- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega
DESEMBA
15, 2016, Katibu Mwenezi wa NCCR-Mageuzi, David Kafulila alitangaza rasmi
kurejea katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya kuwa katika
chama hicho kwa takriban miaka 7 na siku kadhaa tangu alipojiunga nacho mwaka
2009.
Wakati ule
aliitwa ‘mkorofi’ kwa kitendo chake cha kuwasema hadharani na kuwakosoa
viongozi wa Chadema, ambacho kilimgharimu uongozi.
Wengi
wanamkumbuka Kafulila kwa jinsi alivyolivalia njuga sakata la Akaunti ya Tegeta
Escrow katika Benki Kuu (BoT) lililohusu kampuni ya kufua umeme ya IPTL ambapo
mabilioni ya fedha yalichotwa na watu binafsi wakagawana.
Inakumbukwa
jinsi sakata hilo lilivyoiyumbisha serikali kiasi cha kulifumua Baraza la
Mawaziri na kumjengea umaarufu.
Hata
hivyo, wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Kafulila alishindwa kurejea
Bungeni na akashindwa pia kwenye kesi yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi.
Kafulila alikuwa
Mbunge wa Kigoma Kusini kupitia NCCR-Mageuzi kati ya mwaka 2010-2015, alijiunga
baada ya kutangaza kuachana rasmi na Chadema Novemba 18, 2009, zikiwa ni siku
saba tu tangu yeye na Danda Junju walipovuliwa nyadhifa zao na Sekretarieti ya
chama hicho.
Katika
waraka wake wa wazi kuhusu uamuzi wake wa kujitoa NCCR-Mageuzi, Kafulila
alieleza kwamba ameamua kujivua uanachama na nafasi ya uongozi aliyokuwa nayo
na kuelekea Chadema.
Pamoja na
mambo mengine, katika waraka huo Kafulila aliushukuru uongozi wa NCCR-Mageuzi
kwa muda wote aliokuwa nao na akaeleza uamuzi wake wa kujivua nafasi yake ya
uongozi na nia yake ya ‘kufuata mabadiliko’ licha ya ukandamizwaji unaofanywa
na vyombo vya kusimamia haki.
Akasema
kwamba, anaamini hakuna chama ambacho kinaweza kuunganisha nguvu na kuwa na
chama kimoja cha upinzani chenye mikakati thabiti ya kuleta mabadiliko zaidi ya
Chadema.
Mara
kadhaa nimekuwa nikisema; ‘Ukweli wa mwanasiasa ni jina lake tu’, lakini
mengine yote ni mbwembwe za kutafuta maslahi na kuungwa mkono.
Nakumbuka
vizuri kwamba Novemba 10, 2009 Kafulila na Danda teuzi zao zilitenguliwa ndani
ya Chadema – Kafulila ndiye aliyekuwa Msemaji wa Chadema (nafasi ambayo sasa
inashikiliwa na Tumaini Makene) na Danda alikuwa anahusika na masuala ya Bunge.
Kilichowaponza
wakati ule ni uswahiba wao na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa Chadema,
Zitto Zuberi Kabwe, ambaye wakati huo alikuwa na mvutano na uongozi wa juu wa
Chadema, ikiwemo kutaka kugombea uenyekiti.
Kafulila
alishtukia mapema kwamba anatimuliwa kwenye nafasi yake, na hiyo ilifuatia
kikao cha viongozi (Sekretarieti) wa Chadema kilichofanyika Dodoma, ambapo
aliwahi mapema kwenye vyombo vvya habari na kusema kwamba kuna mpango wa
viongozi wa Chadema kutaka kumtimua.
Alipozungumza
na wanahabari Novemba 10, 2009, Kafulila alisema aliambiwa kwa mdomo na Katibu
Mkuu Dk. Wilbrod Slaa, na kwamba aliitwa kwenye kikao cha sekretariati siku
hiyo kuhojiwa kuhusu matamshi yake kwenye vyombo vya habari yaliyomtuhumu
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kufanya kikao kisicho rasmi Dodoma kwa
ajili ya kumwengua uanachama yeye na wenzake.
Dk. Slaa
mwenyewe alisema: "Tena andika wala usiogope ni kwamba, leo kulikuwa na
kikao, nimekiongoza mwenyewe na maamuzi nimeyatoa mwenyewe..., tumetengua
uteuzi wao. Sasa ni wanachama wa kawaida… Tunataka kusafisha chama..., maana
tukiacha hali hii tunaweza kuingia Ikulu na mambo ya ajabu."
