kiganja na
ndiye aliyewaongoza polisi hadi kumkamata ‘tajiri’ Kalinga), na Mihambo
Kanyenga Kamata maarufu kama Bichi (ambaye ni mganga wa jadi).
Mtuhumiwa
mwingine Mwendesha William Mola alifutiwa mashtaka kwa utaratibu wa Nolle Prosequi katika kesi hiyo ambayo
iko katika Mahakama Kuu, Sumbawanga.
Kalinga
aliwaeleza wanausalama mara baada ya kukamatwa kwamba, yeye aliambiwa na mtu
mmoja (jina linahifadhiwa kwa sababu za kiusalama) kuwa kuna ‘mzungu’ anataka
mkono wa albino.
“Aliniambia
kwamba, wazungu wenyewe ni wale Wachina wanaotengeneza barabara. Lakini tangu
nikipate kiganja, nimekuwa nikimpigia simu yake haipatikani,” alikaririwa
akisema.
Aidha,
alisema hata kwenda kwake Dar es Salaam ilikuwa ni katika harakati za kutafuta
wateja, ambao hakuwapata hadi alipotiwa mbaroni.
Esther Jonas amelala hajitambui baada ya kupigwa panga usoni na kunusurika kifo wakati akipambana na watu waliomnyang'anya mwanawe Yohana.
Kisa cha Prisca hakina tofauti na kile cha
Esther Jonas (31), mkazi wa Kitongoji cha Ilyamchele, Kijiji cha Ilelema, Kata
ya Ipalamasa, Tarafa ya Buseresere wilayani Chato, ambaye Februari 15, 2015 saa
1:00 usiku alinyang’anywa mwanaye Yohana (1), mwenye albinism, ambaye alikuwa
amembeba mgongoni.
Katika jitihada za kunyang’anyana mtoto
ndipo ‘watu hao wasiojulikana’ wakamkata panga usoni, akadondoka chini na
kupoteza fahamu huku akivuja damu nyingi.
Wakati tukio linatokea, mumewe, Bahati
Misalaba Malyamchele (40) alikuwa anaota moto kwenye kikome, nje ya nyumba yao, na hakuweza kutoa msaada kwa mkewe
ambaye aliendelea kupambana na watu hao kabla ya kumdhibiti kwa kumkata kwa panga
usoni.
Watu hao wakaondoka na mtoto Yohana na
kutokomea kusikojulikana huku mama huyo akikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya
Bugando jijini Mwanza ambako ndiko walikonusuru maisha yake ingawa naye
wamemwacha na ulemavu wa kudumu.
Lakini Februari 17, 2015 mwandishi wa
makala haya alishuhudia polisi, wakiongozwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Geita, ACP Joseph Konyo, pamoja na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, SP P. J.
Kayumba, walipofanikiwa kuupata mwili wa marehemu Yohana ukiwa hauna mikono
wala miguu.
Ni rahisi kutazama kuku aliyenyonyolewa
manyoya na kukatwa vipapatio na miguu, lakini ni vigumu kukodolea macho
kiwiliwili cha binadamu kikiwa katika taswira hiyo.
Maiti ya marehemu Yohana Bahati baada ya kufukuliwa shambani. (Kunradhi kwa picha hii, lakini maudhui ya kuchapishwa kwake yamelenga kuonyesha unyama na ufedhuli unaofanywa na majahili wanaotafuta utajiri kwa njia za mkato kwa kuwaua ndugu na jamaa zetu albino).
Mwili huo ulikuwa umefukiwa katika shamba
la mtu mmoja, Malunguzya Kerezia, katika Kitongoji cha Mapinduzi, Kijiji cha
Lumasa, yapata kilometa 15 kutoka Kitongoji cha Ilyamchele, Ilelema ambako
Yohana alikuwa akiishi na wazazi wake.
Katika tukio hilo, wananchi waliodai kuchoshwa
na matukio hayo ya mauaji na kujeruhi watu wenye albinism, waliamua kwenda
kuchoma nyumba ya mwanakijiji mmoja, Juma Lupemba Kilobelo (39), ambaye
walimhisi kuhusika na tukio hilo.
