Featured Post

SOMA MAONI YA KAMBI YA UPINZANI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MAKOSA YA MTANDAO 2015



(MAONI HAYA YALITOLEWA JUMATANO, APRILI MOSI, 2015)

MAONI YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, MHESHIMIWA MOHAMED HABIB MNYAA (MB.) KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MAKOSA YA MTANDAO YA MWAKA 2015, YAANI THE CYBERCRIMES ACT, 2015

Mheshimiwa Spika,
Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao, 2015, yaani, The CyberCrimes Act, 2015, ulichapishwa kwenye Gazeti la Serikali la tarehe 20 Februari, 2015. Muswada huu unaletwa kwa Hati ya Dharura, ikiwa na maana kwamba hakutakuwa na mjadala wowote wa maana ndani na nje ya Bunge lako tukufu. Kama tutakavyoonyesha katika Maoni haya, Muswada huu ni muhimu kwa kiasi ambacho hatutalitendea Taifa letu haki kwa kuujadili chini ya kivuli cha Hati ya Dharura.


TEHAMA NA ZAMA MPYA YA HABARI
Mheshimiwa Spika,
‘The World is a Global Village’, yaani ‘Dunia ni Sawa na Kijiji’ ni msemo ambao umekuwa maarufu sana katika miaka ya karibuni. ‘The New Information Age’, yaani ‘Zama Mpya ya Habari’ ni msemo mwingine maarufu. Misemo hii ina maana moja: kwamba maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani yamewezesha mawasiliano kuwa rahisi kwa kuwepo kwa mifumo mingi ya mawasiliano kwa kutumia kompyuta, simu za mezani, simu za mikononi, mifumo ya mawasiliano ya papo kwa hapo kama vile simu, barua pepe, ujumbe mfupi wa maneno hasa kwa njia za mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, WhatsApp, Viber, Twitter, Instagram, Skype na kadhalika.

Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa State of Broadband Report ya mwaka 2014 iliyotolewa hivi karibuni nchini Marekani, watumiaji wa mitandao duniani walikadiriwa kufikia watu bilioni 2.3 katika mwaka 2013. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2014, watumiaji hao walitarajiwa kufikia bilioni 2.9.

Kwa sababu ya kupanuka kwa matumizi haya ya teknolojia za mawasiliano, upatikanaji wa habari mbali mbali zinazohusu masuala mbali mbali umeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Aidha, kwa sababu hiyo hiyo, mipaka ya habari, yaani ‘information barriers’, imevunjwa au kudhoofishwa. Uwezo wa Serikali na mamlaka nyingine za umma au za binafsi wa kudhibiti au kuficha habari zinazohusu matukio muhimu kwa wananchi na nchi umefifishwa na uhuru na uelewa wa wananchi wa masuala mbali mbali yanayowahusu umepanuka.

Hakuna tena uwezekano ‘uliokuwepo zamani’ wa serikali za kiimla kuzuia wananchi kupashana habari kwa kupiga marufuku magazeti, majarida na vitabu wasivyovitaka watawala. Kwa sababu ya YouTube na aina za aina hiyo za mawasiliano ya mtandao, udhibiti wa filamu kwa kutumia censorship hauwezekani tena.

Vile vile, kwa sababu ya maendeleo ya teknolojia za mawasiliano, imewezekana sasa kwa ‘whistle-blowers', yaani raia wema wenye ujasiri wa kuvujisha siri za matendo ya kihalifu yanayofanywa na serikali na watendaji wake, kuweka taarifa za siri za uhalifu unaofanywa na serikali. Mifano maarufu ya miaka ya karibuni ni pamoja na raia wa Australia, Julian Assange wa mtandao wa WikiLeaks, aliyevujisha taarifa za jinsi ambavyo serikali ya Marekani na mashirika yake ya kijasusi imekuwa ikifanya ujasusi dhidi ya serikali mbali mbali duniani, ikiwemo washirika wa karibu wa Marekani.

Aidha, Edward Snowden, raia wa Marekani aliyekuwa mfanyakazi wa Shirika la Ujasusi la Wizara ya Ulinzi ya Marekani, yaani Defence Intelligence Agency (DIA) alivujisha ‘kwa kutumia mtandao’ taarifa za jinsi serikali ya Marekani imekuwa ikifanya ujasusi na upelelezi dhidi ya raia wa Marekani kinyume na sheria za nchi hiyo kwa kutumia teknolojia za mawasiliano ya kimtandao. Bila maendeleo ya sayansi na teknolojia za mawasiliano ingekuwa vigumu kwa dunia kufahamu juu ya uhalifu huu wa serikali ya Marekani dhidi ya raia.

Hapa nchini, bila kuwepo kwa teknolojia za habari na mawasiliano, ingekuwa vigumu sana ‘na pengine isingewezekana kabisa’ kwa wananchi kupata taarifa za uhalifu mkubwa wa wizi wa mabilioni ya fedha za umma, uliofanywa na viongozi na watendaji wa ngazi za juu serikalini kutoka kwenye Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA), rada ya BAE Systems, Richmond/Dowans na wizi wa juzi juzi wa mabilioni ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow.

