- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na
Daniel Mbega
SERIKALI
ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli imeonyesha mabadiliko makubwa
ya utendaji na nidhamu kwa watumishi wa umma sambamba na kupambana kwa vitendo
katika suala zima la rushwa na ufisadi.
Katika
kipindi cha mwaka mmoja tangu aingie madarakani, Rais Magufuli ameweza
kuwafichua na kuwawajibisha watendaji wa serikali ambao kwa namna moja ama
nyingine wamehusika na uzembe, ufisadi na rushwa, ambapo wengine kesi zao zinaendelea
katika mahakama za sheria.
Idara
mbalimbali za umma kama Mamlaka ya Mapato Tanzania – TRA, Mamlaka ya Bandari na
nyinginezo zimeshuhudia vigogo wake wakiwajibishwa kwa sababu ya uzembe na
ufisadi huku idara nyinginezo watumishi mbalimbali wakiendelea ‘kutumbuliwa’
katika kauli-mbiu yake ya ‘utumbuaji majipu’.
Nidhamu
sasa imeanza kuimarika, watu wanachapa kazi, vitendo vya rushwa vinaonekana
kupungua na mafisadi wanaendelea kulia kwa sababu mirija yao imezibwa kama siyo
kung’olewa kabisa.
Lakini
jitihada hizo hazitaweza kukamilika ikiwa serikali hii haitageukia vigogo wengi
walioficha mabilioni ya fedha ughaibuni, hususan nchini Uswisi, jukumu ambalo
linamkabili Rais Magufuli.
Itakumbukwa
kwamba, Ijumaa ya Mei 16, 1997 mara tu baada Laurent Desire Kabila kuipindua
serikali ya mwanahabari Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu
Wa Za Banga nchini Zaire, alitangaza kutaifisha mali zote za dikteta huyo
aliyeitawala kwa mkono wa chuma nchi hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika kwa
miaka 32.
Siku
moja baadaye, yaani Jumamosi Mei 17, 1997 serikali ya Uswisi nayo ikatangaza
kuzuia mali za Mobutu kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya kupokea maelekezo
kutoka kwa utawala mpya wa Kabila, ambaye wakati huo alikuwa ameweka makao yake
makuu jijini Lubumbashi.
Mali
zilizozuiliwa kufuatia uamuzi wa serikali ya Uswisi ni pamoja na hekalu lake
lenye vyumba 300 lililokuwa eneo la Savigny pembezoni mwa ziwa huko Lausanne,
ambalo kwa wakati huo thamani yake ilikuwa yapata Dola 5 milioni. Hili lilikuwa
miongoni mwa vitegauchumi vyake vingi tu barani Ulaya ambako ilielezwa kwamba
vyote kwa pamoja vilikuwa na thamani ya takriban Dola 37 milioni kwa wakati
huo.
Ingawa
kulikuwa na taarifa kwamba Mobutu, ambaye jina lake la ubatizo aliitwa Joseph-Desiré Mobutu, alikuwa ameficha karibu Dola 4 bilioni, lakini
serikali ya Uswisi ilichunguza katika benki zote 400 nchini humo na haikuona fedha zozote zilizowekwa kwa jina lake
au jina la wanafamilia wake.
Taarifa
iliyotolewa na taasisi ya Transparency International kupitia Bribe-Payers Index
ilieleza kwamba, Mobutu na Mohammed Suharto wa Indonesia na Ferdinand Marcos wa
Ufilipino kwa pamoja walifisidi nchi zao jumla ya Dola 50 bilioni, kiasi
ambacho kwa wakati huo kilikuwa sawa na bajeti nzima ya mwaka ya misaada kutoka
nchi wahisani.
Suharto alikomba takriban Dola 35 bilioni katika kipindi cha
utawala wake wa miongo mitatu kabla ya kufukuzwa wakati ambapo Mobutu yeye
alichota nusu ya Dola 12 bilioni za misaada ambazo zilitolewa na Shirika la
Fedha Duniani (IMF) kwa kipindi chote cha utawala wake na kuifanya nchi hiyo
ibaki na madeni makubwa hadi sasa.
