Featured Post

MHANDISI MAKANI ATOA WIKI MBILI KWA WAFANYAKAZI NGORONGORO KUWASILISHA TAARIFA ZA MIFUGO NA MAJENGO YA KUDUMU WANAYOMILIKI NDANI YA HIFADHI HIYO

 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (katikati) akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wilayani Ngorongoro mkoani Arusha jana katika ziara yake ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu. Kulia ni Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Freddy Manongi na Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha (kushoto). 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wilayani Ngorongoro mkoani Arusha jana katika ziara yake ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu,  ametoa wiki mbili kwa watumishi wenye mifugo na majengo ndani ya eneo la mamlaka ya hifadhi hiyo kujiandikisha kwa uongozi wa mamlaka hiyo ikiwa ni mkakati wa utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu. 
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha akichangia katika mkutano huo. Alieleza kuwa salama ya Hifadhi ya Ngorongoro itategemea uwekaji wa mizania sawa baina ya uhifadhi na maendeleo ya wananchi wa eneo hilo.
 Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Freddy Manongi (katikati) akizungmza katika mkutano huo. Kushoto ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexandre Songorwa (kulia).
 Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, Mfaume Taka (kushoto) akizungumza kwenye mkutano huo.
 Sehemu ya watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wakiwa kwenye mkutano huo.

................................................................................................
NA HAMZA TEMBA - WMU
....................................................

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani ametoa wiki mbili na siku tano kwa watumishi wote wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wenye mifugo na majengo ya kudumu  ndani ya eneo la hifadhi hiyo kuorodhesha majina yao kwa uongozi wa mamlaka hiyo  na kusalimisha taarifa ya kile wanachokimiliki ndani ya eneo hilo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa utekelezaji maagizo ya Waziri Mkuu  aliyoyatoa kwa uongozi wa mamlaka hiyo.

Ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na watumishi wa Mamlaka hiyo mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na Ngorongoro katika kikao alichokiitisha kwenye ukumbi wa makao makuu ya NCAA yaliyopo katika wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha kwa ajili ya kufuatilia changamoto za uhifadhi na utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoyatoa kwa mamlaka hiyo hivi karibuni akiwa ziarani mkoani Arusha.

Anasema miongoni mwa maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu ambayo yameshaanza kufanyiwa kazi ni pamoja na kuondolewa mifugo yote maeneo ya Kreta, kuhakikisha upatikanaji wa maji na chumvi kwa ajili ya mifugo na wananchi, idadi ya mifugo kutambuliwa na kupigwa chapa pamoja na kutambua idadi ya wananchi ndani ya eneo la mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na kupewa hati za utambuzi.

“Mpaka ikifika wiki ya pili ya mwezi januari, tarehe 15, kila mtumishi ambaye yeye binafsi ana mifugo ndani ya eneo hili, maana tunaanzia nyumbani, Conservator (Mhifadhi) uweke utaratibu wa kupokea taarifa kutoka kwao, kila mmoja aweze kudeclare (kutangaza) umiliki wake wa mifugo ndani ya eneo la hifadhi, ng’ombe, mbuzi, kondoo.

"Lakini pia kila mtumishi ambaye ana nyumba ya kudumu ndani ya hifadhi, iliyojengwa kwa matofali, mabati, zege nakadhalika atuambie, na mimi nishauri tu kuwa muwazi itakusaidia. Kwasababu haiwezekani sisi tuanze kuwaambia watu wengine, wewe kwanini umejenga nyumba ya kudumu hapa, wakati tunapowaonyesha vidole na wengine sisi tunazo, hatuwezi kwenda kuwaambia wengine, wewe kwanini una mifugo humu 200,000, 2000, 1000 au 500 wakati wengine sisi humu tuna mifugo zaidi yao hata mara mbili", alisisitiza Makani.

Alisema kuwa, kwa wale waajiriwa wapya wapewe elimu juu ya malengo na majukumu mahsusi ya taasisi hiyo pamoja na miiko yake ambayo ni pamoja na uwepo wa maeneo maalum ya uhifadhi yasiyoruhusiwa mifugo na majengo ya kudumu.

Amewataka watumishi wa mamlaka hiyo kusoma kwa makini madhumuni ya kuanzishwa kwa mamlaka hiyo pamoja na majukumu makhsusi iliyopewa ili kufanya vizuri zaidi katika uhifadhi endelevu wa Hifadhi hiyo huku wakitambua kuwa wao ndio wenye jukumu la kwanza la kuhakikisha kuwa taasisi hiyo inastawi.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Makani ametoa muda wa wiki mbili kwa uongozi wa NCAA kumkabidhi taarifa ya mpango mkakati wa utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu. "Zile wiki mbili nilizozisema, ule mpango mkakati wa utekelezaji wa maagizo ya waziri mkuu, sina maana kwamba tutaanza kutekeleza kwenye wiki mbili, hivi tunavyoendelea kutekeleza kwa maana yapo mambo mengine hapa utekelezaji wake ni wa muda zaidi ya hizo wiki mbili, nataka nipate mpango kazi wa utekelezaji wa maagizo hayo tuujadili na kuufanyia kazi kwa haraka".

Alisema miongoni mwa changamoto kubwa za uhifadhi katika eneo hilo kwa sasa ni wingi wa mifugo pamoja na majengo ya kudumu ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro jambo lililohatarisha uhifadhi endelevu wa hifadhi hiyo.

Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Freddy Manongi amesema jukumu kuu la kuazishwa kwa mamlaka hiyo ni kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori na malikale, utalii na jamii iliyopo ndani ya Eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Akizungumzia changamoto  alisema kuna uhaba wa chakula kutokana na wananchi wa eneo hilo kuzuiliwa kulima kisheria, malalamiko kuhusu wanyama wakali kuwashambulia wananchi na ongezeko la magonjwa mbalimbali huku mengi yakisababishwa na muingiliano wa wananchi na  wanyamapori. 

Comments