Ni wazi, kwa sababu hiyo, kwamba sio tu kwamba uhuru halisi wa maoni chini ya ibara ya 18 ya Katiba yetu umewezekana; bali pia Bunge lako tukufu na wananchi kwa ujumla wameweza, kwa kiasi fulani, kuwawajibisha viongozi na watendaji wa serikali waliohusika na uhalifu huo, na hivyo kutimiza ahadi ya ibara ya 8(1)(c) ya Katiba juu ya Serikali kuwajibika kwa wananchi.

MLIPUKO WA UHALIFU WA KIMTANDAO

Mheshimiwa Spika,
Sambamba na kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia ya mawasiliano duniani, kumekuwapo pia na ongezeko kubwa la uhalifu kupitia teknolojia hiyo. Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Mawasiliano Duniani, yaani International Telecommunications Union (ITU) ya mwaka 2013, kumekuwepo na ongezeko kubwa la uhalifu wa kimtandao, ambao umeathiri zaidi ya asilimia 30 ya mitandao duniani.

Aidha, mitandao ya kihalifu ijulikanayo kama ‘Phishing Sites spoofing social networks’ imeongezeka kwa asilimia 125. Ongezeko hili la mitandao hii ya kihalifu limeathiri takriban nusu ya vijana wenye umri kati ya miaka 13 hadi 17 ulimwenguni kote kwa kile kinachoitwa kama unyanyasaji wa kimitandao, yaani ‘Cyber bullying.’ Unyanyasaji wa aina hii umewaletea vijana madhara mengi ikiwemo kujiua, kudhuriwa, n.k.

Mheshimiwa Spika,
Maendeleo haya makubwa ya teknolojia ya mawasiliano yamepanua pia wizi wa kimtandao. Hivyo, kwa mfano, tafiti zilizofanywa The World Federation of Exchanges na The International Organization of Securities Commissions" zimeeleza kuwa nusu ya taasisi za fedha duniani zimekumbwa na uhalifu wa kimtandao ikiwemo wizi wa fedha.

Hadi kufikia mwaka 2013, wizi huo ulikuwa umeathiri sana uchumi wa dunia. Ripoti ya utafiti wa Kampuni ya Kimataifa ya Teknolojia ya Mawasiliano ya Kompyuta (IDC) ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Singapore inaonyesha kuwa, kwa mwaka 2014 peke yake, dunia ilipoteza kiasi cha Dola za Marekani 500 bilioni kwa ajili ya kukabiliana na wizi wa mitandao. Cha kutia wasi wasi mkubwa zaidi ni kwamba takriban robo ya taasisi za kifedha duniani zilielezwa kushindwa kutatua tatizo hilo la wizi wa kimtandao.

Mheshimiwa Spika,
Kupanuka kwa matumizi ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano kumesababisha kuongezeka kwa tatizo lingine: usambazaji wa lugha za matusi, picha chafu na za udhalilishaji na matumizi mengine yasiyofaa ya teknolojia hiyo ya mawasiliano. Aidha, kwa sababu ya matumizi haya ya teknolojia ya mawasiliano, haki ya kuwa na faragha inakabiliwa na hatari kubwa ya kutoweka.

Kila mmoja wetu, mkubwa kwa mdogo, tajiri au maskini, maarufu au asiye maarufu, anaishi kwa hofu kubwa na dhahiri ya faragha yake kuvamiwa na watu wasiojulikana na picha zake za siri au za watu wanaomhusu kusambazwa dunia nzima kwa kutumia mitandao ya kijamii ya kila aina ambayo imelipuka kwa kasi kubwa katika miaka ya karibuni. Hata picha za watu waliofikwa na mauti au waliopata ajali mbaya zimekuwa zikisambazwa bila kujali athari zake kwa jamii.

Mheshimiwa Spika,
Ni wazi, katika mazingira haya mapya, kwamba kuna haja na umuhimu wa kuwa na Sheria itakayoratibu matumizi ya mitandao ya mawasiliano. Ni wazi vile vile, kwa kuzingatia umuhimu wa mitandao ya kijamii katika kujenga jamii yenye uhuru, uwazi na uwajibikaji, kwamba sheria hiyo lazima ilinde haki ya wananchi ya kutafuta, kupata na kusambaza habari kwa njia za mitandao ya mawasiliano kwa nguvu zote dhidi ya tishio la wale ambao wasingependa uhalifu wao dhidi ya umma kujulikana kwa kutumia mitandao hiyo.

Katika mazingira ambayo nchi yetu imekumbwa na kansa ya ufisadi wa aina ya Tegeta Escrow na EPA na Chenji ya Rada na Richmond/Dowans unaohusisha viongozi na watendaji wa ngazi za juu serikalini, watoa siri kwa njia ya kimtandao lazima wapate ulinzi wa kisheria. La sivyo nchi yetu itaangamizwa na wale ambao wamepata dhamana ya utumishi wa umma lakini wakaamua kuinajisi dhamana hiyo kwa manufaa yao binafsi.

