Featured Post

BONGO MOVIE ZINAKERA, SITAZAMI TENA… YA BEN SAANANE SIJUI IMEKWISHAJE!




Na Daniel Mbega
KAMA wanakurupuka, sijui! Lakini kusema ukweli inakera kusikiliza ama kutazama ‘filamu’ za Bongo ambazo huibuka ghafla na kuishia kama hadithi za watoto.
Japokuwa filamu za Kinigeria karibu nyingi lazima zihusishe na uchawi na uganga, lakini ni mara kumi uzitazame hizo kuliko kukodolea macho hizi za Bongo. Sisemi za akina Ray, Walper na wengineo, hapana. Hizi ni filamu nyingine kabisa.

Kwa takriban mwaka mzima nimeshuhudia waigizaji wakubwa wa majukwaani, yaani wanasiasa – hasa wa upinzani – wakija na filamu zenye ‘title’ nzuri, ambazo zimetungwa na wao wenyewe, zikaigizwa na wao wenyewe, zikaongozwa na wao wenyewe, zikahaririwa na wao wenyewe, zikasambazwa na wao wenyewe, lakini zikiwa hazionyeshi mwisho wowote.
Jambo la kusikitisha ni kwamba, kabla filamu moja haijafikia mwisho, wasanii hawa wanasiasa huibuka na filamu nyingine yenye ‘title’ kali zaidi, ambayo nayo kama ya kwanza, wataitangaza kila kona – kitaifa na kimataifa, majukwaani na mitandaoni – na ukiiangalia unaona kwamba hili litakuwa bonge la ‘movie’.
Lakini wala usiwaamini, kwa sababu kama zilivyo zote, hakuna hata moja ambayo itaonyesha mwisho ukoje. Huwezi kujua kama ‘stelingi’ ameshinda au vipi.
Kwa mfano, mpaka sasa sijui ile filamu tamu waliyoitengeneza wapinzani ya Ben Saanane imekwishaje! Kwa hakika sijui ingawa ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa kila mwanajamii kufahamu hatma ya mwanasiasa huyo kijana ambaye haijulikani ametekwa, amejiteka, amefichwa au amejificha, nani kamficha, kwa nini amefichwa au amejificha, na mambo mengine kadha wa kadha.
Nitaeleza msululu wa filamu hizo ulivyo. Zilianza hivi: “Walitokea wapinzani wa Tanzania, kupitia kile walichokiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakiongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho ndani yake hakuna demokrasia bali ubabaishaji mwingi, wakagomea vikao vya Kamati za Bunge, baadaye wakaenda kwenye Bunge la Bajeti, lakini wakagomea kusikiliza hotuba za Bajeti kwa sababu hawakumtaka Naibu Spika Tulia Mwansasu, wakatoka nje… lakini wakalamba posho kabla ya kuzuiwa. Bunge likaendelea bila wao.
Walipona filamu hiyo imeshindwa kufanya vizuri sokoni, wakaamua kuja na nyingine. Hii wakaiita Operesheni Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta), ‘stelingi’ akiwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe. Script ya filamu hiyo ilieleza kwamba, walikuwa wakipinga kile walichokiita ‘udikteta’ wa Rais John Magufuli, ambaye alikuwa amepiga marufuku mikutano ya kisiasa na kuhimiza watu wachape kazi. Ukuta ukabomoka ghafla kwa sababu haukuwa na msingi imara.
Miezi kadhaa baadaye, ‘stelingi’ yule yule wa ‘Ukuta’ akatangaza kuja na Operesheni Kata Funua, ambayo maelezo ya awali yalisema ilikuwa ni kuanzisha vikao vya ndani ya Chadema kila mahali baada ya serikali kupiga marufuku siasa za majukwaani. Script yenyewe inadaiwa kuandaliwa na mwanasiasa kijana Bernard Rabiu Saanane maarufu zaidi kama Ben Saanane, ambaye ameshiriki katika harakati za maandalizi ya ‘filamu’ nyingi za Chadema.
Tukaambiwa kwamba, Ben Saanane, ambaye ni katibu myeka wa Mwenyekiti wa Chadema, alikuwa ameambiwa angepewa mapumziko huko Afrika Kusini kwa gharama za mwenyekiti wake kama ‘asante’ kwa kukamilisha jambo hilo kubwa.
Hakuna aliyejua ‘location’ ya ‘episode’ za filamu hiyo wala namna ambavyo ingeanza isipokuwa Ben na viongozi wa juu wa Chadema.
Lakini takriban mwezi mmoja baadaye, tukaambiwa Ben Saanane ‘amepotea’ tangu Novemba 18, 2016, tarehe ambayo tuliambiwa kwamba ndiyo ambayo kijana huyo alikuwa asafiri kwenda Afrika Kusini ‘kula bata’ baada ya kukamilisha ‘script’ ya ‘Kata Funua’.
Jitihada za familia ya Ben Saanane kujua aliko ndugu yao zikawafikisha polisi baada ya kushindwa kupata maelezo yoyote kutoka kwa ‘waigizaji na waongozaji wa filamu’, lakini siku 25 tangu kupotea kwake ndipo Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, akaibuka mbele ya vimulimuli vya luninga na kusema Ben alikuwa amesema anatishiwa maisha yake.
