Featured Post

SAFARI MPYA YA LOWASSA IKULU 2020 NA ‘RAMLI’ YA T.B. JOSHUA



Na Daniel Mbega
ZILE ndoto za kukaa pale kwenye Nyumba Nyeupe – Magogoni, nadhani sasa itakuwa Chamwino – Dodoma, za mwanasiasa Edward Lowassa, bado zinamjia na safari hii inaonekana zimezidi.

Mwasiasa huyo, ambaye alitangaza ‘safari mpya ya matumaini’ ya kwenda Ikulu mwaka 2020 tangu Alhamisi, Januari 14, 2016 alipozungumza na wafanyabiashara wanaounda Timu ya Mabadiliko kutoka Soko la Kariakoo ofisini kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam akisema yuko tayari kugombea hata ikiwa mara tano, sasa amejipanga kurejea jukwaani kwa staili nyingine.
Tofauti na uchaguzi mkuu uliopita ambapo alitambia mtaji wa kuwa na wafuasi wengi, safari hii Lowassa (64) anategemea zaidi utabiri, na huu si wa mwingine, bali ni wa ‘rafiki yake’ Temitope Balogun Joshua, maarufu kama T. B. Joshua, mchungaji na kiongozi wa Kanisa la Sinagogi la Mataifa Yote (The Synagogue, Church of All Nations - Scoan) la Nigeria.
Sidhani kama rafiki yako anaweza kukutabiria mabaya!
Lowassa, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliwaambia viongozi wa chama hicho mkoani Tabora Jumanne, Desemba 13, 2016 kwamba, ataingia Ikulu baada ya miaka minne ijayo na rafiki yake T.B Joshua amemtabiria kuwa Serikali ijayo itaongozwa na Chadema.
Na utabiri wenyewe aliopewa hata mtoto mdogo angeweza kumtabiria na akaamini, kwamba, ili washinde ni lazima wawe wamoja, washikamane na kuwa majasiri.
“Najua waandishi wa habari wataandika, lakini sijali rafiki yangu Joshua ametabiri Serikali ijayo ya Tanzania itaongozwa na Chadema,” akasema huku akishangiliwa.
Mwanasiasa huyo anaonekana kutokata tamaa licha ya kuangushwa na Dk. John Magufuli wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu uliopita ambapo yeye akigombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alipata kura 6,072,848 (sawa na 39.97%) dhidi ya kura 8,882,935 (58.46%) za Magufuli.
Lowassa, Waziri Mkuu aliyelazimishwa kujiuzulu kufuatia kashfa ya mkataba wa kinyonyaji wa kampuni ya ufuaji umeme wa dharura ya Richmond Development LLC, anashindwa kutambua kwamba katika uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 aliungwa mkono na vyama vinne – Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD – kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mwanasiasa huyo anaamini kwamba ‘alishinda uchaguzi huo lakini akapokwa ushindi’ kwa maelezo kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilichakachua matokeo, lakini bado anaamini kwamba anapendwa na Watanzania na anaweza kushinda, hata kama atagombea mara tano.
Anajipa matumaini makubwa kwamba, hata nchini Marekani kuna mwanasiasa aliyewahi kugombea na kushindwa mara nne lakini akashinda mara ya tano, hivyo anaamini hata yeye atashinda mbele ya safari.
“Hata nchini Marekani kuna mtu aliwahi kugombea urais mara nne, lakini mara ya tano alishinda na alipoingia Ikulu akafanya mambo makubwa ambayo yaliwashangaza watu mpaka wengine wakahoji ni kwa nini tulikuwa hatumpi kura,” alikaririwa akisema Januari mwaka huu.
Lowassa anashindwa kusoma alama za nyakati na mbaya zaidi, hata maswali kadhaa ya msingi hataki kujiuliza.
Kama ni safari ya matumaini nakumbuka ilianza Jumapili, Julai 9, 1995 wakati Lowassa na rafikiye Jakaya Mrisho Kikwete walipowachukua baadhi ya waandishi wakaongozana nao kwenye ndege ya kukodi hadi Dodoma, ambako mapema tu Jumatatu, Julai 10, 1995 wakachukua fomu zao za kuomba ridhaa kupitia CCM.
Baada ya kujeruhiwa katika ile ‘ajali ya kisiasa’ Februari 8, 2008, tunaelezwa kwamba jitihada kubwa zikaanza za ‘kumsafisha na kumtakasa’ ili kuipepelea ‘safari ya matumaini’ ambayo nayo ilinasa kwenye tope kule Dodoma kabla Chadema haijamnasua ambapo alikimbilia upinzani na moja kwa moja safari ya matumaini ikafufuka baada ya kukabidhiwa mikoba aliyokuwa aibebe Dk. Wilbrod Slaa.