Hata hivyo, Yohana hakuwa mtoto pekee wa
Esther mwenye albinism, kwani kati ya watoto wake saba aliokuwa nao, ni Kulwa
na Doto (14), Hoja (10) na Mathias (8) tu ambao hawana ulemavu wa ngozi, lakini
Shija (12) na Tabu (6) nao ni albino ambao kama wengine, maisha yao yako
hatarini.
Kwa ujumla, Yohana hawezi kurudishiwa uhai
wake, ingawa baadhi ya waliopata majeraha na ulemavu wa kudumu, wameweza
kupatiwa viungo bandia walau ili waweze kumudu maisha.
Mwaka 2015, Baraka na watoto wengine albino
waliopoteza viungo vyao kwa vitendo hivyo vya kikatili, walipelekwa jijini New
York, Marekani kupitia Global Medical Relief Fund, mfuko wa hisani ulioanzishwa
na mwanamama Elissa Montanti wa Kisiwa cha Staten mwaka 1997 ili kuwapatia
msaada wa viungo vya bandia watu kutoka maeneo yenye migogoro.
Albino wa Tanzania wakikatiza mitaa ya New York, Marekani wakiwa na Elissa Montanti ambako walikwenda kuwekewa viungo vya bandia.
Baraka (kulia) akimuonyesha rafiki yake Mwigulu Matonange mkono wake wa bandia wakati wakiwa Marekani.
Baraka (kulia) akimuonyesha rafiki yake Mwigulu Matonange mkono wake wa bandia wakati wakiwa Marekani.
Watoto wengine walikuwa Kabula Nkarango
Masanja (17), Mwigulu Magesa Matonange (12), Emmanuel Festo Rutema (14) na
Pendo Sengelema Noni (17).
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, Kabula
Nkrango Masanja, mkazi wa Luhaga, Kahama mkoani Shinyanga, alikatwa mkono wa
kulia mwaka 2010 ambapo kesi yake ilikuwa na jalada lenye Kumb. KAH/IR/1770/2010.
Hata hivyo, baada ya kesi hiyo kusikilizwa,
watuhumiwa wote watatu – Magobo Njige (56), Senga Mabirika (35) na Bupina Mhayo
(43) wote wakazi wa Ilalwe, Ushirombo, waliachiliwa huru na Mahakama Kuu.
Mwigulu Magesa Matonange akifanya mazoezi na kiungo cha bandia.
Mwigulu Magesa Matonange, mkazi wa Kijiji
cha Nsia, Tarafa ya Mtowisa wilayani Sumbawanga, yeye alikatwa mkono wa kushoto
wakati akiwa machungani.
Shauri hilo lenye majalada yenye Kumb. SUM/681/2013
na PI 13/2013 linawakabili washtakiwa 10 ambao ni Kulwa Mashiru, Peter Saidi
Msabato, Ignas Sungura, Faraja Jailosi Mwezimpya, James Patrick Ngalamika, Weda
Mashilimu, Ibrahim Tella, James Paschal, Nickson Ngalamika maarufu kama Kadogoo
na Hamis Rashid Manyanywa.
Kumbukumbu za mahakama na polisi
zinaonyesha kwamba, mtuhumiwa Manyanywa pia anakabiliwa na kesi ya mauaji ya
Lugolola Bunzari (7), albino na mkazi wa Kitongoji cha Kinondoni, Kata ya
Kanoge, Tarafa ya Ulyankulu, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, mauaji ambayo
yalitokea mwaka 2013.
Kesi hiyo iliyopewa majalada yenye Kumb. ULY/IR/45/2013
na MC 12/2013, inawahusisha watuhumiwa wengine ambao ni Simon Said Ndimawasha,
Amon Ruben maarufu kama Anthony Mnembotoyi na Laurent Batakanywa Malembo,
ambaye inaelezwa kwamba ndiye aliyekwamisha kusikilizwa kwa kesi hiyo baada ya
kuugua ugonjwa wa akili na kupelekwa katika Hospitali ya Wagonjwa wa Akili ya Mirembe,
mjini Dodoma. Kesi hiyo iko Mahakama Kuu Kanda ya Tabora na ilikuwa ianze
kusikilizwa tangu Januari 2015.
