Featured Post

HATUWEZI KUENDELEA KWA MISAADA NA MIKOPO



Na Daniel Mbega, Iringa
HIVI karibuni nilitembelea karibu vijiji 20 vya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa kuangalia shughuli mbalimbali za uchumi pamoja na changamoto zinazowakabili wananchi wa huko.
Niliyoyaona huko, ambayo hapa siwezi kuyaeleza kwa kirefu, yanakatisha tamaa na kuzua hoja nyingi zisizo na majibu katika Taifa ambalo kwa miaka 55 iliyopita tangu Uhuru, limekuwa likitajwa kwamba ‘bado ni changa’, tena maskini!

Kama ilivyo kawaida, kwamba karibu asilimia 83 ya Watanzania wanaishi vijijini na wanategemea kilimo kama shughuli yao kuu ya uchumi, ndivyo ilivyo hata katika ukanda huo ambao nilibahatika kuutembelea.
Naam, ardhi ipo – ya kutosha – lakini tayari viongozi wetu wa serikali, kwa kutumia kisingizio cha ‘uwekezaji’, imekwisha ibinafsisha kwa ‘wawekezaji’ na kuwapatia mamia kwa maelfu ya hekta huku wakiwamilikisha kwa karne nzima.
Sera za ubinafsishaji na kujikomba kwa wafadhili kwa ajili ya kupatiwa misaada na mikopo ya maendeleo wakati rasilimali tunazo, huku tukiwamegea wageni mapande makubwa ya ardhi kwa kisingizo cha uwekezaji ndiyo inayoonekana kutamalaki wakati wananchi wakikosa misaada muhimu.
Wananchi wa maeneo hayo, ambao wanafanana na maeneo mengi nchini kote, wana juhudi kubwa za kuzalisha mali, lakini katika sehemu nyingi nilizopita, wamenyimwa barabara nzuri na huduma nyingine za kijamii kiasi kwamba hata mazao yao wanayolima hayawezi kufika sokoni, achilia mbali kupata huduma za afya.
Kwa kunyimwa huku kwa makusudi kabisa, narudia tena kwa makusudi kabisa, ndipo wanapoingia hawa walowezi wapora ardhi na wakoloni wa kesho kwa kisingizio cha uwekezaji na ahadi kwamba ‘watawajengea zahanati na nyumba za walimu’, mambo ambayo hayalingani kabisa na thamani ya ardhi wanayomegewa kwa miaka 100.
Nimesema serikali imefanya makusudi kabisa kuwanyima huduma hizi Watanzania hawa kwa sababu haiwezekani katika kipindi cha miaka 55 ya Uhuru, wananchi wa sehemu hizi hawajawahi kuliona hata greda moja kwa ajili ya kutengeneza barabara, sehemu nyingi magreda hayo yalipita enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere.
Matokeo yake, wananchi ndio wamegeuka magreda. Msishangae, ni kweli kwa sababu hivi sasa wananchi hao ndio wanaochonga barabara kwa majembe ya mikono na nyengo wakati serikali yao inawatazama.
Sasa wakiwatengenezea barabara, wakapata maendeleo, hivi hao jamaa zao ‘wawekezaji’ wakija watapata wapi ardhi ya kujimilikisha? Wananchi hawa si watakwenda mjini kuuza maharage yao na kupata fedha za kujikimu badala ya kuuza ardhi?
Ndiyo, tuliaminishwa tangu enzi za TANU na hasa kwa kurejea misingi ya Azimio la Arusha kwamba maendeleo yanaletwa na watu, siyo fedha, na kwmaba fedha ni matokeo wala si msingi wa maendeleo.
Tuliamini kwamba, maendeleo yanahitaji Watu, Ardhi, Siasa safi na Uongozi Bora, lakini haya yote yaliuawa mwaka ule wa 1991 katika Azimio la Zanzibar lililoruhusu ‘Soko Huria’ ambalo naliita ‘Soko Holela’.
Wakati Azimio la Arusha linazaliwa, Tanzania ilikuwa na watu milioni 10 tu na eneo la ardhi ya kilimo la hekta milioni 5.1, ambayo ni sawa na asilimia 5 ya eneo lote la ardhi ya nchi. Leo hii, kwa kurejea Sensa ya Mwaka 2012, Tanzania ina jumla ya watu milioni 45, ardhi imebaki ile ile.
Kwahiyo basi, watu wapo, ardhi ipo ingawa sasa imekwishanadishwa kwa ‘wawekezaji’ na kutishia kwamba miaka kadhaa ijayo Watanzania watakuwa watumwa katika nchi yao. Watakosa ardhi na kulazimika kulima vibarua kwa ‘walowezi’ kwa sababu tu ya teni pasenti ya viongozi wachache wenye tamaa kama za fisi.