Aidha, kwa kutambua wimbi kubwa la uhalifu wa mitandao, ipo haja ya kutunga sheria kwa ajili ya kudhibiti uhalifu huo. Kwa sababu hizi, tunapendekeza kuchambua Muswada huu kwa kuangalia jinsi utakavyowezesha kudhibiti uhalifu wa kimtandao na wakati huo huo kulinda haki za kimsingi za kikatiba ambazo zitawezesha taifa lenye uwazi na uwajibikaji.

TEHAMA, CYBERCRIME NA MUUNGANO

Mheshimiwa Spika,
Moja ya mambo yanayojitokeza mapema kabisa kwenye Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ni suala la Muungano. Hii ni kwa sababu, aya ya 2 ya Muswada inatamka kwamba "... Sheria hii itatumika Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar." Hata hivyo, licha ya ‘posta na simu’ kuwa mojawapo ya ‘Mambo ya Muungano’ kwenye Nyongeza ya Kwanza ya Katiba yetu, masuala ya teknolojia za habari na mawasiliano sio mambo ya Muungano. Ndio sababu Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia sio mojawapo ya Wizara za Muungano na Zanzibar ina Wizara yake inayoshughulikia masuala hayo.

Mheshimiwa Spika,
Kwa vile masuala yahusuyo Muswada huu sio Mambo ya Muungano, Katiba yetu imeweka masharti mahsusi ya namna ya, na mamlaka za, kutunga sheria kwa ajili yake. Hivyo, kwa mfano, kwa mujibu wa ibara ya 4(3) ikisomwa pamoja na ibara ya 64(1), mamlaka ya kutunga sheria kwa ajili ya Mambo ya Muungano na "... juu ya mambo mengine yote yahusuyo Tanzania Bara yatakuwa mikononi mwa Bunge." Kwa upande mwingine, "mamlaka yoyote ya kutunga sheria katika Tanzania Zanzibar juu ya mambo yote yasiyo ya Muungano yatakuwa mikononi mwa Baraza la Wawakilishi."

Sasa kwa vile masuala ya TEHAMA sio mambo ya Muungano, mamlaka halali ya kuyatungia sheria itakayotumika Zanzibar kwa mujibu wa Katiba sio Bunge lako tukufu, bali ni Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Katiba yetu imeweka wazi madhara ya kupuuza msimamo huu wa kikatiba: "Endapo sheria yoyote iliyotungwa ... na Bunge inahusu jambo lolote ambalo liko chini ya mamlaka ya Baraza la Wawakilishi, sheria hiyo itakuwa batili na itatanguka."

Mheshimiwa Spika,
Katiba yetu imeweka masharti mengine kuhusu utaratibu wa kutunga sheria zitakazotumika Zanzibar. Hivyo, kwa mfano, Katiba inaelekeza kwamba ili sheria yoyote iliyotungwa na Bunge lako tukufu iweze kutumika Zanzibar, ni lazima "... sheria hiyo iwe imetamka wazi kwamba itatumika Tanzania Bara na vile vile Tanzania Zanzibar au iwe inabadilisha, kurekebisha au kufuta Sheria inayotumika Tanzania Zanzibar." Kama ambavyo tumeona, Muswada huu unatamka wazi kwamba Sheria hii itatumika Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Je, tamko hili pekee lina maana kwamba Sheria hii itakuwa halali endapo Muswada huu utapitishwa na Bunge lako tukufu?

Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, ibara ya 64(2) inayolipa Baraza la Wawakilishi mamlaka ya kutunga sheria kwa mambo yote yasiyokuwa ya Muungano ya Zanzibar ndiyo the controlling provision inayodhibiti masharti mengine ya ibara ya 64 kwa upande wa Zanzibar. Hii ina maana kwamba ‘Sheria' zinazotajwa katika ibara ya 64(4) ni zile ambazo Bunge lako tukufu lina mamlaka ya kuzitunga, yaani sheria zinazohusu mambo ya Muungano.

Tafsiri nyingine yoyote ya ibara hii itakuwa na maana kwamba – pamoja na mamlaka yake juu ya mambo yote ya Tanzania Bara yasiyokuwa ya Muungano - Bunge lako tukufu lina mamlaka ya kutunga sheria juu ya jambo lolote lisilokuwa la Muungano kwa Zanzibar ili mradi tu sheria hiyo imetamka kwamba itatumika Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, kama ilivyo kwa Muswada huu.

Endapo tafsiri hiyo itakubaliwa, basi Bunge lako tukufu halitakuwa na mipaka katika mamlaka yake ya kutunga sheria na mfumo mzima wa mgawanyo wa madaraka katika ya mamlaka za Muungano na mamlaka za Zanzibar utakuwa umepinduliwa. Na hiyo ikitokea, muundo mzima wa Muungano ulioangikwa juu ya Mapatano ya Muungano ya mwaka 1964 utakuwa umepinduliwa, na Zanzibar itakuwa imemezwa na Tanganyika, kwa sababu Bunge lako tukufu halitakuwa na kizingiti cha kutunga sheria yoyote juu ya jambo lolote la Zanzibar ambalo liko nje ya Katiba ya sasa na nje ya Mapatano ya Muungano. Kwa vyovyote vile, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inaamini, hii haiwezi kuwa tafsiri sahihi ya ibara ya 64(4) ya Katiba.

