Featured Post

UAMUZI WA KAMATI YA SAA 72 YA UENDESHAJI NA USIMAMIZI WA LIGI

Uchunguzi dhidi ya waamuzi Martin Saanya, Samuel Mpenzu (mechi ya Yanga Vs Simba), Thomas Mkombozi (mechi ya Coastal Union Vs KMC) na Rajab Mrope (mechi ya Mbeya City na Yanga) umekaribia kukamilika.

Hatua ya mwisho ya uchunguzi huo ni wao kufika mbele ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya Saa 72) ambapo watahojiwa ili kutoa ufafanuzi katika masuala mbalimbali yaliyojitokeza katika taarifa zao.

MATUKIO YA LIGI KUU
Mchezo namba 90 (Simba Vs Toto Africans). Klabu ya Toto Africans imepewa onyo kali kutokana na timu yake kuchelewa kufika uwanja kwa dakika saba. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.

Mechi namba 99 (Mwadui Vs Simba). Klabu zote mbili zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa timu zao kuingia uwanjani kwa kutumia mlango wa washabiki, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(48).

Mechi namba 101 (Ruvu Shooting Vs Stand Utd). Ndanda FC imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kosa la timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi,  kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(48).

Nayo Ruvu Shooting ambayo ilikuwa uwanja wa nyumbani, imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika 15. Kitendo hicho ni ukiukwaji wa Kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu, na adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48).

Mechi namba 104 (JKT Ruvu Vs Ndanda). Klabu ya Stand United imepewa onyo kali baada ya wachezaji wake kufanya vurugu wakitaka kuingia uwanjani bila ya kuwa na uthibitisho kuwa wao ni wachezaji wa timu hiyo wakati wa mechi kati ya JKT Ruvu na Ndanda iliyofanyika Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 42(1).

Mechi namba 112 (Majimaji Vs JKT Ruvu). Daktari wa JKT Ruvu, Abdullah Yusuf amefungiwa miezi mitatu, na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi kwa kusababisha usumbufu kwa Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, na kuwatolea maneno machafu Mwamuzi na Mwamuzi wa Akiba. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 41(2).

Mtaalamu wa viungo wa JKT Ruvu, George Minja amefungiwa miezi mitano na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kumvamia Mwamuzi akitaka kumpiga, na pia kutoa lugha ya matusi kwa waamuzi baada ya mechi hiyo. Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41(2).

Nao wachezaji wa JKT Ruvu, Said Kipao jezi namba moja, Samwel Kamuntu (22), Pela Mavuo (16) na paul Mhidzhe (23) wamefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 kila mmoja kwa kuwatukana waamuzi baada ya mchezo kumalizika. Adhabu imezingatia Kanuni ya 37(7).

Mechi namba 116 (Mbao FC Vs Azam FC). Kocha wa Azam FC, Zeben Hernandez amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi (ordered off) kwa kukataa kuheshimu mipaka ya eneo la ufundi (technical area) katika mechi hiyo. Adhabu imezingatia Kanuni ya 40(11).

Mechi namba 117 (Ndanda Vs Stand Utd). Katika mechi hiyo kadri muda ulivyokuwa ukienda ball boyz walichelewesha kurudisha mipira uwanjani, na mbaya zaidi mipira ilikuwa ikifichwa kiasi cha kubaki miwili kati ya sita iliyokuwepo. Msimamizi wa Kituo ameandikiwa barua ili ahakikishe suala hilo halijitokezi tena.

Mechi namba 59 (Yanga Vs Ruvu Shooting). Timu ya Ruvu Shooting imepewa onyo kali kwa kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika 12, jambo ambalo ni kinyume cha Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu.

Kocha wa Yanga, Hans van Pluijm amepigwa faini ya sh. 500,000 na kufungiwa mechi tatu baada ya wakati wa mapumziko kuwazonga waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa. Pia baada ya mechi kumalizika alikwenda kwenye chumba cha waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa. Adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 40(1).

Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya washabiki wake kuwazonga waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa walipokuwa wakiingia vyumbani wakati wa mapumziko. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1).

Mechi namba 60 (Tanzania Prisons Vs Simba). Klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na timu yake kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) na kufika wakati taratibu zote za msingi zikiwa zimemalizika. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu.

Klabu zote (Tanzania Prisons na Simba) zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa timu zao kuingia uwanjani kwa milango isiyo rasmi. Kitendo hicho ni kinyume cha Kanuni ya 14(14), na adhabu imezingatia Kanuni ya 14(48).

