Featured Post

KWA TAARIFA YAKO TU: KAMA SIYO ZINAA, DAR ES SALAAM ISINGEKUWEPO



 Barabara ya Ocean
Mchoro kuonyesha Waarabu wakiwa katika Bandari ya Dar es Salaam.

 Mtaa wa Acacia enzi za Mjerumani, ambao ndio Mtaa wa Samora sasa
 Bandari ya Dar wakati wa Mjerumani.

Na Daniel Mbega
DAR ES SALAAM, bandari kuu ya Tanzania katika Bahari ya Hindi, ni neno la Kiarabu lenye maana 'Bandari Salama' (Haven of Peace). Lakini chanzo chake hakikuwa na salama yoyote kwani kilisababishwa na mtu mmoja aliyejinonga, kama alivyoandika Morwenna Hartall katika kitabu cha Tanganyika Notes and Records, mnamo Aprili 1937.
Asili yake inahusisha kunyongwa kwa mtoto wa tajiri mmoja wa Kihindi aliyekamatwa akizini na mtoto wa kiongozi mmoja mashuhuri wa jadi.
Morwenna Hartall anasema hadithi ya jina 'Dar es Salaam' imetokana na kumbukumbu za maandishi zilizokuwa zikihifadhiwa na mtawala mmoja wa jadi, Pazi Degelubozi bin Mlawa, wa kabila la Wazaramo ambaye alisema maandishi hayo yaliandikwa kutokana na maelekezo yake na kwamba yeye alikuwa amesimuliwa hadithi hiyo na baba yake.
Hadithi hiyo ilisahihishwa na kuongezwa kumbukumbu nyingine na Ali bin Said, Mwarabu ambaye baadaye akaja kuwa 'akida' wa kwanza wa Dar es Salaam. Ali bin Said aliwasili Mzizima mwaka 1860 na akasema aliwafahamu watu wote walioandikwa katika historia hiyo ya Hartall.
Siku hizo hapo Mzizima aliishi bepari mmoja aliyeitwa Mamula. Wakati mtoto wa Mamula, Mtoro, alipokuwa akifanya mapenzi na binti ya Kitembe, mtawala wa jadi, wawili hao walikamatwa nyumbani kwa baba wa binti.
Kaka wa binti huyo, Mwinshehe, alikasirika sana kwa yule kijana wa Kihindi kuzini na dada yake, hivyo akamnyonga Mtoro. Babaye Mtoro akampeleka Mwinshehe kwa chotara mmoja wa Kiarabu, Said bin Abdallah. Said alikuwa mtoto wa Abdallah Maharubi, aliyekuwa akiishi Unguja.
Mamaye Said alikuwa mtumwa wa Abdallah aliyemfanya baadaye kuwa suria (kimada) wake, aliyeitwa Binti Nyaganyaga, Mzaramo kutoka ukoo wa akina Pazi Degelubozi bin Mlawa.
Said bin Abdallah alimweleza Kitembe, babaye Mwinshehe, kwamba Mzizima ilikuwa nchi isiyo na sheria, hivyo yeye Said angekwenda Unguja kushauriana na Sultani Majid. Wakati Said bin Abdallah alipokutana na Sultan Majid, hakueleza chochote kuhusu kunyongwa kwa Mtoro, ambaye ndiye aliyepelekea yeye afunge safari kwenda huko, badala yake akamwambia kwamba Mzizima, iliyokuwa Bara, ilikuwa nchi nzuri.
Baada ya kusikia hivyo, Sultani Majid akafunga safari kwa kutumia jahazi hadi Mzizima. Akaweka nanga karibu na bandari kisha akamtuma Said bin Abdallah aliyekwenda kwa mtumbwi hadi ufukweni kwa lengo la kwenda kumwita Kitembe na viongozi wengine wa jadi kutoka ukoo wa Shomvi. Wakati Kitembe alipokwenda kwa Sultan Majid, sultan akamwambia: "Nimekuita kwa sababu ninataka kuishi katika nchi yako."
Mtawala mmoja wa Washomvi, Mwinyimkee Chimba, akasimama na kusema: "Hatutaki uishi nchini kwetu." Lakini Kitembe alimwambia: "Huu siyo ustaabu. Ni jukumu letu kumwacha akae hapa kama atakuja kwa amani."
Sultani Majid, baada ya kuona mawazo yalikuwa yametofautiana, akaamua kuliacha suala hilo kwa Washomvi wenyewe wajadili, akamwambia Said bin Abdallah: "Waambie warudi majumbani mwao kwa sasa wakafikiri na kisha uwaite, lakini kila mmoja lazima awepo wakati watakapotoa majibu."
Said bin Abdallah aliyekuwa anaifahamu vyema lugha ya Kizaramo na ile ya Kiarabu hivyo kuwa mkalimani, akawaambia Washomvi jinsi Sultani Majid alivyosema na kisha kuashauri viongozi hao: "Msimkatae huyu kuishi hapa, mruhusuni aishi kwa amani."
Viongozi hao badaye walikubaliana na ushauri huo. Wakarejea wakiwa na majibu yao kwa sultani ambaye alifurahi na kuwaambia: "Sasa nakwenda kwanza Unguja. Badaye nitarejea na kuja na wau wangu ili wajenge katika nchi yenu."
Aliporejea tena, sultani aliingia moja kwa moja na kuweka nanga mahali ambapo leo hii iko bandari. Baada ya watawala wote wa jadi kkusanyika mahali hapo, fundi seremala mmoja aliyejulikana kwa jina la Baruti wadi Baruti, akatengeneza kahawa ya amani kabla ya kuanza kujenga nyumba za mawe.
Sultani Majid alikaa kwa miezi kadhaa hapo Mzizima, kipindi ambacho pia kilikuwa na sherehe nyingi, na akawapatia watawala wa jadi zawadi mbalimbali.
Kisha akawatuma Waarabu wote waliosafiri naye kutoka Unguja: "Pandeni mbegu (minazi) ambazo nitawaagizia kutoka Unguja na limeni nchi yangu ambayo sasa naipenda, mimi, Said Majid. Haitaitwa Mzizima tena, bali jina lake ni Bandar-es-Salaam - bandari ya salama, Bandari ya Amani - kwa sababu nimeipata kwa amani. Sikupigana na watawala wa jadi kuipata nchi hii."
Watawala wa jadi nao wakasema: "Nasi pia tunafurahi kwa sababu wewe na watu wako mnaishi hapa kwa amani na hamgombani na watu wetu." Hivyo ndivyo Mzizima ilivyobadilika na kuitwa Dar es Salaam, ambapo Mwarabu akaanza biashara zake Bara pamoja na kujitwalia eneo la Pwani ya Bahari ya Hindi.
Katika kuiita Mzizima Bandar-es-salaam, inaelezwa kwamba Sulani Majid alikuwa amemuiga Haroun-al-Rashid wa Iraq, ambaye aliuita mji wa Baghdad 'Dar es Salaam' kwa sababu naye pia aliutwaa bila kumwaga damu.
Kwa hiyo utaona kwamba, kama yule kijana asingefanya zinaa na binti wa watu, Sultan asingeweza kuja Bara, hivyo hata mji wa Mzizima usingebadilishwa jina na kuitwa Dar es Salaam na huenda usingekuwa mkubwa kama ulivyo sasa.

Comments