Suala la siasa safi sitaki hata kulisikia, kwa sababu hilo liliondoka na Mwalimu Nyerere mwenyewe. Zilizobaki sasa ni siasa za maji taka, za kuchafuana, kubezana, kupigana vijembe na hata wale tuliowaamini wamegeuka malenga wazuri wa ngonjera, tenzi na majigambo.
Uongozi bora nao ulitoweka na Mwalimu Nyerere, kilichopo sasa ni bora uongozi. Wote tuliowachagua na kuwateua wamegeuka wajasiriamali na wajasiriajamii wazuri kwa kutumia nyadhifa zao. Zile ahadi 10 za Mwana-TANU zilizorithiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho ndicho chenye serikali yake, zimechomwa moto kitambo zisionekane. Fitina, majungu, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka vimekuwa sehemu ya viongozi wa serikali yetu.
Watu tunao na ardhi tunayo. Lakini kwa kutowajibika kwa viongozi wetu, matokeo yake nchi, kwa maana ya ardhi na rasilimali zake, inauzwa huku tunaangalia, wengine wanachekelea. Na lazima wacheke, kwa sababu wanajua wapo madarakani kwa kitambo, wataondoka, watakaobaki watajua wenyewe.
Leo hii, kwa uzembe tu wa serikali yetu, tumegeuka Taifa la ombaomba, viongozi wetu wakuu wanatembeza bakuli Ulaya na kwingineko kuomba misaada, ikiwezekana mikopo, huku wakilalamika kwamba nchi yetu ni maskini.
Wahisani hao nao wanatumia udhaifu wa viongozi pamoja na huo ‘uamskini’ wetu kuingilia mpaka siasa za ndani.
Leo hii Marekani imegoma kutoa takriban Shs. 1.2 trilioni kwa ajili ya miradi ya MCC, kwa sababu tu ya suala la mgogoro wa Zanzibar!
Ni kweli, suala hilo bado tata, lakini kwa namna moja ama nyingine, ni mambo yetu ya ndani ambayo yanapaswa kushughulikiwa na kumalizwa na sisi wenyewe, siyo wao watuwekee vikwazo kwa sababu tu wanatusaidia.
Hii si mara ya kwanza kwa wahisani kutunyima fedha kwa sababu tu ya mambo yetu ya ndani. Walifanya hivyo katika Bajeti ya mwaka 2014/2015 lilipoibuka suala la Tegeta Escrow pamoja na tuhuma nyingi za ufisadi.
Ni kweli zinapaswa kushughulikiwa. Lakini wao siyo wa kutumia fimbo ya misaada kutuchapa na kutulazimisha tufanye kile wanachokitaka.
Kwa sababu ya mambo hayo na kutegemea mikopo na misaada, miradi mingi ya maendeleo imeshindwa kutekelezwa. Ardhi ya wananchi nayo inapigwa mnada kila siku huku wananchi wa vijijini wakishindwa kupatiwa huduma muhimu ikiwemo miundombinu hata ya barabara.
Tunawezaje kuendelea kwa mikopo na misaada wakati kumbe uzembe wao ndio unaolifanya taifa letu lionekane maskini? Hivi wananchi hawa wa vijijini wakiwekewa miundombinu bora ya barabara, wakajengewa zahanati, shule, nyumba za walimu na huduma nyingine muhimu pamoja na kupatiwa pembejeo za kutosha na masoko ya mazao yao ya uhakika, hawawezi kuzalisha na ziada?
Hatukatai msaada au mkopo, lakini tukumbuke kwamba kujitawala ni kujitegemea. Hatuwezi kujitawala kwa kutegemea msaada kutoka taifa jingine. Mingi kati ya misaada na mikopo hii ina walakini, tusipoangalia tutaiuza nchi yetu, na tumeanza kwa kuwamilikisha wageni ardhi kwa karne nzima.
Watanzania wana imani na serikali ya awamu ya tano chini ya Dk. John Magufuli, lakini matumaini yao yatakuwa hai ikiwa tu sekta muhimu za uzalishaji mali, hasa kilimo, zipatapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa wakulima kuwezeshwa, kupatiwa mikopo na taasisi za fedha, kuwekewa miundombinu na kutengenezewa mazingira bora ya masoko ya bidhaa zao.
Kusanyeni kodi, wekeni miundombinu bora, ondoeni ubinafsi na kurejea misingi ya wazee wetu, kinyume chake hata mifupa yenu itakuja kusutwa na vitukuu wenu.

0656-331974

Comments