Pia Tanzania Prisons imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya gari la Jeshi la Magereza namba MT 0084 aina ya Toyota Land Cruiser Pick Up likiwa na watu 15 kuingia uwanjani kwa nguvu, na kusababisha kupigwa na kuumizwa kwa mlinzi wa getini. Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1).

Kamishna wa mechi hiyo Jimmy Lengwe kutoka Morogoro amepewa onyo kali kwa kutoripoti baadhi ya matukio ya wazi yaliyotokea kabla ya mechi hiyo kuanza.

MATUKIO YA LIGI DARAJA LA KWANZA

GROUP A
Mechi namba 17  (Polisi Dar Vs Ashanti Utd). Kiongozi wa Polisi Dar, Ulimwengu Hamimu amefungiwa miezi sita na kupigwa faini ya sh. 200,000 kwa mujibu wa Kanuni ya 41(2). Kiongozi huyo alichukua mpira na kuupiga kwenye jukwaa la timu ya Ashanti Utd na kutaka kumpiga Mwamuzi akiwa na mchezaji wake Pascal Theodory mwenye jezi namba 15. Mchezaji huyo amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 100,000.

Mechi namba 19 (Pamba Vs African Sports). Klabu ya African Sports imepewa onyo kali kwa kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) kwa dakika nne, na kufika na viongozi watatu badala ya wanne.

Mchezaji Shaban Kimaro amefungiwa mechi sita na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kumpiga kichwa Mwamuzi Msaidizi Namba Mbili. Mwamuzi alimtoa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa hilo alilolifanya dakika 83. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 24(6) ya Ligi daraja la Kwanza.

Naye Salum Omari pia wa African Sports amefungiwa mechi tatu na faini sh. 300,000. Akiwa mchezaji wa akiba aliingia uwanjani kwa nia ya kutaka kumshambulia Mwamuzi, lakini Polisi walimuwahi na kumtoa.

Mechi namba 20 (Kiluvya Utd Vs Mshikamano). Mchezaji Ayoub Upatu wa Mshikamano amesimamishwa na suala lake limepelekwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF kwa hatua zaidi baada ya Kiluvya Utd kuwasilisha pingamizi dhidi yake kuwa ni mchezaji wao, kwani wana leseni yake. Katika leseni ya Kiluvya Utd ametumia jina la Ayoub Kassim Lipati.

Mechi namba 25 (Ashanti Utd Vs Lipuli). Kamati imetupa malalamiko ya timu ya Lipuli dhidi ya Ashanti Utd kuwa katika mechi yao ilimchezesha mchezaji Patrick James mwenye jezi namba 15 wakati akiwa na kadi tatu za njano. Kamati imebaini wakati James akicheza mechi hiyo alikuwa na kadi mbili za njano, na si tatu.

Mechi namba 27 (Kiluvya Utd Vs Friends Rangers). Kocha Msaidizi wa Friends Rangers, Fadhili Ndumba amefungiwa mechi mbili na faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi na Mwamuzi kwa kutoa lugha ya matusi kwa Mwamuzi Msaidizi Namba Moja. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.

GROUP B
Mechi namba 23 (Kurugenzi Vs Kimondo). Viongozi wa Kimondo, Eric Ambakisye, Selestine Mashenzi, na Mussa Minga wamefungiwa miezi sita, na kupigwa faini ya sh. 500,000 kila mmoja kwa kuwafuata waamuzi hotelini baada ya mechi ambapo walimpiga Mwamuzi Mussa Gabriel na kumjeruhi wakishirikiana na baadhi ya wachezaji wao.

Wachezaji waliohusika katika tukio hilo ambapo wamefungiwa mechi sita na faini ya sh. 500,000 kila mmoja ni; January Daraja Mwamlima, Daniel Douglas Silvalwe, Abiud Kizengo na Monte Stefano Mwanamtwa. Adhabu zote ni kwa mujibu wa Kanuni ya 24(6) ya Ligi Daraja la Kwanza.

GROUP C
Mechi namba  23 (Alliance Vs Mvuvumwa). Kocha Msaidizi wa Mvuvumwa, Ezekiel Chobanga amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi dakika ya 59 kwa kumtolea lugha chafu Mwamuzi. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mechi namba 24 (Polisi Dodoma Vs Rhino Rangers). Mchezaji Sameer Mwishehe wa Rhino Rangers amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumrushia Mwamuzi chupa ya maji baada ya mchezo kumalizika. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 37(7) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mechi namba 25 (Polisi Dodoma Vs Mgambo Shooting). Kocha wa Mgambo, Athuman Kairo amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kumshambulia kwa maneno Mwamuzi wa Akiba. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 40(11).