Mheshimiwa Spika,
Kuna masharti mengine ya kikatiba. Hata kama ikiamuliwa kwamba masuala ya TEHAMA ni sehemu ya ‘posta na simu’ na kwa hiyo ni mambo ya Muungano, Katiba yetu imeelekeza kwamba "Muswada wa Sheria kwa ajili ya kubadilisha ... masharti yoyote ya Sheria yoyote yanayohusika na jambo lolote kati ya mambo yaliyotajwa katika Orodha ya Pili kwenye Nyongeza ya Pili ... utapitishwa tu iwapo utaungwa mkono kwa kura za Wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Zanzibar."

Mheshimiwa Spika,
Ili kuhakikisha kwamba Bunge lako tukufu linafahamu fika mipaka yake ya kutunga sheria kwa mambo ya Muungano, Katiba yetu imefafanua maana ya maneno ‘kubadilisha masharti ya Katiba hii au masharti ya Sheria.’ Maana ya maneno hayo, kwa mujibu wa ibara ya 98(2), "... ni pamoja na kurekebisha au kusahihisha masharti hayo au kufuta na kuweka masharti mengine badala yake au kusisitiza au kubadilisha matumizi ya masharti hayo."

Katika mazingira haya, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako ukufu inapendekeza kwamba ili kutimiza matakwa na masharti ya Katiba yetu, aya ya 2 ya Muswada irekebishwe ili isomeke kwamba sheria hii itatumika Tanzania Bara tu. Vinginevyo, kama pendekezo hili haliwezekani, basi masharti ya ibara ya 98(1)(b) ya Katiba yafuatwe katika kupitisha Muswada huu. Nje ya hapo, masharti ya ibara ya 64(5) yatapata nguvu: "... Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri nzima ya Muungano na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka masharti yaliyomo katika Katiba hii, Katiba ndiyo itakuwa na nguvu, na sheria hiyo nyingine, kwa kiasi inachokiuka Katiba, itakuwa batili."

Mheshimiwa Spika,
Hata kama masharti ya ibara ya 98(1)(b) yatafuatwa kikamilifu katika kupitisha Muswada huu, bado kuna masharti zaidi ambayo yamewekwa katika Katiba ya Zanzibar, 1984, kama ilivyorekebishwa mwaka 2010. Kwa mujibu wa ibara ya 132(1) ya Katiba hiyo, "hakuna sheria yoyote itakayopitishwa na Bunge la Muungano ambayo itatumika Zanzibar mpaka sheria hiyo iwe ni kwa ajili ya mambo ya Muungano tu na ipitishwe kulingana na maelekezo yaliyo chini ya vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano."

Na ili kuhakikisha kwamba Bunge lako tukufu linazingatia mamlaka yake, ibara ya 132(2) imeweka masharti ya ziada kwamba "Sheria kama hiyo lazima ipelekwe mbele ya Baraza la Wawakilishi na Waziri anayehusika." Kwa sababu hizi, Mheshimiwa Spika, endapo Bunge lako tukufu litapitisha Muswada huu bila kujali mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu kuhusu utaratibu mahsusi wa kuupitisha, ifahamike kwamba uwezekano wa Muswada kukataliwa kutumika Zanzibar utakuwa mkubwa sana.

MAKOSA YA KIMTANDAO

Mheshimiwa Spika,
Kama jina lake linavyopendekeza, Muswada huu unatengeneza makosa ya kimtandao. Sehemu yote ya II ya Muswada inahusu ‘makosa na adhabu’ zake. Sehemu hii ina orodha ndefu ya makosa ya kimtandao. Aya ya 4(1) inatengeneza kosa la ‘kuingia kinyume cha sheria’ na inakataza mtu yeyote kuingia au "kusababisha kuingiliwa mfumo wa kompyuta kinyume cha sheria na kwa makusudi." Aya ya 4(2) inapendekeza adhabu ya "... faini ya kiasi ambacho ni kikubwa kati ya kiwango kisichopungua shilingi milioni tatu au mara tatu ya thamani ya faida iliyopatikana kinyume cha sheria, au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja au vyote."

Mapendekezo haya yana mapungufu yafuatayo. Kwanza, kosa linalopendekezwa haliangalii sababu au nia ya mkosaji. Kosa linalopendekezwa ni aina ya makosa yanayojulikana kwa lugha ya kisheria kuwa makosa ya strict liability, yaani makosa ambayo hayaangalii sababu au nia ya mkosaji.