Kwa upande mwingine, Pendo Sengelema Noni,
mkazi wa Ugasa, Kata ya Usinge, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, alikatwa mkono wa
kulia mwaka 2014.
Shauri hilo lililopewa majalada yenye Kumb.
KAU/IR/835/2014 na CC. 63/2014 kwa kosa la ‘Kujaribu Kuua’, washtakiwa ni John
Fumbuka na Maduka Nzuki, ambapo kesi hiyo inasubiri ripoti ya Mkemia Mkuu wa
Serikali ili jalada lipelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi.
Emmanuel Rutema, mkazi wa Isebya, Kagoma
wilayani Biharamulo, alikatwa mkono wa kushoto katika tukio lililotokea
Jumatatu, Novemba 12, 2007 majira ya saa 1:30 usiku.
Mtuhumiwa Zacharia Petro (37), kabila Muha
na mkazi wa Songambele – Kagoma, alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa
la kujaribu kuua. Hukumu hiyo ilitolewa Novemba 4, 2011.
Wakati akizungumza na mwandishi wa makala
haya, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi wa Polisi
(ACP) Joseph Konyo, alisema, katika matukio mengi ya mauaji, kujeruhiwa na
kutekwa nyara kwa albino, wahanga wakubwa ni wanawake ambao mara kadhaa
hupambana ili kuwalinda ndugu ama watoto wao wenye albinism.
“Taarifa za kipelelezi zinaonyesha kuwa
wanaume, wakiwemo wazazi na ndugu wa albino, ndio wanaohusishwa moja kwa moja
kwa ama kupanga njama ama kushiriki vitendo hivyo,” alisema.
Alitolea mfano wa Bi. Esther Jonas, mama wa
marehemu Yohana, jinsi alivyopambana na majahili kiasi cha kunusurika kupoteza
uhai wake kabla ya wauaji hao hawajampora mtoto mgongoni na kwenda kumuua na kumkata
viungo huku mumewe, ambaye alikuwa nje, akishindwa kutoa msaada wowote.
Kumbukumbu za kipolisi pia zinaonyesha
kwamba, katika tukio la kutekwa nyara kwa mtoto Pendo Emmanuel Nundi huko
Kwimba usiku wa Desemba 27, 2014, mama wa binti huyo ndiye aliyeonekana
kupambana na watu hao waliovunja mlango kwa kutumia jiwe kubwa (maarufu kama
Fatuma) na kwenda kunyakua na kutokomea naye kusikojulikana.
Licha ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Mwanza wakati huo, SACP Valentino Mlowola (sasa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa – Takukuru), kutangaza dau la Shs. Milioni 3 kwa
atakayetoa taarifa za kufanikisha kukamatwa kwa majahili na kupatikana kwa
Pendo, lakini mpaka sasa hakuna taarifa zozote.
Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo,
wananchi bado wanabeza utendaji kazi wa vyombo vya dola wakisema hauonyeshi
dhamira ya dhati ya kukomesha mauaji hayo.
“Serikali inaonekana haina dhamira ya dhati
ya kukomesha mauaji haya, mbona tunasikia watu wamehukumiwa kunyongwa lakini
hawanyongwi?” anahoji Petro Shija, mkazi wa Katoro wilayani Geita.
Shija anaongeza: “Matukio ya mauaji na
kujeruhiwa kwa albino yanatishia usalama wa Watanzania wenzetu, ndugu zetu, wenye
ulemavu wa ngozi na jamii kwa ujumla, kwa sababu wahusika wanaondoa roho za
watu wasio na hatia huku wakiwaacha wengine na ulemavu wa kudumu.”
Kauli ya Shija haina tofauti na ya Bi. Limi
Lupamba, mkazi wa Kachwamba wilayani Chato, ambaye anasema kama serikali
ingewanyonga wale waliopatikana na hatia ingeweza kuwatia hofu wengine ambao
watafanya ama wanataka kufanya vitendo hivyo.