Siku tisa baada  ya kauli ya Lissu, yaani Desemba 22, 2016, Mbowe naye akaibuka na kusema ameamua kukaa kimya kwa sababu kama atazungumza waliomteka wanaweza kumuua! He! Kumbe ametekwa na ‘wasanii’ hawa wanajua? Kila mmoja akaanza kujiuliza.
Wasanii wengine wahusika kwenye filamu hiyo, sijui kama wameshiriki kwa ‘upande wa maadui’ (villains) au namna gani, wakaja na kubwa kuliko baada ya kumfanya Ben mtaji kwa kuchapisha fulana ambazo walizipiga kwa buku 20 kila moja. Wakatengeneza fedha kweli kweli ambazo hatujui zilipatikana kiasi gani, familia yake ilipata kiasi gani, wala hatujui kama zilikuwa na baraka ya ‘chama kubwa’ la Chadema.
 “Wakati filamu hiyo iko katikati, wasanii hao wakaibuka na hoja ya kupigania haki ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, wakitaka ‘haki itendeke’ ili apate dhamana kutokana na kesi zake zinazomkabili. Kikundi kingine kikajitokeza na kuchapisha fulana za ‘Justice 4 Lema’. Nacho kikapiga fedha za kutosha!  Naam. Kufa kufaana bwana! Filamu hiyo inaendelea lakini ni wachache wanaoifuatilia.
Kwa kuona filamu zile hazijaleta matokeo mazuri sokoni, ‘wasanii hao’ wameibuka na filamu nyingine ambayo inaitwa ‘Njaa Tanzania’, ambayo imemshirikisha msanii mahiri Zitto Kabwe. Imeanza kwa kueleza akiba ya chakula iliyopo serikalini. Kwa kutazama ukame uliozikumba nchi nyingi za Afrika na duniani kwa ujumla, filamu hii ikapata watazamaji wengi sana.
Zimetafutwa location nyingi za filamu hiyo zinazoonyesha ukame na mazao yakiwa yamekauka. Wengine wakasema hata mifugo inakufa kwa kukosa malisho na maji. Lawama zote zimeelekezwa serikalini.
Lakini hakuna anayewakumbusha wananchi kwamba, suala la ukame lilitabiriwa tangu mwaka 2016 na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambayo wengi wamekuwa akiibeza kuwa ‘inabahatisha tu’. Ilielezwa pia katika taasisi za kimataifa kwamba mwaka 2017 kutakuwa na El Nina, lakini watu hawakutilia maanani suala la kuhifadhi chakula.
Ndiyo kwanza mwaka 2016 wafanyabiashara wa chakula wakaiomba serikali iondoe zuio la kusafirisha chakula nje ya nchi ambako wao walisema kuna bei nzuri. Wakapeleka.
Leo hii ukame uliotabiriwa umeonekana, wanasiasa wasanii wale wale wameibuka na kutumia kama fimbo ya kuiadhibu serikali. Hakuna hata mwanasiasa mmoja anayewahoji wananchi kwa nini hawakujiwekea japo akiba kidogo.
Filamu hii inaendelea. Lakini hakuna mwanasiasa mwenye kumbukumbu japo kidogo kwamba suala la ukame siyo mara ya kwanza kutokea Tanzania. Na daima ukame unakuja na njaa kwa sababu katika kipindi kama hiki ambacho kilifaa kuwa cha masika, watu walitegemea wawe wamepanda, wamelima na wanaendelea kupalilia mazao yao.
Sasa kwa ukame huu, ni mwananchi gani hata akiwa  na chakula atathubutu kukitoa chakula chake wakati hana uhakika mvua itanyesha lini? Ni mwanasiasa gani aliyepita vijijini kufanya uchunguzi na kubaini kwamba hakuna chakula?
Kwa mfano, kuna yeyote ambaye alikwenda vijiji vya Ngomai, Hemba Hemba, Njoge na vinginevyo katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma kujionea jinsi baadhi ya wakulima wakubwa walivyo na maghala makubwa ya chakula na hawajayafungua kwa kusita kutokana na ukame?
Filamu hii ingekuwa nzuri zaidi kama wasanii hawa wangeweza kufanya uchunguzi kila kona vijijini, siyo uchunguzi wa siasa za majukwaani, bali uchunguzi kwa maana ya uchunguzi.
Tumekuwa na njaa baada ya uhuru katika miaka ya 1964, 1974, 1984 na miaka mingine kadhaa iliyoendelea ambayo hata hivyo haikuwa kubwa kama ile ya kwanza. Tulikula mahindi ya ‘Yanga’ kutoka Brazil na Marekani, tulikula Bulga na kadhalika. Yote hiyo ni kwa jitihada za serikali, siyo za wapiga kelele wasanii wa upinzani.
Leo serikali inaposema hakuna njaa Tanzania, inashangaza kuona wapinzani wakibeza kana kwamba wao ndio wako jikoni. Hivi hawaelewi kama ‘jicho la gari analijua dereva’!
Kwa mawazo ya wasanii hawa, wanadhani serikali itawaacha wananchi wake wafe kwa njaa? Sasa itaongoza akina nani?
Kama ni ‘kick’ ya kutokea kisiasa, nadhani watafute nyingine siyo hii.
Vinginevyo Watanzania tumechoka kuzitazama filamu za Kibongo zinazoandaliwa na kuchezwa na wapinzani kwa sababu hazina mwisho mzuri na zinachusha. Wajjipange upya!
0656-331974

Comments