Mfano mzuri wa makosa haya ni makosa ya usalama barabarani kama vile kuendesha gari bila leseni au kwenda mwendo kasi katika maeneo ambayo mwendo kasi umedhibitiwa. Haijalishi kama dereva asiyekuwa na leseni ameendesha gari kwa lengo jema la kuokoa maisha ya mgonjwa au kwa sababu leseni yake imeibiwa. Anahesabika kuwa ametenda kosa la jinai na anastahili adhabu iliyowekwa na sheria.

Makosa ya aina hii ni departure kutoka kwa kanuni kuu ya uwajibikaji wa kijinai, yaani ili kitendo chochote kihesabike kuwa kosa la jinai ni lazima mwenye kutenda kitendo hicho awe pia na nia mbaya, mens rea kwa lugha ya kisheria, katika kutenda kitendo hicho. Kisheria, bila kuthibitika uwepo wa mens rea, kitendo chochote ‘hata kiwe kibaya namna gani’ hakiwezi kuwa kosa la jinai.

Mheshimiwa Spika,
Kosa la kuingia kinyume cha sheria linalopendekezwa katika aya ya 4 litawahusu pia whistle-blowers (wapuliza vipenga), yaani raia wema wanaoingia au kusababisha kuingiliwa kwa mifumo ya kompyuta kwa malengo ya kupata ushahidi wa wizi au ufisadi au makosa mengine yanayofanywa na viongozi na watendaji wakuu wa taasisi na idara za serikali na mashirika ya umma na hata makampuni binafsi.

Ni muhimu kwa Bunge lako tukufu kutambua kwamba kashfa kubwa za wizi na ubadhirifu mkubwa wa fedha na mali nyingine za umma ambazo zimetikisa nchi yetu katika miaka ya karibuni kama vile EPA, Akaunti ya Tegeta Escrow, Richmond/Dowans, Chenji ya Rada na nyinginezo zilianzia kwa whistle-blowers kuingia katika mifumo ya kompyuta ya wahusika au ya kibenki na kuvujisha siri za wahalifu hao. Bila ya hivyo, kashfa hizo zisingejulikana, wahusika wasingegundulika na kuwajibishwa na taifa letu lisingepona kwa ulafi wa mafisadi hao.

Mheshimiwa Spika,
Kwa mapendekezo ya aya ya 4, ‘wapiga vipenga’ dhidi ya mafisadi na wahalifu wanaotumia nyadhifa zao za umma kulihujumu taifa na kujitajirisha binafsi nao watafanywa kuwa wahalifu na watastahili kuadhibiwa kwa kifungo cha miaka mitatu au faini isiyopungua shilingi milioni 3 au vyote kwa pamoja. Kwamba raia wema hawa wanafanya hivyo kwa nia njema ya kuokoa mali ya umma na kufichua mafisadi na wahalifu wengine waliojificha katika mavazi ya utumishi wa umma haitakuwa utetezi mahakamani.

Kwa mapendekezo haya, hata kama sio lengo lake, watoa taarifa za uhalifu ndio watakuwa wahalifu na watastahili adhabu zinazopendekezwa, wakati wezi wakubwa, mafisadi na wahalifu wa aina hiyo wanaoficha taarifa zao kwenye mifumo ya kompyuta watapata ulinzi wa sheria. Hili haliwezi kuwa mojawapo ya malengo ya sheria ya kupiga vita makosa ya kimtandao kama wanavyojinasibu watetezi wa Muswada huu.

Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inapendekeza kwamba aya ya 4 ifanyiwe marekebisho kwa kuongeza aya ndogo ya (3) itakayolinda whistle-blowers wanaopuliza vipenga pale wanapopata taarifa za, au ushahidi wa, uhalifu unaofichwa katika mifumo ya kompyuta na hivyo kuwezesha uhalifu huo kufichuliwa na wahalifu husika kuwajibishwa.

Mheshimiwa Spika,
Mapungufu ya aya ya 4 ya Muswada huu yanahusu pia makosa ya ‘matumizi ya mfumo wa kompyuta kinyume cha sheria’, ‘kuingilia mawasiliano kinyume cha sheria’, ‘kuingilia data kinyume cha sheria’ na ‘ujasusi data.’ Aidha, makosa ya ‘kuingilia mfumo kinyume cha sheria’, ‘kifaa kisicho halali’, ‘kutoa taarifa za uongo’, ‘taarifa zinazotumwa bila ridhaa’ na ‘ukiukaji wa haki bunifu usiohusiana na masuala ya kibiashara’, nayo pia yanahusika na msimamo kuhusu aya ya 4. Kwa mapendekezo haya pia, mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu kuhusu ulinzi wa wapiga vipenga dhidi ya wahalifu yanahusika vile vile.