“Hawa watu wanyongwe tu, maana hata huko
jela wanamaliza ugali wa bure,” anasema Limi.
Gerald Ruhere ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali (NGO) mkoani Geita, ambaye anabainisha kwamba, lazima
jamii ifike mahali na kubadilika kutokana na imani potofu kuwa viungo vya
albino vinaleta utajiri au madaraka.
“Huu wote ni ujinga tu, inawezekanaje
kiungo cha binadamu mwenzako kikakupatia utajiri, kama ni hivyo, yeye mwenyewe
si angekuwa tajiri zaidi?” anasema.
Anahimiza kwamba, ni wajibu wa serikali
pamoja na taasisi mbalimbali kutoa elimu kwa jamii ili kuachana na imani hizo
potofu na kuwataka wanajamii kuwa na hofu ya Mungu, kwani kuwanyonga wahusika
tu hakuwezi kuwa suluhu ya tatizo lenyewe.
Wakati
wa kilele cha maadhimisho ya siku ya wenye albinism duniani jijini Arusha Juni
13, 2015, Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa
Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliahidi kwamba angesaini
hukumu ya kunyongwa kwa washtakiwa wa mauaji ya albino.
“Kati ya watu waliohukumiwa kunyongwa, wawili kesi zao
ziko katika hatua ya mwisho kufikishwa kwangu, zitakapofika mezani kwangu nitazitendea
haki stahiki,” alisema na kuonya kwamba, masuala hayo yanapaswa kuwa na subira.
Baadhi
ya wananchi wanaeleza kwamba, mara baada ya Rais wa Tanzania kuchaguliwa, huwa
anatoa kiapo kuilinda, kuitetea na kuitekeleza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, jambo mojawapo la kikatiba likiwa kuidhinisha kutekelezwa kwa hukumu
ya kifo inapotolewa na mahakama.
“Kuidhinisha
hukumu ya kifo ni jambo ambalo marais karibu wote wa Tanzania wamekuwa
wanakataa kulifanya,” anaeleza Kassimu Machimu, mkazi wa Kahama.
Machimu
anasema, ingawa hapendezwi na hukumu za kifo kwa ujumla, lakini yuko radhi
kuona washtakiwa wa mauuaji ya albino nchini wakinyongwa kwani kitendo
wanachokifanya ni cha kinyama.
“Watanzania
tumeshuhudia jinsi ndugu zetu albino wanavyouawa au kukatwa viungo kikatili na
hawa watu kwa sababu ya kutafuta utajiri kwa njia za kishirikina… Kama Nyerere
aliudhiwa sana na kifo cha Dk. Kleruu hadi kuidhinisha hukumu ya kifo bila
kusita, ni wajibu wa rais wetu kusaini hukumu hizo ikiwa kweli naye anaudhiwa
na mauaji haya ya albino.
“Mimi
na Watanzania wenzangu, na dunia kwa ujumla, tunaudhiwa sana na ukatili huu
dhidi ya albino. Hivyo tungependa kutoa ujumbe kwamba jambo hili linatuchukiza
Watanzania kiasi kwamba hatusiti kuidhinisha hukumu ya kifo kwa wauaji, japo
tunaweza tukawa hatuipendi hukumu ya kifo kwa ujumla. Tunataka kufanya hivi ili
pia iwe ujumbe kwa wale wote wenye mawazo ya kudhuru ndugu zetu albino, kwamba
tukiwashika, tutawanyonga hadi kufa,” anasema.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya sheria wanasema, suala
la kusaini hukumu ya kunyongwa ni la kisheria linaloambatana na haki za
binadamu, hivyo linahitaji kuchukuliwa kwa uzito unaostahili, huku wafungwa hao
wakipewa haki ya kukata rufaa kupinga hukumu hizo.
Lakini kutosainiwa kwa hukumu hizo kumeendeleza ‘msimamo’ wa
kutoidhinisha vifo wa wakuu wa nchi, akiwemo Mwalimu Julius Nyerere, ambaye
katika utawala wake anadaiwa kusaini hukumu moja ya Said Mwamwindi, ambaye
alimuua kwa risasi aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Wilbert Kleruu na
kwenda kuikabidhi maiti yake kituo cha polisi.