Mechi namba 28 (Alliance Vs Singida Utd). Baada ya Alliance kupata bao, watu wa huduma ya kwanza walipokuwa wakiitwa kuingia uwanjani, walikuwa wanakwenda kwa kupoteza muda. Msimamizi wa Kituo ameandikiwa barua ya kuwakumbusha watu wa huduma ya kwanza kutekeleza majukumu yao wawapo uwanjani, na kuhakikisha kuwa tukio la aina hiyo halitokei tena.

LIGI DARAJA LA PILI
GROUP A
Mechi namba 4 (Bulyanhulu Vs Green Warriors). Mechi hiyo haikuchezwa kutokana na wachezaji wa Bulyanhulu kutokuwa na leseni, na vilevile kutokuwepo mawasiliano kati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Kamishna wa mechi hiyo juu ya tatizo hilo. Hivyo, mechi hiyo itapangiwa tarehe nyingine na kuchezwa katika uwanja huru (neutral ground).

Mechi namba 7 (Mji Mkuu Vs Bulyanhulu). Mechi hiyo haikuchezwa baada ya wachezaji wa Bulyanhulu wakiongozwa na Katibu Mkuu wao Alphonce Innocent kugomea wakitaka wachezaji watano wa Mji Mkuu ambao hawakuwa na leseni, lakini walikuwa na utambulisho maalum kutoka TFF wasicheze.

Licha ya Kamishna kuwataka wacheze na baadaye wawasilishe malalamiko yao kwake, walikataa huku Katibu wao Innocent akimzonga Kamishna na kumtukana. Bulyanhulu imepoteza mechi hiyo kwa kusababisha ivurugike kwa kuzingatia Kanuni ya 29(4) ambapo pia imepigwa faini ya sh. 1,000,000. Mji Mkuu imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu.

Pia Katibu Mkuu wa Bulyanhulu, Aplhonce Innocent amefungiwa miezi sita kutojihusisha na shughuli yoyote inayohusu mpira wa miguu. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 29(6) ya Ligi Daraja la Kwanza.

GROUP B
Mechi namba 1 (African Wanderers Vs AFC). Klabu ya African Wanderers imepigwa faini ya sh. 200,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mechi licha ya kuwa ni wenyeji. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili.

Mechi namba 5 (African Wanderers Vs Kitayosce). Wachezaji Ally Rashid na Israel Said wa African Wanderers wamefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kila mmoja kwa Mwamuzi kuwatoa kwa kadi nyekundu baada ya kwenda nje ya uwanja na kupigana na washabiki. Adhabu imezingatia Kanuni ya 37(3) ya Ligi Daraja la Pili.

Mechi namba 12 (JKT Oljoro Vs African Wanderers). Mechi hiyo haikuchezwa baada ya kutokea mkanganyiko wa mawasiliano kati ya African Wanderers na ofisi ya Bodi ya Ligi, hivyo itapangiwa tarehe nyingine.

GROUP D
Mechi namba 2 (Namungo Vs Sabasaba). Baada ya Namungo kufunga bao, washabiki wa timu hiyo waliingia uwanjani kushangilia. Klabu hiyo pamoja na Msimamizi wa Kituo wamepewa onyo kali kuhakikisha tukio hilo halitokei tena. Pia sehemu kubwa ya uwanja huo hauna nyasi, hivyo klabu husika imetakiwa kuhakikisha nyasi zinapandwa kabla ya kuanza mzunguko wa pili.

Mechi namba 9 (Mbarali United Vs Mkamba Rangers). Kamati imefuta kadi nyekundu aliyoonyeshwa mchezaji David Francis mwenye jezi namba 5 wa Mkamba Rangers baada ya kubaini kuwa ilitolewa kimakosa.

MIN 34/MSC/2016 - MAOMBI YA MVUVUMWA KUCHEZA SHINYANGA
Kamati imeridhia maombi ya timu ya Mvuvumwa kuhamishia mechi zake za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga kutoka Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma. Hivyo, kuanzia Mzunguko wa Pili wa SDL, mechi za Mvuvumwa zitachezwa mjini Shinyanga.

Comments