Mheshimiwa Spika,
Upungufu wa pili wa mapendekezo ya aya ya 4 ni kwamba kuna dhana kwamba kila anayetenda kosa hilo anafanya hivyo kwa lengo la kujinufaisha binafsi kifedha. Dhana hii ni ya makosa. Sio kila anayetenda kosa la kuingia kinyume cha sheria anafaidika na kitendo hicho. Whistle-blowers wengi wanaotoa taarifa za uhalifu unaofichwa kwenye mifumo ya kompyuta wanafanya hivyo bila kufaidika kifedha kwa kutoa siri za uhalifu unaofanywa na wakubwa. Hata mapendekezo ya aya ya 24(2)(a) yanaelekea kutambua suala hili.

Ukweli ni kwamba wapiga vipenga hawa wanajiweka katika hatari kubwa ya maisha yao ama ajira zao kwa kufichua uhalifu unaofanywa na wakubwa na kuhifadhiwa katika mifumo ya kompyuta. Kwa sababu hiyo, sambamba na mapendekezo ya kuwapa kinga ya kisheria wapiga vipenga hao, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inapendekeza kwamba adhabu za faini zinazopendekezwa zisitolewe pale ambapo wakosaji hawakunufaika kifedha na vitendo vilivyokatazwa.

MASHARTI YA MAADILI YA KIDINI?

Mheshimiwa Spika,
Huu sio Muswada wa kutengeneza maadili ya kidini bali ni Muswada wa kudhibiti makosa ya kimtandao. Hata hivyo, mapendekezo ya aya ya 14 yanaingiza dhana ya religious morality kwenye Muswada huu. Kwanza, aya ya 14(1)(a) inapiga marufuku kile kinachoitwa uchapishaji wa ponografia. Pili, aya ya 14(1)(b) inapiga marufuku uchapishaji wa "ponografia yoyote iliyo ya kiasherati au chafu." Adhabu kwa kosa la kwanza ni "... faini isiyopungua shilingi milioni ishirini au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka saba au vyote." Adhabu inayopendekezwa kwa kosa la pili ni "... faini isiyopungua shilingi milioni thelathini au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka kumi au vyote."

Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu haikubaliani na mapendekezo haya kwa sababu zifuatazo. Kwanza, maneno ‘ponografia’ au ‘ponografia iliyo ya kiasherati au chafu’ hayajatafsiriwa wala kufafanuliwa mahali popote katika Muswada huu. Hii ni omission ya kushangaza kwa vile maneno ‘ponografia za watoto’ yametafsiriwa kwenye aya ya 3 ya Muswada.
Kamusi ya Kiingereza Oxford Advanced Learners' Dictionary inatafsiri neno ‘pornopgraphy’ kuwa ni "the describing or showing of naked people or sexual acts in order to cause sexual excitement", yaani ‘kuelezea au kuonyesha watu walio uchi au matendo ya ngono kwa lengo la kusababisha mhemuko wa ngono.’ Kama hii ndio tafsiri ya kawaida ya ‘ponografia', je, kuna kipimo chochote cha mtu kuwa uchi?

Swali hili ni muhimu kwa sababu, kwa kadri ya ufahamu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, hakuna kipimo kinachokubalika na watu wote. Kwa mfano, kwa Waislamu, mwanamke yeyote ambaye hajavaa hijab au niqab anahesabika kuwa yuko uchi; wakati katika utamaduni wa kiMagharibi mwanamke aliyevaa chupi ndogo na sidiria tu hahesabiki kuwa yuko uchi!!! Aidha, kuna watu wanaoamini kwamba wanawake wanaovaa sketi au kaptula fupi au nguo za kubana wako uchi.

Je, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inataka kujua, Muswada huu unapendekeza kupiga marufuku uchapishaji wa picha zozote za watu waliovaa lingerie na brassiere, au sketi za mini au suruali za kubana? Je, Muswada huu unapendekeza kupiga marufuku picha za ngono hata zile za watu wazima zinazouzwa katika maduka halali ya vifaa vya elektroniki dunia nzima?

Je, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inaomba kufahamishwa, Muswada huu unapendekeza kupiga marufuku kuchapisha au kuonyesha au kusambaza picha za filamu maarufu kama picha za ‘X' hata kama ni kwa matumizi binafsi ya watu wazima? Kama huku sio kutaka kuingilia masuala binafsi ya watu wazima ambayo yanalindwa na haki ya faragha chini ya ibara ya 16 ya Katiba yetu ni nini? Kwa sababu hizi, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inapendekeza aya yote ya 14 ifutwe katika Muswada huu.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapinga mapendekezo ya aya za 15 na 16 za Muswada vile vile. Aya ya 15 inakataza mtu yeyote kujifanya kuwa mtu mwingine kwa kutumia mfumo wa kompyuta; na inapendekeza adhabu ya "... faini ya kiasi ambacho ni kikubwa kati ya kiwango kisichopungua shilingi milioni tano au mara tatu ya thamani ya faida iliyopatikana kinyume cha sheria, au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka saba au vyote."

Kwa upande wake, aya ya 16 inafanya kosa kwa mtu yeyote kutoa taarifa, data au maelezo kwa njia ya picha, maandishi, alama au aina nyingine yoyote kwenye mfumo wa kompyuta, "endapo taarifa, data au maelezo hayo ni ya uongo, yanapotosha au yasiyo sahihi...." Adhabu inayopendekezwa kwa kosa hili ni "... faini isiyopungua shilingi milioni tatu au kutumikia adhabu ya kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita au vyote."

Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, makosa haya na adhabu zake hayajafanyiwa tafakuri ya kutosha. Kwanza, kuna tatizo la kukosekana kwa mens rea au nia mbaya katika kitendo kinachokatazwa, ambalo limejadiliwa kwa kirefu kuhusiana na aya ya 4 ya Muswada. Sio kila mtu anayefanya impersonation mtandaoni anafanya hivyo kwa malengo haramu au kwa nia mbaya. Na sio kila mtu anayetengeneza picha ya uongo ya mtu mwingine, mfano kiongozi wa nchi, kwa kutumia photoshop mtandaoni anafanya hivyo kwa malengo au nia haramu.

Watu wengi wanafanya hivyo kwa malengo mbali mbali ikiwemo kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya matendo au kauli au tabia za watu hao. Vitendo hivyo havina tofauti sana na uchoraji na usambazaji wa katuni katika magazeti, ambalo ni jambo la kawaida kabisa katika taaluma ya uandishi habari. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, vitendo vyote hivi vinalindwa na haki ya uhuru wa mawazo na maoni chini ya ibara ya 18 ya Katiba ya nchi yetu na hakuna haja wala sababu yoyote ya maana ya kuvijinaisha.

Mheshimiwa Spika,
Yapo mapendekezo mengine ambayo pia yanakiuka haki ya uhuru wa mawazo na maoni na, kwa sababu hiyo, yanapingana na Katiba. Kwa mujibu wa aya ya 19(1) ya Muswada, "mtu hatachapisha au kusababisha kuchapishwa vitu vinavyochochea, kukanusha, kupunguza au kuhalalisha matendo yanayopelekea mauaji ya kimbari na makosa dhidi ya ubinadamu kwa kupitia mfumo wa kompyuta." Adhabu ya kosa hilo inapendekezwa kuwa "... faini isiyopungua shilingi milioni kumi au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu au vyote." Mapendekezo haya yana mapungufu makubwa yafuatayo.
Kwanza, hakuna tafsiri ya ‘matendo yanayopelekea mauaji ya kimbari' wala ya ‘makosa dhidi ya binadamu.' Je, ni matendo kama yale yaliyofafanuliwa katika Mkataba wa Roma ulioanzisha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai? Muswada uko kimya. Muswada uko kimya pia kuhusu mauaji ya kimbari ambayo ni makosa kuyakanusha kwa mapendekezo ya aya ya 19. Je, ni Mauaji ya Kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994? Au ni Holocaust, yaani mauaji ya kimbari ya Wayahudi yaliyofanywa na utawala wa kiNazi wa Adolf Hitler kabla na wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia? Au ni mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Wazungu dhidi Wenyeji wa Asili wa Amerika ya Kaskazini ambao ulipelekea Wenyeji wa Asili kutoweka kabisa katika uso wa dunia?

Mheshimiwa Spika,
Katika historia ya ukoloni katika Afrika na kwingineko katika nchi za ulimwengu wa tatu zilizotawaliwa na Wazungu, kulikuwa na matukio mengi ambayo wanahistoria wa sasa wanayataja kuwa ni mauaji ya kimbari. Kwa mfano, katika kuzima Maasi ya Maji Maji mwaka 1905-07 nchini mwetu, Wajerumani waliua zaidi ya watu laki moja na elfu ishirini wa makabila ya Wangoni, Wamatumbi, Wangindo, n.k. Wajerumani pia waliua zaidi ya watu laki moja wa makabila ya Wanama na Waherero wa Namibia wakati wakizima Maasi ya Wanama na Waherero ya mwaka 1904-05.

Aidha, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Caroline Elkins, Waingereza walisababisha mauaji ya zaidi ya Wakikuyu laki moja wakati wa kuzima Maasi ya Mau Mau nchini Kenya kati ya mwaka 1952-60. Yote haya, kwa tafsiri ya sasa ya historia, yanahesabika kuwa ni mauaji ya kimbari. Je, kwa mapendekezo ya aya ya 19 ya Muswada, kukanusha au kupunguza au kuhalalisha matendo yaliyopelekea mauaji haya ya kimbari ni kosa lenye kustahili adhabu ya faini ya shilingi milioni kumi au kifungo cha miaka mitatu kama inavyopendekezwa? Muswada huu uko kimya.

Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo ya Muswada huu katika maeneo ambayo tumeyaonyesha yamewekwa kwa lugha pana ambayo inaweza kuingiza wahalifu wa kweli na wananchi wa kawaida kabisa ambao hata hawaelewi kuwa wanafanya makosa makubwa ya jinai. Mfano mzuri wa lugha pana ya aina hii ni neno ‘kuchapisha' ambalo limetumika katika aya za 13, 14 na 19 za Muswada. Kwa mujibu wa aya ya 3, ‘kuchapisha' maana yake ni "usambazaji, uwasilishaji, uwekaji wazi, kubadilishana, uchapishaji, au usambazaji wa aina yoyote ile."