Waliohukumiwa kifo
Mpaka Kikwete
anakabidhi madaraka Novemba 5, 2015, jumla ya washtakiwa 24 walikuwa
wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya watu
nane wenye albinism tangu mauaji hayo yalipoibuka mwaka 2006.
Uchunguzi
uliofanywa na mwandishi wa habari hizi katika kipindi cha miezi nane unaonyesha
hata hivyo kwamba, mmoja kati ya waliohukumiwa kunyongwa alifia mahabusu wakati
kesi ikiendelea.
Hukumu ya
mwisho dhidi ya wauaji hao ilitolewa Septemba 16, 2015 na Jaji Robert Makaramba
wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ambapo washtakiwa watano walihukumiwa kunyongwa
hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Aaron Nongo, mkazi wa
Ibanda-Relini jijini Mwanza.
Mwandishi
wa makala haya alihudhuria kesi hiyo kwa siku tano mfululizo jijini Mwanza
kabla ya kutolewa hukumu, ambapo ilielezwa mahakamani kwamba, marehemu Nongo
aliuawa Juni 26, 2009 majira ya saa tatu usiku akiwa nyumbani kwake
Ibanda-Relini, jijini Mwanza ambapo wauaji hao walimkata usoni na kisha kumkata
miguu yake yote miwili kwa kutumia shoka na kutoweka nayo pamoja na meno mawili
ya mbele.
Waliokumbwa
na adhabu hiyo katika shauri hilo Namba 213 la mwaka 2014 lenye kumbukumbu
namba MWZ/IR/5397/2009 na MCC No. 32/2009 ni Chacha
Jeremia Mlimi, Mathew Jeremia Mlimi (mdogo wa Chacha), Paschal Lugoye Mashiku na
Joseph Bugwema au Alex Joseph maarufu kama Bugwema Silola Jangalu.
Mshtakiwa
mwingine, Paulo Lumanija Genji alifariki katika mahabusu ya Magereza, wakati
ambapo mganga wa jadi Kishosha Lutambi, ambaye anadaiwa kuchochea mauaji hayo, alifariki
kufuatia kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira mwaka 2009.
Wakati wa
usikilizaji wa mwenendo wa kesi hiyo, shahidi wa sita wa upande wa mashtaka, Mrakibu
Msaidizi wa Polisi (wakati huo akiwa Mkaguzi wa Polisi) David Mhanaya, Mei 12,
2015 aliifanya mahakama izizime kwa hofu na simanzi baada ya kutoa mfupa wa mguu
wa marehemu ambao uliwasilishwa kama kielelezo mahakamani hapo baada ya
kuthibitishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa ndio wa marehemu Nongo.
Hukumu
hiyo ilitolewa takriban miezi mitatu na nusu baada ya Mahakama Kuu Kanda ya
Mbeya kuwahukumu wengine wanne kunyongwa mpaka kufa.
Hukumu ya
kesi hiyo ya mauaji yenye kumbukumbu Namb. KIW/IR/49/2008 na PI 5/2013,
ilitolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Dk. Revila Jumanne, Juni 30, 2015 jijini
Mbeya, ambapo washtakiwa wanne kati ya watano walihukumiwa kunyongwa hadi kufa
kutokana na mauaji ya kijana Henry Mwakajila (17) aliyekuwa na albinism.
Akisoma
hukumu hiyo, Jaji Dk. Revila alisema mahakama ilijiridhisha pasi na shaka na
ushahidi wa upande wa mashtaka kwamba washtakiwa hao wanne walitenda kosa hilo
na hivyo wanastahili adhabu hiyo.
Waliohukumiwa
kunyongwa mpaka kufa ni mganga wa jadi Asangalwisye Kayuni maarufu kama Katiti
au Mwakatoga na Gerard Korosso Kalonge (wakazi wa Kijiji cha Mbembati wilayani
Ileje), na Leonard Msalage Mwakisole na Hakimu Mselem Mwakalinga (wakazi wa
Kiwira wilayani Rungwe).