Lowassa anashindwa kutambua – ama hataki kukubali – kwamba, kilichomsaidia katika uchaguzi wa 2015 kwanza ni mtandao aliokuwa ameuimarisha ndani ya CCM, kwa sababu wanamtandao hao waliamini mwanasiasa huyo ndiye angeweza kushinda.
Wengi ‘wakatoroka’ naye kwenda Chadema, wakiwemo makada waandamizi wa CCM kama Kingunge Ngombale-Mwiru, Frederick Sumaye, John John Guninita, Matson Chizii, Mgana Izumbe Msindai, Makongoro Mahanga, Balozi Juma Mwapachu (ambaye amerejea CCM), Lawrence Masha, Hamisi Mgeja na wengineo wengi.
Na walitoroka wakiamini kwamba, baada ya Oktoba 25, 2015 Lowassa atakapokuwa Ikulu, basi nao wangeweza kuwa ‘jirani’ naye kwa maana ya kupewa nafasi mbalimbali za uongozi. Ndoto zile zikapotea.
Lakini pili, Lowassa hataki kuamini kwamba, alipata nguvu kubwa katika upinzani kutokana na nguvu ya Ukawa. Wananchi walikuwa na imani na umoja huo tangu ulipoundwa mwaka 2014 kupinga mwenendo wa majadiliano ya Bunge Maalum la Katiba, wakata kuona mabadiliko, ambayo hawakuyaainisha kama ni mabadiliko chanya au hasi.
Kwa maana nyingine, nguvu ya Lowassa ilitokana na uchu wa Watanzania kuona changamoto zilizokuwa zikiwakabili zinapatiwa ufumbuzi na serikali. Walikuwa wanaamini CCM imeshindwa kupambana na ufisadi na kutatua kero za wananchi, hivyo licha ya Lowassa kukabiliwa na tuhuma za ufisadi zilizonadiwa kwa nyimbo na mapambio na Chadema, bado wananchi walitaka kufanya mabadiliko – waitoe CCM.
Lowassa anapaswa kujiuliza, kama kwa nguvu ya ‘mabadiliko’ iliyokuwa nyuma yake alishindwa kuingia Ikulu, sasa anawezaje kutegemea utabiri wa TB Joshua kuwa atashinda 2020?
Lowassa anapaswa kujiuliza pia kwamba, kama Ukawa ilikuwa na nguvu kipindi kile licha ya wananchi ‘kufumbia macho’ mchezo mchafu uliotokea siku chache kabla ya kuanza kampeni, hivi sasa umoja huo umezikwa, na unaonekana ulikuwa ukibebwa sana na Chadema, lakini baada ya uchaguzi inaonekana dhahiri kila mtu ‘amekufa na chake’. Chadema imefanikiwa kuzoa viti vingi vya ubunge na udiwani kwa mgongo huo huo wa Ukawa, CUF nayo imepata viti vya kutosha Tanzania Bara kwa mara ya kwanza katika historia yake, lakini NCCR imeambulia kiti kimoja tu wakati NLD haikupata chochote.
Jambo baya zaidi ni kwamba, Chadema yenyewe imekumbwa na kashfa nyingi zinazoidhoofisha.
Nguvu ya Chadema iliyokuwepo mwaka 2010 haipo sasa na hata hamasa ya 2015 iliyoonekana kama chamchela nayo imedorora.
Kitendo cha kumkaribisha Lowassa, mtu ambaye Chadema hao hao walimwanika hadharani kwamba ni miongoni mwa mafisadi 11 wanaoiangamiza Tanzania katika ile ‘Orodha ya Aibu’ (List of Shame) pale Mwembeyanga Jumamosi ya Septemba 15, 2007 pamoja na tuhuma ambazo hazijajibiwa za kwamba walipewa Shs. 10 bilioni ili kumkaribisha mwanasiasa huyo, kimewaondolea kabisa nguvu ya kuwa chama kikuu cha upinzani nchini.
Lowassa amekuwa akienda Lagos, Nigeria kuhudhuria ibada za T.B Joshua, ‘rafiki yake’ kama ananvyosema, na safari yake ya kwanza kabisa ilikuwa Juni 12, 2011 wakati alipohudhuria kwa mara ya kwanza ibada akiwa katika harakati za kujitakasa baada ya ‘ajali mbaya ya kisiasa’.
Lakini T.B. Joshua ndiye kiongozi wa dini ambaye tabiri zake nyingi zina mashaka.
Novemba 6, 2016 alitabiri kwamba, mgombea urais nchini Marekani kwa tiketi  ya chama cha Democratic, Hillary Clinton, angeshinda uchaguzi huo, lakini matokeo yake akaangukia pua mbele ya mgombea wa Republican, Donaldo Trump.
Ndiyo maana mara baada ya kushinda, Trump alitangaza hataki kumuona mtabiri huyo nchini Marekani.
Umoja, mshikamano na uvumilivu ndizo silaha za ushindi katika maisha, hivi na hili nalo unasubiri mpaka mtabiri TB Joshua akueleze?
Nadhani kama kukonyeza gizani, basi kumezidi na kwa hakika safari ya matumaini ya 2020 inaonekana kutokuwa na mwelekeo. Akae chini atafakari.

0656-331974
www.brotherdanny.com

Comments