Mobutu, ambaye alithubutu kulipa Dola 10 milioni kwa
mabondia Muhammad Ali na George Foreman (Dola 5 milioni kila mmoja) ili
wakapigane jijini Kinshasa Oktoba 30, 1974, hakuona shida yoyote kutumia fedha
hata kwenda kufanya ‘shopping’ Ulaya na ndiye rais pekee Afrika kutumia midege
mikubwa na ghali zaidi duniani, Concorde.
Mwaka
1989, Mobutu alikodi ndege ya Concorde yenye namba za usajili F-BTSD kutoka
Shirika la Ndege la Ufaransa (Air France) kwa ajili ya safari ya Juni 26– Julai
5 kwenda tu kutoa hotuba kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa jijini New York,
Marekani, Julai 16 akakodi ndege hiyo kwenda Paris, Ufaransa kuhudhuria sherehe
za nchi hiyo baada ya kualikwa na Rais François Mitterrand, Septemba 19 akakodi
dege hilo kutoka Paris hadi mjini Gbadolite, Zaire na safari nyingine ya moja
kwa moja kutoka Gbadolite hadi jijini Marseille akiwa na kwaya ya vijana wa
Zaire.
Kwa
kutumia fedha za Wazaire, aliamua kujenga uwanja maalum mjini Gbadolite, kaskazini
mwa nchi hiyo ambako ndiko alikotokea, ili kuliwezesha dege la Concorde litue
na kuruka. Uwanja huo uliokuwa kwenye
kilele cha meta 460 kutoka usawa wa bahari, njia yake ya kurukia ilikuwa na
urefu wa meta 3,200 (kilometa 3.2) na upana wa meta 60.
Lakini
kama tulidhani zama za akina Mobutu, Suharto na akina Marcos zimekwisha,
tutakuwa tunajidanganya, kwa sababu mpaka sasa bado viongozi na maofisa wa
kawaida wa serikali zetu, hasa kwa nchi za dunia ya tatu kama Tanzania,
wanaendelea kukomba fedha za wananchi na kuzificha ughaibuni – mara nyingi
wakitumia majina ya washirika wao kwa kuhofisa yasiwapate kama yaliyowakumba
wengine.
Kwa
miaka kadhaa sasa, tumeelezwa kwamba wapo vigogo wengi wa Tanzania – viongozi
wa serikali, wafanyabiashara na hata viongozi wa dini – ambao mbali ya kuwa na
mahekalu ughaibuni, pia wameficha mabilioni huko ng’ambo.
Wapo
ambao majina yao yamekuwa yakitajwa kwa minong’ono, lakini kuna wale ambao
licha ya kuanikwa hadharani, baadhi yao wamewahi hata kutoa kauli za kejeli
kwamba “ni vijisenti tu”, kama alivyosema Mwanasheria Mkuu wa zamani wa
Serikali, Andrew Chenge, mwaka 2008 baada ya kubainika kwamba alificha karibu
Dola 1 milioni huko Uingereza.
Taarifa
zinasema, orodha iliyopo ni ya Watanzania
walioficha zaidi ya Dola 3.5 milioni kila mmoja, ambapo inaelezwa kwamba fedha
nyingi za wanasiasa zimewekwa na makampuni ya nje yenye shughuli Tanzania.
Katika
majina ambayo yamekuwa yakinong’onwa, wamo vigogo waliopata kuwa mawaziri
katika serikali zilizopita, lakini pia Julai 2015, Kiongozi Mkuu wa Chama cha
ACT-Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe, katika mkutano wake jijini Dar es Salaam,
alitoa orodha ya Watanzania 99 wenye asili ya Kiasia ambao wameficha takriban
Dola 114 bilioni katika benki mbalimbali nchini Uswisi.
Inafahamika
kwamba Uswisi ni ‘kisiwa’ salama kwa watu kuficha fedha zao kutokana na mfumo
na sheria za kifedha za nchi hiyo, ambapo wahusika hawaulizwi ‘maswali ya
ajabu’ wanapotaka kufungua akaunti zao, hali ambayo inafanya hata fedha chafu
zote zihifadhiwe huko.
Kati
ya waliotajwa na Zitto, wapo wafanyabiashara ambao wametajwa katika kashfa
nyingi za mikataba inayoendelea kulitafuna taifa hadi sasa, zikiwemo kashfa za
ufisadi za EPA, Richmond, na mikataba ya Radar, ununuzi wa ndege na magari ya
jeshi na kadhalika.