Maneno mengine yenye tafsiri pana katika Muswada huu ni ‘taarifa zinazotumwa bila ridhaa' ambayo yametumika katika aya ya 20. Kwa mujibu wa aya ya 20(3), maneno hayo yana maana ya "... taarifa au data za kielektroniki ambazo hazijaombwa na mpokeaji." Maana ya tafsiri hii ni kwamba mtu yeyote ‘hata Mbunge - anayetuma sms au picha ya Whatspp juu ya jambo lolote kwa Mbunge au mtu mwingine yeyote bila kuombwa na mpokeaji anafanya kosa la ‘taarifa zinazotumwa bila kuombwa' na akipatikana na hatia "... atawajibika kulipa faini ya kiasi ambacho ni kikubwa kati ya kiwango kisichopungua shilingi milioni tatu au mara tatu ya thamani ya faida iliyopatikana kinyume cha sheria, au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja au vyote."

Hata neno ‘kuingilia' ambalo limetumika mahali pengi katika Muswada huu lina maana isiyokuwa na kikomo. Kwa mujibu wa aya ya 3, ‘kuingilia' kuhusiana na utendaji kazi wa kompyuta "inajumuisha upatikanaji, utazamaji, usikilizaji au kunukuu data yoyote ya mawasiliano ya kompyuta au mifumo ya kompyuta kwa njia yoyote ya kielektroniki." Hivyo, kwa mfano, mtu yeyote anayetumia earphone kusikiliza muziki kutoka kwenye simu ya mkononi au kompyuta anadakwa na wavu wa kosa hili na anastahili adhabu iliyotajwa katika aya ya 4 ya Muswada.

Mheshimiwa Spika,
Kwa tafsiri hizi, vitendo vyote ambavyo Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa mamilioni nje ya Bunge hili tukufu wanavifanya katika maisha yao ya kila siku kwa kutumia simu zao za mkononi au kompyuta za maofisini au majumbani kwao, vinahesabika kuwa ni ‘kuchapisha' na kwa hiyo ni makosa ya jinai yenye kustahili adhabu kubwa zinazopendekezwa na Muswada huu.

Mheshimiwa Spika,
Muswada wenye masharti yaliyoandikwa kwa lugha ya jumla jumla na pana kiasi hiki ni mtego wa panya: una uwezo wa kukamata panya waliolengwa na hata wanadamu ambao hawajalengwa na mtego huo. Ndio maana, Mahakama ya Juu ya India, katika kesi iliyoamuliwa Jumanne ya wiki iliyopita, imetamka kwamba kifungu cha 66A cha Sheria ya Teknolojia ya Habari ya India kinakiuka Katiba ya nchi hiyo kwa sababu "kinavamia haki ya uhuru wa maoni kwa kuwa kila neno lililotumika kwenye kifungu hicho lina maana pana (‘nebulous')."

Kama ilivyo kwa Sheria ya Teknolojia ya Habari ya India, mapendekezo ya Muswada huu ni hatari na tishio kwa haki za kikatiba za uhuru wa mawazo na maoni kwa wananchi wa Tanzania. Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inaliomba Bunge hili tukufu kukataa kupitisha Muswada huu wa hatari kwao wenyewe na kwa wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika,
Sehemu ya Tatu ya Muswada inahusu ‘Mamlaka ya Mahakama’ na inapendekeza utaratibu wa kusikiliza kesi za makosa ya mtandao. Kwa mujibu wa aya ya 30(1), Mahakama zitakuwa na uwezo wa kusikiliza shauri lolote chini ya Sheria hii pale ambapo kosa au sehemu ya kosa limetendeka ndani ya Jamhuri ya Muungano; au kwenye meli au ndege iliyosajiliwa Tanzania; au limetendwa na Mtanzania au Mtanzania anayeishi nje ya Tanzania, n.k.

Aya ya 30(2) inatafsiri neno ‘mahakama’ kumaanisha ‘mahakama yenye mamlaka.’ Tafsiri hii ni ya hovyo na haina maana yoyote kisheria. Je, ‘mahakama’ kwa minajili ya makosa ya mtandao ni pamoja na Mahakama ya Mwanzo, au Mahakama ya Wilaya, au Mahakama ya Hakimu Mkazi, au Mahakama Kuu ya Tanzania au ya Zanzibar, au Mahakama ya Rufani ya Tanzania? Au ni Mahakama ya Mkoa kwa Zanzibar? Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu haitaki kuamini kwamba inawezekana Muswada huu umeandaliwa na mtaalamu mwelekezi asiyekuwa na ufahamu wowote wa mfumo wa kimahakama wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika,
Kwa sababu zote hizi, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu haiwezi kuunga mkono Muswada wenye mapungufu kama Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao.

-----------------------------------------------
LUCY FIDELIS OWENYA (MB)
K.N.Y. MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Bottom of Form

Comments