Featured Post

KUMEKUCHA AZAM SPORTS FEDERATION CUP


Azam Sports Federation Cup (ASFC) itakayoshirikisha timu 86 msimu huu, itaanza rasmi kesho Novemba 19, 2016 kwa uzinduzi rasmi utakaofanyika mkoani Tanga kwa kuzikutanisha Bingwa wa Mkoa wa Tanga, Muheza United na Sifa Politan ya Temeke, Dar es Salaam kwenye  Uwanja wa Mkwakwani jijini humo.
 
Siku hiyo kabla ya mchezo kutakuwa na shamrashamra kupamba michuano hiyo ambako wachezaji wa zamani wa Coastal Union na African Sports za Tanga zitachuana kabla ya kuanza kwa mchezo huo wa uzinduzi. Timu hizo za maveterani, zitachezwa kuanzia saa 8.00 mchana.

Pia kutakuwa na shamrashamra za wasanii walioandaliwa na Wadhamini Azam Tv ambayo kwa msimu wa 2016/17 zimeongezwa timu 22 kutoka mabingwa wa mikoa-- Muheza na Sifa Politan ni miongoni mwa timu hizo. Ongezeko hilo tofauti na msimu uliopita ambako kulikuwa na timu 64.

Mwaka huu kuna timu 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL); timu zote 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), timu zote 24 za Daraja la Pili (SDL) na timu 22 za mabingwa wa mikoa. Mashindano hayo yatakuwa ni ya mtoani na yataendeshwa kwa raundi tisa (9).

Raundi ya Kwanza itashirikisha timu zote 22 za Mabingwa wa Mikoa katika makundi manne ya timu sita na timu tano ambako timu mbili za juu zitaingia raundi ya pili.

Raundi ya Pili itashirikisha timu nane zilizofuzu za RCL katika raundi ya kwanza na kujumlisha timu 24 za Daraja la Pili (SDL) kufanya jumla ya timu zote kuwa 32 kwa hatua ya pili.

Raundi ya Tatu itashirikisha timu 16 zilizofuzu hatua ya pili kushindana ili kupata timu nane zitakazoingia hatua ya nne.

Raundi ya Nne itashirikisha timu zote za Daraja la Kwanza (24) na kumulisha timu nane (8) zilizoshinda Raundi ya Tatu (3) kufanya timu zote kuwa 32.

Raundi ya Tano, itashirikisha timu 16 zilizofuzu Raundi ya Nne (4) na kumuisha timu zote 16 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kufanya timu zote katika raundi hii kuwa 32.

Raundi ya Sita itashirikisha timu zote 16 zilizofuzu katika Raundi ya Tano na mzunguko huo utaitwa Hatua ya 16 Bora.

Raundi ya Saba (7) itashirikisha timu nane zilizofuzu katika raundi ya sita na mzunguko huo kutambuliwa kuwa Nane Bora au Hatua ya Robo fainali .

Raundi ya Nane ambayo itashirikisha timu nne zilizofuzu Raundi ya Saba (Robo Fainali) na mzunguko huo utatambuliwa kuwa ni Nusu Fainali.

Raundi ya Tisa itashirikisha timu mbili zilizofuzu Raundi ya Nane na washindi hao wa Nusu Fainali na kumpata Bingwa wa Azam Sport Federation Cup kwa msimu wa 2016/2017.

Comments