Swali ni
kwamba, vyombo husika vina taarifa? Kama taarifa zipo, zimefanyiwa kazi? Kama
kazi imefanyika, matokeo yake yakoje? Ikiwa havina taarifa, viko hapo vinafanya
nini? Kuna umuhimu wowote wa kuendelea na vyombo hivyo kama haviwezi kufuatilia
hata minong’ono na kuchunguza kama minong’ono hiyo ina ukweli wowote?
Jibu
ni kwamba taarifa zipo. Kama ilivyo kawaida ya nchi hii, hakuna anayejali.
Lakini hapana, wanajali sana. Tatizo ni kwamba, hata huyo aliyetakiwa
kushughulikia wahusika, naye ni mhusika. Hapo ndipo penye tatizo.
Julai
2012, Benki Kuu ya Tanzania kupitia kitengo chake cha Financial Intelligence
Unit (FIU) ilisema kwamba imeanza kuchunguza madai ya Watanzania walioficha
fedha Uswisi kama wanavyofanya wenzao wa mashirika ya kijasusi ya CIA
(Marekani), MI6 (Uingereza), RAW (India), DGSE (Ufaransa), FSB (Urusi), ISI (Pakistan),
Mossad (Israel) na MSS (China), ambayo yamekuwa yakifuatilia nyendo za fedha
haramu hasa za kighaidi dunia.
Inaelezwa kwamba, fedha nyingi kati ya hizo
zilizofichwa huko zinadaiwa kutokana na biashara zilizofanywa na watendaji wa
Serikali na wafanyabiashara kwenye Sekta za Nishati na Madini na kwamba sehemu
kubwa ya fedha zililipwa na kampuni za utafutaji mafuta na gesi katika pwani ya
Mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.
Serikali ya awamu ya nne kupitia Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma mwaka 2012 ilianza kuwachunguza baadhi ya mawaziri wake pamoja
na wabunge kutokokana na kujilimbikizia mali nyingi tofauti na kipato chao
halali, lakini hakuna matokeo yoyote yaliyowekwa hadharani.
Ripoti ya Global Financial Integrity (GFI)
ya mwaka 2008 ilionyesha kwamba kumekuwa na ongezeko la kiasi cha fedha
kinachotoroshwa katika nchi mbalimbali duniani kutoka Dola za Marekani 1.06
trilioni za mwaka 2006 hadi kukaribia Dola 1.26 trilioni za mwaka 2008.
Katika kiasi hicho cha fedha, wastani wa
Dola 725 bilioni hadi 810 bilioni zilitoroshwa kwa mwaka tangu mwaka 2000 hadi
2008 kutoka katika nchi zinazoendelea.
Ripoti hiyo inaonyesha pia kwamba,
Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, zinaongoza kwa asilimia 24.3, nchi
zinazoendelea za Ulaya asilimia 23.1, Afrika asilimia 21.9 na Asia asilimia
7.85.
Katika ripoti hiyo, nchi 10 zinazoongoza
duniani kwa kuwa na kiwango kikubwa cha fedha kilichotoroshwa kati ya mwaka huo
2000 hadi 2008 na kiasi katika mabano ni China (Dola 2.18trilioni), Russia
(Dola 427bilioni), Mexico (Dola 416 bilioni), Saudi Arabia (Dola 302bilioni),
Malaysia (Dola 291bilioni), Umoja wa Falme za Kiarabu (Emirates, Dola 276
bilioni), Kuwait (Dola 242bilioni), Venezuela (Dola 157bilioni), Qatar (Dola
138bilioni) na Nigeria (Dola 130bilioni).
Benki ya Dunia (WB) ilianzisha mpango wa
Stolen Asset Recovery Initiative StAR (Juhudi za Kurejesha Mali na Fedha Zilizoibwa) na
kuongeza kwamba juhudi hizo zinafanya kila nchi na taasisi kama BoT kufahamu
fedha za watu wake zilizofichwa nje.
Ni wakati muafaka sasa kwa serikali ya
awamu hii kulivalia njuga suala la mabilioni hayo ya Uswisi, wahusika wahojiwe
walivyoyapata, kama hakuna majibu ya kuridhisha, wataifishwe kwa sababu huo ni
uhujumu uchumi.
0656-331974
Comments
Post a Comment