Mshtakiwa
wa nne, Mawazo Philemon Figomole, mkazi wa Kiwira wilayani Rungwe, aliachiliwa
huru na mahakama hiyo baada ya ushahidi wa upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha
ushiriki wake katika mauaji hayo.
Ilielezwa
mahakamani hapo kwamba, mnamo Februari 5, 2008 majira ya saa 12:00 na saa 1:00
jioni huko katika Kijiji cha Ilolo, Kata ya Kiwira, Tarafa ya Ukukwe, wilayani
Rungwe katika Mkoa wa Mbeya, washtakiwa hao walimteka nyara kijana Henry
Mwakajila, ambaye ni mlemavu wa ngozi aliyekuwa akisoma kidato cha pili katika
Shule ya Sekondari Ukukwe na kisha kumuua.
Wakati wa
mwenendo wa kesi, ilielezwa na mashahidi wa upande wa mashtaka kwamba mshtakiwa
wa kwanza Asangalwisye Kayuni maarufu kama Katiti au Mwakatoga ambaye ni mganga
wa jadi, mkazi wa Kijiji cha Mbembati, Wilaya ya Ileje, alikutwa na utumbo
unaodhaniwa kuwa wa binadamu na ulipopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali
ukathibitika kwamba ni utumbo wa marehemu Henry.
Mshtakiwa
wa pili, Gerard Korosso Kalonge wa Kijiji cha Mbembati wilayani Ileje alikutwa
na vidole vinne na mifupa kumi (10) vyote vinavyodhaniwa kuwa vya binadamu na
baada ya uchunguzi wa Mkemia Mkuu wa Serikali ilibainika kwamba ni viungo vya
marehemu Henry.
Ilielezwa
pia kwamba, washtakiwa Leonard Msalage Mwakisole, Mawazo Philemon Figomole na
Hakimu Mselem Mwakalinga ndio waliodaiwa kumteka nyara mtoto huyo na kumuua,
kisha kupeleka viungo kwa mganga wa kienyeji Asangalwisye Kayuni.
Mshtakiwa
wa tano, Hakimu Mselem Mwakalinga, tayari alikwishahukumiwa kunyongwa mpaka
kufa katika kesi nyingine ya mauaji ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Rungwe, John Mwankenja, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake Mei
19, 2011.
Inadaiwa
kwamba, chanzo cha mauaji ya Mwankenja, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama
cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rungwe, kilitokana na kiongozi huyo kufahamu
kwamba hao ndio waliomuua albino Henry, na alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha
watuhumiwa wanachukuliwa hatua za kisheria.
Mshtakiwa
Mwakalinga, ambaye ndiye aliyetekeleza mauaji ya Mwenyekiti huyo wa
Halmashauri, alitajwa na washatakiwa wanne ambao tayari walikuwa mahabusu,
hivyo akaamua kwenda kumuua kiongozi huyo ili kupoteza ushahidi akitumia
bunduki ambayo ilidaiwa kuibwa nchini Zambia.
Hata
hivyo, makachero wa Jeshi la Polisi walifanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa huyo
na mbali ya kushtakiwa kwa mauaji ya mwenyekiti wa halmashauri, aliunganishwa
pia kwenye kesi ya mauaji ya Mwakajila.
Hukumu ya
kesi ya mauaji ya mwenyekiti wa halmashauri iliyokuwa na kumbukumbu Namba
131/2012 ilitolewa Novemba 13, 2013 ambapo ilielezwa kwamba watuhumiwa
walitenda kosa hilo Mei 19, 2011 katika Kijiji cha Mpandapanda, Kata ya Kiwira,
Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.
Ingawa
watuhumiwa walikuwa wanne, lakini Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya chini ya Jaji
Samwel Karua iliwahukumu kunyongwa mpaka kufa mshtakiwa wa kwanza Hakimu
Mwakalinga na mshtakiwa wa pili Daudi Mwasipasa kwa maelezo kwamba walihusika
moja kwa moja na mauaji hayo ya kukusudia.