Ndicho
kipindi ambacho zengwe la kutaka kumng’oa Zitto lilikuwa limeshika kasi huku
wakimtuhumu mwanasiasa huyo kutaka kukigawa chama hicho ambacho wakati huo
kilikuwa ‘kinapambana na ufisadi’ wa majukwaani.
Na hata
Kafulila alipoondoka Chadema na kujiunga na NCCR-Mageuzi, bado aliendelea na
uswahiba wake na Zitto kiasi kwamba iliripotiwa kuwa hata magari aliyotumia
wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010 yalikuwa ya Zitto.
Kuenguliwa
kwa Kafulila na Danda katika nafasi zao kuliwafurahisha wanachama wengi ambao
waliowaona wanasiasa hao ni wakorofi na wenye kutaka kuleta migogoro isiyokuwa
na sababu.
Nakumbuka
Zitto alimtetea kwa nguvu zote Kafulila kupitia kwenye mitandao na akawakosoa
wale wote waliokuwa wakichangia mijadala kwamba ndio wanaotaka kusababisha
migogoro kwenye chama.
Katika
majibizano hayo, Zitto aliwahi kusema: “Can
you back up your allegations? Don’t spin! Mambo ya Chadema tuachie Chadema sawa?
Why are you defensive? Justice will
prevail.”
Hata hivyo,
baada ya kupata taarifa rasmi, Zitto, ambaye alikuwa nje ya nchi, alionekana
kutofurahishwa na uamuzi huo na katika ujumbe wake kwa gazeti moja la kila
siku, alisema: "Ninasikitika kuwa tunachukua maamuzi kama haya kipindi
hiki ambacho nchi inahitaji chama imara cha upinzani. Kafulila ni mgombea
mtarajiwa wa ubunge katika Jimbo la Kigoma Kusini ambalo CCM wamefanya vibaya
katika uchaguzi wa serikali za mitaa kuliko majimbo yote nchini. Uamuzi huu
unaweza kuwashtua sana wanachama wetu Kigoma Kusini na mkoa wa Kigoma kwa
ujumla."
Zitto
alikumbusha kuwa Kafulila aligombea uenyekiti wa jumuiya ya vijana ya Chadema
na akashinda, lakini uchaguzi ulivurugwa na kufutwa na hivyo utarudiwa na hivyo
uamuzi wa kumfukuza Kafulila ni dalili za wazi za watu waliofuta uchaguzi huo
kuleta vurugu kwenye chama kwani wanachama hawatakubali uonevu.
"Kwangu
mimi Kafulila ni kijana mahiri mwenye kukipenda chama chetu na ndio maana
niliamua kumgroom (kumkuza) ili aje kuwa mgombea ubunge na baadaye mbunge
katika Jimbo la Kigoma Kusini. Anakipenda chama chake, ana akili nyingi na
mjuzi wa kujenga hoja katika kutetea chama bila woga," alisema Zitto.
Kama
katika kipindi kile walau alikuwa na mtetezi ndani ya Chadema (Zitto Kabwe),
je, safari hii nani atamtetea ikitokea kwamba misimamo yake itaendelea kubaki
ile ile? Au kwa vile Dk. Slaa sasa hayupo?
Je,
amerejea Chadema kwa nia ya dhati au kwa sababu amekosa ubunge kupitia
NCCR-Mageuzi na hakusaidiwa wakati wa kesi yake? Au amemfuata mkewe, Jesca
Kishoa, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum?
Kama
wakati ule aliamua kuondoka Chadema baada ya kuvuliwa uongozi kwa sababu ya
kuusema uongozi, je, wana-Chadema leo waamini kwamba amebadilika na hataweza
kuwakosoa viongozi wake kama ilivyokuwa mwanzo?
Kuna
mashaka na kurejea kwake na haifahamiki ni kutangatanga kusaka madaraka ama
kweli amesukumwa na msimamo wa Chadema, kama anavyodai mwenyewe kwamba ndicho
chama kitakacholeta mabadiliko.
NCCR-Mageuzi
ni miongoni mwa vyama vilivyokuwa vikiunda umoja mfu wa Ukawa, na Kafulila
anatambua kwamba yeye pia alikuwa mmoja aliyeunga mkono umoja huo. Sasa ana
uhakika gani kama Chadema itakuwa na nguvu kama ilivyokuwa mwaka 2015 chini ya
Ukawa?
Tusubiri
tuone itakavyokuwa, vinginevyo ni staili zile zile za wanasiasa za kutangatanga
kusaka tonge na kusahau walichokisema jana.
0656331974
Comments
Post a Comment