Mshtakiwa
namba tatu Obote Mwanyingili yeye alitiwa hatiani kutokana na kosa la
kumhifadhi mtuhumiwa namba moja baada ya kutoka kufanya mauaji wakati mshtakiwa
namba nne Kelvin Myovela alitiwa hatiani kutokana na kuhifadhi silaha
iliyotumika katika mauaji hayo ingawa hakuhusika na kitendo hicho moja kwa
moja, hivyo wote wawili walihukumiwa kifungo cha miaka saba jela.
Hata
hivyo, Myovela tayari alikwishahukumiwa katika kesi nyingine kifungo cha miaka
20 jela kwa kukutwa na silaha kinyume cha sheria.
Uchunguzi
unaonyesha kwamba, hukumu ya kwanza kabisa ya
kunyongwa mpaka kufa katika mfululizo wa kesi za mauaji ya albino ilitolewa
Januari 2, 2009 ikihusisha Shauri namba MCC 25/2008 na BAR/IR/2460/2008 la
mauaji ya Lyaku Willy (50) wa Bariadi, ambapo washtakiwa wote wanne Mboje Mawe,
Nchinyenye Kishiwa, Sayi Gamaya na Sayi Masizi walihukumiwa kunyongwa.
Washtakiwa
Masumbuko Madata, Charles Karamji na Merdard Maziku walihukumiwa kunyongwa
katika kesi mbili za mauaji ya albino, ya kwanza ikiwa ya Esther Charles (10)
wa Shilela wilayani Kahama na Matatizo Dunia (13) wa Bunyihuna, Ushirombo, mkoani
Geita, mauaji yote yakiwa yametokea mwaka 2008.
Katika
Shauri la mauaji ya Esther Charles lililokuwa na jalada lenye kumbukumbu namba
KAH/IR/433/2008 washtakiwa wake Masumbuko Madata, Charles Karamuji na Merdard
Maziku walihukumiwa Juni 3, 2011 na baadaye mwaka huo 2011 wakahukumiwa tena
kunyongwa mpaka kufa katika Shauri la mauaji ya Matatizo Dunia lililokuwa na
jalada lenye kumbukumbu namba USH/IR/1879/2008. Marehemu Matatizo alikatwa mguu
wa kulia ambao polisi waliukuta nyumbani kwa Masumbuko Madata.
Katika
Shauri lenye jalada namba MCC No. 01/2007 la mauaji ya Mariam Emmanuel wa
Kijiji cha Nyangomango wilayani Misungwi, washtakiwa waliohukumiwa kunyongwa
mpaka kufa ni Kazimili Mashauri na Mathias Ikangalange. Tukio la mauaji hayo
lilitokea Januari 21, 2007 majira ya saa 2:30 usiku katika kijiji hicho cha
Nyangomango.
Shauri
namba MCC
No. 10/2008 la mauaji ya Zawadi Mgindu wa Kijiji cha
Nyamalulu, Kata ya Imalambegete mkoani Geita aliyeuawa Machi 11, 2008 ndilo
lilikuwa la kwanza kutolewa hukumu kama hiyo mwaka 2015 ambapo washtakiwa
Nassoro Said Isakwisa, Singu Siyantemi, Masalu Kahindi na Ndahanya Lumola
Ndahanya walihukumiwa kitanzi Machi 5, 2015 katika Mahakama Kuu Kanda ya Geita.
Hukumu
nyingine ya kunyongwa mpaka kufa ilitolewa Juni 15, 2015 katika Shauri lenye
jalada namba MCC No.28/2009 la mauaji ya Jesca Charles Joshua wa
Shamaliwa-Igoma jijini Mwanza aliyeuawa Juni 21, 2009 ambapo washtakiwa
waliopewa adhabu ya kifo ni Malikiadi Christopher Manumbu na Yohana Maduka
Mwanamalundi.
Fuatilia mfululizo wa ripoti hii maalum: Kuwanasa wauaji wa albino, hata mbinu za kivita zinatumika.
+255 656-331974
Comments
Post a Comment